Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Peter A, MD
19 Aprili 2020 14:56:19
Kwashiakoo
Utapiamlo ni hali ya kiafya inayosababishwa kwa kula chakula chenye virutubisho vingi au vichache zaidi ya vinavyo takiwa na hivyo kudhuru mwili.
Utapiamlo wa protini ni hali ya kiafya inayosababishwa kwa kula vyakula vyenye protini nyingi au kidogo zaidi ya mahitaji ya mwili.
Ni muhimu kutambua kua utapiamlo unaweza kusababishwa kwa virubisho fulani vya chakula kuzidi ama kupungua mwilini.
Protini ni muhimu mwlini kwani ndio hujenga mwili. Tunaweza kusema kua ni matofali ya mwili. Sehemu za mwili kama vile nywele, kucha, misuli ngozi na kadhilika zimeundwa kwa sehemu kubwa na protini.
Vyanzo vya protini
Baadhi ya vyanzo vya protini ni;
Mayai
Nyama
Maziwa
Samaki
Karanga
Maharagwe
Soma zaidi katika makala zingine za ULY CLINIC kuhusu vyakula vya protini kwa uelewa zaidi wa vyakula vyenye protini kwa wingi
Kazi za protini mwilini.
Kujenga na kukurabati mwili unapoumia au kuugua. Mfano ni kujenga mifupa, misuli, ngozi, nywele n.k
Inaunda homoni ambozo husimamia kazi zote za mwili mfano kukua, kuzaliana, hisia n.k hivyo kutufanya mtu kuwa mkamilifu kiafya.
Protini inaunda kinga ya mwili kupambana na magonjwa na maambukizi mbalimbali.
Protini huunda vimeng’enya ambavyo hurekebisha kazi zote za kimetaboli mwilini.
Protini husafirisha kemikali mbalimbali mwili ili mwili ufanye kazi vizuri. Mfano damu imebeba protini ambazo husafirisha hewa ya oksijeni mwili mzima.
Huzalisha nishati ya kuupa mwili nguvu wakati wanga na mafuta havitoshi kufanya hivyo mfano wakati mtu amefunga au kukosa chakula kwa siku nyingi.
Nishati kutokana na protini hupatika zaidi kwa kubomolewa kwa misuli ya mwili hivyo mtu hukonda sana na ni chaguo la mwisho la mwili baada ya kukosa wanga na mafuta.
Dalili
Upungufu wa protini hudhihirika kwa dalili zifuatazo:
Uzito chini ya wastani ukilinganisha na umri wa mtoto(au mtu mzima).
Kudumaa kwa Watoto
Kuvimba kwa tumbo
Kuvimba kwa miguu (kutokana na kuvia maji)
Kukosa hamu ya kula
Kuharisha
Kukonda sana na sehemu ya mifupa kuonekana chini ya ngozi
Mabadiliko ya nywele, nywele huwa laini na kubadilika rangi kuwa na rangi ya kahawia na kunyonyoka kirahisi
Upungufu wa damu huweza kuwepo hivyo viganja na ulimi hupauka na kuwa vyeupe kuliko kawaida
Kupatwa na magonjwa ya mara kwa mara kutokana na kinga ya mwili kushuka
Uso kuoneka wa mduara
Kumbuka
Kwa pamoja dalili hizi huitwa kwashiakoo. Utapiamlo wa protini huwapata zaidi Watoto japo kua watu wazima hususani wazee wanaweza kuathiriwa pia. Upungufu wa protini huambatana na upungufu wa virutubisho vingine kama vile wanga na hata vitamini na madini.
Matibabu
Utapiamlo wa protini hutibika na matibabu hupatikana hospitalini kwa kupewa virutubisho maalumu pamoja na mlo kamili. Pia matibabu huusisha matibabu ya hali nyingine kama vile maambukizi ya bakteria ambayo huweza.
Kinga
Mama anaenyonyesha afuate maelekezo ya wataalumu wa afya anayopewa
Kula mlo kamili
Kuhakikisha familia zinaweka akiba ya chakula
Maandalizi sahihi ya chakula
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 20:02:52
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. MSD manual professional version. Protein-Energy Undernutrition (PEU). https://www.msdmanuals.com/professional/nutritional-disorders/undernutrition/protein-energy-undernutrition-peu. Imechukuliwa 18.04.2020
2. Mediscape. Protein energy malnutrition. https://emedicine.medscape.com/article/1104623-overview. Imechukuliwa 18.04.2020
3. Encyclopedia of chhildrens health. Protein energy malnutrition. http://www.healthofchildren.com/P/Protein-Energy-Malnutrition.html. Imechukuliwa 18.04.2020