Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
ULY CLINIC

21 Mei 2026, 13:51:28
Kutokwa na damu ukeni kwenye komahedhi
Kutokwa na damu baada ya komahedhi ni hali ya kuona damu ukeni miezi sita au zaidi baada ya mwanamke kuingia rasmi kwenye komahedhi, yaani baada ya kuacha kabisa kupata hedhi. Wanawake wengi huingia katika kipindi cha komahedhi wanapofikisha umri wa takribani miaka 45 au zaidi, ingawa umri unaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.
Kutokwa na damu ukeni baada ya komahedhi ni ishara muhimu ya tahadhari, kwani mara nyingi huashiria uwepo wa tatizo kubwa katika mfumo wa uzazi, ikiwemo saratani ya mfuko wa kizazi, shingo ya kizazi au ovari. Hata hivyo, si kila damu baada ya komahedhi husababishwa na saratani; sababu nyingine zinaweza kuwa maambukizi ya njia ya uzazi, matumizi ya homoni za estrogen, au kusinyaa na kukauka kwa uke. Damu inayotoka inaweza pia kuashiria tatizo kwenye uke, shingo ya kizazi, ndani ya mfuko wa kizazi, ovari au mirija ya mayai.
Damu inayotoka baada ya komahedhi huweza kuwa ya rangi ya kahawia au nyekundu, na inaweza kutoka kama matone machache au damu nyingi. Kwa baadhi ya wanawake, damu hutokea wanapojaribu kujisafisha ndani ya uke au wanaposhiriki tendo la ndoa. Wanawake wengi, hasa wale waliokuwa na historia ya hedhi nzito kabla ya komahedhi, huweza kupuuzia dalili hii, hali inayosababisha kuchelewa kufika hospitali. Endapo utapata dalili ya kutokwa na damu ukeni baada ya komahedhi, ni muhimu kufika hospitali au kuonana na daktari mapema kwa uchunguzi na matibabu sahihi.
Visababichi vya kutokwa damu ukeni baada ya komahedhi
1. Saratani ya ukuta wa ndani wa kizazi (Satatani ya endometria)
Hiki ndicho kisababishi kikuu na cha kwanza kinachopaswa kuondolewa kama kisababishi kwa mwanamke yeyote anayepata damu ukeni baada ya komahedhi. Saratani ya ukuta wa ndani wa kizazi husababisha seli za ukuta huu kukua isivyo kawaida na hatimaye kuvunjika na kutoa damu. Mara nyingi damu hutoka bila maumivu na inaweza kuwa matone, damu ya kahawia au damu nyingi kama hedhi. Hatari huongezeka kwa wanawake wenye uzito mkubwa, kisukari, shinikizo la damu, au waliotumia estrojeni pekee bila projesteroni.
2. Saratani ya shingo ya kizazi
Hatua za awali za saratani ya shingo ya kizazi husababisha kutokwa na matone ya damu ukeni au wakati mwingine damu nyingi. Damu mara nyingi hutokea baada ya kushiriki tendo la ndoa, kujisafisha kwa kuingiza kitu ukeni, au hutoka yenyewe bila sababu dhahiri. Damu huwa ya rangi ya pinki, inaweza kuambatana na harufu mbaya, na maumivu wakati wa kujamiana. Saratani inapoendelea, dalili huweza kujumuisha maumivu ya mgongo wa chini, sayatika, kuvimba mguu mmoja, kupungua uzito, kukojoa damu, maumivu wakati wa kukojoa, au kutokwa na damu kupitia njia ya haja kubwa.
3. Saratani ya ovari
Saratani ya ovari ni miongoni mwa saratani hatarishi kwa sababu hujitokeza bila dalili za awali zilizo wazi. Saratani hii huweza kuzalisha homoni ya estrogen, ambayo husababisha kuta za uzazi kujengwa upya na kisha kuvunjika, hivyo kuleta damu baada ya komahedhi. Damu inayotokana na saratani ya ovari mara nyingi haitokani na tendo la ndoa au kujisafisha. Uchunguzi unaweza kuonyesha uvimbe upande mmoja wa nyonga (kushoto au kulia), kujaa tumbo, gesi, au maumivu ya nyonga. Uvimbe mdogo wa ovari si rahisi kugundulika bila vipimo maalum.
