Mwandishi:
Mhhariri
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Charles W, MD
Jumatatu, 1 Novemba 2021
U.T.I
Maelezo ya makala hii yamejikita sana kwenye U.T.I inayotokea kwa wanawake, hata hivyo yanaweza kutumika kwa wanaume na watoto pia.
U.T.I ni moja ya ugonjwa unaosumbua sana wanawake, hii inaweza changiwa na mambo mbalimbali ikiwa pamoja na hali ya maumbile ya mfumo wa mkojo. Ugonjwa huu husababishwa sana na bakiteria hata hivyo huweza kusababishwa na vimelea wengine pia. Bakteria wanaosababisha U.T.I huishi maeneo ya njia ya haja kubwa na ngozi inayozunguka karibu na maeneo hayo.
Mfumo wa mkojo wa binadamu
Mfumo wa mkojo wa binadamu umegawanywa katika sehemu kuu mbili, mfumo wa chini wa mkojo unaohusisha kibofu na mrija wa urethra, na mfumo wa juu wa mkojo uliotengenezwa na figo pamoja na mirija miwili ya ureta.
Bakteria wanaosababisha U.T.I wanaweza kukwea kwenye mrija wa urethra kisha kuingia kwenye kibofu cha mkojo, mirija ya ureta na hatimaye kufika kenye figo. Bakteria wanaofika kwenye figo wanaweza kupenya na kuingia kwenye mzunguko wa damu pia.
Mfumo gani wa mkojo huathiriwa zaidi?
Mfumo wa chini wa mkojo huathiriwa sana na bakteria kuliko mfumo wa juu wa mkojo, ingawa maambukizi ya mfumo wa juu hutokea, kutokea kwake ni kwa nadra sana. Vihatarishi kadhaa vinaweza kuchangia kupata maambukizi ya U.T.I katika mfumo wa juu wa mkojo ambavyo ni;
Kisukari
Matumizi ya dawa za kushusha kinga ya mwili
Matumizi ya dawa za kutibu saratani (mionzi na dawa za kumeza au kuwekwa kwenye mishipa)
Kupandikizwiwa figo
Magonjwa mengine sugu
U.T.I ikitokea kwenye mfumo wa juu husababisha madhara makubwa na kama mgonjwa hatapata matibabu mapema huweza sababisha figo kuferi ghafla (kushindwa kufanya kazi) n.k
Kwa nini wanawake wanapata UTI zaidi?
Wanawake wanapata U.T.I mara mara kuliko wanaume kutokana na kuwa na maumbile rafiki, maumbile rafiki humaanisha kuwa na mrija mfupi wa urethra ukilingnaisha na wanaume. Mrija wa urethra kwa wanawake una wastani wa urefu wa sentimita 3 hadi 4 wakati huwa na wastani wa sentimita 18 hadi 20.
Kwanini kuwa na mrija mfupi hupelekea kupata sana U.T.I kwa wanawake?
Mrija mfupi huwapa safari fupi ya kufika kwenye kibofu cha mkojo vimelea wanaosababisha U.T.I. Mrija mrefu kwa wanaume hufanya vimelea wawe na safari ndefu na kabla ya kufika huweza kututana na mkojo kisha kuondolewa wakati wa kukojoa.
U.T.I hutokeaje mara kwa mara?
U.T.I hutokea mara kwa mara kwa wanawake kutokana na kuwa na mrija mfupi pamoja na sababu zingine zinazopelekea kuwa na mfumo dhaifu wa njia ya mkojo.
Mkojo mara nyingi huwa msafi, na na kemikali ya urea yenye uwezo wa kuuwa vimelea vinavyojaribu kuingia kwenye mfumo wa mkojo.
Mwili pia unauwezo wa kuzuia vimelea vya magonjwa kukwea kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mfumo asili wa kinga ulio kwenye mfumo wa mkojo.
Kama mtu ana mfumo dhaifu wa kinga ya mwili au ana maumbile rafiki ya vimelea kukwea kwenye mfumo huu, vimelea hupenya na kuingia kwenye mfumo huu kisha kuzaliana kwenye kibofu kabla ya kuanza kuonyesha dalili.
Mbali na mfumo wa kinga dhaifu, baadhi ya vimelea pia hujibadilisha umbile ili kuepuka mashambulizi kutoka kwenye mfumo wa kinga hivyo kufanikiwa kuingia kwenye kibofu.
Vimelea gani husababisha UTI?
Bakteria Escherician coli (E.coli) husababisha U.T.I kwa asilimia zaidi ya 80 wa wagonjwa wanaopata dalili za U.T.I, kimelea huyu makazi yake ni mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na hupatikana maeneo ya njia ya haja kubwa na ngozi inayozunguka maeneo hayo. Bakteria huyu akihama maeneo yake na kuingia ukeni huweza kuingia kwenye mfumo wa mkojo kisha kusababiasha ugonjwa wa UTI.
