top of page

Mwandishi:

Dkt. Salome A, MD

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

30 Julai 2021 17:50:44

Image-empty-state.png

Mtoto mwenye uzito mkubwa

Kwa kawaida mtoto anatakiwa kuzaliwa na uzito kati ya kilo 2.5 mpaka kilo 3.9 sawa na gramu 2500 mpaka gramu 3900. Kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa hutokea pale kichanga anapokuwa na uzito wa gramu 4000 au zaidi bila kujali ana wiki ngapi za ujauzito. Utambuzi wa mtoto mkubwa kabla ya kujifungua umekuwa mgumu kutokana na sababu mbalimbali na hivyo kupelekea watoto hawa kugundulika baada ya kuzaliwa. Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa lakini visa vingi husababishwa na tatizo la obeziti pamoja na ugonjwa wa kisukari kwa mama kabla au wakati wa ujauzito. Kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa huweza kuwa jambo la kufurahisha wazazi lakini mara nyingi huambatana na madhara mbalimbali kwa mama na mtoto kama vile kifo cha kichanga na mama au kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2, magonjwa ya moyo na saratani kwa watoto hao katika siku za usoni. Ili kukabiliana na tatizo hili wajawazito wote wenye vihatarishi wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa karibu wakati wa kliniki ya wajawazito ili kutambua mapema na kupunguza madhara yanayotarajiwa kutokea kwa ujauzito wa mtoto mkubwa. Makala hii ni mahususi kwa kina mama wote wenye ujauzito na imezungumzia maana ya mtoto mkubwa, vihatarishi, utambuzi na mambo ya kufanya baada ya kubaini ujauzito wa mtoto mkubwa.


Uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa


Uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa unategemea sababu mbalimbali kutoka kwa mama mwenyewe na mazingira ya ujauzito. Uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa umegawanywa katika makudi matatu yanayosaidia kuonesha uzito wa kawaida na ule usio wa kawaida.


Mtoto anatakiwa kuzaliwa na kilo ngapi?


Kuna makundi matatu ya uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa yaani uzito wa kawaida, uzito mdogo na uzito mkubwa. Mtoto anatakiwa kuzaliwa akiwa na uzito wa kawaida ili yeye na mzazi wake wasipatwe na madhara. Maelezo zaidi ya uzito wa kawaida yanapatikana kwenye aya inayofuata.


Uzito wa kawaida


Uzito wa kawaida wa mtoto wakati wa kuzaliwa hutakiwa kuwa kati ya gramu 2500 hadi 4000 Watoto wengi huzaliwa na wastani wa gramu 3000.


Uzito mkubwa


Uzito mkubwa wa mtoto wakati wa kuzaliwa ni uzito unaoanzia gramu 4000 au zaidi na mara nyingi huweza kufikia mpaka gramu 5000. Watoto wachache huzaliwa na uzito huu.


Uzito mdogo


Uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa chini ya gramu 2500 huitwa uzito mdogo na umegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni;

Uzito mdogo – kati gramu 1500- 2500

Uzito mdogo sana- kati ya gramu 1000-2500

Uzito mdogo uliokithiri- chini ya gramu 1000


Sababu zinazoathiri uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa


Kuna sababu nyingi zinazoathiri uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa na kupelekea kuwa na aidha uzito wa kawaida au usio wa kawaida. Baadhi ya sababu hizo ni;


 • Umri wa mimba wakati wa kuzaliwa

 • Jinsia ya mtoto

 • Urefu wa mama

 • Uzito wa mama kabla ya ujauzito na wakati wa ujauzito

 • Utaifa

 • Vinasaba

 • Magonjwa ya mama kama vile kisukari na shinikizo la damu

 • Umri wa mama nk.