4. Saratani ya uke
Saratani ya uke ni nadra lakini hutokea zaidi kwa wanawake waliovuka komahedhi. Kabla ya kutokwa na damu, wanawake wengi hupata majimaji ukeni yasiyo ya kawaida. Damu inaweza kutoka bila kuamshwa au ikatokea baada ya kujamiana au kujisafisha. Dalili zingine ni kidonda kigumu ukeni, maumivu wakati wa tendo la ndoa, kukojoa mara kwa mara, maumivu ya kibofu cha mkojo, maumivu ya nyonga, maumivu ya puru, au kutokwa na damu kupitia njia ya haja kubwa.
5. Kukua kupitiliza kwa seli za ndani ya kizazi (Endometria haipeplasia)
Hali hii hutokea pale seli za ukuta wa ndani wa kizazi(ikifahamika pia kama utando wa ndani ya kizazi) zinapokua kupita kiasi kutokana na athari ya estrojeni bila uwiano wa projesteron. Endometria haipeplasia inaweza kuwa hatua ya awali ya saratani ya kizazi. Dalili kuu ni kutokwa na damu baada ya komahedhi, mara nyingi bila maumivu. Uchunguzi wa mapema ni muhimu ili kuzuia kugeuka kuwa saratani.
6. Polipsi kwenye shingo ya kizazi au ndani ya kuta za uzazi
Polipsi ni uvimbe mdogo laini unaofanana na kidole unaoota kwenye shingo ya kizazi au ndani ya ukuta wa uzazi. Polipsi zinaweza kusababisha damu ya rangi ya pinki au yenye makamasi, hasa wakati wa kujamiana, kujisafisha ukeni au wakati wa kutoa haja kubwa. Wagonjwa wengi hawana dalili, lakini wengine hupata kutokwa na damu ya mara kwa mara au uchafu ukeni.
7. Kusinyaa na kukauka kwa uke
Baada ya komahedhi, kiwango cha estrojeni hupungua na kusababisha kuta za uke kuwa nyembamba, kavu na rahisi kujeruhiwa. Wanawake wanaoshiriki tendo la ndoa au kujisafisha kwa kuingiza kitu ukeni huweza kupata michubuko midogo inayosababisha kutokwa na damu. Dalili nyingine ni uke mkavu, muwasho, hisia ya kuungua, maumivu wakati wa kujamiana, kutoa majimaji meupe, kusinyaa kwa mashavu ya uke na kinembe, pamoja na kutokwa na matone ya damu.
8. Matumizi ya dawa
Baadhi ya dawa hutumiwa kipindi cha komahedhi zinaweza kusababisha damu ukeni. Dawa zinazosababisha hali hii mara nyingi ni zile za kurejesha homoni baada ya komahedhi (HRT), hasa zinazotumia estrojeni pekee bila projesteroni. Tatizo hili huwa nadra kwa wanawake wanaotumia mchanganyiko wa estrojeni na projesteroni.
9. Maambukizi ya mfuko wa kizazi
Maambukizi ndani ya mfuko wa kizazi au uke yanaweza kusababisha kutokwa na damu baada ya komahedhi. Dalili huweza kujumuisha damu ukeni, maumivu ya nyonga, uchafu ukeni wenye harufu mbaya, na wakati mwingine homa. Uchunguzi na matibabu ya mapema ni muhimu ili kuzuia madhara makubwa.
10. Faibroidi za kizazi
Ingawa faibroidi nyingi hupungua baada ya komahedhi, baadhi zinaweza kuendelea kuwepo au kubadilika na kusababisha kutokwa na damu isiyo ya kawaida. Damu inaweza kuwa kidogo au nyingi, na mara nyingine huambatana na maumivu ya nyonga au hisia ya kubanwa tumboni.
11. Majeraha ya mfumo wa uzazi
Majeraha yanaweza kusababishwa na tendo la ndoa, uchunguzi wa kitabibu, ajali au kuingiza vitu ukeni. Majeraha haya huweza kusababisha damu ya ghafla ukeni, mara nyingi ikiwa na maumivu.
12. Kutokwa na damu isiyotoka kwenye uke
Wakati mwingine damu hutoka kwenye njia ya mkojo au njia ya haja kubwa na kudhaniwa kimakosa kuwa ni ya ukeni. Ndiyo maana ni muhimu kwa daktari kufanya uchunguzi kamili ili kubaini chanzo halisi cha damu.
Je, kutokwa na damu baada ya komahedhi ni hatari?
