top of page

Majadiliano na Wataalamu

Public·804 members

Natambuaje UKIMWI bila kupima?

  1. Itachukua siku ngapi kutambua nina UKIMWI bila kupima?

  2. Dalili za UKIMWI huonekana baada ya siku ngapi?

  3. Itachukua siku ngapi kutambua nina HIV bila kupima?

  4. Inachukua siku ngapi kujitambua nina maambukizi ya virusi vya UKIMWI bila kupima?

  5. Nitatamtabuaje mtu mwenye UKIMWI bila kupima?

  6. Ninawezaje kumtambua mwathirika wa VVU?

220 Views

Hayo ni maswali watu wengi wamekuwa wakiuliza na yamejibiwa kwenye Makala hii fupi


Ni muhimu ufahamu kwanza?



Maswali yote yamelenga kuuliza namna ya kutambua maambukizi ya VVU/ UKIMWI bila kupima. Hii inaweza kuwa ngumu kwa baadhi ya nyakati kwa sababu kuna maambukizi mengine ambayo yanaweza kuleta dalili zinazofanana na dalili za mwanzo za UKIMWI, mfano maambukizi ya virusi wengine kama kirusi cha mafua (influenza), UVIKO-19 au corona n.k

Endapo unahisi umepata maambukizi ya VVU njia pekee ya kutambua ni kwa kupima naam hata kama upo hatua za mwisho, kwa sababu unaweza kuwa na ugonjwa wowote ule unaoleta dalili kama za UKIMWI. Endapo utapima na kutambulika mapema na kuanza dawa, utadhibiti dalili nyingi na kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine wasio na maambukizi.


Je inachukua siku ngapi kuanza kuona dalili za ukimwi pasipo kupima?


Swali hili linajibiwa vema kwa kutumia dalili za kila hatua za maambukizi ya Virusi vya UKIMWI


Hatua ya kwanza ya maambukizi ya VVU


Hatua ya kwanza huambatana na dalili ambazo hutokea kwa kipindi cha ndani ya siku 14 hadi 28 baada ya kupata maambukizi na hudumu kwa siku au wiki chache.


  • Homan na kutetemeka

  • Kutokwa jasho wakati wa usiku

  • Kuvimba tezi limfu

  • Maumivu ya misuli

  • Kukauka kwa koo

  • Harara kwenye ngozi au vipele

  • Uchovu mkali

  • Vidonda ndani ya kinywa


Dalili hizi huonekana chini ya asilimia 70 ya walioapata VVU


Hatua ya pili ya maambukizi ya VVU


Unaweza kupita hatua ya kwanza bila kutambua una VVU kwa sababu hujapata dalili na kuingia kwenye hatua hii ya pili.


Ni dalili gani huonekana kwenye hatua ya pili?


Hatua ya pili inaweza kuchukua kipindi cha miaka 10 hadi 15, na huwa haina dalili yoyote hasa katika hatua za awali. VVU huzaliana kwa wingi na kuharibu mfumo wa kinga ya mwili inayopelekea kuingia hatua ya tatu. Kwenye hatua ya pili karibia na kuingia hatua ya tatu dalili zifuatazo zinaweza kuonekana kwa kiasi kidogo tu;


  • Kupoteza uzito bila sababu chini ya asilimia 10 ya uzito wa mwanzo

  • Maambukizi ya mfumo wa upumuaji kama sinusaitizi, kupata matezi n.k

  • Kama mkanda wa jeshi

  • Kupasuka pembe za midomo

  • Vidonda vya mara kwa mara kwenye pembe za midomo

  • Kuzuka kwa upele mwili mzima unaowasha wenye rangi ya zambarau

  • Fangasi wa kwenye vidole

  • Magonjwa mengine ya ngozi


Hatua ya tatu ya maambukizi ya VVU


Hatua ya tatu ni kuonekana kwa dalili za Upungufu wa Kinga MWilini yaani UKIMWI, hatua hii huonekana miaka 10 au 15 baada ya kupata maambukizi ya VVU bila kupata tiba. Dalili zinazoonekana kwenye hatua ya tatu ya maambukizi ya VVU ni matokeo ya kuharibiwa kwa mfumo wa kinga ya mwili. Maradhi mbalimbali humpata mwathirika kwa sababu kinga ya mwili kushindwa kumlinda mwathirika dhidi ya maambukizi mbalimbali. Dalili za hatua ya tatu ya UKIMWI zinajumuisha;


  • Kupoteza uzito kwa kasi

  • Homa za mara kwa mara

  • Kutokwa jasho jingi wakati wa usiku

  • Kuchoka sana mwili kusiko na sababu muhimu

  • Kuvimba kwa tezi limfu kwenye shingo, kwapa na maeneo ya kinena

  • Kuharisha kwa muda mrefu na kwa kujirudia rudia

  • Kuugua magonjwa ya mfumo wa mapafu kama nimonia

  • Vidonda kwenye midomo, na maeneo ya haja kubwa

  • Kupoteza uzito zaidi ya asilimia 10 ya uzito wa awali

  • Kupotezakumbukumbu, mdongo wa mawazo

  • Dalili zingine za uharibifu wa mfumo wa neva


Hatua ya nne ya UKIMWI


Hii ni hatua mbapo mgonjwa anapata dalili kali zaidi ya zile za hatua ya tatu na hata kupata saratani. Hatua hii huchukua miezi michache kabla ya mgonjwa kupatwa na umauti hata akianza dawa za ART, endapo atafanikiwa kuishi ndani ya mwaka mmoja wa kwanza, asilimia 95 ya wagonjwa hufa ndani ya miaka mitano. Dalili hizo ni;


  • Kukonda sana kiasi cha kuonekana kwa mifupa

  • Nimonia ya PCP

  • Nimonia ya kujirudia rudia

  • Kifua kikuu cha nje ya mapafu

  • Maambukizi ya toxoplasmosis

  • Saratani ya kaposis(Kuota upele mgumu wenye rangi ya pinki, kahawia au zambarau maeneo mbalimbali ya mwili)

  • Maambukizi ya fangasi kwenye umio

  • Fistula

  • Saratani ya tezi limfu

  • Na magonjwa mengine


Rejea za mada hii


  1. HV. Gov. Symptoms of HIV. https://www.hiv.gov/hiv-basics/overview/about-hiv-and-aids/symptoms-of-hiv. Imechukuliwa 21.06.2021

  2. Jennifer L. Weinberg, et al. The WHO Clinical Staging System for HIV/AIDS. https://journalofethics.ama-assn.org/article/who-clinical-staging-system-hivaids/2010-03#. Imechukuliwa 21.06.2021

  3. INTERIM WHO CLINICAL STAGING OF HIV/AIDS AND HIV/AIDS CASE DEFINITIONS FOR SURVEILLANCE. https://www.who.int/hiv/pub/guidelines/clinicalstaging.pdf. Imechukuliwa 21.06.2021

  4. Aids Map. The stages of HIV infection. https://www.aidsmap.com/about-hiv/stages-hiv-infection. Imechukuliwa 21.06.2021

  5. Tanzania standard treatment guideline (STG) toleo la 2021



Kuhusu kundi

Uliza swali pamoja na kusoma majibu ya maswali yaliyoulizwa,...

bottom of page