top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin M, DM, MMMeD

25 Juni 2026, 12:37:12

Mbegu za Papai zinaweza kuzuia mimba? Tafisi zinasema nini hasa?

Mbegu za Papai na Afya ya Uzazi: Sayansi Inasema Nini Hasa?

Utangulizi

Papai (Carica papaya) ni tunda la kitropiki linaloliwa duniani kote kutokana na thamani yake ya lishe na manufaa mbalimbali ya kiafya. Ingawa sehemu yake ya ndani yenye rangi ya machungwa na ladha tamu ndiyo inayojulikana zaidi, mbegu ndogo nyeusi zinazopatikana katikati ya tunda zimevutia watafiti wengi kutokana na uwezekano wake wa kuathiri uzazi, mfumo wa uzazi na utendaji wa homoni.


Kwa miongo kadhaa, watafiti wamekuwa wakichunguza iwapo mbegu za papai zina uwezo wa kufanya kazi kama njia ya asili ya kuzuia mimba na kama zinaweza kuathiri homoni za uzazi kwa wanaume na wanawake.

Kuongezeka kwa matumizi ya tiba za asili kumewafanya watu wengi kutafuta mbadala wa njia za kawaida za uzazi wa mpango na matibabu ya matatizo ya uzazi. Kutokana na hali hiyo, madai kwamba mbegu za papai ni “njia ya asili ya kuzuia mimba” yameenea sana kupitia mitandao ya kijamii, blogu mbalimbali na simulizi za watu. Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya ushahidi wa kisayansi na madai maarufu kabla ya kufanya maamuzi yanayohusu afya.


Makala hii inachambua kile ambacho tafiti za kisayansi zimegundua kuhusu mbegu za papai, athari zake zinazowezekana katika uzazi na homoni, jinsi zinavyoweza kufanya kazi mwilini, masuala ya usalama, pamoja na mipaka ya maarifa yaliyopo kwa sasa.


Mbegu za Papai ni nini?

Mbegu za papai ni mbegu ndogo nyeusi zinazopatikana katika sehemu ya katikati ya tunda lililoiva. Mbegu hizi zina kemikali mbalimbali zenye uwezo wa kuathiri mifumo ya kibaolojia mwilini, zikiwemo:

  • Alkaloidi

  • Flavonoidi

  • Kampaundi za phenoliki

  • Benzyl isothiocyanate

  • Asidi za mafuta (fati asidi)

  • Vimeng'enya vinavyovunja protini (Vimengenya vya proteolytic)

Kemikali hizi zimeonekana kuchangia athari mbalimbali zilizobainishwa katika tafiti za maabara na tafiti za wanyama. Watafiti wanaamini kuwa baadhi ya kampaundi hizi zinaweza kuathiri viungo vya uzazi pamoja na udhibiti wa homoni mwilini.


Je, Mbegu za Papai zina homoni?

Mojawapo ya dhana potofu zinazojirudia mara nyingi ni kwamba mbegu za papai zina homoni za kuzuia mimba kama vile levonorgestrel, progesterone au estrogen.


Hata hivyo, tafiti za kisayansi bado hazijapata ushahidi wowote unaoonyesha kuwa mbegu za papai zina levonorgestrel kwa asili. Levonorgestrel ni homoni ya kutengenezwa viwandani inayotumika katika vidonge vya dharura vya kuzuia mimba na baadhi ya njia nyingine za uzazi wa mpango.


Kwa hiyo, mbegu za papai hazina dawa hii na haziwezi kuchukuliwa kama chanzo cha asili cha levonorgestrel.

Badala yake, watafiti wamekuwa wakichunguza kama kemikali zilizopo kwenye mbegu za papai zinaweza kuathiri mfumo wa uzazi kwa njia zisizo za moja kwa moja. Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa baadhi ya kampaundi hizo zinaweza kubadilisha michakato inayohusiana na uzazi, hasa katika tafiti za wanyama wa maabara.


