top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Sospeter B, MD

Imeboreshwa:

29 Januari 2026, 13:34:50

Kinyesi cheusi kwa watu wazima: Visababishi, Dalili, Vipimo na Matibabu

Kinyesi cheusi kwa watu wazima: Visababishi, Dalili, Vipimo na Matibabu

Kujisaidia kinyesi chenye rangi nyeusi ni dalili inayoweza kumtia hofu mgonjwa, hasa kinapokuwa cheusi sana, kinang’aa au kinafanana na lami. Ingawa wakati mwingine hali hii inaweza kusababishwa na chakula au dawa, mara nyingine huashiria kutokwa damu ndani ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, hali inayohitaji uchunguzi wa haraka wa kitabibu.


Makala hii inaeleza kwa kina maana ya kinyesi cheusi, visababishi vyake, dalili hatarishi, uchunguzi na matibabu, pamoja na maswali yanayoulizwa mara kwa mara.


Kinyesi chenye rangi Nyeusi ni nini?

Kinyesi chenye rangi nyeusi (kitaalamu hujulikana kama melena) ni kinyesi chenye rangi nyeusi au kahawia iliyokolea, mara nyingi chenye harufu kali na muonekano wa kung’aa kama lami.

Rangi hii hutokana na:

  • Damu iliyomeng’enywa ndani ya njia ya chakula, hasa damu inayotoka sehemu za juu kama tumbo au utumbo mdogo

  • Au athari za vyakula na dawa fulani zisizo hatarishi


Tofauti kati ya Kinyesi Cheusi cha Kawaida na Melena

Kipengele

Kinyesi cheusi cha kawaida

Melena

Sababu

Chakula/dawa

Kutokwa damu

Harufu

Ya kawaida

Kali sana

Muonekano

Kavu au kawaida

Laini, kung’aa

Hatari

Ndogo

Kubwa (dharura)

Visababishi vya Kinyesi Chenye Rangi Nyeusi


1. Kutokwa na Damu Ndani ya Mfumo wa Chakula (Sababu Kuu ya Melena)


Hiki ndicho kisababishi kikuu na hatarishi zaidi cha kujisaidia kinyesi chenye rangi nyeusi (melena). Melena hutokea pale damu inapovuja kwenye sehemu za juu za mfumo wa chakula (upper gastrointestinal tract), kisha damu hiyo humeng’enywa na asidi ya tumbo na vimeng’enya, na hatimaye kutoka kama kinyesi cheusi chenye harufu kali isiyo ya kawaida.

Kutokwa damu kunaweza kutokana na hali zifuatazo:


a) Vidonda vya tumbo

Vidonda hivi hutokea kwenye tumbo au duodenum, mara nyingi kutokana na:

  • Maambukizi ya Helicobacter pylori

  • Matumizi ya muda mrefu ya dawa za NSAIDs (mf. diclofenac, ibuprofen)

  • Msongo wa mawazo makali au magonjwa sugu


Vidonda vikianza kutoa damu polepole, mgonjwa anaweza asiwe na maumivu makali, lakini akaanza kuona kinyesi cheusi na dalili za upungufu wa damu.


b) Homa ya tumbo(Gastraitis )

Gastritis ni hali ya kuvimba kwa kuta za tumbo, inayoweza kusababishwa na:

  • Pombe

  • Dawa jamii ya NSAID( kama diclofenac n.k_

  • Maambukizi

  • Msongo wa mawazo wa muda mrefu


Gastraitis inaweza kusababisha kutokwa damu kidogo kidogo, damu inayotosha kubadilisha rangi ya kinyesi bila kutapika damu.


c) Vidonda vya umio

Vidonda hivi hutokea kwenye umio (esophagus), mara nyingi kutokana na:

  • Kucheua tindikali (GERD)

  • Dawa fulani

  • Maambukizi kwa wagonjwa wenye kinga dhaifu

Hali hii inaweza kusababisha melena, maumivu ya kifua, au maumivu wakati wa kumeza.


d) Varices za umio

Hii ni hali ya kuvimba kwa mishipa ya damu ya umio, mara nyingi kwa wagonjwa wa:

