Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
9 Julai 2025, 06:03:22

Je, ni salama kuendelea na mimba ya mapema baada ya kujifungua kwa upasuaji kwenye ujauzito mbili zilizopita?
Ujauzito ni baraka, lakini wakati mwingine hujitokeza katika mazingira yanayohitaji umakini wa hali ya juu kitabibu. Mmoja wa changamoto zinazojitokeza ni pale ambapo mama anapata mimba ndani ya muda mfupi baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji wa mara mbili.
Hii ni hali inayoleta maswali makubwa kwa mama na pia kwa watoa huduma za afya: Je, ni salama kuendelea na mimba? au kuna ulazima wa kuisitisha kwa usalama wa mama?
Makala hii inalenga kutoa mwongozo wa kina kwa wagonjwa na wataalamu wa afya kuhusu hatari, tathmini ya kitaalamu, na chaguzi salama kwa hali hiyo.
Kisa halisi kinachoibua hoja
Mama anayeuliza:
“Mtoto wa kwanza na wa pili nilijifungua kwa upasuaji. Mtoto wa pili nilimzaa miezi 6–7 iliyopita. Sasa nina ujauzito wa wiki 2 na nina wasiwasi—niiache au niitoe?”
Swali hili linaonyesha haja ya uamuzi ulio makini, na wa kitaalamu.
Muktadha wa kitabibu: Mimba ya haraka baada ya kujifungua mara mbili kwa upasuaji
a) Kipindi kifupi kati ya ujauzito
Hii ni hali ambapo mama anapata mimba mpya kabla ya miezi 18 kupita tangu alipojifungua kwa mara ya mwisho. Ikiwa amezaa kwa upasuaji, muda mfupi huu huongeza hatari zaidi.
b) Kujifungua mara mbili kwa upasuaji
Kila upasuaji unaacha kovu kwenye ukuta wa uterasi. Kadri upasuaji unavyojirudia, ndivyo kovu hilo linavyoweza kuwa dhaifu zaidi. Mimba mpya ndani ya miezi michache inaweza kuliweka kovu hilo kwenye hatari kubwa ya kupasuka.
Uwezekano wa kujifungua salama katika hali hii
Ikiwa mama aliyejifungua kwa upasuaji mara mbili atapata mimba ndani ya miezi 6–7 na apate ufuatiliaji wa karibu katika huduma ya uzazi ya hatari kubwa, uwezekano wa kujifungua salama unaweza kufikia 80–90%, kwa sharti kwamba uchungu hautaanza kabla ya upasuaji kupangwa, na kondo liwe limejishikiza mahali salama. Hata hivyo, bila ufuatiliaji wa karibu au ikiwa uchungu utaanza ghafla, hatari ya kuchanika kwa kizazi huongezeka hadi 2–5% au zaidi, na inaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto. Aina ya mshono wa upasuaji wa awali (hasa ikiwa ulikuwa wa “wima”) huongeza zaidi hatari. Hivyo basi, maamuzi yahusishe tathmini ya kina ya kitabibu, huduma za hali ya juu, na mawasiliano ya wazi kati ya mama na mtaalamu wa afya.
Jedwali: Uwezekano wa kujifungua salama na hatari zinazohusiana na mimba ya mapema baada ya upasuaji mbili wa kujifungua
Hali ya mama | Uwezekano wa kujifungua Salama | Hatari Kuu zinazohusiana | Mahitaji muhimu ya usalama |
Anafuatiliwa kwenye huduma ya uzazi wa hatari kubwa , Upasuaji wa kujifungua unapangwa mapema kabla ya uchungu | ✅ 80–90% | Kupasuka kwa uterasi (<2%) - Kondo previa/Kondo akreta | - Ultrasound ya kizazi na kondo - Mipango ya upasuaji wa kujigunfua wa mapema - Huduma ya uzazi wa kitaalamu |
Hapewi ufuatiliaji wa karibu au uchungu unaanza kabla ya kufika hospitali | ❌ <70% | - Kuchanika kwa kizazi (2–5% au zaidi) - Upotevu wa damu - Hatari kwa maisha ya mama na mtoto | - Huduma ya dharura - Upasuaji wa haraka - Tathmini ya kitabibu iliyochelewa |
Aina ya mshono wa awali ni “wima” | ⚠️ Hatari kubwa zaidi ya kuchanika kwa kizazi | - Kuchanika mapema kwa kizazi - Kupoteza mimba au kizazi | - Hujumuisha uamuzi wa mapema kuhusu usalama wa kuendelea na mimba |
Hatari zinazoweza kujitokeza katika hali hii
A. Kuchanika kwa kizazi
Ni hatari inayotokea pale ambapo mshono wa upasuaji uliopita unapasuka kutokana na shinikizo la mimba inayokua. Hali hii hujitokeza zaidi kwenye nn'gwe ya pili au ya tatu ya ujauzito, na ni dharura inayoweza kusababisha:
Kupoteza damu kwa kiasi kikubwa
Kupoteza mimba
Hatari ya kufa kwa mama na mtoto
B. Kondo kujishikiza sehemu isiyo kawaida au kushikamana na kuta za kizazi (Kondo Previa na Kondo Akreta)
Upasuaji huongeza hatari ya placenta kujishikiza sehemu zisizo za kawaida:
Kondo Previa – kufunika mlango wa kizazi, kusababisha kutokwa na damu
Kondo Akreta – kushikamana sana na ukuta wa kizazi, na wakati mwingine hadi kwenye viungo vya karibu (mfano kibofu)
Hizi ni hali hatari sana wakati wa kujifungua na mara nyingine huhitaji kufanyiwa hysterectomy (kuondoa uterasi).
