Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Jumanne, 29 Juni 2021

Amibiasis
Amibiasis ni ugonjwa wa tumbo unaosababishwa na protozoa asiyeonekana kwa macho mwenye jina la Entamoeba histolytica, au kifupi E. histolytica. Watu wengi hufahamu amiba kama amibiasis lakini si kweli kwa kuwa amiba ni kimelea na amibiasis ni ugonjwa wa tumbo unaosababishwa na amiba.
Makala hii imezungumzia zaidi kuhusu ugonjwa wa amibiasis. Kupata maelezo zaidi kuhusu kimelea amiba ingia kwenye makala sehemu nyingine ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC
Dalili za amibiasis
Baadhi ya watu huwa hawaonyesi dalili kali za amibiasis. Endapo zitatoke hutokea kati ya wiki 2 hadi 4 toka mtu amepata maambukizi. Baadhi ya watu hata hivyo huanza kupata dalili siku chache na ni asilimia 10 hadi 20 tu ya wagonjwa wenye maambukizi huonyesha dalili ambazoni kati ya zifuatazo;
Kupata kinyesi laini au kuharisha
Kunyonga kwa tumbo kunakopelekea maumivu ya tumbo
Maumivu ya tumbo
Kuharisha damu
kuharisha kinyesi chenye makamasi mengi
Endapo dalili za awali za maambukizi kwenye tumbo hazitatibia, maambukizi hayo yanaweza kuhama na kwenda kwenye sehemu nyingine za mwili na hivyo kuleta dalili katika mfumo uliothiriwa. Soma zaidi kuhusu dalili za amibiasis kwenye makala ya 'dalili za amibiasis' ndani ya tovuti hii.
Wakati gani uwasiliane na daktari haraka unapokuwa na amibiasis?
Wasiliana na daktari wako haraka endapo una dalili zifuatazo;
Kuharisha damu au kinyesi chenye kamasi
Kuharisha kunakodumu zaidi ya wiki mbili
Maumivu ya tumbo
Homa
Kuvimba kwa tumbo
Maumivu ya tumbo upande wa kulia sehemu ya juu au chini ya mbavu upande wa kulia
​
​
Vihatarishi vya kupata amibiasis
Ugonjwa huu tuokea sana kwenye nchi ambazo hazina miundo mbinu mizuri ya maji taka, haswa nchi zinazoendelea.
Vihatarishi vingine ni;
Kusafiri kwenda nchi zenye miundimbinu mibovu ya maji taka
Kushikana mikono na mgonjwa ambaye hajasafisha mikono vema
Kukaa kwenye nchi au maeneo yasiyo na miundombinu mizuri ya maji taka
Kuishi kwenye mazingira yenye miundombinu mibaya ya maji taka kama gelezani n.k
Ngono ya mwanaume kwa mwanaume
Kuwa na kinga ya mwili iliyo chini kutokana na magonjwa mbalimbali
Kisababishi
Amibiasis husababishwa na protozoa E. histolytica, kimelea ambaye huambukizwa kwa kula vyakula au maji yaliyo na kimelea huyu.Kimelea pia anaweza kuingia ndani ya mwili wa binadamu kwa kupenya kwenye ngozi endapo mtu atakanyaga maji yaliyo na kimelea.
Kimelea anaweza kuishi kwenye arithi kwa miezi kadhaa katika fomu ya sisti bila kufa baada ya kutupwa kwa njia ya kinyesi. Sisti za kimelea huweza patikana kwenye udongo, mbolea au maji ambayo yamechafuka na kimelea.
Vyakula pia vinaweza kuchafuka na kimelea endapo vimeandaliwa na mtu mwenye ugonjwa huu ambaye hazingatii usafi wa mikono na hivyo kuambukiza watu wengine wanaokula vyakula hivyo.
Baadhi ya watu hupata maambukizi wakati wa kujamiana ume kwa tundu la haja kubwa au ngono ya mdomo kwa tundu la haja kubwa.