  • Ini sugu (cirrhosis)

  • Shinikizo kubwa kwenye mshipa wa portal (portal hypertension)

Varices zikipasuka, huweza kutoa damu nyingi sana na kusababisha:

  • Kinyesi cheusi ghafla

  • Kutapika damu

  • Kupoteza fahamu

Hii ni dharura ya kitabibu.


e) Saratani ya tumbo au umio

Saratani hizi huweza kutoa damu taratibu kwa muda mrefu bila dalili za awali. Wagonjwa wengi huja hospitali wakiwa na:

  • Kinyesi cheusi

  • Kupungua uzito

  • Uchovu sugu

  • Upungufu wa damu


2. Dawa Fulani Zinazosababisha Kinyesi Cheusi

Sio kila kinyesi cheusi kinamaanisha kutokwa damu. Baadhi ya dawa hubadilisha rangi ya kinyesi bila hatari kubwa, lakini ni muhimu kutofautisha.


a) Dawa za madini chuma

Dawa hizi hutumika kutibu upungufu wa damu na mara nyingi:

  • Hufanya kinyesi kuwa cheusi au kijani-kibichi

  • Hakuna harufu kali

  • Hakuna dalili za kizunguzungu au udhaifu

Hii ni hali ya kawaida na si hatari.


b) Dawa Bismuth subsalicylate (mf. Pepto-Bismol)

Dawa hii hutumika kutibu:

  • Kuhara

  • Maumivu ya tumbo

Huungana na salfa kwenye tumbo na kuunda dutu nyeusi, hivyo kufanya kinyesi kuwa cheusi kwa muda.


c) NSAIDs

Ingawa NSAIDs zinaweza kubadilisha rangi ya kinyesi, hatari kubwa ni kwamba:

  • Zinaweza kusababisha vidonda

  • Zinaweza kusababisha kutokwa damu kwa ndani

Hivyo kinyesi cheusi kwa mtumiaji wa NSAIDs lazima kichunguzwe.


3. Vyakula vinavyoweza kusababisha Kinyesi cheusi

Baadhi ya vyakula vyenye rangi nzito vinaweza kufanya kinyesi kuwa cheusi bila kuashiria ugonjwa:

  • Damu iliyokaangwa au chakula chenye damu nyingi

  • Maini

  • Mchicha mwingi

  • Licorice nyeusi

  • Matunda jamii ya Blueberries kwa wingi


Kinyesi kutokana na vyakula:

  • Hakina harufu kali sana

  • Hakina dalili za udhaifu

  • Hurudi kawaida ndani ya siku 1–2


Dalili zinazoambatana na Kinyesi cheusi (Dalili hatarishi)

Kinyesi cheusi kikisababishwa na kutokwa damu, huambatana na dalili zifuatazo:

  • Maumivu ya tumbo au kifua

  • Kichefuchefu au kutapika

  • Kutapika damu au matapishi yanayofanana na kahawa

  • Kizunguzungu au kupoteza fahamu

  • Uchovu mwingi

  • Mapigo ya moyo kwenda haraka

  • Ngozi kuwa ya rangi ya njano au kupauka

  • Dalili za upungufu wa damu (anemia)


Dalili hizi ni ishara ya dharura ya kitabibu.


Uchunguzi wa Kitabibu


Aina ya uchunguzi

Kinaangaliwa nini

Lengo la kipimo

Historia ya mgonjwa (History taking)

Historia ya ulaji wa vyakula (mf. maini, chuma), matumizi ya dawa (NSAIDs, aspirin, iron, bismuth), matumizi ya pombe, sigara, magonjwa ya awali kama vidonda vya tumbo au ugonjwa wa ini, na dalili zinazoambatana (maumivu, kutapika damu, kizunguzungu).

Kutofautisha kati ya kinyesi cheusi kinachosababishwa na chakula/dawa na kile kinachosababishwa na kutokwa damu ndani ya mfumo wa chakula.

Kipimo cha damu (Hb, FBC)

Kiwango cha hemoglobini (Hb), idadi ya seli nyekundu, nyeupe na sahani za damu.

Kutathmini kama kuna upungufu wa damu (anemia) unaotokana na kutokwa damu, na kutathmini uzito wa tatizo.