Upimaji wa uzito wa mtoto akiwa tumboni


Bado kuna changamoto ya utambuzi wa mtoto mkubwa wakati wa ujauzito kupitia vipimo, kwani majibu ya vipimo hivi huwa sio sahihi kwa asilimia kubwa. Njia pekee ya uhakika ni kupima uzito wa mtoto kwa kutumia mizani mara baada ya kuzaliwa . Pamoja na changamoto hizi njia zinazoweza kutumika kutambua uzito wa mtoto tumboni mwa mama licha ya kutokuwa na usahihi wa asilimia 100 ni njia ya kupima kimo cha mimba na njia ya kipimo cha mawimbi sauti au ultrasound.


Kimo cha mimba


Hiki sio kipimo bali ni njia ya uchunguzi ambayo hufanyika wakati wa kliniki kwa kutumia kipimo cha mkanda. Kimo cha mimba hupimwa na kuhesabiwa kwa sentimita, kisha kimo hicho hulinganishwa na umri wa mimba kwa wiki, endapo kimo cha mimba ni kikubwa kuliko umri wa mimba hii huashiria kuwa mtoto ni mkubwa. Hata hivyo kuna sababu nyingi zinazosababisha kimo cha mimba kuwa kikubwa kuliko umri wa mimba kama vile mimba ya mapacha, maji mengi ya amniotic nk.


Kipimo cha mawimbi sauti


Kipimo hiki hutumia mawimbi ya sauti kupata taswira ya mtoto akiwa tumboni. Uzito wa mtoto huweza kupimwa kwa kuangalia kiwango cha maji ya amniotic, mzunguko wa tumbo la mtoto na uzito kwa gramu au kilogramu kwa kutumia fomula maalumu iliyopo katika mfumo wa kifaa hiki. Majibu ya kipimo hiki hutegemea umakini na uzoefu wa anayefanya kipimo, kwahiyo sio kipimo cha kuaminiwa sana.

Sababuza kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa


Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa, pamoja na kuwepo kwa sababu hizo, baadhi ya watoto huzaliwa na uzito mkubwa bila sababu yoyote ile inayotambulika Kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanyika, sababu za uzito mkubwa kwa mtoto anayezaliwa hutokana na sababu za mama na sababu za mtoto kama zilivyoelezewa hapa chini.


Sababu za mama zinazopelekea kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa


Hizi ni sababu zinazopelekea mtoto mkubwa ambazo zinamgusa mama moja kwa moja ambazo ni;


 • Kisukari wakati wa ujauzito

 • Uzito mkubwa kabla ya ujauzito

 • Uzito mkubwa wakati wa ujauzito

 • Umri wa mimba uliozidi wiki 40

 • Idadi ya zao

 • Urefu wa mama

 • Historia ya kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa

 • Utaifa wa mama


Maelezo zaidi ya kila kisababishi yameandikwa chini ya aya hii.


Kisukari wakati wa ujauzito


Kisukari ni sababu kubwa ya mtoto mkubwa ulimwenguni kote. Kisukari hiki huhusisha kisukari kabla ya ujauzito yaani kisukari aina ya 1 au aina 2, pamoja na kisukari cha ujauzito( kisukari kinacho sababishwa na ujauzito) Mama anapokuwa na sukari nyingi katika damu hupelekea kongosho ya mtoto kuzalisha kiwango kikubwa cha homoni ya insulin ili kuweza kutumia sukari hiyo iliyotoka kwa mama kupitia damu, matumizi makubwa ya sukari katika mwili wa mtoto hupelekea kuongezeka uzito kwa kasi isiyo ya kawaida.


Uzito mkubwa kabla ya ujauzito


Uzito wa mama kati ya kilo 80 na zaidi, kabla ya kupata ujauzito humuweka katika hatari ya kujifungua mtoto mkubwa kupita kiasi.

