top of page

Imeandikwa na ULY CLINIC

25 Machi 2021 10:04:44

Kukojoa kwa shuruti

Kukojoa kwa shuruti

Kukojoa kwa shuruti ni neno limetumika kumaanisha hamu ya kwenda kukojoa haraka iwezekanavyo pasipo kusubiri. Hali hii hutokea kwa baadhi ya watu na inawezekana kumaanisha dalili ya hali au ugonjwa fulani ndani ya mwili.


Majina mengine ya hali hii ni, hamu ya kukojoa kwa lazima, hamu ya kukojoa haraka


Baadhi ya visababishi vimeelezewa hapa chini.


Visababishi

Maambukizi ya njia ya mkojo- UTI

Mfumo wa mkojo huundwa na figo, njia ya mkojo inayotoka kwenye figo hadi kwenye kibofu (yureta), kibofu cha mkojo na njia ya mkojo inayotoka kwenye kibofu hadi nje ya mwili(yurethra). Maambukizi ya bakteria huweza kuathiri sehemu yoyote ya mfumo huu. Maambukizi kwenye njia hizi husababisha mtu apate hamu ya kukojoa mara kwa mara


Saratani ya tezi dume

Kwa kawaida chembechembe za mwili huzaliwa na kufa kila siku, hii hutokana na asili ya binadamu na kuna seli ambazo zinafanya kazi ya kuharibu chembe ambazo zimezeeka. Endapo chembechembe zinazounda tezi za prostate hazifu na zimekuwa na tabia tofauti au kutofanana na chembe asilia, hii husababisha kutokea kwa saratani ya tezi dume inayopelekea kugandamizi mrija wa urethra na kuleta dalili ya hamu ya kukojoa mara kwa mara.Maambukizi ya kichocho cha mkojo (Schistosomiasis au bilharzia)

Ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea wenye jina la schistosoma, vimelea wanapoingia kwneye njia ya mkojo husababisha kuinuka kwa kinga za mwili kwenye njia hizo. Kinga za mwili zinapoinuka kupambana na vimelea hao hupelekea dalili za mtu kupata hisia za kutaka kukojoa mara kwa mara.


Saratani ya Kibofu cha mkojo

Endapo saratani ya kibofu cha mkojo ipo, mtu hupata dalili mbalimbali ikiwa pamoja na hisia za kutaka kwenda kukojoa kwa shuruti. Dalili zingine zinaweza kutokea, ni muhimu kusoma kuhusu dalili zingine au kuwasiliana na daktari wako kabla ya kusema kuwa una saratani.


Kisukari

Ni ugonjwa unaosababishwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu. Sukari hii inapokuwa nyingi kwenye damu huleta madhara kwnye mishipa ya damu na mishipa ya fahamu. Endapo sukari imekuwa nyingi kwenye damu kwa kipindi kirefu, mtu huyu hupata dalili ya kuhisi kwenda kukojoa kwa shuruti kwa sababu mishipa yake ya fahamu haina uwezo wa kuzuia mkojo kutoka.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia namba za simu au kwa kubonyeza 'Pata tiba' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

7 Februari 2022 19:27:31

Rejea za mada hii

1. MP Fitzgerald, J Jaffar, L Brubaker International Urologynecology Journal 12(4), 237-240, 2001.

2. Neurourology and Urodynamics: Official journal of the international continence society 27(6), 466-474, 2008.

3-Urgency: the key to defining the overactive bladder.Paul Abrams,BJU international 96, 1-3, 2005.

bottom of page