Ndiyo, inaweza kuwa hatari au isiwe hatari, lakini:
Haiwezekani kujua bila uchunguzi
Kila tukio la damu baada ya komahedhi linahitaji tathmini ya daktari
Utambuzi wa mapema huokoa maisha, hasa endapo kisababishi ni saratani.
Vipimo na uchunguzi vinavyoweza kufanyika
Daktari anaweza kuagiza:
Kipimo cha picha sauti ya via vya uzazi (ultrasound)
Kipimo cha kuchukua sampuli ya ukuta wa kizazi (bayopsi)
Kipimo cha Pap smia
Kipimo cha CT scan au MRI (endapo kuna sababu)
Vipimo vya maambukizi
Matibabu
Matibabu hutegemea kisababishi, na yanaweza kujumuisha:
Dawa (homoni, antibayotiki)
Upasuaji mdogo wa kuondoa vinyama
Matibabu ya saratani endapo itagundulika
Ushauri wa kiafya na ufuatiliaji wa karibu
Wakati wa kumuona daktari haraka
Wasiliana na daktari mara moja ikiwa:
Umewahi kufikia komahedhi na ukaona damu ukeni
Damu inarudiarudia
Kuna maumivu ya nyonga
Kuna harufu mbaya au uchafu usio wa kawaida
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Kutokwa na damu ukeni baada ya komahedhi ni nini?
Kutokwa na damu ukeni baada ya komahedhi ni hali ambapo mwanamke ambaye tayari ameacha kuona hedhi kwa miezi 12 mfululizo anaona damu tena ukeni. Hali hii huitwa kitaalamu “postmenopausal bleeding.” Baada ya komahedhi, mwili huwa umepunguza sana uzalishaji wa homoni za estrojeni na projesteroni, hivyo hedhi huwa imekoma kabisa. Ndiyo maana kuona damu tena si jambo la kawaida.
Damu inaweza kutoka kwa kiwango tofauti. Wengine huona matone machache ya damu ya kahawia au nyekundu, huku wengine wakiona damu nyingi kama hedhi ya kawaida. Wakati mwingine damu inaweza kuonekana baada ya tendo la ndoa au baada ya kufanya kazi nzito.
Ingawa wakati mwingine sababu inaweza kuwa ndogo kama ukavu wa uke, kutokwa na damu baada ya komahedhi kunaweza pia kuwa ishara ya tatizo kubwa zaidi kama saratani ya mfuko wa uzazi. Kwa sababu hiyo, mwanamke yeyote anayepata hali hii anashauriwa kufika hospitali kwa uchunguzi mapema.
2. Je, ni kawaida kuona damu baada ya hedhi kukoma?
Hapana. Baada ya mwanamke kufikia komahedhi, hapaswi kuona damu ya hedhi tena. Hivyo, damu yoyote inayotoka ukeni baada ya kipindi hicho huchukuliwa kuwa si ya kawaida na inahitaji uchunguzi wa daktari.
Baadhi ya wanawake hudhani kuwa damu ndogo si tatizo, hasa ikiwa imetokea mara moja tu. Hata hivyo, hata matone machache yanaweza kuwa ishara ya mabadiliko ndani ya mfuko wa uzazi au shingo ya kizazi. Wakati mwingine hali hii huwa ni dalili ya mwanzo ya saratani ambayo inaweza kutibika vizuri ikigundulika mapema.
Ni muhimu kutafuta ushauri wa kitabibu bila kuchelewa. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kubaini chanzo halisi na kuanza matibabu mapema kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.
3. Damu kidogo ya kahawia baada ya komahedhi ina maana gani?
Damu ya kahawia mara nyingi huwa ni damu ya zamani ambayo imekaa muda kabla kutoka nje ya mwili. Kwa wanawake waliopo baada ya komahedhi, hali hii inaweza kusababishwa na ukavu wa uke kutokana na kupungua kwa homoni ya estrojeni.
Ukuta wa uke unapokuwa mwembamba na mkavu, unaweza kupata michubuko midogo na kutoa damu kidogo ya kahawia au nyekundu. Wakati mwingine damu hiyo inaweza kuonekana baada ya tendo la ndoa au baada ya kujisafisha sehemu za siri.
Ingawa mara nyingi damu ya kahawia inaweza kuwa na sababu zisizo hatari sana, bado haipaswi kupuuzwa. Inaweza pia kuwa dalili ya vinyama ndani ya kizazi, maambukizi, au hata saratani ya mfuko wa uzazi. Ndiyo maana ni muhimu kufanya uchunguzi hospitalini.