Vimelea wengine pia ambao husahaurika sana na wataalamu wa afya kuwa ni chanjo cha UTI ni bakteria Staphylococcus saprophyticus, Proteus species, Klebsiella species, enteroccocus faecalis, enterobactericeae na fungus. Baadhi ya vimelea hawa hawatibikii kwa dawa za kawaida zinazofahamika kutibu UTI.
Baadhi ya vimelea husababisha maambukizi kwenye umri fulani, mfano wanawake wenye umri mdogo hupata U.T.I sana kutokana na bakteria staphylococcus saprophyticus.
Vihatarishi vinavyoweza kufanya upate U.T.I ni vipi?
Sababu zifuatazo zinaweza kukusababisha upate U.T.I
Kuwekewa mpira wa mkojo kwenye njia ya mkojo wakati unapata matibabu hospitalini. Hii hutokea sana kama mpira wa mkojo utakaa kwa muda mrefu bila kutolewa. Kwa hiyo ni vema kubadilishiwa mpira huu baada ya wiki mbili au tatu ili kuzuia kupata U.T.I
Baadhi ya wagonjwa hunyanyua mpira wa mkojo kiasi cha kusababisha mkojo kutoka kwenye kifuko na kuingia kwenye kibofu, hii husababisha kuingiza mkojo mchafu unaoweza kuwa na vimelea na hivyo kusababisha U.T.I ya kibofu cha mkojo.
Pia uchunguzi usio salama wa maumbile ya uke na njia ya haja kubwa unaweza kusababisha kuchukua kimelea kutoka kwenye njia ya haja kubwa au ngozi inayozunguka maeneo hayo kisha kuingizwa ukeni na kwenye mrija wa mkojo.
Kufanya tendo la ndoa kinyume na maumbile (Kuingiza uume kati ya uke na njia ya haja kubwa)
Matumizi ya kizuizi cha shingo ya kizazi kama njia ya uzazi wa mpango huwapa mazingira rafiki bakteria kukua ukeni.
Matumizi ya dawa za kuua manii hupelekea pia kutengeneza mazingira rafiki kwa ukuaji wa bakteria
Wanawake wajawazito na wenye madhaifu ya kuzaliwa ya maumbile ya mfumo wa mkojo , mfano maumbile yanayozuia mkojo kutoka kirahisi
Kufanyiwa upasuaji wa kutoa au kupandikiza figo mpya kisha kuwekwa kwenye dawa za kushusha kinga ya mwili
Mabadiliko ya homon yanayoambatana na athari katika mfumo wa mkojo mfano kuingia koma hedhi ( wakati huu homon estrogen hupungua na via vya mkojo hubadilika)
Tatizo la kucheua kwa mfumo wa mkojo
Kushuka kwa kinga ya mwili kutokana na magonjwa sugu kama kisukari
Dalili za U.T.I
Zipi ni dalili za UTI?
Dalili ya awali ya mtu mwenye UTI ni maumivu wakati wa kukojoa yanayoambatana na;
Kupata haja kali na endelevu ya kwenda kukojoa
Kukojoa mkojo kidogo mara kwa mara wakati wowote
Hisia za kuungua wakati wa kukojoa
Kupata mkojo usio wa kawaida mfano mkojo unaweza kuwa mzito au wenye mawingu
Hisia za kibofu kujaa mkojo hata baada ya kukojoa mkojo wote
Hisia za hali isiyo ya kawaia kwenye tumbo la chini ya kitovu kitovu
Maumivu ya katikati ya nyonga na maeneo ya chini ya kitovu ( sehemu kibofu kilipo)
Maumivu nyuma ya mgongo kwenye miishio
Kutokwa na damu kwenye mkojo (huweza onekana kama mkojo mwekundu, uliopauka au rangi ya kokakola)
Homa, kutetemeka, mwili kuchoka vinaweza kuwepo kwa mtu mwenye maambukizi kwenye kibofu ingawa vinahusiana na maambukizi ya mfumo wa juu wa mkojo
Hata hivyo dalili za U.T.I pia zimegawanyika kulinga na sehemu ya mfumo wa mkojo iliyoathiriwa na vimelea. Dalili hizo zimeelezewa hapa chini.