C. Mwili haujapona kikamilifu
Muda wa kupona baada ya upasuaji wa kujifungua ni zaidi ya miezi 6. Mimba mapema huchosha mwili, huongeza resiko la upungufu wa damu, shinikizo la damu, kisukari cha mimba, na matatizo ya kisaikolojia hasa ikiwa mama bado ananyonyesha au bado ana mtoto mchanga.
Hatua za kuchukua
Anza kliniki mapema
Ujauzito wa wiki 2–3 hauwezi kuonekana kwa ultrasound mara moja. Fanya ultrasound baada ya wiki 5 kuthibitisha mimba ipo ndani ya uterasi, si mimba ya nje ya kizazi, na tathmini hali ya uterasi. Vipimo vya damu (CBC, HB) vinaweza kusaidia kutathmini hali ya mwili kwa sasa.
Pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa magonjwa ya uzazi
Daktari atapitia aina ya upasuaji uliopita: je, upasuaji ulikuwa wa mlalo au wa wima? Upasuaji wa wima huongeza hatari zaidi ya kupasuka kwa kizazi. Atatathmini afya ya sasa, historia ya matatizo ya mimba za nyuma, na uwezo wa wako wa kuhimili ujauzito mwingine.
Zingatia chaguzi mbili zilizopo
1. Kuendelea na mimba kwa ufuatiliaji wa karibu sana
Hii inahitaji:
Ufuatiliaji wa mara kwa mara wa mshono na placenta
Huduma ya uzazi wa hatari
Mpango wa kujifungua kwaupasuaji kabla ya uchungu kuanza
Utayari wa dharura kama kupasuka kwa kizazi
2. Kusitisha mimba kwa njia salama
Ikiwa mtaalamu atabaini kuwa mimba ni hatari kwa maisha ya mama au mtoto
Kusitisha hufanyika kwa dawa au kwa upasuaji mdogo, kutegemea umri wa mimba na hali ya mama
Sheria ya nchi na sera za afya za uzazi huongoza mchakato huu
Maamuzi ya kimaadili na kisaikolojia
Ni kawaida kwa mama kuwa na hofu, hatia au mkanganyiko. Uamuzi huu haupaswi kufanywa kwa pupa au kwa shinikizo, bali kwa msaada wa mtaalamu, mume, au mshauri wa afya ya akili.
Mtoa huduma wa afya atatoa taarifa sahihi, ushauri bila hukumu, na kukusaidia mama kufanya maamuzi yaliyo salama kwa afya yako na familia.
Wito kwa watoa huduma na familia
Kwa watoa huduma
Tambua hali kama hii ni kama dharura ya kiushauri , si tu hali ya kawaida ya kliniki ya wajawazito. Unapaswa kuzingatia historia yake, vipimo, na uhakikishe mama anapata fursa ya kuelewa kila hatari na faida ya chaguzi zote.
Kwa familia na jamii
oeni msaada wa kisaikolojia na kihisia. Usimhukumu mama. Msaidie kupokea huduma bora na afanye uamuzi kwa amani na heshima.
Hitimisho
Mimba ya mapema baada ya kujifungua kwa upasuaji mara mbili huongeza hatari ya kupasuka kwa uterasi na matatizo ya placenta. Kwa ufuatiliaji wa karibu na huduma ya hali ya juu, hadi 90% ya wanawake wanaweza kujifungua salama.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
9 Julai 2025, 05:58:12
Rejea za mada hii
American College of Obstetricians and Gynecologists. Practice Bulletin No. 184: Vaginal Birth After Cesarean Delivery. Obstet Gynecol. 2017;130(5):e217–33.
Zhang J, Troendle J, Yancey MK, et al. Recurrent cesarean delivery: short-term maternal outcomes and risk factors. Am J Obstet Gynecol. 2005;193(3 Pt 2):1173–8.
Guise JM, Eden K, Emeis C, et al. Vaginal birth after cesarean: new insights. Evidence Report/Technology Assessment No. 191 (Prepared by the Oregon Health & Science University Evidence-based Practice Center). AHRQ Publication No. 10-E003. Rockville, MD: Agency for Healthcare Research and Quality; 2010.
Bujold E, Gauthier RJ. Risk factors for uterine rupture: what do we know? Semin Perinatol. 2010;34(4):254–8.
Roberge S, Chaillet N, Boutin A, et al. Maternal morbidity associated with multiple repeat cesarean deliveries. Am J Obstet Gynecol. 2017;216(4):444.e1–7.
Knight M, Bunch K, Tuffnell D, et al., editors. Saving Lives, Improving Mothers’ Care – Lessons learned to inform maternity care from the UK and Ireland Confidential Enquiries into Maternal Deaths and Morbidity 2016–18. Oxford: National Perinatal Epidemiology Unit, University of Oxford; 2020.
Leung AS, Qureshi F, Knowles S, et al. Uterine rupture: risk factors and pregnancy outcomes. Obstet Gynecol. 1993;81(3):345–8.
Silver RM. Cesarean delivery risks and complications. UpToDate. 2023. Available from: https://www.uptodate.com/contents/cesarean-delivery-risks-and-complications
WHO. WHO recommendations on maternal health: guidelines approved by the WHO Guidelines Review Committee. Geneva: World Health Organization; 2017.
Conde-Agudelo A, Rosas-Bermúdez A, Kafury-Goeta AC. Effects of birth spacing on maternal health: a systematic review. Am J Obstet Gynecol. 2007;196(4):297–308.
