Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD
26 Machi 2021 09:42:41
Maumivu ya koo
Maumivu ya koo ni dalili ya hisia za kuhisi maumivu, ukavu au kukwanguliwa kwa koo. Tatizo hili huwapata watu wengi duniani.
Mara nyingi maumivu ya koo husababishwa na maambukizi ya virusi na hewa kavu kwenye mazingira na mara nyingi dalili hii hupotea yenyewe bila matibabu.
Dalili ya maumivu ya koo pia inaweza kuelezewa na watu wengine kama, koo kuwaka moto, koo kuchomachoma, koo kukwaruza na koo kukaba
Aina
Kuna aina tatu za maumivu ya koo zinatokana na sehemu ya koo iliyoathiriwa, aina hizo ni;
Maumivu kutoka kwenye uvimbe wa koromeo (pharynx)
Maumivu kutoka kwenye uvimbe wa findo ( tonsils)
Maumivu kutoka kwenye uvimbe wa zoloto (larynx)
Vishiria
Viashiria vya maumivu ya koo ni pamoja na;
Hisia za kukwanguliwa koo
Hisia za kuungua koo
Kukauka kwa koo
Kukereketa kwa koo
Maumivu ya koo likishikwa
Kuonekana kwa usaha au mabaka meupe kwenye koo
Dalili zinazo ambatana na maumivu ya koo
Dalili zingine zinazoweza ambatana na maumivu ya koo ni pamoja na;
Homa na kutetemeka
Kikohozi
Kubadilika kwa sauti
Kuchuruzika kwa kamasi
Kujaa kwa kamasi puani
Kupiga chafya
Kupoteza hamu ya kula
Kushindwa kumeza au maumivu wakati unameza chakula
Kuvimba kwa mitoki shingoni
Maumivu ya kichwa
Dalili
Endapo una maumivu ya koo yanayoambatana na dalili zifuatazo, wasiliana na daktari wako haraka kwa uchunguzi na tiba;
Kukakama kwa shingo
Kukohoa damu au kutoa mate yeye damu
Kushindwa kufungua kinywa
Kushindwa kumeza chakula
Kushindwa kupumua vema au maumivu ukiwa una pumua
Kuwa na homa nyuzi joto zaidi ya 38
Maumivu makali ya koo
Maumivu ya koo yaliyodumu zaidi ya wiki moja
Maumivu ya mungio ya mwili
Maumivu ya shingo
Maumivu ya sikio
Visababishi
Kuna hali na magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha maumivu ya koo ambayo yameorodheshwa hapa chini, kusoma zaidi nenda katika Makala husika ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC. Visababishi hivi vemeorodheshwa kutegemea kipi kinasababisha kwa asilimia kubwa
Maambukizi ya virusi kwenye koo kama kirusi cha influenza, mononucleosis, measle na chickenpox
Maambukizi ya bakteria kooni kama bakteria Streptococcus, gonorrhea na chlamydia
Mzio kwenye poleni, vumbi la ndani ya nyumba. Kemikali kwenye mzingira au dawa mbalimbali za kunywa na kuua wadudu
Hewa kavu kwenye mazingira
Uvutaji wa sigara au tumbaku na matumizi ya kemikali mbalimbali zinazochokoza koo
Majeraha kwenye koo
Ugonjwa wa Kucheua tindikali huu husababisha kuungua kwa koo
Saratani ya koo
Vipimo
Mara nyingi maumivu ya koo huchunguzwa kwa historia ya ugonjwa na dalili kabla ya kupewa dawa. Endapo kuna uhaja wa vipimo, vipimo muhimu kufanyika ni;
Kipimo cha kuotesha vimelea kutoka kwenye sampuli inayochukuliwa kooni- malengo yakiwa kutambua bakteria wanaosababisha maumivu ya koo, majibu ya kipimo hiki huchukua masaa 24 hadi 48 kutoka. Kipimo hiki hufahamika kitiba kama ‘throat culture’
Kipimo cha cha antigeni, kipimo hiki majibu yake hupatikana hapo hapo
Kipimo cha kutambua moja kwa moja kimelea streptococcus
Matibabu
Matibabu ya maumivu ya koo hulenga kwenye tiba ya kisababishi kama vilivyoorodheshwa hapo juu, ni vema ukawasiliana na daktari wako ili kufahamu ni dawa gani inafaa kwako. Baadhi ya tiba huhusisha;
Matibabu ya dawa za kuondoa maumivu kama acetaminophen(panado), ibuprofen au aspirin(haifai kwa watoto na vijana wadogo). Kumbuka dawa hizi haziondoi tatizo bali zinapunguza maumivu tu
Dawa za kuzuia kikohozi, phenol na methanol - hizi hazitibu tatizo bali hupunguza dalili tu. Dawa hizi huwa na kemikali zinazoleta ganzi kwenye koo hivyo utapoteza hisia za maumivu lakini tatizo litaendelea kuwa pale pale
Dawa za kuzuia uzalishaji wa tindikali, kwa wagonjwa wa kucheua tindikali. Dawa hizo ni kama vile omeprazole, pantoprazole, cimetidine, famontidine n.k
Dozi ya dawa jamii ya corticosteroid
Dawa za antibiotic, kupambana na maambukizi ya bakteria kwenye koo au au za antiviral ili kupambana na maambukizi ya virusi endapo ndo kisababishi.
