Jinsi ya kufahamu kama utoaji mimba kwa dawa umefanikiwa
Maelezo ya Msingi:
Nimetumia dawa ya kutoa mimba ila nina mashaka siamini kua iyo mimba imetoka na nilikua nataka kama haijatoka uniambie njia nyingine ya kutoa au unishauri nifanyaje.
Majibu

Ninaelewa mashaka yako, na ni muhimu kuhakikisha afya yako iko salama. Baada ya kutumia dawa za kutoa mimba, ni muhimu kufuatilia dalili na ishara zinazoonyesha kama mchakato umefanikiwa. Hata hivyo, dalili hizi peke yake hazithibitishi kuwa mimba imetoka kikamilifu. Kwa hiyo, inashauriwa kufanya uchunguzi wa kiafya baada ya wiki chache ili kuhakikisha kuwa hakuna mabaki ya mimba yaliyosalia. Ikiwa vipimo vitaonyesha uwepo wa homoni za ujauzito, au ikiwa dalili za ujauzito zinaendelea, ni muhimu kuwasiliana na mtoa huduma wa afya kwa uchunguzi zaidi na ushauri. Kama umetumia dawa ya kutoa mimba lakini hauna uhakika kama imetoka kabisa au la, maelezo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata uelewa.
Dalili zinazoashiria ufanisi wa dawa ya utoaji mimba
Baada ya kutumia dawa ya kutoa mimba kama mifepristone na misoprostol, dalili zinazotarajiwa kuonekana na kuwa ishara ya mimba inatoka/imetoka ni pamoja na:
Maumivu ya tumbo kama la hedhi au makali zaidi
Kutokwa na damu nyingi kuliko hedhi ya kawaida, na inaweza kuchanganyika na mabonge.
Kupotea au kupungua na kuisha kwa dalili za ujauzito kama kichefuchefu na matiti kujaa siku chache baada ya kutumia dawa.
Dalili zinazoashiria mimba haijatoka kikamilifu au imebaki
Ukipata dalili hizi ni ishara kuwa mimba haijatoka au kuna masalia yamebakia;
Kutokwa na damu kidogo sana au damu kukata haraka sana.
Dalili za ujauzito kuendelea baada ya siku kadhaa.
Kuhisi uvimbe tumboni au maumivu makali yasiyoisha.
Homa au uchafu wenye harufu mbaya (inaweza kuwa ishara ya maambukizi kwenye kizazi).
Nini unachopaswa kufanya?
Onana na daktari- haraka kwa mazungumzo ya kitaalamu na ushauri
Pima Ujauzito- Baada ya siku 10-14, tumia kipimo cha ujauzito kwa njia ya mkojo ili kuona kama mimba bado ipo. Kipimo cha damu cha homoni ya ujauzito (hCG) kinaweza kutoa majibu ya uhakika haraka zaidi.
Fanya kipimo cha Utrasound– Ikiwa una wasiwasi, tembelea hospitali ili daktari afanye uchunguzi wa kizazi kuhakikisha kama mfuko wa mimba upo safi na hakuna masalia ya mimba.
Njia nyingine za utoaji mimba
Ikiwa mimba bado ipo au haijatoka kikamilifu, daktari wako anaweza kukushauri mambo yafuatayo;
Kutumia dawa nyingine za kusaidia kutoa masalia ya mimba (kama misoprostol, chini ya usimamizi wake).
Upasuaji mdogo wa kufyonza masalia ya mimba katika kizazi, njia hii ni salama na yenye ufanisi mkubwa wa kusafisha mfuko wa uzazi.
Ushauri muhimu
Usijaribu kutumia dawa nyingine bila mwongozo wa daktari ili kuepuka hatari za kutokwa na damu nyingi au maambukizi.
Pata msaada wa kitaalamu haraka ikiwa unahisi dalili mbaya kama maumivu makali, homa, au kutokwa na damu kupita kiasi.
Kutokwa na damu baada ya kutumia dawa za kutoa mimba hakumaanishi kuwa mimba imetoka kikamilifu; uchunguzi wa kiafya unahitajika kuthibitisha hilo.
Rejea za mada hii:
Planned Parenthood. How can I tell if my abortion worked? What are the signs of pregnancy after you’ve had an abortion? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. inapatikana: https://www.plannedparenthood.org/blog/how-can-i-tell-if-my-abortion-worked-what-are-the-signs-of-pregnancy-after-youve-had-an-abortion. Imechukuliwa 02.04.2025
Aid Access. How do you know if you have a continuing pregnancy? [Internet]. 2023 [cited 2025 Apr 2]. Inapatikana: https://aidaccess.org/en/page/463/how-do-you-know-if-you-have-a-continuing-pregnancy
Mayo Clinic. Medical abortion: What you need to know [Internet]. 2023 [cited 2025 Apr 2]. Inapatikana: https://www.mayoclinic.org/tests-procedures/medical-abortion/about/pac-20394687. Imechukuliwa 02.04.2025
National Health Service (NHS). Abortion: What happens? [Internet]. 2024 [cited 2025 Apr 2]. Inapatikana: https://www.nhs.uk/conditions/abortion/what-happens/. Imechukuliwa 02.04.2025