top of page

Mwandishi:

Mhhariri

Dkt. MangwellaS, MD

Dkt. Lugonda B, MD

Jumapili, 18 Julai 2021

Kuvunjika fupakola

Kuvunjika fupakola

Kuvunjika kwa fupakola ni aina ya jeraha linalotokea sana kwa watoto na vijana wadogo. Fupakola ni mfupa unaounga mkono kwenye sehemu ya juu ya fupatiti.


Miongoni mwa visababishi vikuu vya kuvunjika kwa fupakola ni ajali ya kunguka wakati umesambaza mikono, kuangukia bega au kupata ajali ya gari.


Vichanga mara nyingi huvunjika fupakola wakati kuzaliwa endapo njia ya uzazi ni ndogo, mtoto ni mkubwa sana, kujifungua kwa kuvutwa na vifaa au kukwama kwa bega la mtoto wakati wa kujifungua.


Unapaswa kutafuta msaada wa huduma za afya mara upatwapo na tatizo hili. Hata hivyo mara nyingi mfupakola uliovunjika hupona wenyewe bila kufanyiwa matibabu endapo hautajongeshwa na kuupa subira.


Utatakiwa kuukanda kwa barafu na kutumia dawa za maumivu au kuufunga mkono ili usijongee kuharakisha uponyaji.


Kama mfupa umevunjika vibaya, utahitaji upasuaji ili kuufanya uunge haraka na katika anatomia yake ya kawaida.


Kuvunji kwa fupakola hufahamika kwa majina mengine ya 'Kuvunjika clavicle' na 'Kuvunjika kwa klaviko'


Dalili


Dalili za kuvunjika kwa fupa kola ni pamoja na;


  • Maumivu ya mkono yanayoongezeka wakati wa kujongea kwa bega

  • Uvimbe

  • Maumivu sehemu iliyovunjika endapo pataguswa

  • Kuvia kwa damu sehemu mfupa ulipo

  • Kuhisi sauti ya kusagana kwa mifupa wakati wa bega linajongea

  • Kupoteza uwezo wa kujongesha bega

  • Kukakamaa kwa bega

  • Kwa vichanga kushindwa kujongea kwa mkono siku kadhaa baada ya kuzaliwa

  • Kichanga kulia anapoguswa mkono uliovunjika


Wakati gani uonane na daktari haraka?


Ukiona dalili yoyote ya kuvunjika fupakola unapaswa kawasiliana na daktari au kufika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ushauri na tiba mara moja.


Visababishi


Visababishi vikuu vya kuvunjika fupakola ni;


  • Kuangukia bega au kuangukia mkono uliosambaa nje

  • Kupigwa na kitu kwenye bega

  • Ajali ya gari, pikipiki au baiskeli

  • Majeraha wakati wa kichanga anapita kwenye njia ya uzazi( kwa vichanga)


Vihatarishi


Vihatarishi vya kuvunjika fupa kola ni;


  • Kuwa na umri chini ya miaka 20

  • Kuwa mzee


Fupakola hukomaa mara nyingi mtu anapofikia umri wa miaka 20, hii ndio maana watoto na vijana wadogo wapo kwenye hatari ya kuvunjika mfupa huu. Baada ya kuvuka umri wa miaka 20, hatari hupungua lakini huongezeka tena wakati wa uzeeni.


Madhara


Fupakola mara nyingi hupona bila madhara yoyote kwa watu wengi, hata hivyo baadhi ya watu wanaweza kupata madhara yafuatayo;


  • Majeraha ya mishipa ya damu na fahamu

  • Kuunga vibaya au kuchelewa kuunga

  • Uvimbe kwenye bega

  • Michomo kinga kwenye maungio ya fupakola


Majeraha ya mishipa ya damu na fahamu

Sehemu zilizochongoka za mfupa uliovunjika zinaweza kutoboa au kukata mishipa ya damu na fahamu hivyo kuleta dalili mbalimbali za kuhisi baridi, ganzi kwenye mkono au kuvilia kwa damu ndani ya bega.


Kuunga vibaya au kuchelewa kuunga

Kama mfupa umevunjika vibaya, unaweza kuchelewa kuunga au kuunga vibaya. Kuunga vibaya kunaweza kuleta mwonekano tofauti wa anatomia ya bega mfano mfupa kuwa mfupi kuliko ulewa mkono mwingine.


Uvimbe wa bega

Uvimbe hutokea sehemu ambayo vipande vya mifupa vimeungana, hii ni moja ya hatua za kuunga kwa mfupa. Baada ya miaka kadhaa, uvimbe huu unaweza kuisha kabisa kwa watu walio wengi au kubakia kwa baadhi ya watu.


Michomo kinga kwenye maungio ya fupakola

Hii hutokea sana kama fupakola umevunjika maeneo ya karibu unapounganika na fupatiti au fupabapa (skapula). Michomo hii huambatana na maumivu makali ya maungio ya bega wakati wa kujongea mkono na uvimbe.


