top of page

Majadiliano na Wataalamu

Public·804 members

Upara wa jinsia zote

Neno 'Upara wa jinsia zote' katika makala hii imetumika kumaanisha 'tatizo la upara kwa wanawake na wanaume'


Upara ni nini?

Upara ni tatizo la kupoteza nywele za kichwa, hujulikana kwa jina jingine la kitiba kama 'alopesia', na hutokea kwa wanaume na wanawake.


Kuota upara ni tatizo linalofahamika sana kwa wanaume na huchukuliwa kama mabadiliko ya kawaida kwao haswa katika umri mkubwa, linapotokea kwa wnawake huwa linawapelekea kupata msongo wa mawazo kwa sababu ya kubadilika kwa mwonekano. Tafiti zinaonyesha, kuota upara huambatana na kiwango kikubwa cha homoni ya 'testosterone' kwenye shina linalozalisha nywele lakini hata hivyo kiwango kiwango kilicho kwenye damu huwa cha kawaida.

Kuna aina mbili za tatizo la upara ambazo ni, upara wa kichwa kizima na upara unaoathiri eneo dogo la kichwa, aina zote huwapata watu wa jinsia zote. Upara unaweza kuota sehemu ndogo ya kichwa au kichwa kizima.

Visababishi vya upara


Ni jambo la kawaida binadamu kupoteza nywele kila siku haswa wakati wa kuchana na kadhalika, kupotea huku kwa nywele huwa hakuleti upara kwa sababu nywele zingine huota kutoka kwenye shina la nywele linalozaa. Hata hivyo kuna baadhi ya visababishi ambavyo hupelekea nywele zinazo katika kutoota tena na kupelekea kuonekana kwa upara kuonekana. Sababu hizo ni pamoja na.

Kurithi jeni za upara


Upara wa wanaume hurithiwa kwenye jeni zinazotoka kwa mama na baba, mara nyingi upara huu hutokea jinsi umri unavyoongezeka kwa mwanaume au mwanamke.

Mabadiliko ya homoni mwilini na magonjwa


Kuna aina kadhaa ya magonjwa na hali zinazoweza kupelekea kupoteza nywele kwa muda mfupi au moja kwa moja. Mabadiliko ya homoni yanayoweza kusababishwa na


Magonjwa yanayosababisha upara ni;

  • Maambukizi ya minyoo kichwani na

  • Tatizo la kuvutika kwa nywele

Matumizi ya dawa aina Fulani


Mfano wa dawa zinazosababisha upara ni;

  • Dawa za kutibu saratani

  • Dawa za kutibu matatizo ya maungio ya mwili

  • Dawa za kutibu gauti

  • DAwa za kutibu magonjwa ya moyo na shinikizo la damu

Matibabu kwa njia ya mionzi


Matibabu haya husababisha nywele kuwa nyembaba kwa mienzi kadhaa na kisha kunyonyoka na kuacha vipara. Nywele hupotea kwa kipindi fulani cha matibabu na baadae hurejea miezi kadhaa baada ya matibabu kusimama.

Kuwa na kipindi kigumu cha mawazo


Watu wengi hupoteza nywele kipindi wakiwa na mawazo mengi kuhusu mambo kadhaa katika maisha yao, mfano kufukuzwa kazi uliyokuwa unaitegemea, kuachwa na mpenzi, kupoteza pesa au kitu cha thamani, kufiwa n.k wakati huu nywele huwa nyembamba na kunyonyoa na kuacha upaa, tatizo la kupoteza nywele linazosababishwa na hali hii huwa ni la muda tu.

Utengenezaji wa nywele


Baadhi ya staili zinazopelekea kuvutwa sana kwa nywele upande mmoja ili kutengeneza mwonekano unaotaka (mfano mabutu yanaacha nafasi kati ya butu moja na jingine), staili hizi huacha eneo kwenye kichwa lisilo na nywele na kuharibu mashina hayo ya nywele wa kuvita sana. Kutumia mafuta ya moto kwa ajili ya kutengeneza nywele zako kunaweza sababisha michomo kwenye gozi ya kichwa na kuharibu mashina ya nywele na hivyo kupelekea nywele kupotea milele eneo lilliloathiriwa.

