Swali la msingi
Habari daktari, je PEP hufanyaje kazi kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI?
Majibu

Asante kwa swali zuri, makala hii ni mahususi kujibu swali lako ili kupata uelewa. Mwishoni mwa makala hii pia kuna linki ya video ya namna dawa za Ukimwi zinavyofanya kazi kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, tazama pia kwa uelewa zaidi.
PEP inazuiaje maambukizi ya VVU?
PEP, hufanya kazi kwa kuzuia Virusi vya Ukimwi (VVU) visijijenge mwilini baada ya mtu kujianika kwenye maambukizi kwa njia mbalimbali. Dawa hizi huwa ni mchanganyiko wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) zinazotumika kwa siku 28 mfululizo ili kuzuia uzalishaji wa virusi na kuenea kwake mwilini. Njia kuu za ufanyaji kazi wa PEP zimeelezewa hapa chini.
Njia za utendajikazi wa PEP
PEP hufanya kazi kupitia hatua kuu tatu:
1. Kuzuia kimeng'enya Reverse Transcriptase
PEP mara nyingi hujumuisha dawa za vizuia nucleoside reverse transcriptase (NRTIs) kama vile tenofovir (TDF) na emtricitabine (FTC). Dawa hizi huzuia kimeng'enya cha reverse transcriptase, ambacho VVU hutumia kubadilisha RNA yake kuwa DNA, hivyo kuzuia virusi kujishikiza kwenye seli za binadamu.
2. Kuzuia VVU kujishikiza kwenye DNA ya binadamu
Baadhi ya dawa za PEP zinazofanya kazi hii ni zile jamii ya vizuia integrase (INSTIs) kama raltegravir (RAL) au dolutegravir (DTG). Dawa kundi hili huzuia virusi kuingiza vinasaba vyake kwenye seli za binadamu, hivyo kuzuia maambukizi mapya.
3. Kudhibiti kuzaliana kwa VVU
Kwa kutumia mchanganyiko wa dawa hizi, PEP huzuia ongezeko la idadi ya virusi mwilini na huipa kinga ya mwili nafasi ya kuvidhibiti kabla havijaenea.
Video ya namna dawa za UKIMWI zinavyofanya kazi
Rejea za mada hii:
Mwongozo wa Kimatibabu kuhusu PEP. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6502541/. Imechukuliwa 03.04.2025
Tafiti kuhusu ufanisi wa ARVs kwa kuzuia VVU. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/32013422/. Imechukuliwa 03.04.2025