Vipimo na utambuzi


Baada ya kufika hospitali, utachukuliwa historia ya tatizo na kufanyia uchunguzi wa mwili kwenye bega lililoathirika kisha utafanyiwa vipimo kati ya;


  • X-ray ya bega

  • CT scan


Matibabu


Msingi wa matibabu ya fupakola uliovunjika ni kupunguza mjongeo wa bega lililovunjika, kufanya hivi huzuia kutonesha, kuharibu harakati za uponyaji na huharakisha mfupa kuunga. Unaweza kufungwa na kitambaa au kupewa kivalo maalumu cha kushikiria mkono wako ili kupunguza mjongeo.

Kwa vichanga ambao wamevunjika wakati wa kuzaliwa, mara nyingi hawavalishwi chochote, mzazi unatakiwa kuwa makini tu na mkono uliovunjika na kudhibiti maumivu tu.


Ni kwa muda gani utatakiwa kutojongesha mkono uliovunjika?

Muda wa kutojongesha mkono au kuvaa kivalo cha kubeba mkono hutegemea aina na ukubwa wa jeraha la kuvunjika. Hata hivyo mara nyingi kwa watoto fupakola huunga baada ya wiki tatu hadi 6 , wakati watu wazima huchukua wiki 6 hadi 12. Baada ya fupakola kuunga unaweza kuacha kutumia kivalo cha kushikiria mkono.


Matibabu ya dawa

Ili kupunguza maumivu na uvimbe, daktari anaweza kukupa dawa za kupunguza maumivu jamii ya nakotiki kwa muda wa siku chache tu. Kisha utaendelea kusubiria mkono upone wenywe. Utahitajika kupunguza mijongeo ya mkono ulioathirika ili kupunguza maumivu. Dawa jamii ya NSAIDS kama Diclofenac, aspirin hazitumiki mara nyingi kwa kuwa huongeza hatari ya kuvia kwa damu kwenye mishipa iliyopasuka.


Mfano wa dawa jamii ya nakotiki ni;


  • Codeine

  • Oxycodone

  • Hydrocodone

  • Tramadol

  • Morphine

  • Hydromorphone

  • Fentanyl

  • Carfentanil


Matibabu kwa vichanga na watoto wadogo

Mara nyingi vjichanga hawahitaji kufanyiwa chochote kile na mdupa hupona ndani ya wiki 3 hadi 6. Unaweza kufundishwa kubana mkono uliovunjika kwa kitambaa au nguo aliyovaa mbele ya mwili ili kuzuia kujongea sana wakati unasubiri mfupa upone wenywe (Angalia kwenye picha namba tatu kwa mfano)


Epuka mambo yafuatayo mpaka baada ya wiki 4 hadi 6


  • Kunyanyua mkono wenye shida juu ya usawa wa bega

  • Kuweka mgandamizo au mjongeo kwenye bega lililovunjika

  • Kubebesha uzito kwenye mkono wa bega lililovunjika


Tiba upasuaji

Kama fupakola umevunjika na kuchomoza nje ya mwili au vipande vimetengena sana au umevunjika kwenye vipande vingi, utahitaji upasuaji ili kuondoa vipande, kukutanisha mifupa kwa kuwekewa vyuma ndani au nje ya mfupa.


Tiba mazoezi

Baada ya kupata matibabu ya awali, unaweza kufundishwa mazoezi madogo ya kufanya ili kuzuia kukakamaa kwa mkono. Mazoezi mengine pia utafundishwa kuyafanya wakati mfupa umeshaunga. Unashaurwa usifanye mazoezi ambayo yanaongeza mjongeo kwenye mfupa uliovunjika hivyo kuchelewesha kupona.


Matibabu ya nyumbani

Wakati upo nyumbani unaweza kufanya mambo yafutayao ili kupunguza uvimbe na maumivu pasipo dawa na kuharakisha mfupa kupona;


  • Kukanda eneo lililoathirika kwa barafu kwa muda wa dakika 20 hadi 30siku mbili hadi 3 za kwanza toka mfupa umevunjika

  • Kula mlo kamili kutoka kwenye makundi matano ya chakula

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

26 Oktoba 2021 18:07:59

Rejea za mada hii:

1. American Academy of Orthopaedic Surgeons. Clavicle fracture (broken collarbone). http://orthoinfo.aaos.org/topic.cfm?topic=A00072. Imechukuliwa 18.07.2021

2. Hatch RL, et al. Clavicle fractures. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 18.07.2021

3. Peters MDJ. Surgical versus conservative interventions for treating broken collarbones in adolescents and adults. Orthopedic Nursing. 2014;33:171.

4. McKee-Garrett TM. Neonatal birth injuries. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 18.07.2021

5. The Big List of Narcotic Drugs. https://americanaddictioncenters.org/the-big-list-of-narcotic-drugs. Imechukuliwa 18.07.2021

6. Andreas F Mavrogenis, et al. Birth fracture of the clavicle. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22123402/. Imechukuliwa 18.07.2021

7. B Kaplan , et al. Fracture of the clavicle in the newborn following normal labor and delivery. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/9849706/. Imechukuliwa 18.07.2021

bottom of page