Uzito mkubwa wakati wa ujauzito


Ni kawaida kuongezeka uzito wakati wa ujauzito, lakini kuongezeka uzito kuliko pitiliza husababisha mtoto kuwa mkubwa hivyo kuongezeka uzito isivyokawaida. Hatari huongeza zaidi iwapo mama alikuwa na obeziti kabla ya kupata ujauzito na kuwa na uzito wa kilo 80 na zaidi wakati wa kujifungua.


Umri wa mimba uliozidi wiki 40


Kwa kawaida umri wa mimba huwa kwa kipindi cha wiki 40, zaidi ya wiki hizi (wiki 41 na kuendelea) huwa ni ujauzito uliopitiliza. Jinsi umri wa mimba unavyo ongezeka ndivyo mtoto anavyozidi kukua na hivyo kuongeza hatari ya mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa uliopitiliza.


Idadi ya zao


Jinsi mama anavyokuwa na zao nyingi ndivyo anavyozidi kujifungua watoto wenye uzito mkubwa. Hii ni kinyume na wale wenye zao chache. Kuwa na zao nyingi hakuhusiani moja kwa moja na mtoto mkubwa isipokuwa kuna muweka mama katika hatari ya kupata kisukari na obeziti, hivyo kupelekea mtoto mkubwa. Tafiti zinaonesha kuwa hatari hii huongeza kwa wanawake wenye zao zaidi ya tatu.


Umri wa mama


Wajawazito katika umri wa miaka 35na zaidi wapo katika hatari ya kujifungua watoto wenye uzito mkubwa kuliko wale walio na umri mdogo. Hata hivyo tafiti nyingine zinaonesha kuwa wamama kati ya miaka 20-34 katika baadhi ya maeneo wapo katika hatari ya kujifungua watoto wakubwa kupita kiasi.


Urefu wa mama


Urefu wa mama huathiri uzito wa mtoto, katika tafiti nyingi mama mrefu yupo katika hatari ya kujifungua mtoto mkubwa kuliko mama mfupi,hata hivyohakuna kiwango maalumu cha urefu au ufupi kilichoainishwa.


Historia ya kujifungua mtoto mkubwa


Historia ya kujifungua mtoto mkubwa ni sababu inayojitegemea katika kusababisha mtoto mkubwa.

Mwanamke aliyewahi kujifungua mtoto mkubwa yupo katika hatari ya kujifungua tena mtoto mkubwa katika mimba zinazofuata kuliko yule ambaye hana historia ya kujifungua mtoto mkubwa.


Utaifa wa mama


Katika baadhi ya mataifa wanawake hujifungua watoto kubwa, hii huhusishwa zaidi na vinasaba.


Sababu za mtoto zinazopelekea kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa

Hizi ni sababu zinazochangiwa na mtoto aliye tumboni kuwa na uzito mkubwa wakati wa kuzaliwa ambazo ni;


 • Jinsia ya mtoto

 • Maji mengi kwenye chupa ya uzazi

 • Kasoro za vinasaba na maumbile ya mtoto


Maelezo zaidi yanafuata kwenye aya inayofuata


Jinsia ya mtoto


Katika hali ya kawaida watoto wa kiume huwa wakubwa na wazito kuliko watoto wa kike, hivyo hali hii inawaweka katika hatari ya kuzaliwa na uzito mkubwa. Hata hivyo hakuna sababu maalumu iliyothibitishwa inayoplekea watoto wa kiume kuwa katika hatari ya kuwa wakubwa kuliko watoto wa kike.


Maji mengi kwenye chupa ya uzazi


Kuna uhusiano uliopo kati uzito wa mtoto na maji ya amniotic. Jinsi maji haya yanavyokuwa mengi ndivyo ukubwa wa mtoto huongezaka, na yanavyokuwa machache ndivyo uzito wa mtoto hupungua. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa wajawazito wenye maji mengi ya amniotic hujifungua watoto wakubwa.