Jinsi mbegu za Papai zinavyoweza kuathiri uzazi wa wanaume

Moja ya maeneo yaliyofanyiwa utafiti mkubwa zaidi kuhusu mbegu za papai ni athari zake katika uzazi wa wanaume.


Tafiti kadhaa za wanyama zimeonyesha kuwa dondoo za mbegu za papai zinaweza kupunguza kwa muda uzalishaji wa mbegu za kiume, uwezo wa mbegu hizo kujongea, na uwezo wa jumla wa kuzaa.

Watafiti waliona athari hizi baada ya wanyama kupewa maandalizi ya mbegu za papai kwa kipindi fulani cha muda.


Inaaminika kuwa mbegu za papai zinaweza kuvuruga ukomavu wa mbegu za kiume ndani ya epididimisi, sehemu ya mfumo wa uzazi wa mwanaume ambapo mbegu za kiume hukomaa na kupata uwezo wa kuogelea kuelekea yai kwa ajili ya urutubishaji.


Baadhi ya tafiti zimeonyesha kwamba idadi ya mbegu za kiume inaweza kubaki karibu na kiwango cha kawaida, lakini uwezo wake wa kujongea na kurutubisha yai hupungua kwa kiasi kikubwa.


Jambo la kuvutia ni kwamba tafiti nyingi zimeonyesha kuwa athari hizi zinaweza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kusitisha matumizi ya mbegu za papai. Baada ya muda, viashiria vya uzazi vilianza kuimarika na kurejea karibu na hali ya kawaida.


Matokeo haya ndiyo yaliyowafanya baadhi ya watafiti kuanza kuchunguza uwezekano wa kutumia misombo inayopatikana kwenye mbegu za papai katika kutengeneza dawa za baadaye za uzazi wa mpango kwa wanaume.


Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kuwa ushahidi kwa binadamu bado ni mdogo sana. Matokeo ya tafiti za wanyama hayawezi kutumika moja kwa moja kwa binadamu bila tafiti za kliniki zilizopangwa vizuri.


Athari za mbegu za Papai kwa Homoni za Uzazi kwa wanawake

Tafiti zilizofanywa kwa wanyama wa kike wa maabara pia zimeonyesha uwezekano wa mbegu za papai kuathiri mfumo wa uzazi.


Katika baadhi ya tafiti, kampaundi za mbegu za papai zilionekana kubadilisha kazi za ovari na kuathiri viwango vya homoni za uzazi. Wanasayansi walibaini mabadiliko katika mzunguko wa uzazi, muundo wa tishu za ovari na ukuaji wa mfuko wa uzazi.


Baadhi ya tafiti zilionyesha kupungua kwa kiwango cha progesterone, homoni muhimu katika maandalizi ya ujauzito na kuendelea kwa ujauzito katika hatua za awali.

Progesterone ina jukumu kubwa katika kusaidia yai lililorutubishwa kujipandikiza kwenye mfuko wa uzazi na kudumisha ujauzito. Kupungua kwa homoni hii kunaweza, kwa nadharia, kupunguza uwezo wa kushika mimba.


Kutokana na matokeo hayo, watafiti wamependekeza kuwa baadhi ya dondoo za mbegu za papai zinaweza kuathiri uzazi kupitia njia zinazohusisha homoni pamoja na njia zisizohusisha homoni.


Hata hivyo, matokeo haya bado hayajawa thabiti katika tafiti zote, na ushahidi mwingi unatokana na tafiti za wanyama badala ya majaribio ya kliniki kwa binadamu.


Mbegu za Papai zinawezaje kufanya kazi mwilini?

Watafiti wanaamini kuwa mbegu za papai zinaweza kuathiri uzazi kupitia njia kadhaa kwa wakati mmoja.

