top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

20 Novemba 2025, 09:30:35

Kipimo cha mkojo kuonyesha uwepo wa damu (Hematuria): Maana, na Hatua za kuchukua

Kipimo cha mkojo kuonyesha uwepo wa damu (Hematuria): Maana, na Hatua za kuchukua

Kipimo cha uchunguzi wa mkojo (urinalisis) ni uchunguzi wa kawaida unaotumika kutathmini afya ya mfumo wa mkojo na figo. Moja ya vitu vinavyoangaliwa ni uwepo wa damu kwenye mkojo, unaojulikana kwa jina jingine la kitiba kama hematuria. Wakati mwingine damu huonekana kwa macho (hematuria dhahiri), lakini mara nyingi hugundulika tu kwenye vipimo vya maabara (hematuria isiyo ya wazi).


Kuonekana kwa damu kwenye kipimo cha mkojo ni dalili ya tatizo fulani linalohitaji kufahamika na kutibiwa kulingana na chanzo.


Aina za hematuria

1. Hematuria inayonekana kwa macho (hematuria dhahiri)

Hupa mkojo rangi nyekundu, pinki au kahawia.


2. Hematuria isiyo dhahiri

Hapa chembe nyekundu za damu (RBC) huonekana kwa hadubini au njiti ya kipimo cha mkojo hata kama mkojo unaonekana wa kawaida.


Kipimo cha mkojo kinaangalia nini?

Katika kipimo cha mkojo, njiti ya kupimia hubaini uwepo wa:

  • Chembe nyekundu za damu (RBC)

  • Hemoglobin (ikiwa seli zimepasuka)

  • Mayoglobin (kutoka kwenye misuli)

Vipimo vya maabara (hadubini) hutofautisha kati ya RBC halisi na zile zilizopasuka.


Matokeo ya hematuria kwenye kipimo na tafsiri zake


1. Uwepo mdogo wa chembe nyekundu za damu kwenye mkojo (0–3 RBC/hpf)
  • Mara nyingi huchukuliwa kuwa kawaida.

  • Inaweza kutokea baada ya mazoezi makali, msongo au hedhi kwa wanawake.


2. Uwepo wa kiwango cha kati au kikubwa cha chembe nyekundu za damu

Ikiwa kipimo kinaonyesha chembe nyekundu za damu(RBC) kuwa nyingi (≥3 RBC/hpf), inaashiria:

  • Uwezekano wa maambukizi

  • Uchubukaji wa tishu kwenye mfumo wa mkojo

  • Matatizo ya figo au vifuko vya mkojo


3. Njiti ya kipimo cha mkojo kuwa chanya lakini hadubini kuonyesha hakuna chembe nyekundu za damu

Hii inaweza kutokea kutokana na:

  • Hemoglobinyuria – seli za damu zimepasuka

  • Maoglobinyuria – uharibifu wa misuli

  • Baada ya mazoezi makali


Visababishi vikuu vya uwepo wa damu kwenye mkojo


1. Maambukizi ya njia ya mkojo
  • Dalili: Maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara, uchafu wa mkojo.

  • Kipimo: chembe nyekundu za damu, chembe nyeupe za damu, naitreti.


2. Mawe kwenye figo au kibofu

Dalili: Maumivu makali ya pembeni cheni ya mbavu (sehemu zinazpokaa figo), damu kwenye mkojo.


3. Magonjwa ya figo
  • Glomerulonephraitis, nephritik sindromu

  • Dalili: uvimbe mwilini, shinikizo la damu, protini kwenye mkojo.


4. Majeraha kwenye mfumo wa mkojo

Ajali, kupigwa, kuanguka, au taratibu za kitabibu (kuingiziwa mpira kwenye njia ya mkojo).


5. Saratani ya figo au kibofu

Mara nyingi ina hematuria bila maumivu.


