top of page

Majadiliano na Wataalamu

Public·804 members

Je, madhara ya PID sugu yanatibika?

PID sugu inatibika?

Swali la msingi


PID inanisumbua sana dawa nimetumia sana hosptiali mbalimbali lakini hazijasaidia. Shida ni nini?


Majibu


Kwa maelezo yako unaweza kuwa na PID sugu au PID isiyosikia dawa, makala hii imezungumza kuhusu aina hizi mbili za PID. PID sugu ni hali ya kuwa na maambukizi ya muda mrefu katika viungo vya uzazi kama vile mfuko wa uzazi, ovari, na mirija ya falopia. Hii hutokea baada ya maambukizi ya awali ya PID kutibiwa isivyo sahihi au kutopata matibabu kwa wakati. Hali hii inaweza kuwa sugu na kuendelea kwa muda mrefu, na inaweza kusababisha madhara makubwa ya afya ya uzazi.


Madhara ya PID sugu yanaweza kuwa ya kudumu na yanaweza kuwa magumu kutibika, hasa ikiwa maambukizi yalichelewa kutibiwa au yalirudi mara kwa mara. Hata hivyo, baadhi ya madhara yanaweza kupunguzwa au kutibiwa kupitia matibabu ya mapema na matibabu endelevu.


Dalili za PID Sugu

Kuwa na PID ambayo inasumbua au inarejea baada ya matibabu na kuambatana na dalili zifuatazo huashiria kuwa na PID sugu;

  • Maumivu ya tumbo la chini ambayo yanachukua muda mrefu au yanajirudiarudia.

  • Maumivu ya chini ya mgongo.

  • Kutokwa na uchafu ukeni wenye mchanganyiko wa damu au usaha.

  • Ugumu wa kupata ujauzito (utasa)

  • Maumivu wakati wa tendo la ndoa.

  • Mabadiliko kwenye mzunguko wa hedhi.


Matibabu ya madhara ya PID sugu ni nini?

Hapa chini kuna baadhi ya madhara ya PID na jinsi yanavyoweza kutibika au kudhibitiwa;


Utasa

Maambukizi ya PID yanaweza kuharibu mirija ya falopia, ambayo inahusika na kusafirisha yai kutoka kwa ovari hadi kwenye kizazi. Ikiwa mirija hiyo itaharibika, inaweza kuzuia mimba.


Matibabu

Matibabu ya utasa yanaweza kuwa na uwezo wa kurekebisha baadhi ya madhara ya PID. Hii inaweza kujumuisha upasuaji ili kufungua au kurekebisha mirija ya falopia iliyojaa. Katika hali ambapo mirija ya falopia haiko katika hali nzuri ya kufanya kazi, mbinu ya kuchavusha kwenye chupa- IVF inaweza kuwa chaguo la kupata mimba.


Maumivu sugu ya tumbo la chini

Maambukizi ya PID yanaweza kusababisha maumivu ya tumbo la chini yanayodumu kwa muda mrefu, hata baada ya maambukizi kutibiwa.


Matibabu:

Dawa za maumivu kama vile NSAIDs zinaweza kusaidia kupunguza maumivu. Matibabu mengine kama tiba ya kimwili inayohusisha mabadiliko ya mtindo wa maisha (kama vile kuepuka mazoezi makali kupinduika) yanaweza kusaidia kupunguza maumivu. Katika hali usugu, upasuaji unaweza kuhitajika ikiwa kuna madhara makubwa kwenye tishu au viungo vya uzazi. Katika baadhi ya hali, kama vile majeraha makubwa ya mirija ya falopia au matatizo ya ovari, upasuaji unaweza kuwa muhimu ili kurekebisha au kuondoa maeneo yaliyoathirika.


Mimba ya nje ya kizazi

PID inaweza kuathiri mirija ya falopia na kuongeza hatari ya mimba kutungwa nje ya kizazi, ambapo yai linajikuta limechavushwa nje ya kizazi.


Matibabu:

Matibabu ya mimba ya nje ya kizazi mara nyingi yanahitaji upasuaji ili kuondoa mimba iliyotungwa na tatizo hili linahitaji matibabu ya haraka ili kuepuka madhara zaidi kwa afya ya mama.


Uharibifu katika mfumo wa uzazi

Katika hali sugu ya PID, kuna uwezekano wa majeraha ya kudumu kutokea kwenye tumbo la uzazi, ovari, na mirija ya falopia, ambayo yanaweza kuathiri uwezo wa kushika mimba au kufanya shughuli za uzazi kwa ufanisi.


Matibabu:

Upasuaji unaweza kusaidia kurekebisha sehemu zilizoharibika, lakini mara nyingi baadhi ya madhara yanaweza kuwa ya kudumu, kama vile uharibifu wa tishu au viungo. IVF inaweza kuwa mbadala wa kupata mimba katika hali ya uharibifu wa viungo vya uzazi.


Madhara kwa kinga ya mwili

PID inaweza kusababisha madhara kwa mfumo wa kinga na kuzorotesha uwezo wa mwili kupambana na maambukizi.


Matibabu

Matibabu ya PID, ikiwa ni pamoja na antibayotiki na dawa za kurekebisha kinga, yanaweza kusaidia kurejesha mfumo wa kinga kwa afya bora.


PID isiyosikia dawa

PID isiyosikia dawa inaweza kutambuliwa kwakufanya vipimo maalumu kama culture ans sensiticity ili kutambua vimelea hao wanasikia dawa gani. Hata hivyo kama kuna madhara ambayo yameshatokea, matibabu baada ya kipimo yanaweza kuua vimelea na kupunguza dalili lakini hakuondoi dalili za madhara ambayo yameshasababishwa na PID.


Hitimisho

Madhara ya PID yanaweza kutibika au kupunguzwa ikiwa yatatibiwa mapema, lakini baadhi ya madhara yanaweza kuwa ya kudumu, hasa ikiwa maambukizi yalichelewa kutibiwa. Matibabu ya PID sugu ni muhimu ili kupunguza madhara, na upasuaji au mbinu za uzazi kama IVF zinaweza kusaidia wanawake waliokutana na madhara ya uzazi kupata mtoto.


Wapi utapata maelezo ya ziada?

Kama una wasiwasi kuwa una PID au madhara yake, ni muhimu kuona daktari wako kwa uchunguzi na matibabu ya haraka.


Rejea za mada hii

15 Views

Kuhusu kundi

Uliza swali pamoja na kusoma majibu ya maswali yaliyoulizwa,...

bottom of page