Dalili za U.T.I ya figo
Dalili za U.T.I iliyopanda kwenye figo ni pamoja na;
Maumivu nyuma ya mgongo au ya pembeni ya mwili chini kidogo ya mbavu
Homa kali
Kutetemeka na kutokwa jasho
Kichefuchefu
Kutapika
Dalili za U.T.I ya kibofu cha mkojo
Hisia za mgandamizo kwenye via vilivyo ndai ya nyonga
Kutojihisi vema kwenye tumbo la chini
Kukojoa mara kwa mara kunakoambatana na maumivu
Kukojoa damu
Dalili za U.T.I ya mrija wa urethra
Hisia za kuungua wakati wa kukojoa
Kutokwa na uchafu ukeni
Kumbuka
Kuwa na historia ya kutoa uchafu ukeni inayoambatana na dalili ya maumivu wakati wa kukojoa Inaweza kusababishwa pia na uambukizo wa vimelea ukeni, kwenye shingo ya kizazi au kwenye mfumo wa kizazi kwa kwa jingine la PIDna U.T.I pia.
Daktar atachukua historia yako ili ajiridhishe kwamba tatizo lako ni UTI au ugonjwa mwingine.
Ili kutofautisha U.T.I na magonjwa mengine, utaulizwa historia ya mahusiano yako na historia inayolenga kutambua magonjwa ya zinaa.
Vipimo gani vinafanyika kugundua kwamba una U.T.I?
Mara baada ya kuchukuliwa historia dalili zako, na kufanyiwa uchunguzi wa mwili, daktari ataagiza uchukuliwa sampuli tayari kwa vipimo.
Vipimo vinavyoweza kufanyika ni vile vyenye malengo ya kutambua ishara za U.T.I, kipimo cha kuotesha bakteria na vingine vya kutofautisha U.T.I na magonjwa mengine.
Magonjwa yanayofanana na U.T.I
Baadhi ya magonjwa yanayofanana sana dalili na U.T.I ni;
Maambukizi ya klamidia (ugonjwa wa zinaa)
Saratani ya kibofu cha mkojo
Uambukizo wa kirusi cha herpes kenye njia ya mkojo
Michomo kinga kwenye kibofu isiyotokana na vimelea
Michomo kinga ya kuta za kibofu kutokana na kemikali
Maambukizo ya vimelea kwenye via vya uzazi
Maambukizo ya vimelea ukeni
Matibabu ya UTI?
Kuna aina kadhaa za matibabu ya U.T.I yanayotegemea majibu ya vipimo, aina ya kimelea, ukali wa ugonjwa na hali ya mama ( mjamzito au la). Matibabu hayo huhusisha
Matumizi a dawa jamii ya antibayotiki kama maambukizi yanasababishwa na bakteria
Kwa mtu aliye na U.T.I iliyosababishwa na fangasi, atapewa dawa za kuua fangasi
Wakati mwingine kama figo imeferi kwa sababu ya U.T.I sugu unaweza kutolewa figo hiyo na kuwekewa nyingine kama itawezekana
Madhara ya UTI
Madhara ya UTI ni pamoja na;
U.T.I ya kujirudia rudia
Kuharibika kwa figo ( figo kuferi ghafla au tatizo sugu la kuferi) kama isipotibiwa mapema
Ongezeko la hatari ya kujifungua mtoto njiti au kabla ya wakati
Kufanyika kwa makovu kwneye mrija wa urethra kutokana na maambukizi ya mara kwa mara haswa kutokana na U.T.i ya kimelea anayesababisha gono
Kusambaa kwa vimelea kwenye damu. Huongeza hatari ya kupoteza maisha
Mahusiano ya U.T.I, chakula na maji
Kunywa maji mengi kunasaidia ondoa vimelea wanaosababisha U.T.I kwenye mfumo wa mkojo wakati wa kukojoa
Kunywa juisi ya matunda mfano beri nyekundu au ya blu inapunguza kwa kiasi kikubwa kupata U.T.i kwa kuwa hupunguza uwezo wa bakiteria kun'gang'ania kwenye kuta za kibofu hivo hutolewa kirahisi na mkojo wakati wa kukojoa
Namnaya kujikinga na U.T.I
Kojoa mara baada ya kushiriki tendo la ndoa, hii husaidia kuondoa vimelea waliojishikiza kwenye mirija ya mkojo wakati wa tendo hilo.
Kunywa maji ya kutosha, kusaidia mwili wako kusafisha njia ya mkojo na vimelea waliopo wakati wa kukojoa
Jisafishe kutoka mbele kwenda nyuma kila baada ya kwenda haja kubwa au ndogo. Kufanya hivi husaidia ondoa vimelea walio maeneo kati ya uke na njia ya haja kubwa.
Epuka kutumia kemikali chokozi katika mfumo wa mkojo. Mfano wake ni kutumia kemikali au sabuni kujisafisha ndani ya uke, Kuweka kemikali za marashi na zinazofanana na hizo ukeni. Kemikali nyingi huharibu uasili wa maeneo haya na kufanya mazingira rafiki kwa vimelea kushambulia na kupelekea U.T.I
Badilisha njia ya uzazi wa mpango kutoka kwenye kizuizi kinachowekwa kwenye shingo ya kizazi au dawa za kuua manii na kutumia njia zingine kama kondomu n.k