Nini kinatokea amiba anapoingia ndani ya tumbo
Amiba kwenye fomu ya sisti anapoingia kwenye tumbo, hufanya makazi kwenye kuta za utumbo. Kifuko hupasuka na kutoa kimelea kinachoitwa trophozoiti. Kimelea hujizalia kisha kusambaa kwenye utumbo mdogo na mpana. Kwa vile kimelea anaweza kujichimbia kwenye utumbo, baadhi ya wakati mtu mwenye maambukizi hupata dalili ya kuharisha damu, michomo kwenye utumbo mpaka ( kolaitiz) na kuharibiwa kwa tishu za utumbo au kusafiri kwenda kwenye damu na kusababisha maambukizi mapya kwenye Ini na kuleta jipu la amiba au kwenda kwenye mapafu, moyo na ubongo.
Mgonjwa anapojisaidia, kinyesi huwa na vimelea hivyo vinavyoweza kusambaa vyanzo vya maji vilivyo karibu na shimo la choo alichojisaidia mgonjwa au chanzo cha maji.
Vipimo na utambuzi wa amibiasis
Daktari atatambua ugonjwa ulionao kwa kukuuliza historia ya tatizo lako na dalili ulizonazo kabla ya kuamua kufanya vipimo. Endapo kuna uhaja wa kufanya vipimo ili kutofautisha au kuthibitisha amibiasis dhidi ya magonjwa mengine vipimo vifuatavyo vitaagizwa kufanyika;
Kipimo cha stool analysis
Kipimo cha kazi za ini
Kipimo cha ultrasound au CT scan ya tumbo
Kipimo cha kolonoskopi
Enzyme immunoassay (EIA)
Indirect hemagglutination (IHA)
Matibabu
Matibabu ya amibiasis huhusisha matumizi ya dawa metronidazole kwa muda wa siku 10 au zaidi kulingana na tatizo lako, unaweza kupewa dawa zingine pia na daktari wako kutegemea dalili zingine ulizonazo
Endapo kuna ogani imetobolewa na kimelea kama vile utumbo au ogani nyingine, matibabu yatahusisha pia kufanyiwa upasuaji. matibabu mengine kama upasuaji ili kuondoa vimelea hao
Madhara
Endapo matibabu yasipofanyika mapema, mgonjwa anaweza kupata madhara ambayo yanaweza kuwa kati ya yafuatayo;
Kuvimba kwa utumbo mpaka
Amoebomafistula kati ya uke na njia ya haja kubwa
Kuoza kwa utumbo
Kupasuka kwa peritoneum
Kusambaa kwa usaha na vimelea kwenye sehemu zingine za mwili kama ini, ubongo n.k
Kufanyika kwa jipu la amiba kwenye ubongo
Kufanyika kwa jipu la amiba kwenye ini
Kupasuka kwa utumbo
Kutokwa na damu njia ya haja kubwa
Kupata makovu kwenye matumbo
Peritonaitiz
Intusasepsheni
Usaha kwenye peritoniamu
Magonjwa mengine yanayofana na amibiasis
Magonjwa yanayofanana na amibiasis ambayo yanaweza kuleta kuharisha na wakati mwingine kuharisha damu ni;
Shigelosis
Salmonelosis
Compylobacteriosis
Maambukizi ya enteroinvasive na enterohemorrhagic Escherichia coli
Ugonjwa wa inflamatori boweli
Iskemiki kolaitiz
Madhaifu ya mwingiliano wa arteri na veini
Daivetikulaitiz
Namna kinga
Ili kujikinga na ugonjwa wa amibiasis, unapaswa kuzingatia kanuni za kiafya haswa kwa kufanya usafi wa unachokula na mazingira kwa;
Kuosha vema matunda na mboga za majani zinazoliwa bila kupikwa kwa maji safi na salama
Usile matunda na mboga za majani isipokuwa endapo umemenya kabla ya kula
Kunywa maji ya chupa endapo upo sehemu mbali na maji salama
Tumia maji ya kunywa yaliyotiwa iodine na chlorine au yaliyochemshwa
Usinywe maji kutoka kwenye chemichemi au kutumia barafu asili
Usitumie maziwa, maziwa mgando ambayo hayajatakaswa
Usitumie vyakula vya mitaani au vilivyopikwa pasipo kuzingatia kanuni za usafi katika maandalizi.
​​
Majina mengine ya ugonjwa wa amibiasis
Ugonjwa wa amibiasis kwa wengine huufahamu kama
Amiba
Ameba
Amoeba
Ugonjwa wa Amebiasis
Amibiasis
Ugonjwa wa amiba
Ugonjwa wa amibiasis
Ugonjwa wa amoebiasis