Kipimo cha damu kwenye kinyesi (FOBT)

Uwepo wa damu isiyoonekana kwa macho kwenye kinyesi.

Kuthibitisha kama kinyesi cheusi kina asili ya damu hata kama hakuna dalili nyingine wazi.

Endoscopy ya mfumo wa juu wa chakula (OGD)

Umio (esophagus), tumbo (stomach), na sehemu ya juu ya utumbo mdogo (duodenum).

Kutambua chanzo halisi cha damu kama vidonda, gastraitis, mipasuko, au saratani; pia huruhusu tiba ya moja kwa moja (kufunga damu inayovuja).

Ultrasound ya tumbo

Ini, wengu, mishipa ya portal, na viungo vya tumbo.

Kusaidia kutambua ugonjwa wa ini au dalili za shinikizo la damu kwenye mishipa ya vena ya umio.

CT Scan ya tumbo

Muundo wa kina wa viungo vya ndani ya tumbo.

Hutumika pale ambapo chanzo hakijaonekana kwenye OGD au kuna shaka ya uvimbe, saratani, au kutokwa damu kwa ndani kwa kiwango kikubwa.


Muhimu Kukumbuka

  • OGD ndiyo kipimo cha msingi na muhimu zaidi kwa mgonjwa mwenye kinyesi cheusi.

  • Kadri Hb inavyoshuka, ndivyo hatari ya mgonjwa inavyoongezeka na kuhitaji uangalizi wa karibu au kulazwa.

  • Uchunguzi wa mapema huongeza nafasi ya tiba sahihi na hupunguza hatari ya madhara makubwa.


Matibabu

Matibabu hutegemea chanzo:


Ikiwa ni kutokwa damu:

  • Kulazwa hospitali

  • Dawa za kupunguza asidi (PPIs)

  • Endoscopic hemostasis (kufunga chanzo cha damu)

  • Kuongezewa damu endapo Hb imeshuka sana

  • Tiba ya ugonjwa wa ini au saratani kama inahusika


Ikiwa ni dawa au chakula:

  • Kusimamisha au kubadilisha dawa (chini ya ushauri wa daktari)

  • Ufuatiliaji wa dalili


Nini cha kufanya nyumbani ukiwa na kinyesi cheusi?


Usipuuzie kinyesi cheusi kisichoelezeka

Kinyesi chenye rangi nyeusi (hasa kinapokuwa na utelezi kama lami) kinaweza kuashiria kutokwa damu ndani ya mfumo wa chakula. Hata kama hakina maumivu au kimetokea mara moja, ni muhimu kukichukulia kwa uzito na kufuatilia kwa karibu—ikiwemo kuangalia mabadiliko ya rangi, harufu, na wingi wa kinyesi.


Epuka matumizi ya dawa za NSAIDs bila ushauri wa daktari

Dawa kama aspirin, ibuprofen, diclofenac, na naproxen zinaweza kuchochea au kuzidisha vidonda vya tumbo na kusababisha kutokwa damu. Ikiwa tayari unazitumia kwa sababu nyingine, wasiliana na daktari haraka ili apitie usalama wa kuendelea nazo au kukupatia mbadala salama.


Usijaribu dawa za kienyeji au kujitibu ili kuficha dalili

Kunywa mitishamba, mchanganyiko wa asili, au dawa za kupunguza asidi bila ushauri kunaweza kuficha dalili muhimu na kuchelewesha uchunguzi sahihi. Baadhi ya dawa zinaweza hata kuongeza hatari ya kutokwa damu au kuingiliana vibaya na matibabu ya kitabibu.


Pumzika na epuka vyakula vinavyochochea tumbo

Epuka pombe, vyakula vyenye pilipili kali, kahawa nyingi, na sigara kwa kuwa vinaweza kuongeza uchochezi wa tumbo. Kula mlo mwepesi na kunywa maji ya kutosha huku ukisubiri tathmini ya daktari.


