top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dkt. Glory, MD

ULY CLINIC

6 Septemba 2025, 01:24:44

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Jinsi ya kufahamu kama utoaji mimba kwa dawa umefanikiwa

Swali la msingi:


Habari daktari, nimetumia dawa ya kutoa mimba ila nina mashaka siamini kua iyo mimba imetoka na nilikua nataka kama haijatoka uniambie njia nyingine ya kutoa au unishauri nifanyaje?


Majibu

Ninaelewa mashaka yako, na ni muhimu kuhakikisha afya yako iko salama. Baada ya kutumia dawa za kutoa mimba, ni muhimu kufuatilia dalili na ishara zinazoonyesha kama mchakato umefanikiwa. Hata hivyo, dalili hizi peke yake hazithibitishi kuwa mimba imetoka kikamilifu. Kwa hiyo, inashauriwa kufanya uchunguzi wa kiafya baada ya wiki chache ili kuhakikisha kuwa hakuna mabaki ya mimba yaliyosalia. Ikiwa vipimo vitaonyesha uwepo wa homoni za ujauzito, au ikiwa dalili za ujauzito zinaendelea, ni muhimu kuwasiliana na mtoa huduma wa afya kwa uchunguzi zaidi na ushauri. Kama umetumia dawa ya kutoa mimba lakini hauna uhakika kama imetoka kabisa au la, maelezo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata uelewa.


Dalili zinazoashiria ufanisi wa dawa ya utoaji mimba

Baada ya kutumia dawa ya kutoa mimba kama mifepristone na misoprostol, dalili zinazotarajiwa kuonekana na kuwa ishara ya mimba inatoka/imetoka ni pamoja na:

  • Maumivu ya tumbo kama la hedhi au makali zaidi

  • Kutokwa na damu nyingi kuliko hedhi ya kawaida, na inaweza kuchanganyika na mabonge.

  • Kupotea au kupungua na kuisha kwa dalili za ujauzito kama kichefuchefu na matiti kujaa siku chache baada ya kutumia dawa.


Dalili zinazoashiria mimba haijatoka kikamilifu au imebaki

Ukipata dalili hizi ni ishara kuwa mimba haijatoka au kuna masalia yamebakia;

  • Kutokwa na damu kidogo sana au damu kukata haraka sana.

  • Dalili za ujauzito kuendelea baada ya siku kadhaa.

  • Kuhisi uvimbe tumboni au maumivu makali yasiyoisha.

  • Homa au uchafu wenye harufu mbaya (inaweza kuwa ishara ya maambukizi kwenye kizazi).


Nini unachopaswa kufanya?

  • Onana na daktari- haraka kwa mazungumzo ya kitaalamu na ushauri

  • Pima Ujauzito- Baada ya siku 10-14, tumia kipimo cha ujauzito kwa njia ya mkojo ili kuona kama mimba bado ipo. Kipimo cha damu cha homoni ya ujauzito (hCG) kinaweza kutoa majibu ya uhakika haraka zaidi.

  • Fanya kipimo cha Utrasound– Ikiwa una wasiwasi, tembelea hospitali ili daktari afanye uchunguzi wa kizazi kuhakikisha kama mfuko wa mimba upo safi na hakuna masalia ya mimba.


Njia nyingine za utoaji mimba 

Ikiwa mimba bado ipo au haijatoka kikamilifu, daktari wako anaweza kukushauri mambo yafuatayo;

  • Kutumia dawa nyingine za kusaidia kutoa masalia ya mimba (kama misoprostol, chini ya usimamizi wake).

  • Upasuaji mdogo wa kufyonza masalia ya mimba katika kizazi, njia hii ni salama na yenye ufanisi mkubwa wa kusafisha mfuko wa uzazi.


Ushauri muhimu

  • Usijaribu kutumia dawa nyingine bila mwongozo wa daktari ili kuepuka hatari za kutokwa na damu nyingi au maambukizi.

  • Pata msaada wa kitaalamu haraka ikiwa unahisi dalili mbaya kama maumivu makali, homa, au kutokwa na damu kupita kiasi.

  • Kutokwa na damu baada ya kutumia dawa za kutoa mimba hakumaanishi kuwa mimba imetoka kikamilifu; uchunguzi wa kiafya unahitajika kuthibitisha hilo.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara

1. Daktari naomba msaada, nilimeza dawa ya kutoa mimba inaitwa Famiclean Kit ya vidonge 5. Baada ya hapo nilitokwa na vinyama pamoja na damu kwa siku moja tu, kisha damu ikakata. Baada ya wiki mbili nilipima mimba ikawa bado ipo. Nikabadilishiwa dawa nyingine na muuguzi wangu nikameza jana usiku, lakini mpaka sasa hakuna damu kutoka. Maumivu yalikuwepo jana lakini sasa yameisha bila damu. Kwa nini inatokea hivi?