Kwanza, baadhi ya kemikali zake zinaweza kuathiri utando wa seli za mbegu za kiume na kupunguza uwezo wake wa kujongea. Bila uwezo mzuri wa kujongea, mbegu za kiume hushindwa kufikia na kurutubisha yai.


Pili, misombo hai iliyopo kwenye mbegu za papai inaweza kubadilisha uzalishaji wa homoni katika mfumo wa uzazi. Mabadiliko hayo yanaweza kuathiri utoaji wa yai, ukuaji wa mbegu za kiume na kazi za tishu za uzazi.


Tatu, tafiti za maabara zinaonyesha kuwa baadhi ya kemikali za mbegu za papai zinaweza kuongeza hali ya msongo wa oksijeni huru katika tishu za uzazi. Hali hii hutokea pale ambapo mwili huzalisha kemikali hatarishi kwa wingi kuliko uwezo wake wa kuzidhibiti, jambo ambalo linaweza kuharibu seli na kupunguza uwezo wa uzazi.


Nne, baadhi ya tafiti zimeonyesha athari za moja kwa moja kwenye korodani, epididimisi, ovari na mfuko wa uzazi. Mabadiliko ya kimuundo yaliyoonekana chini ya darubini yanaashiria kuwa njia nyingi za uzazi zinaweza kuathiriwa kwa wakati mmoja.


Hata hivyo, mifumo hii bado inaendelea kuchunguzwa na haijaeleweka kikamilifu.


Je, mbegu za Papai zinaweza kutumika kama njia ya kuzuia mimba?

Kwa sasa, ushahidi wa kisayansi hauungi mkono matumizi ya mbegu za papai kama njia ya kuaminika ya kuzuia mimba.

Ingawa tafiti za wanyama zimeonyesha uwezo wa kupunguza uzazi, bado hakuna ushahidi wa kutosha kwa binadamu unaoweza kueleza:

  • Kiwango sahihi cha matumizi

  • Muda wa athari kudumu

  • Ufanisi wake katika kuzuia mimba

  • Usalama wake

  • Athari za muda mrefu kwa afya ya uzazi


Njia yoyote ya kuzuia mimba lazima iwe na uwezo wa kuzuia ujauzito kwa uhakika na kwa kiwango kinachotabirika. Kwa sasa, mbegu za papai hazijafikia kiwango hicho cha ushahidi.

Watu wanaotaka kuzuia mimba kwa uhakika wanashauriwa kutumia njia za uzazi wa mpango zilizoidhinishwa na wataalamu wa afya badala ya kutegemea mbegu za papai.


Je, mbegu za Papai ni salama kuliwa?

Katika maeneo mengi duniani, mbegu za papai hutumiwa kwa kiasi kidogo kama chakula au kiungo cha ladha. Pia zimekuwa zikitumika katika tiba za jadi kwa miaka mingi.

Kwa watu wazima wenye afya njema, matumizi ya kiasi kidogo kwa ujumla huonekana kuwa salama.

Hata hivyo, matumizi ya kiasi kikubwa au matumizi ya dondoo zilizokolezwa hayajafanyiwa tafiti za kutosha ili kuthibitisha usalama wake wa muda mrefu.

Baadhi ya madhara yanayoweza kutokea ni pamoja na:

  • Uchokonozi wa mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

  • Mzio

  • Athari kwa mfumo wa uzazi

  • Mabadiliko ya homoni muda mrefu

  • Sumu iwapo yatatumika kwa kiasi kikubwa sana

Wanawake wajawazito wanapaswa kuwa waangalifu zaidi kwa sababu tafiti za wanyama zinaonyesha kuwa viwango vikubwa vya kemikali za mbegu za papai vinaweza kuathiri michakato ya uzazi.


Mapungufu ya tafiti za sasa

Ingawa matokeo ya tafiti hizi yanavutia, yapo mapungufu kadhaa muhimu. Tafiti nyingi zimefanywa kwa panya, sungura, nyani au seli za maabara. Mfumo wa uzazi wa binadamu ni changamano zaidi, hivyo matokeo yanaweza kutofautiana.