6. Dawa na vyakula
  • Dawa za kuyeyusha damu

  • Kiazi chekundu, rangi fulani za chakula (lakini hizi hazionyeshi RBC kwenye njiti ya kipimo cha mkojo)


7. Mazoezi mazito

Inayoitwa hematuria ya mazoezi


8. Hedhi kwa wanawake

Inaweza kuchangia matokeo yasiyo sahihi (uchafuzi wa mkojo na damu wakati wa kukusanya sampuli ya mkojo)


Dalili zinazoambatana na damu kwenye mkojo

Watu wengine hawana dalili kabisa, ila wanaweza kupata:

  • Maumivu ya chini ya mbavu upande wa kushoto au kulia

  • Maumivu wakati wa kukojoa

  • Kukojoa mara kwa mara

  • Homa

  • Mkojo wenye harufu isiyo ya kawaida

  • Mkojo wenye mawingu au rangi isiyo ya kawaida


Vipimo vinavyofuatia baada ya kugundua damu kwenye mkojo


Jedwali 1: VIpimo na nini kinafuata;

Kipimo

Kinachotafuta

Kipimo cha hadubini ya mkojo

Kuthibitisha Chembe nyekundu za damu, Chembe nyeupe za damu, Kasti

Kipimo cha kuotesha vimelea kwenye mkojo

Kutambua vimelea wa UTI

Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Kuangalia kreatenini na yurea)

Kazi ya figo

Ultrasound ya figo na kibofu

Mawe, uvimbe, kuziba kwa mirija

CT-scan

Uchunguzi wa mawe au uvimbe

Sistoskopi

Kuchunguza kibofu kwa ndani, hasa kwa wazee


Matibabu

Matibabu ya damu kwenye mkojo hutegemea chanzo kama ilivyoelezewa kwa ufupi hapa chini;


Jedwali 2: Matibabu kwa Kila Kisababishi cha Damu Kwenye Mkojo

Kisababishi

Matibabu ya Hospitali

Ushauri wa ziada/Matibabu ya nyumbani

1. Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

  • Antibiotiki kulingana na majibu ya kipimo cha kuotesha vimelea kwenye mkojo

  • Dawa za maumivu kama parasetamo

  • Kunywa maji mengi

  • Kunywa maji 2–3 L/ siku

  • Epuka kujinyima mkojo

  • Safisha sehemu za siri kwa usahihi

2. Mawe kwenye figo au kibofu

  • Dawa za maumivu

  • Kuongezewa maji mwilini kwa njia ya mishipa

  • Kuyeyusha mawe (ESWL)

  • Ureteroscopi / upasuaji kama mawe ni makubwa

  • Kunywa maji mengi

  • Kutembea na kufanya mazoezi mepesi kusaidia jiwe kutoka

  • Epuka chumvi na protini kupita kiasi

3. Magonjwa ya figo Glomerulonephraitis / Nephritik sindromu

  • Steroid kutegemea aina ya ugonjwa

  • Dawa za kushusha shinikizo

  • Dawa za kupunguza maji mwilini

  • Udhibiti wa protini kwenye mlo

  • Punguza chumvi

  • Kula chakula chenye protini kidogo kwa ushauri wa daktari

  • Fuata ufuatiliaji wa BP na uzito

4. Majeraha ya mfumo wa mkojo

  • Ultrasound/CT-scan kutathmini majeraha

  • Upasuaji kama kuna kupasuka kwa figo/kibofu

  • Dawa za maumivu

  • Pumzika

  • Epuka kunyanyua vitu vizito

  • Kunywa maji ya kutosha

5. Saratani ya figo au kibofu

  • Upasuaji (nephrectomy / TURBT)

  • Kemotherapia au radiotherapia kutegemea aina ya saratani

  • Ufuatiliaji wa karibu wa daktari

  • Mlo wenye lishe bora na kupunguza uvutaji sigara

6. Dawa na vyakula

  • Kupunguza dozi ya blood thinners kama inahitajika

  • Badilisha dawa kama zinasababisha hematuria (kwa ushauri wa daktari)

  • Epuka vyakula vinavyopaka rangi kama kiazi chekundu endapo vinachanganya matokeo