Hali hii inaweza kuwa na sababu kadhaa:

  1. Masalia ya mimba bado yapo kwenye kizazi, hivyo mwili haujaanza tena mchakato wa kuyatoa.

  2. Dozi au muda wa dawa unaweza usiwe sahihi kwa hatua ya ujauzito uliokuwa nayo.

  3. Kizazi chenye mikazo mikali au kusinyaa mapema kinaweza kusababisha damu isivuje, hata kama masalia yapo ndani.

  4. Ikiwa mimba bado inaendelea (bado inakua), dawa ya awali haikufanikiwa kuikomesha.


Hii ni hali inayohitaji kipimo cha ultrasound cha haraka ili kujua kama kijusi bado kipo au kuna masalia, na kuamua kama upasuaji mdogo (kama wa kuondoa uchafu kwenye kizazi) unahitajika.

2. Ni lini baada ya kutumia dawa ya kutoa mimba napaswa kufanya kipimo cha ujauzito?

  • Mara nyingi, mabaki ya homoni ya ujauzito (hCG) hubaki mwilini kwa hadi wiki 4–6 hata baada ya mimba kutoka.

  • Kipimo cha mkojo kinafaa kufanywa baada ya siku 10–14, lakini kama unataka uhakika wa mapema zaidi, kipimo cha damu (serum hCG) kinaweza kufanywa siku chache baada ya kutumia dawa na kurudiwa baada ya siku 2–3 ili kuona kama kiwango kinashuka.

3. Kipimo cha ujauzito changu kimeonyesha matokeo chanya wiki mbili baada ya kutumia dawa. Je, ina maana bado nina ujauzito?

  • Si lazima. Matokeo chanya yanaweza kuwa kutokana na homoni zilizobaki mwilini hata kama mimba imetoka.

  • Lakini ikiwa kiwango cha homoni hakishuki au kimeongezeka, inaashiria ujauzito unaendelea au masalia bado yapo.

  • Kufuatilia kwa ultrasound au kupima hCG kwa kurudiwa ni njia ya uhakika.

4. Kwa nini baadhi ya wanawake hutokwa na damu kidogo baada ya dawa badala ya nyingi?

  • Kiasi cha damu hutegemea mambo kama:

    1. Umri wa ujauzito (kadiri mimba ilivyokuwa ndogo, damu inaweza kuwa kidogo).

    2. Mwili kujibu dawa — kwa baadhi ya wanawake, mchakato wa kutoa masalia unaweza kuwa wa polepole.

    3. Mimba kutotoka kikamilifu — kama kizazi kimefunga lakini bado kina masalia, damu inaweza kuwa kidogo lakini matatizo yanaweza kutokea baadaye.

  • Kutokwa kidogo mno, hasa bila mabonge, inaweza kuwa ishara ya mchakato kutofanyika kikamilifu.

5. Naweza kutumia dawa zaidi ya mara moja bila kuonana na daktari?

  • Haishauriwi. Kutumia dawa mara kwa mara bila usimamizi wa mtoa huduma ya afya huongeza hatari ya:

    • Kutokwa na damu nyingi kupita kiasi.

    • Maambukizi makubwa kwenye kizazi.

    • Uharibifu wa mfuko wa mimba ikiwa misoprostol itatumika vibaya.

  • Kila dozi inapaswa kutolewa kwa mpango maalum kulingana na umri wa ujauzito na hali ya afya ya mama.

6. Kuna madhara gani ikiwa masalia ya mimba yatasalia kwenye kizazi?

  • Madhara yanaweza kuwa makubwa, ikiwemo:

    • Maambukizi (sumu ya bakteria kwenye damu) ambayo yanaweza kuhatarisha maisha.

    • Kutokwa na damu kidogo inayoendelea kwa wiki au miezi.

    • Maumivu ya tumbo yasiyoisha.

    • Hatari ya kuunda makovu ndani ya kizazi (Sindromu ya Asherman) ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito baadaye.

  • Ndiyo maana kufanyiwa ultrasound ni hatua muhimu baada ya dawa.

7. Je, dawa za kutoa mimba zinaweza kushindwa kabisa kuondoa ujauzito?

  • Ndiyo, hasa kama:

    • Dawa hazikutumiwa katika mpangilio sahihi (mfano, mifepristone kabla ya misoprostol).

    • Umri wa ujauzito ni mkubwa kuliko ulivyodhaniwa.

    • Ubora wa dawa ni duni au zimehifadhiwa vibaya.

  • Wakati mwingine mimba inaweza kuendelea kukua, na hii ni hatari kwa mtoto na mama.