4. Ni magonjwa gani makubwa yanaweza kusababisha damu baada ya komahedhi?
Moja ya magonjwa yanayotiliwa hofu zaidi ni saratani ya mfuko wa uzazi. Wanawake wengi wenye saratani hii huanza kwa kuona damu kidogo baada ya komahedhi. Saratani ya shingo ya kizazi pia inaweza kusababisha damu, hasa baada ya tendo la ndoa.
Tatizo jingine ni kukua kupita kiasi kwa ukuta wa ndani wa kizazi. Hali hii hutokea pale seli za ukuta huo zinapoongezeka kupita kawaida kutokana na mabadiliko ya homoni. Wakati mwingine hali hii inaweza kubadilika na kuwa saratani ikiwa haitatibiwa mapema.
Pia kuna vinyama vya uzazi vinavyoitwa polyps na uvimbe usio wa saratani kama faibroidi. Ingawa baadhi si hatari, vinaweza kusababisha damu na kuhitaji matibabu au ufuatiliaji wa karibu wa daktari.
5. Je, maambukizi yanaweza kusababisha damu baada ya komahedhi?
Ndiyo. Maambukizi ndani ya uke, shingo ya kizazi au mfuko wa uzazi yanaweza kusababisha kutokwa na damu baada ya komahedhi. Maambukizi haya yanaweza pia kuambatana na harufu mbaya ukeni, maumivu ya nyonga, kuwashwa au uchafu usio wa kawaida.
Baada ya komahedhi, uke huwa mwembamba na mkavu zaidi kutokana na kupungua kwa homoni ya estrojeni. Hali hii inaweza kufanya uke kuwa rahisi kupata majeraha na maambukizi. Wakati mwingine hata maambukizi madogo yanaweza kusababisha damu kutoka.
Ni muhimu kupata uchunguzi wa daktari ili kujua aina ya maambukizi yaliyopo. Matibabu yanaweza kuwa dawa za bakteria, fangasi au dawa nyingine kulingana na chanzo cha tatizo.
6. Dawa za homoni zinaweza kusababisha damu baada ya komahedhi?
Ndiyo. Baadhi ya wanawake wanaotumia dawa za homoni baada ya komahedhi wanaweza kupata damu ukeni. Dawa hizi hutumika kusaidia kupunguza dalili za komahedhi kama joto la ghafla mwilini, ukavu wa uke na kukosa usingizi.
Dawa nyingine kama tamoxifen, ambayo hutumika kwa baadhi ya wagonjwa wa saratani ya matiti, pia inaweza kuongeza uwezekano wa kutokwa damu baada ya komahedhi. Hii hutokea kwa sababu dawa hiyo inaweza kuathiri ukuta wa ndani wa kizazi.
Hata kama damu inahisiwa kuwa imesababishwa na dawa, bado ni muhimu kumwona daktari. Wakati mwingine dawa inaweza kuficha tatizo jingine kubwa zaidi ndani ya mfuko wa uzazi.
7. Je, damu inaweza isitoke ukeni bali ikaonekana kama ya ukeni?
Ndiyo. Wakati mwingine mwanamke anaweza kudhani damu inatoka ukeni wakati chanzo chake ni sehemu nyingine ya mwili. Damu inaweza kutoka kwenye njia ya mkojo kutokana na maambukizi ya kibofu, mawe au matatizo ya figo.
Pia damu inaweza kutoka kwenye njia ya haja kubwa kutokana na bawasiri, vidonda au matatizo mengine ya utumbo. Hali hii inaweza kumchanganya mtu na kufikiri kuwa damu inatoka kwenye uke.
Kwa sababu hiyo, daktari hufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha damu. Uchunguzi huu husaidia kuhakikisha mgonjwa anapata matibabu sahihi kulingana na tatizo lililopo.
8. Vipimo gani hufanywa kwa mwanamke anayepata damu baada ya komahedhi?
Daktari huanza kwa kumuuliza mgonjwa historia ya tatizo lake, ikiwa ni pamoja na muda wa kuanza damu, kiasi cha damu na dawa anazotumia. Pia huuliza kama kuna maumivu, harufu mbaya au historia ya saratani kwenye familia.
Baada ya hapo, uchunguzi wa mwili na uke unaweza kufanyika ili kuangalia kama kuna vidonda, maambukizi au vinyama kwenye shingo ya kizazi. Mara nyingi kipimo cha ultrasound hutumika kuangalia mfuko wa uzazi na ukuta wake wa ndani.