Kasoro za vinasaba na maumbile ya mtoto


Baadhi ya kasoro za kimaumbile zinahusishwa na kuongezeka kwa uzito wa mtoto, hii ni kwasababu matatizo mengi ya kimaumbile huambatana na kasoro za kimetabolisimu zinazo husika na uzito wa mtoto.


Kasoro ambazo zimethibitishwa kusababisha uzito mkubwa wa mtoto ni;

 • Sindromu ya Beckwith – weiderman

 • Sindromu ya Sotos

 • Sindromu ya Fragile X

 • Sindromu ya Weaver


Madhara yatokanayo na kujifungua mtotomwenye uzito mkubwa


Kuwa na ujauzito wa mtoto mkubwa huweza kuambatana na madhara mbalimbali kwa mama na mtoto wakati au baada ya kujifungua. Madhara hayo baadhi yake ni kupata uzazi mgumu, kujifungua kwa upasuaji, kufa kwa kichanga, mtindio wa ubongo kwa mtoto, mama kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua, kifo cha mtotowakati wa kujifungua n.k Maelezo zaidi yameelezwa kwenye aya inayofuata.


Madhara kwa mama


Mtoto mkubwa husababisha madhara yafuatayo kwa mama;


 • Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua

 • Kuchanika msamba

 • Kuwa na uchungu uliopitiliza

 • Kuwa na uchungu pingamizi

 • Kuchanika kwa kizazi

 • Kujifungua kwa oparesheni


Madhara kwa mtoto


Madhara ya kuwa na uzito mkubwa kwa mtoto hutokea ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa lakini pia hujitokeza wakati wa utoto na utu.


Madhara kwa mtoto wakati wa kujifungua


Yafuatayo ni madhara ya muda mfupi ambayo hutokea wakati wa kuzaliwa na muda mfupi baada ya kuzaliwa;


 • Kukosa hewa ya oksijeni na kuzaliwa akiwa amechoka

 • Kukwama kwenye nyonga kwa bega la mtoto wakati wa kujifungua

 • Shida ya kupumua

 • Kuumia wakati wa kuzaliwa- kupata michubuko, kuvunjika kwa fupakola nk.

 • Kushuka kwa kiwango cha sukari kweney damu.


Madhara ya muda mrefu kwa mtoto


Yafuatayo ni madhara ambayo huweza kujitokeza hasa katika kipindi cha utu uzima


 • Obeziti utotoni na wakati wa utu uzima

 • Kisukari

 • Magonjwa ya moyo

 • Saratani

 • Kiharusi


Jinsi gani mama mwenye obeziti na kisukari anaweza kuzuia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa na madhara yake?


Ni vigumu sana kuzuia kuzaliwa kwa mtoto mkubwa lakini kunauwezekano wa kuzuia baadhi ya sababu ambazo zinapelekea kuzaliwa kwa mtoto mkubwa na kuzuia madhara yanayoambatana na mtoto mkubwa. Njia mbalimbali zinaweza kutumika kupunguza tatizo hili hasa kwa zile sababu ambazo zinaweza kuzuilika, na kwasababu zisizoweza kuzuilika bado kuna uwezekano wa kupunguza madhara yake hasa yale yanayojitokeza wakati wa kujifungua na muda mfupi baada ya kujifungua.

Kwa mama mwenye kisukari

Inabidi kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwa mama mwenye kisukari na kisukari cha mimba katika kipindi chote cha ujauzito, ili kuweka sukari yake katika kiwango kinachotakiwa kwa kufanya yafuatayo;


Kufanyiwa kipimo cha sukari mara kwa mara ili kujua maendeleo yake

Kuanzishiwa dawa ya insulin


Kula vyakula vinavyoshauriwa kwa mtu mwenye kisukari

Kwa mama mwenye obeziti Jitihada zifuatazo zinaweza kumsaidia mama mwenye obeziti kabla na wakati wa ujauzito;