Aidha, viwango vya mbegu za papai vilivyotumika katika tafiti nyingi ni vikubwa zaidi kuliko kiasi ambacho mtu angeweza kula kwa kawaida.


Pia, maandalizi ya mbegu za papai hutofautiana sana kutoka utafiti mmoja hadi mwingine. Njia tofauti za kutengeneza dondoo zinaweza kutoa matokeo tofauti ya kibaolojia.


Kwa sasa bado hakuna majaribio makubwa ya kliniki yaliyofanywa kwa binadamu yanayoweza kutoa majibu ya uhakika.


Ujumbe muhimu wa kukumbuka

Mbegu za papai zina kemikali hai zinazoweza kuathiri mfumo wa uzazi katika tafiti za maabara na za wanyama. Ushahidi unaonyesha uwezekano wa kupunguza uwezo wa uzazi kwa wanaume na wanawake, hasa kupitia mabadiliko ya kazi za mbegu za kiume na homoni za uzazi.

Hata hivyo, mbegu za papai hazina levonorgestrel wala homoni nyingine za dawa zinazotumika katika uzazi wa mpango.

Kwa sasa hakuna ushahidi wa kutosha wa kupendekeza matumizi ya mbegu za papai kama njia ya kuzuia mimba au kama tiba ya matatizo ya uzazi.

Watu wanaovutiwa na afya ya uzazi wanapaswa kuzingatia kuwa utafiti kuhusu mbegu za papai bado uko katika hatua za awali na haujafikia kiwango cha kutumika kama mwongozo rasmi wa kitabibu.


Hitimisho kutokwa kwa mwandishi

Ingawa ushahidi wa kisayansi kwa binadamu bado ni mdogo, taarifa nyingi za uzoefu kutoka kwa watumiaji katika jamii mbalimbali zinaonyesha kuwa mbegu za papai zinaweza kuwa na athari katika kupunguza uwezekano wa kupata ujauzito. Mwandishi anaamini kuwa ushahidi huu wa matumizi ya muda mrefu unastahili kuchunguzwa zaidi kisayansi ili kuthibitisha au kupinga madai haya. Hata hivyo, kwa sasa madai hayo bado hayajathibitishwa na tafiti za kliniki za kiwango cha juu.


Maswali yanayoulizwa mara kwa Mara Kuhusu Mbegu za Papai na uzazi

1. Je, mbegu za papai zinaweza kusababisha utasa wa kudumu?

Kwa sasa, ushahidi wa kisayansi hauonyeshi kwamba mbegu za papai husababisha utasa wa kudumu kwa wanaume au wanawake. Tafiti nyingi zilizofanyika kwa wanyama zimeonyesha kuwa matumizi ya dondoo za mbegu za papai yanaweza kupunguza uwezo wa uzazi kwa muda, lakini athari hizo zilianza kupungua na hatimaye kurejea katika hali ya kawaida baada ya matumizi kusitishwa.


Katika tafiti kadhaa za wanyama wa kiume, watafiti waliona kupungua kwa uwezo wa mbegu za kiume kusogea na kurutubisha yai. Hata hivyo, baada ya kuacha kutumia dondoo za mbegu za papai kwa muda fulani, uzalishaji wa mbegu za kiume na uwezo wa uzazi ulianza kuimarika hatua kwa hatua.


Ni muhimu kufahamu kwamba tafiti hizi zilifanyika kwa wanyama na si kwa binadamu. Hivyo, ingawa matokeo yanaonyesha uwezekano wa athari za muda mfupi kwa uzazi, bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mbegu za papai zinaweza kusababisha utasa wa kudumu kwa binadamu.