Vipimo vingine vinaweza kujumuisha Pap smear, kuchukua sampuli ya ukuta wa ndani wa kizazi (bayopsi), na vipimo vya maambukizi. Vipimo hivi husaidia kugundua kama kuna saratani, maambukizi au matatizo mengine ndani ya mfumo wa uzazi.
9. Damu baada ya komahedhi hutibiwa vipi?
Matibabu hutegemea chanzo halisi cha damu. Ikiwa tatizo ni ukavu wa uke, daktari anaweza kupendekeza dawa za estrojeni au vilainishi maalumu vya uke kusaidia kupunguza ukavu na michubuko.
Ikiwa chanzo ni maambukizi, mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutibu bakteria au fangasi. Kwa wanawake wenye vinyama au fibroid, upasuaji mdogo unaweza kufanyika kuviondoa.
Iwapo saratani itagundulika, matibabu yanaweza kujumuisha upasuaji, dawa maalumu, mionzi au tiba nyingine kulingana na hatua ya ugonjwa. Kugundua tatizo mapema huongeza nafasi ya matibabu kufanikiwa.
10. Ni lini nimwone daktari haraka nikiona damu baada ya komahedhi?
Unapaswa kwenda hospitali haraka mara tu unapoona damu yoyote baada ya komahedhi, hata kama ni kidogo sana. Usisubiri damu iongezeke au ijirudie mara nyingi ndipo utafute matibabu.
Pia wahi hospitali ikiwa damu inaambatana na maumivu ya tumbo au nyonga, harufu mbaya ukeni, kizunguzungu, uchovu mkubwa au kupungua uzito bila sababu. Dalili hizi zinaweza kuashiria tatizo kubwa zaidi linalohitaji matibabu ya haraka.
Ikiwa damu ni nyingi kiasi cha kulowanisha pedi mara kwa mara, unazimia au unapata shida ya kupumua, tafuta huduma ya dharura mara moja. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kuzuia madhara makubwa na kuongeza uwezekano wa kupona vizuri.
Nina miaka 45 ila naona mabadiliko kwenye tumbo langu uchafu mweupe kutoka ukeni mfululizo natumbo kua kubwa je inaweza ikawa ni dalili ya kukoma hedhi?
Ndiyo, baadhi ya wanawake wenye umri wa miaka 45 wanaweza kuanza kupata dalili za kuelekea kwenye komahedhi, kipindi kinachoitwa "kipindi cha kuingia hedhi". Katika kipindi hiki homoni za estrojeni na projesteroni huanza kubadilika, na mwanamke anaweza kupata mabadiliko kama kuongezeka uzito hasa tumboni, hedhi kubadilika, joto la ghafla mwilini, usingizi kuvurugika au hisia kubadilika.
Hata hivyo, uchafu mweupe kutoka ukeni mfululizo na tumbo kuongezeka si dalili zinazomaanisha moja kwa moja kuwa ni komahedhi. Uchafu mweupe unaweza kusababishwa na maambukizi ya uke, fangasi, bakteria, au mabadiliko ya homoni. Tumbo kuwa kubwa linaweza kutokana na kuongezeka uzito, gesi tumboni, uvimbe wa kizazi kama fibroid, uvimbe kwenye ovari, au matatizo mengine ya kiafya.
Ni muhimu zaidi kumuona daktari ikiwa:
Uchafu una harufu mbaya
Kuna kuwashwa au maumivu
Tumbo linaendelea kuongezeka
Unapata maumivu ya nyonga
Hedhi zimebadilika sana
Unahisi kushiba haraka au kupungua uzito bila sababu
Daktari anaweza kufanya uchunguzi, vipimo vya damu na ultrasound ya tumbo au via vya uzazi ili kujua chanzo halisi. Usihitimishe kuwa ni komahedhi pekee bila uchunguzi wa kitabibu.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 15:59:23
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1.The woman with postmenopausal bleeding,Alison H Brand,Australian family physician 36(3),116,200
2.-How should we investigate women with postmenopausal bleeding? Janeth Kumar Gupta, Sheena Wilson,Pershant Desai, Cathy Hau ,Acta obstetricia et gynecologica scandinava 75(5),475-479, 1996
3.Histopathological fingings in women with pastmenopausal bleeding,Thomas Gredmark , Sonja Kvint, Guillaume Havel, Lars-Ake ,Mattson-BJOG: An International Journal of Obstetrics &Gynaecology 102(2), 133-136,1995