8. Baada ya kutumia dawa na kufanikiwa kutoa mimba, ni lini naweza kupata hedhi tena?

  • Kwa kawaida hedhi ya kwanza hurudi ndani ya wiki 4–6.

  • Ikiwa haijarudi baada ya wiki 8, unapaswa kufanyiwa kipimo ili kuondoa uwezekano wa ujauzito mpya au matatizo ya homoni.

9. Nifanye nini kama sina dalili zozote baada ya kutumia dawa ya kutoa mimba?

  • Kukosa dalili kunaweza kumaanisha:

    1. Dawa haijafanya kazi.

    2. Kipimo cha dawa kilikuwa kidogo.

    3. Mwili wako haukujibu dawa kutokana na tofauti za kimaumbile.

  • Inashauriwa kufanya ultrasound au kipimo cha hCG haraka ili kuchukua hatua mapema.

10. Ni muda gani salama wa kujaribu kupata ujauzito tena baada ya kutumia dawa ya kutoa mimba?

  • Madaktari wengi wanashauri kusubiri angalau mzunguko mmoja wa hedhi ili mwili upone na kizazi kurudi kwenye hali ya kawaida.

  • Kusubiri pia hupunguza hatari za matatizo kwa ujauzito unaofuata na hukupa muda wa kupona kiafya na kiakili.

11. Nikitumia dawa ya kutoa mimba, kisha baada ya wiki mbili bado nipime nikute mimba ipo, halafu nirudie dawa tena bila kupata damu wala maumivu — je, hii inamaanisha mimba bado ipo?”

Kama mtu ametumia dawa ya kutoa mimba mara ya kwanza na baada ya wiki mbili akapima bado akaona mimba ipo, kisha akarudia kutumia dawa tena lakini hakupata damu wala maumivu, hii mara nyingi ina maana kwamba mimba bado ipo na dawa hazikufanya kazi ipasavyo.

Kutopata damu au maumivu baada ya kutumia dawa mara ya pili kunaonyesha dawa haikuletea mabadiliko yoyote tumboni. Hivyo, mimba haikutoka.


Jambo la muhimu zaidi ni kwenda hospitali kufanyiwa ultrasound ili kuthibitisha kama mimba ipo, na kama ipo, daktari atashauri njia salama na sahihi ya kuendelea — badala ya kuendelea kutumia dawa mara kwa mara bila uangalizi.


Rejea za mada hii:
  1. Planned Parenthood. How can I tell if my abortion worked? What are the signs of pregnancy after you’ve had an abortion? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.plannedparenthood.org/blog/how-can-i-tell-if-my-abortion-worked-what-are-the-signs-of-pregnancy-after-youve-had-an-abortion

  2. Aid Access. How do you know if you have a continuing pregnancy? [Internet]. 2023 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://aidaccess.org/en/page/463/how-do-you-know-if-you-have-a-continuing-pregnancy

  3. Mayo Clinic. Medical abortion: What you need to know [Internet]. 2023 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.mayoclinic.org/tests-procedures/medical-abortion/about/pac-20394687

  4. National Health Service (NHS). Abortion: What happens? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.nhs.uk/conditions/abortion/what-happens/

  5. Medical News Today. How do you know the abortion pill worked? [Internet]. 2025 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.medicalnewstoday.com/articles/how-do-you-know-the-abortion-pill-worked

  6. Healthline. How do you know if the abortion pill worked? [Internet]. 2025 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.healthline.com/health/healthy-sex/how-do-you-know-if-the-abortion-pill-worked

  7. Planned Parenthood. What are the abortion pill’s side effects? [Internet]. 2025 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.plannedparenthood.org/learn/abortion/the-abortion-pill/what-can-i-expect-after-i-take-the-abortion-pill

  8. UCLA Health. FAQ: Post-abortion care & recovery [Internet]. 2025 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.uclahealth.org/medical-services/obgyn/family-planning/patient-resources/faq-abortion-care-and-recovery

  9. Aid Access. FAQs complications – Signs of pregnancy after abortion pills [Internet]. 2025 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://aidaccess.org/en/page/7393640/faqs-complications

  10. ThrivE Savannah. How do I know if my abortion failed? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://thrivesavannah.org/how-do-i-know-if-my-abortion-failed/

  11. NHS. Recovery after an abortion [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.nhs.uk/tests-and-treatments/abortion/recovery/

  12. Cleveland Clinic. Medical abortion: What it is, pain, risks & recovery [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://my.clevelandclinic.org/health/treatments/21899-medical-abortion

  13. Mayo Clinic. Elective abortion: Does it affect subsequent pregnancies? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Available from: https://www.mayoclinic.org/healthy-lifestyle/getting-pregnant/expert-answers/abortion/faq-20058551


Imeandikwa:

7 Juni 2025, 19:22:50

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page