Kikohozi cha ghafla kinachodumu muda mrefu, shida ni nini?
Swali la msingi
Habari samahani mimi huwa napata tatizo za kikohozi cha ghafra kikavu sana kinaumiza koo, naweza kohoa hata dakika 30 mfululizo baada ya hapo kinaisha kabisa narudi hali ya kawaida. Shida inaeza kuwa nini?
Majibu

Kutokana na maelezo yako, kikohozi cha ghafla, kikavu, kinachoendelea kwa muda mrefu (hadi dakika 30) na kisha kuisha ghafla kinaweza kusababishwa na mambo kadhaa, kama vile:
Visababishi vya kikohozi cha ghafla kinachodumu muda mrefu
Mzio
Kikohozi cha ghafla kinaweza kusababishwa na mzio wa vumbi, harufu kali, poleni, au vinywaji na vyakula aina fulani ambavyo vikigusa koo hulikereketa na kupelekea kikohozi kikavu kinachodumu kwa mdua mrefu.
Pumu ya Kikohozi
Hali hii husababisha kikohozi kikavu bila dalili zingine za kawaida za pumu kama kubanwa kwa kifua na kutoa miruzi wakati wa kupumua.
Kucheua tindikali
Asidi kutoka tumboni inaweza kusafiri hadi kwenye koo na kusababisha mkereketo unaopelekea kikohozi cha ghafla, hasa baada ya kula au kulala.
Msisimko mkali wa neva kwenye koo
Baadhi ya watu wengine huwa na neva zinazosisimuka kirahisi na hivyo huchochea kikohozi ghafla kisichodhibitika.
Kukauka kwa koo au hewa kavu
Hali ya hewa kavu au kutumia kiyoyozi kunaweza kukausha koo na kusababisha kikohozi kikavu.
Maambukizi ya virusi au bakteria
Ingawa maambukizi ya kawaida huja na dalili zingine kama homa, yanaweza pia kusababisha kikohozi cha muda mfupi.
Je, unatibu vipi kikohozi cha muda mrefu nyumbani?
Ikiwa kikohozi chako hakihusiani na maambukizi na kinatokea mara chache, unaweza kutumia njia za nyumbani. Lakini kama kinajirudia mara kwa mara, ni vyema kuonana na daktari kwa uchunguzi zaidi.
Wakati unapanga kuonana na daktari haraka kwa uchunguzi na tiba, unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kudhibiti dalili baada ya kushauriana na daktari wako kama njia hiyo inafaa kulingana na afya yako;
Unywaji wa maji ya moto
Kunywa maji ya uvuguvugu au chai ya tangawizi, asali, na ndimu kunaweza kusaidia kutuliza koo. Kama ksiababishi ni Kucheua tindikali, ndimu na tangawizi vinaweza kusababisha tatizo kuwa kubwa zaidi.
Matumizi ya asali
Kumeza kijiko cha asali kabla ya kulala au pale kikohozi kinapojitokeza kunaweza kusaidia kupunguza kikohozi.
Mvuke wa maji moto
Kuoga maji ya moto au kuvuta mvuke wa maji yenye majani ya eucalyptus au mafuta ya peppermint kunaweza kusaidia kupunguza kikohozi.
Epuka vichochezi
Epuka mazingira yenye vikereketa vya koo na mfumo wa hewa kama harufu kali, moshi wa kuni au sigara, au hewa kavu na chafu.
Kutumia lozenges au peremende za koo
Pipi kifua hizi zinaweza kusaidia kutuliza koo na kupunguza hisia ya kukohoa.
Lala ukiwa umenyanyua kichwa juu ya usawa wa moyo
Kama una tatizo la kucheua tindikali, kulala kwakutumia mto kunaweza kukusaidia kupunguza dalili hii ya kikohozi.
Wakati gani wa kuonana na daktari unapokuwa na kikohozi hiki?
Onana na daktari haraka ikiwa kikohozi kinaendelea kwa muda mrefu au kinaanza mara kwa mara na kuambatana na dalili zifuatazo;
Kupumua kwa shida au kifua kubana
Unakohoa damu au kupata kikohozi cha usiku kisichoisha.
Kama unahisi dalili za ugonjwa wa kucheua tindikali kama kiungulia cha mara kwa mara.
Rejea za mada hii:
Mayo Clinic. (2023). Chronic Cough: Symptoms, Causes, and Treatment. Retrieved from https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/chronic-cough/symptoms-causes/syc-20351575
American Lung Association. (2023). Understanding Chronic Cough. Retrieved from https://www.lung.org/lung-health-diseases/lung-disease-lookup/chronic-cough
National Health Service (NHS). (2023). Cough: Causes, Symptoms, and Treatment Options. Retrieved from https://www.nhs.uk/conditions/cough/
Cleveland Clinic. (2023). Dry Cough: Causes, Diagnosis, and Home Remedies. Retrieved from https://my.clevelandclinic.org/health/diseases/17754-cough
Harvard Health Publishing. (2023). Why You Keep Coughing: Common Causes and Solutions. Retrieved from https://www.health.harvard.edu/diseases-and-conditions/why-you-keep-coughing