2. Je, mbegu za papai huongeza au hupunguza homoni testosterone?

Testosterone ni homoni kuu ya uzazi kwa wanaume na ina jukumu muhimu katika uzalishaji wa mbegu za kiume, ukuaji wa misuli, nguvu za mwili na hamu ya tendo la ndoa. Watafiti wamejaribu kuchunguza kama mbegu za papai zinaweza kuathiri kiwango cha homoni hii.


Baadhi ya tafiti za wanyama zimeonyesha mabadiliko madogo katika viwango vya testosterone baada ya matumizi ya dondoo za mbegu za papai, huku tafiti nyingine zikionyesha kutokuwepo kwa mabadiliko makubwa. Tofauti hizi zinaweza kutokana na aina ya dondoo iliyotumika, kiwango cha matumizi na aina ya mnyama aliyefanyiwa utafiti.


Kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha kwa binadamu, haiwezekani kusema kwa uhakika kama mbegu za papai huongeza au hupunguza testosterone. Tafiti zaidi za kliniki zinahitajika ili kutoa majibu ya uhakika kuhusu suala hili.

3. Je, mbegu za papai zinaweza kuharibu DNA ya mbegu za kiume?

DNA iliyopo ndani ya mbegu za kiume ndiyo hubeba taarifa za urithi zinazohitajika kwa ukuaji wa mtoto. Ubora wa DNA ya mbegu za kiume ni muhimu katika kupata ujauzito wenye afya na maendeleo mazuri ya kijusi.


Baadhi ya tafiti za maabara zimeonyesha kuwa dondoo za mbegu za papai zinaweza kuongeza kiwango cha uharibifu wa DNA ya mbegu za kiume, hali inayojulikana kama DNA fragmentation. Uharibifu huu unaweza kupunguza uwezo wa mbegu za kiume kurutubisha yai au kuathiri ubora wa ujauzito.


Hata hivyo, matokeo haya yalipatikana katika mazingira ya maabara au kwa kutumia viwango maalumu vya dondoo za mbegu za papai. Bado hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba kula mbegu za papai kwa kiasi cha kawaida kunaweza kusababisha uharibifu wa DNA ya mbegu za kiume kwa binadamu.

4. Mbegu za papai hupunguzaje uwezo wa mbegu za kiume kusogea?

Uwezo wa mbegu za kiume kusogea, unaojulikana kama sperm motility, ni muhimu ili mbegu hizo ziweze kufika kwenye yai na kulirutubisha. Mbegu zisizoweza kusogea vizuri huwa na nafasi ndogo ya kusababisha ujauzito.


Watafiti wanaamini kuwa baadhi ya kemikali zilizopo kwenye mbegu za papai zinaweza kuathiri uzalishaji wa nishati ndani ya mbegu za kiume. Bila nishati ya kutosha, mbegu hizo hupoteza uwezo wa kuogelea kwa kasi na kwa ufanisi kuelekea kwenye yai.


Aidha, tafiti zimependekeza kuwa mbegu za papai zinaweza kuvuruga hatua za ukomavu wa mbegu za kiume ndani ya epididymis. Hii inaweza kusababisha mbegu za kiume kuwa na uwezo mdogo wa kusogea hata kama idadi yake inabaki katika kiwango cha kawaida.

5. Je, mbegu za papai zinaweza kuathiri matibabu ya uzazi kama IVF?

IVF ni mojawapo ya mbinu za kisasa zinazotumika kusaidia watu wenye matatizo ya uzazi kupata watoto. Mafanikio ya IVF hutegemea ubora wa mbegu za kiume, mayai na mazingira ya uzazi.


Kwa sasa hakuna tafiti za kliniki zilizochunguza moja kwa moja athari za mbegu za papai kwa watu wanaopata matibabu ya IVF. Hivyo, haiwezekani kusema kwa uhakika kama mbegu hizi zinaweza kuongeza au kupunguza mafanikio ya matibabu hayo.