  • Fuata maelekezo ya dawa kwa usahihi

7. Mazoezi mazito

  • Hakuna tiba maalum mara nyingi

  • Uchunguzi zaidi kama dalili zinaendelea >48h

  • Pumzika 24–48h

  • Kunywa maji ya kutosha

  • Punguza mazoezi ya kiwango cha juu kwa muda

8. Hedhi kwa wanawake

  • Hakuna matibabu—ni uchafusi wa sampuli

  • Rudia kipimo baada ya hedhi

  • Kusanya sampuli vizuri (mkojo wa katikati ya kukojoa)

  • Epuka kukusanya mkojo siku za hedhi


Matibabu ya nyumbani

Tiba saidizi za nyumbani kama utakavyoshauriwa na daktari wako ni pamoja na;

  • Kunywa maji ya kutosha

  • Epuka kujinyima mkojo muda mrefu

  • Epuka mazoezi mazito kwa muda kama dalili zimejitokeza baada ya mazoezi

  • Kwa wanawake: kukusanya mkojo kabla au baada ya hedhi ili kuepuka uchafuzi wa sampuli

  • Epuka dawa zinazoongeza hatari ya kutokwa damu bila ushauri wa daktari


Wakati wa Kumwona Daktari

  • Mkojo mwekundu au kahawia ghafla

  • Maumivu makali ya kiuno au chini ya tumbo

  • Homa, kutetemeka, au udhaifu

  • Uwepo wa damu bila maumivu (inahitaji uchunguzi wa haraka, hasa kwa watu >40 years)

  • Matokeo ya kipimo kuonyesha RBC nyingi bila sababu inayoeleweka


Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara

1. Je, mkojo kuwa mwekundu lazima iwe damu?

Hapana. Rangi inaweza kutokana na vyakula (mfano kiazi chekundu), dawa, au upungufu wa maji. Vipimo vya maabara huthibitisha kama ni RBC halisi.


2. Je, maumivu wakati wa kukojoa na damu ni UTI tu?

La. Mawe kwenye figo, michubuko au magonjwa ya kibofu pia hutoa dalili hizi.

3. Je, hematuria inaweza kujiponya bila matibabu?

Inawezekana ikiwa imesababishwa na mazoezi au ugonjwa mdogo. Lakini usipuuze—chanzo cha tatizo ni muhimu kutambuliwa.

4. Je, hedhi inaweza kupa matokeo ya uongo?

Ndiyo. Wanawake wanashauriwa kukusanya mkojo nje ya siku za hedhi.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

20 Novemba 2025, 09:26:24

Rejea za mada hii

  1. Simerville JA, Maxted WC, Pahira JJ. Urinalysis: A comprehensive review. Am Fam Physician. 2005;71(6):1153–1162.

  2. Grossfeld GD, Litwin MS, Wolf JS Jr, et al. Evaluation of asymptomatic microscopic hematuria in adults: The American Urological Association best practice policy—Part I. Urology. 2001;57(4):599–603.

  3. Khadra MH, Pickard RS, Charlton M, et al. A prospective analysis of 1930 patients with hematuria to evaluate current diagnostic practice. J Urol. 2000;163(2):524–527.

  4. Fogazzi GB. Urinalysis: Core curriculum 2008. Am J Kidney Dis. 2008;51(6):1052–1067.

  5. Davis R, Jones JS, Barocas DA, et al. Diagnosis, evaluation and follow-up of asymptomatic microhematuria (AMH) in adults: AUA guideline. J Urol. 2012;188(6 Suppl):2473–2481.

  6. Nash K, Hafeez A, Hou S. Hospital-acquired hematuria. Cleve Clin J Med. 2002;69(11):870–884.

  7. Kelly JD, Fawcett DP, Goldberg LC. Assessment of haematuria. BMJ. 2009;338:a3021.

  8. Copley JB. Hematuria in adults: Classification and diagnostic approach. In: StatPearls [Internet]. Treasure Island (FL): StatPearls Publishing; 2024.

  9. Flores-Mireles AL, Walker JN, Caparon M, Hultgren SJ. Urinary tract infections: Epidemiology, mechanisms, and treatment options. Nat Rev Microbiol. 2015;13(5):269–284.

  10. Pearle MS, Calhoun EA, Curhan GC. Urologic diseases in America project: Urolithiasis. J Urol. 2005;173(3):848–857.

bottom of page