 • Elimu ya lishe

 • Kufanya mazoezi

 • Kuacha ulaji wa vyakula taka na badala yake kula lishe bora yenye mlo kamili

 • Kuhakikisha uzito wake hauzidi kiwango kinachotakiwa katika kipindi chote cha ujauzito


Namna ya kuzuia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kwa wajawazito wote wenye vihatarishi


Kwa bahati mbaya sababu zingine zinazoplekea mtoto mkubwa haziwezi kuzuilika kwa mfano jinsia ya mtoto, urefu wa mama nk. Wanawake katika kundi hili wanaweza kusaidiwa kwa kuwakinga wao na watoto wao dhidi ya matatizo yatokanayo na mtoto mkubwa kama ifuatavyo;


 • Kubaini wanawake wote walio katika hatari ya kupata watoto wakubwa na kufanya ufuatiliaji wa karibu

 • Kupanga njia salama ya kujifungua wanapokaribia wiki 40 za mimba

 • Kuhakikisha watoto wakubwa wanahudumiwa katika chumba maalumu cha watoto wachanga mara baada ya kuzaliwa.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

29 Septemba 2021 18:55:16

Rejea za dawa

 1. Macrosomia in 23 developing countries: an analysis of a multicountry, facility-based, cross-sectional survey. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(12)61605-5/fulltext. Imechukuliwa 26.07.2021

 2. Pamela J Surkan et al. Reasons for increasing trends in large for gestational age births. Obstet Gynecol. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/15458892/. Imechukuliwa 26.07.2021

 3. Abdulai Abubakari, et al. Prevalence of abnormal birth weight and related factors in Northern region, Ghana. https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-015-0790-y. Imechukuliwa 26.07.2021

 4. Myles T D, et al. Relationship between normal amniotic fluid index and birth weight in term patients presenting for labor Reprod. Med. 2001 Jul. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/11499190/pp. Imechukuliwa 26.07.2021

 5. Waller D K, et al. Do infants with major congenital anomalies have an excess of macrosomia?. Teratology. 2001 Dec. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/11754173/. Imechukuliwa 26.07.2021

 6. Yi Li, et al.Weight Gain in Pregnancy, Maternal Age and Gestational Age in Relation to Fetal Macrosomia. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4418414/. Imechukuliwa 26.07.2021

 7. Saemundur Gudmundsson,Anne-Charlotte Henningsson,Pelle Lindqvist. Correlation of birth injury with maternal height and birthweight. https://doi.org/10.1111/j.1471-0528.2004.00545.x. Imechukuliwa 26.07.2021

 8. Aisha Salim Said, at al. Risk factors and outcomes of fetal macrosomia in a tertiary centre in Tanzania: a case-control study. BMC Pregnancy and Childbirth volume 16, Article number: 243 (2016). https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-016-1044-3#ref-CR18. Imechukuliwa 26.07.2021

 9. Healthline. Macrosomia. https://www.healthline.com/health/macrosomia#what-to-ask-your-doctor. Imechukuliwa 26.07.2021

 10. Julia Milner and Jane Arezina.The accuracy of ultrasound estimation of fetal weight in comparison to birth weight: A systematic review. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5810856/. Imechukuliwa 26.07.2021

 11. Oliver Preyer, et al. Fetal weight estimation at term – ultrasound versus clinical examination with Leopold’s manoeuvres: a prospective blinded observational study. BMC Pregnancy and Childbirth volume 19, Article number: 122 (2019). https://bmcpregnancychildbirth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12884-019-2251-5. Imechukuliwa 26.07.2021 12.

 12. Medscape. Estimation of fetal weight.https://emedicine.medscape.com/article/262865-overview#a1. Imechukuliwa 26.07.2021

 13. Medscape. Macrosomia.https://emedicine.medscape.com/article/262679-overview#a2. Imechukuliwa 26.07.2021

 14. Akanmode AM, et al. Macrosomia. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK557577/. Imechukuliwa 26.07.2021

bottom of page