Kwa sababu baadhi ya tafiti za maabara zimeonyesha uwezekano wa mbegu za papai kuathiri ubora wa mbegu za kiume na homoni za uzazi, watu wanaotarajia kupata matibabu ya IVF wanashauriwa kushauriana na daktari kabla ya kutumia mbegu za papai au virutubisho vinavyotokana nazo.

6. Je, mbegu za papai zina nguvu zaidi kuliko mimea mingine inayodaiwa kuzuia mimba?

Katika tiba za jadi kuna mimea mingi inayodaiwa kuwa na uwezo wa kupunguza uzazi au kuzuia mimba. Hata hivyo, mimea mingi haijafanyiwa tafiti za kutosha kuthibitisha madai hayo.


Mbegu za papai ni miongoni mwa mimea iliyofanyiwa tafiti nyingi zaidi katika eneo la afya ya uzazi, hasa kwa wanaume. Hata hivyo, bado hakuna ushahidi wa kutosha unaoruhusu kulinganisha nguvu au ufanisi wake dhidi ya mimea mingine inayotumika katika jamii mbalimbali.


Kwa sasa, hakuna mimea ya asili ikiwemo mbegu za papai ambayo imeonyesha kiwango cha ufanisi kinacholingana na njia za kisasa za uzazi wa mpango zilizothibitishwa kisayansi.

7. Je, mbegu za papai zinaweza kuzuia yai lililorutubishwa kujipandikiza kwenye mfuko wa uzazi?

Baada ya urutubishaji kutokea, yai lililorutubishwa lazima lijipandikize kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi ili ujauzito uanze rasmi. Mchakato huu unategemea homoni mbalimbali, hasa projesteroni.


Baadhi ya tafiti za wanyama zimeonyesha kuwa mbegu za papai zinaweza kupunguza kiwango cha progesterone au kuleta mabadiliko katika mfuko wa uzazi. Mabadiliko haya kwa nadharia yanaweza kufanya upandikizaji wa yai kuwa mgumu zaidi.


Hata hivyo, ushahidi huu unatokana na tafiti za wanyama pekee. Hadi sasa hakuna utafiti wa binadamu uliothibitisha kwamba mbegu za papai zinaweza kuzuia upandikizaji wa yai lililorutubishwa au kuzuia ujauzito kwa njia hiyo.

8. Kwa nini wanasayansi wanachunguza mbegu za papai kama njia ya uzazi wa mpango kwa wanaume?

Kwa miaka mingi, watafiti wamekuwa wakitafuta njia salama, nafuu na zinazoweza kurejeshwa za uzazi wa mpango kwa wanaume. Mbegu za papai zimevutia watafiti kutokana na matokeo yaliyopatikana katika tafiti za wanyama.


Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa mbegu za papai zinaweza kupunguza uwezo wa uzazi bila kusababisha uharibifu mkubwa wa kudumu katika korodani au kusimamisha kabisa uzalishaji wa homoni za kiume. Hili limeonekana kuwa jambo la kuvutia kwa watafiti wanaotafuta njia mpya za uzazi wa mpango.


Pamoja na matumaini hayo, bado kuna hatua nyingi za kisayansi zinazohitajika kabla ya mbegu za papai au kemikali zake kuweza kutumika kama dawa rasmi ya uzazi wa mpango kwa wanaume.

9. Je, mbegu za papai hufanya kazi sawa na vidonge vya kuzuia mimba?

Vidonge vya kisasa vya kuzuia mimba hutengenezwa kwa kutumia homoni maalumu ambazo zimefanyiwa majaribio makubwa ya kisayansi ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake.


Kwa upande mwingine, mbegu za papai zina kemikali za asili ambazo zinaweza kuathiri mfumo wa uzazi kupitia njia tofauti kabisa. Kemikali hizi hazijathibitishwa kuwa na uwezo wa kuzuia mimba kwa kiwango kinachotabirika kama ilivyo kwa vidonge vya uzazi wa mpango.