Madhara ya maumivu ya koo kutokana na maambukizi ya bakteria
Maambukizi ya koo kwa watoto huweza kupelekea bakteria kuingia kwenye damu na kufika kwenye moyo na mapafu. Bakteria wanapofika kwenye moyo, hujizalia kwa wingi kwenye milango ya moyo na hivyo kusababisha homa ya moyo (rheumatic fever) na nimonia. Endapo magonjwa haya hayatatibiwa ipasavyo mtoto anaweza kupata madhara makubwa zaidi kama vile ugonjwa wa rheumatism ya moyo
Kinga
Kujikinga na maumivu ya koo unaweza fanya mambo yafuatayo
Kaa mbali na mtu anayeumwa koo kutokana na maambukizi ya bakteria au virusi
Nawa mikono mara kwa mara unaposhika vitu kabla ya kula au kuweka vidole kinywani
Jizuie na vyakula vyenye viungo na pilipili kwa wingi
Acha kutumia na kaa mbali na kemikali mbalimbali zinazochokoza koo pamoja na moshi wa sigara
Kwa wale wanaofanya ngono inayohusisha kulamba au kunyonya uke au ume, ni vema kuepuka kwa kuwa maeneo haya huwa na bakteria na virusi wanaoweza kuleta shida kwenye koo lako
Matibabu ya nyumbani
Kusoma kuhusu matibabu ya nyumbani ya maumovu ya koo, ingia kwenye sehemu ya matibabu ya nyumbani au kwa kutafuta kwenye kiboksi cha tafuta hapa kuhusu 'maumivu ya koo- matibabu ya nyumbani'
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 19:53:27
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
​
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. Emily H. Stewart, et al. Rapid Antigen Group A Streptococcus Test to Diagnose Pharyngitis: A Systematic Review and Meta-Analysis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4219770/. Imechukuliwa 26.03.2021
2. Graham Worrall. Acute sore throat. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3135445/. Imechukuliwa 26.03.2021
3. Nader Shaikh, et al. Prevalence of Streptococcal Pharyngitis and Streptococcal Carriage in Children: A Meta-analysis. http://pediatrics.aappublications.org/content/126/3/e557. Imechukuliwa 26.03.2021
4. Bertold Renner, et al. Environmental and non-infectious factors in the aetiology of pharyngitis (sore throat). https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3439613/. Imechukuliwa 26.03.2021
5. Josef Brinckmann, et al. Safety and efficacy of a traditional herbal medicine (Throat Coat) in symptomatic temporary relief of pain in patients with acute pharyngitis: a multicenter, prospective, randomized, double-blinded, placebo-controlled study. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/12804082. Imechukuliwa 26.03.2021
6. Koromeo. http://www.elimuyetu.co.tz/subjects/arts/eng-swa/p.html. Imechukuliwa 26.03.2021
7. Behnam Sadeghirad, et al. Corticosteroids for treatment of sore throat: systematic review and meta-analysis of randomised trials. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pubmed/28931508. Imechukuliwa 26.03.2021
8. National Institute on Deafness and Other Communication Disorders.Taking care of your voice. http://www.nidcd.nih.gov/health/voice/pages/takingcare.aspx. Imechukuliwa 26.03.2021
9. Chow AW, et al. Evaluation of acute pharyngitis in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 26.03.2021
10. Kellerman RD, et al. Pharyngitis. In: Conn's Current Therapy 2019. Philadelphia, Pa.: Elsevier; 2019. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 26.03.2021
11. Centers for Disease Control and Prevention. Common colds: Protect yourself and others. https://www.cdc.gov/features/rhinoviruses/index.html. Imechukuliwa 26.03.2021
12. Kahrilas, PJ. Clinical manifestations and diagnosis of gastroesophageal reflux in adults. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 26.03.2021
13. Gonzalez MD, et al. New developments in rapid diagnostic testing for children. Infectious Disease Clinics of North America. 2018;32:19.
14. Centers for Disease Control and Prevention . AIDS and opportunistic infections. https://www.cdc.gov/hiv/basics/livingwithhiv/opportunisticinfections.html. Imechukuliwa 26.03.2021
15. Shelov SP, et al. Ears, Nose and Throat. In: Caring for Your Baby and Young Child: Birth to Age 5. 6th ed. New York, N.Y.: Bantam Books; 2014.