Vihatarishi vya kupata upara

Kupoteza nywele eneo kubwa la kichwa huongezeka endapo una;


  • Mvurugiko wa homoni ( vichochezi) mwilini ( homon imbalance)

  • Msongo wa mwilini kutokana na kufanyiwa upasuaji au kuugua ugonjwa

  • Homa kali inayozidi nyuzi joto za selishiaz 39, inayoweza sababishwa na homa ya mbu (malaria), maambukizi ya influenza, homa ya brusela na pia kwenye homa inayosababishwa na magonjwa ya michomo kutokana na kinga za mwili tumboni.

  • Utapiamlo- huambatana na kupungua kiwango cha protini kwenye damu na kuleta upaa

  • Upungufu wa madini chuma mwilini na kiwango kidogo cha protini kwenye damu huchangia lakini sio sababu kuu

  • Mgonjwa ya kurithi

  • Mabadiliko ya homoni kama kiwango cha juu cha homoni ya Thyroid, kiwango cha chini cha homoni zinazotolewa na pituitary na Kisukari aina ya kwanza

  • Matumizi ya dawa, dawa za saratani, dawa za kuyeyusha damu, dawa za kushusha kinga za mwili na baadhi ya dawa za kushusha homoni ya thyroid, Ciclosporin

Namna ya kujikinga kupata upara

Mara nyingi tatizo la upara haliwezi kuzuilika kama ni la kurithi. Hata hivyo unaweza kufanya mambo yafuatayo ili kujikinga kupoteza nywele nyingi zaidi

  • Zuia staili za kuvuta au kubana sana nywele

  • Zuia kuvuta, kuweka msuguano mkali kwenye nywele

  • Zihudumie nywele zako taratibu na zuia kuzivuta sana kwa brashi au kitana. Tumia kitana au chanuo lenye meno makubwa kuzuia kuvuta nywele sana

  • Zuia kuzihudumia nywele kwa kutumia rola za moto, kuzipiga pasi na kuziwekea mafuta ya moto

  • Zuia kutumia dawa zinazosababisha upara

  • Zuia nywele zako zisipigwe mwanga wa jua mara kwa mara

  • Acha kuvuta sigara

  • Tumia kofia ya kupooza kichwa endapo unatumia dawa za saratani

Matibabu ya upara kwa wanaume na wanawake

Matibabu ya upara hulenga kisababishi, mfano kama nywele zimepotea kwa sababu ya matatizo ya homoni mgonjwa hupewa homoni mbadala au kama ni kwa sababu ya msongo, ushauri wa kuukabiliana na msongo utatolewa na kisha tatizo litaisha.


​Upara kwa wanaume hukubalika na baadhi ya makabila huwapa heshima wenye upara kuwa wana hekima, hivyo mara nyingi huwa hawahitaji matibabu.


Dawa zinazootesha nywele


Dawa zinazopatikana na zinazotumika kuzuia kuota kwa upara na kuongeza uotaji wa nywele mfano wake ni minoxidil. Dawa hii hutumika kwa kupaka kila siku. Ufanisi wa dawa hii ni wa asilimia 50, yaani kati ya wanaume 100 waliopata upara, wanaoweza kuota nywele tena kama awali ni wanaume 50.


Kuna dawa zingine za kutibu upara?


Ndio! Wataalamu wa tiba asili wameweza kuvuna viini mbalimbali venye uwezo wa kuamsha mashina ya nywele kutengeneza nywele. Dawa hizo zinazopatikana katika fomu ya mafuta na maji, hufanya kazi kwa watu walikuwa na nywele kabla ya kupata upara.


