top of page

Majadiliano na Wataalamu

Public·804 members

Kukabiliana na dalili za kipindi cha tatu cha ujauzito

Swali la msingi


Habari daktari, niko na ujauzito wa wiki 29 lakini napata tabu sana kwenye kula, kulala, mwili unaisha nguvu na chini ya tumbo naumia sana, na kuhema nashindwa, adi mgongo unaumaa mnoo, shida ni nini na nifanyajee kupunguza dalili hizi?


Majibu

Pole sana kwa hali unayopitia, dalili unazozieleza zinaweza kuwa za kawaida kwa baadhi ya wajawazito hasa kipindi cha tatu cha ujauzito (wiki 28 na kuendelea), lakini pia zinaweza kuashiria matatizo fulani yanayohitaji uangalizi wa haraka wa kitabibu.


Dalili Ulizotaja

  1. Kukosa hamu ya kula / kushindwa kula vizuri

  2. Kuchoka sana / mwili kuishiwa nguvu

  3. Maumivu chini ya tumbo

  4. Kushindwa kupumua vizuri

  5. Maumivu makali ya mgongo

Hali na magonjwa yanayoweza kusababisha dalili hizi ni kama zifuatazo;


Shinikizo la mtoto anavyokua

Mtoto anapokuana kuongezeka umbo, anaweza ongeza shinikizo ndani ya tumbo na viungo vya karibu kama vile mapafu, matumbo, na neva za mgongoni hivyo kupelekea;

  • Kushindwa kula vizuri kwa sababu tumbo linabana.

  • Maumivu ya mgongo (hasa sehemu ya chini).

  • Maumivu chini ya tumbo kutoka kwa misuli au kizazi kinayopanuka.

Upungufu wa damu

Unapoishiwa damu unaweza kujisikia kuchoka, kuishiwa nguvu, kushindwa kupumua vizuri, na wakati mwingine maumivu ya kichwa. Hii ni kawaida kwa wajawazito lakini inahitaji uchunguzi na matibabu.


Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) au matatizo ya kibofu

Hii inaweza kusababisha maumivu chini ya tumbo na mgongo.


Dalili za leba mapema

Kama maumivu yako ni ya kudumu au yanakuja kwa vipindi, yanaweza kuwa dalili ya uchungu wa leba kabla ya wakati.


Mambo unayoweza kufanya

Nenda kituo cha afya au hospitali karibu nawe kufanya vipimo hivi:

  • Kupima damu kuona kama una upungufu wa damu (Kipimo cha HB)

  • Kupima mkojo kuona kama una UTI

  • Kupimwa shinikizo la damu

  • Kufanya kipimo cha picha ya mionzi sauti ili kuona hali ya mtoto na placenta


Mambo yanayoweza kukusaidia

  • Kula kidogo kidogo mara nyingi badala ya milo mikubwa.

Tumia vyakula vyenye virutubisho (mboga za majani, matunda, protini kama maharagwe, mayai).

  • Pumzika kwa kutosha kwa kulala kwa upande wa kushoto ukiweka mto kati ya miguu, hii huongeza mzunguko wa damu.

  • Kunywa maji ya kutosha.

  • Epuka kufanya kazi nzito.

  • Tumia magnesiamu au kalsiamu kama umepewa na daktari, inaweza kupunguza maumivu ya mgongo na miguu.

  • Fanya mazoezi mepesi kama kutembea kwa dakika 15-30 kila siku kama huna vizuizi vya kiafya.


Wakati gani uwasiliane na daktari haraka?

Ukiona dalili zifuatazo tafadhali enda hospitali haraka:

  • Maumivu makali ya tumbo yanayoendelea au kuja kwa vipindi.

  • Kutokwa na damu au maji ukeni.

  • Mtoto kutocheza kama kawaida.

  • Maumivu makali ya kichwa, kuona ukungu au kuvimba uso na miguu haraka.


Rejea za mada hii:

  1. Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Dashe JS, Hoffman BL, Casey BM, et al. Williams Obstetrics. Toleo la 25. New York: McGraw-Hill Education; 2018.

  2. World Health Organization. WHO recommendations on antenatal care for a positive pregnancy experience. Geneva: WHO; 2016.

  3. American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG). Practice Bulletin No. 222: Preterm Labor. Obstet Gynecol. 2020;135(2):e106–e119.

  4. Mayo Clinic. Pregnancy week by week: 29 weeks pregnant [Intaneti]. Mayo Clinic; 2023 Imechukuliwa 06.04.2025 kutoka.

  5. March of Dimes. Pregnancy symptoms and discomforts [Intaneti]. March of Dimes; 2022 Imechukuliwa 06.04.2025 kutoka.

  6. National Institute for Health and Care Excellence (NICE). Antenatal care for uncomplicated pregnancies. Mwongozo wa kliniki [CG62]. London: NICE; 2008.

8 Views

Kuhusu kundi

Uliza swali pamoja na kusoma majibu ya maswali yaliyoulizwa,...

bottom of page