Kwa sababu hiyo, mbegu za papai haziwezi kuchukuliwa kama mbadala wa vidonge vya kuzuia mimba au njia nyingine za kisasa za uzazi wa mpango ambazo zimeidhinishwa na mamlaka za afya.

10. Je, dawa za baadaye zinaweza kutengenezwa kutoka kwenye mbegu za papai?

Historia ya tiba inaonyesha kuwa dawa nyingi za kisasa zimetokana na mimea au kemikali zilizopatikana kwenye viumbe hai. Hivyo, si jambo la ajabu kwa watafiti kuchunguza mbegu za papai kama chanzo cha dawa mpya.


Tafiti za sasa zimebaini kemikali mbalimbali ndani ya mbegu za papai ambazo zina uwezo wa kuathiri mfumo wa uzazi. Watafiti wanaendelea kuchunguza kemikali hizi ili kuelewa jinsi zinavyofanya kazi na kama zinaweza kutumiwa kutengeneza dawa salama na zenye ufanisi.


Hata hivyo, mchakato wa kutengeneza dawa mpya ni mrefu sana na unahitaji majaribio mengi ya maabara, wanyama na binadamu. Hivyo, ingawa kuna matumaini ya kisayansi, bado ni mapema sana kusema kama dawa za uzazi zitakazotokana na mbegu za papai zitapatikana katika siku za karibu.


Imeandikwa:

25 Juni 2026, 12:35:36

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

Rejea za mada hii:

  1. Lohiya NK, Goyal RB, Jayaprakash D, Ansari AS, Sharma S. Antifertility effects of aqueous extract of Carica papaya seeds in male rats. Planta Med. 1994;60(5):400-404.

  2. Lohiya NK, Pathak N, Mishra PK, Manivannan B. Reversible contraception with chloroform extract of Carica papaya Linn. seeds in male rabbits. Reprod Toxicol. 1999;13(1):59-66.

  3. Lohiya NK, Mishra PK, Pathak N, Manivannan B, Jain SC. Reversible azoospermia by oral administration of the benzene chromatographic fraction of the chloroform extract of the seeds of Carica papaya in rabbits. Adv Contracept. 1999;15(2):141-161.

  4. Lohiya NK, Manivannan B, Mishra PK, Pathak N, Sriram S, Bhande SS, et al. Chloroform extract of Carica papaya seeds induces long-term reversible azoospermia in langur monkey. Asian J Androl. 2002;4(1):17-26.

  5. Verma RJ, Chinoy NJ. Effect of papaya seed extract on contractile response of cauda epididymal tubules. Asian J Androl. 2002;4(1):77-78.

  6. Verma RJ, Nambiar D, Chinoy NJ. Toxicological effects of Carica papaya seed extract on spermatozoa of mice. J Appl Toxicol. 2006;26(6):533-535.

  7. Udoh PB, Essien IO, Udoh FV. Effects of Carica papaya (paw paw) seeds extract on the morphology of pituitary-gonadal axis of male Wistar rats. Phytother Res. 2005;19(12):1065-1068.

  8. Udoh FV, Udoh PB, Umoh EE. Activity of alkaloid extract of Carica papaya seeds on reproductive functions in male Wistar rats. Pharm Biol. 2005;43(6):563-567.

  9. Ghaffarilaleh V, Fisher D, Henkel R. Carica papaya seed extract slows human sperm. J Ethnopharmacol. 2019;241:111972.

  10. World Health Organization. WHO laboratory manual for the examination and processing of human semen. 6th ed. Geneva: World Health Organization; 2021.

  11. World Health Organization. Family planning: a global handbook for providers. 4th ed. Geneva: World Health Organization; 2022.

  12. National Library of Medicine. PubMed Database [Internet]. Bethesda (MD): National Center for Biotechnology Information; [cited 2026 Jun 25]. Available from: https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov

bottom of page