Viinirishi na dawa mbadala ambazo zimefanyiwa tafiti na kuonekana zina uwezo wa kutibu upara kwa kipindi cha muda mbalimbali zimeorodheshwa hapa chini;


  • Amino acid ya L cysteine

  • Mafuta ya Capsaicin

  • Curcumin ( Jamii nyingine ya tangawizi )

  • Juisi ya kitunguu

  • Mafuta kutoka viumbe wa baharini

  • Mafuta ya kahawa

  • Mafuta ya kahawa

  • Mafuya ya capsacin

  • Mafuta ya tangawizi

  • Mafuta ya mbegu za boga

  • Mafuta ya mbegu za saw

  • Melatonin

  • Procyanidin

  • Vitamin B7 (biotin),

  • Vitamin D,

  • Vitamin E,

  • Zinc


Ufanisi wa tiba mbadala kwenye matibabu ya upara kwa wanawake na wanaume


Dawa mbadala zilizoorodheshwa hapo juu huwa na uwezo wa kutibu tatizo la upara kwa muda tofauti, kuanzia wiki 3 na kuendelea. Ikitegemea aina ya upara na matibabu yaliyotumika, baadhi ya watu, tatizo la upara hujirudia baada ya muda wa wiki au miezi kadhaa kupita na wengine hupotea kabisa


Unashauriwa kuongea na daktari wako kwanza kuhusu aina ya dawa hizi mbadala kama zinafaa kwa afya yako au la, kama zina mwingiliano na dawa unazotumia, kiasi gani utumie na kwa muda gani ili upate matokeo unayotaka. Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa maswali na majibu kupitia kitufe cha ‘mawasiliano yetu’ chini ya tovuti hii


Matibabu ya upasuaji


Mbali na matibabu ya kutumia dawa, baadhi ya wagonjwa huchagua kufanyiwa matibabu ya kuotesha mashina mapya ya nywele kichwani. Upasuaji huu unaweza kuchukua mashina ya nywele kutoka sehemu za mwili au kichwa ambapo nywele zinaota kisha kuzipandikiza sehemu ambazo hakuna nywele. Upasuaji huwa wa hatua zaidi ya moja kabla ya kupata matokeo ambayo unayataka.


Kupata majibu zaidi ya tatizo la upara kwa wanawake, tatizo la upara kwa wanaume, matibabu ya upara kwa wanaume na wanawake, soma zaidi kwa kubofya hapa


Rejea za mada hii;


  1. Hutchingson text book of internal medicine chapisho la 20

  2. ABCs of dermatology toleo la 4, 2003

  3. Absolute dermatology iliyopitiwa na Hugh Morris Gloster, na wengine

  4. C. Herbert Pratt, et al. Alopecia areata. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5573125/. Imechukuliwa 11.07.2021

  5. McElwee KJ, et al. Comparison of alopecia areata in human and nonhuman mammalian species. Pathobiology : journal of immunopathology, molecular and cellular biology. 1998;66:90–107. 2. Xing L, et al. Alopecia areata is driven by cytotoxic T lymphocytes and is reversed by JAK inhibition. Nat Med. 2014;20:1043–1049. doi: 10.1038/nm.3645.

  6. Duvic M, et al. The national alopecia areata registry-update. J Invest Dermat Symp Proc. 2013;16:S53.

  7. Petukhova L, et al. Genome-wide association study in alopecia areata implicates both innate and adaptive immunity. Nature. 2010;466:113–117.

  8. Shi Q, et al. Health-Related Quality of Life (HRQoL) in alopecia areata patients-a secondary analysis of the National Alopecia Areata Registry Data. J Invest Dermat Symp Proc. 2013;16:S49–50.

  9. Anna-Marie Hosking, et al. Complementary and Alternative Treatments for Alopecia: A Comprehensive Review. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6388561/. Imechukuliwa 11.07.2021

205 Views

Kuhusu kundi

Uliza swali pamoja na kusoma majibu ya maswali yaliyoulizwa,...

bottom of page