Nenda hospitali mapema ikiwa dalili zinaendelea au zinaongezeka

Ikiwa kinyesi cheusi kinaendelea zaidi ya siku 1–2, kinaambatana na kizunguzungu, udhaifu, mapigo ya moyo kwenda kasi, kutapika damu au matapishi yanayofanana na kahawa, usisubiri—fika hospitali haraka. Uchunguzi wa mapema unaweza kuzuia madhara makubwa na kuokoa maisha.

Kumbuka: Kinyesi cheusi si dalili ya kawaida. Hatua ya busara nyumbani ni kufuatilia kwa makini na kutafuta msaada wa kitaalamu mapema badala ya kujitibu.

Hitimisho

Kujisaidia kinyesi chenye rangi nyeusi si dalili ya kupuuzwa. Ingawa wakati mwingine huwa hakina hatari, mara nyingi huashiria tatizo kubwa la kiafya linalohitaji uchunguzi wa haraka. Kutambua chanzo mapema huokoa maisha.


Wakati wa kumwona Daktari haraka

  • Kinyesi cheusi kinaendelea zaidi ya siku 1–2

  • Kuna kizunguzungu, udhaifu au kupoteza fahamu

  • Unatapika damu

  • Una historia ya vidonda, ugonjwa wa ini au saratani


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Kujisaidia kinyesi cheusi maana yake nini?

Mara nyingi huashiria damu iliyomeng’enywa kutoka sehemu za juu za mfumo wa chakula, ingawa wakati mwingine husababishwa na chakula au dawa.

2. Je, kinyesi cheusi ni hatari kila wakati?

Hapana. Kinaweza kuwa si hatari ikiwa kimesababishwa na chakula au dawa, lakini kikitokea ghafla bila sababu wazi, ni hatari.

3. Melena ni nini?

Melena ni kinyesi cheusi chenye harufu kali kinachosababishwa na damu iliyomeng’enywa ndani ya njia ya chakula.

4. Je vidonge vya madini chuma vinaweza kufanya kinyesi kuwa cheusi?

Ndiyo. Vidonge vya madini chumas ni chanzo cha kawaida na mara nyingi si hatari.

5. Kinyesi cheusi kinaweza kuashiria saratani?

Ndiyo, hasa saratani ya tumbo au umio, ingawa si kila kinyesi cheusi ni saratani.

6. Ni tofauti gani kati ya damu nyekundu na kinyesi cheusi?

Damu nyekundu huashiria kutokwa damu sehemu za chini, wakati kinyesi cheusi huashiria damu kutoka juu ya mfumo wa chakula.

7. Je, mtoto anaweza kupata kinyesi cheusi?

Ndiyo, lakini ni nadra. Hutokea kwa kumeza damu au matatizo ya tumbo, na huhitaji uchunguzi wa haraka.

8. Kinyesi cheusi kinaweza kuambatana na maumivu ya tumbo?

Ndiyo, hasa kama chanzo ni vidonda au gastraitis.

9. Ni lini niende hospitali haraka?

Pindi kinyesi cheusi kinapoambatana na kizunguzungu, kutapika damu, au udhaifu mkubwa.

10. Je, kinyesi cheusi kinaweza kuisha chenyewe?

Kinaweza kuisha ikiwa chanzo ni chakula au dawa, lakini kama chanzo ni damu, hakiwezi kuisha bila matibabu.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

29 Januari 2026, 13:34:50

Rejea za mada hii

  1. Longstreth GF. Evaluation of patients with melena. Am J Gastroenterol. 2018;113(3):353–360.

  2. Rockall TA, Logan RF, Devlin HB, Northfield TC. Risk assessment after acute upper gastrointestinal haemorrhage. Gut. 1996;38(3):316–321.

  3. Cappell MS. Safety and efficacy of endoscopy for gastrointestinal bleeding. Nat Rev Gastroenterol Hepatol. 2010;7(9):483–493.

  4. Laine L, Jensen DM. Management of patients with ulcer bleeding. Am J Gastroenterol. 2012;107(3):345–360.

  5. Kumar V, Abbas AK, Aster JC. Robbins and Cotran Pathologic Basis of Disease. 10th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020.

  6. NICE. Acute upper gastrointestinal bleeding in over 16s. NICE guideline [NG12]. 2016.

bottom of page