Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
Imeboreshwa:
18 Mei 2025, 09:43:56

Unafanya nini unapokuwa na wasiwasi wa kupitiliza muda wa kujifungua?
Swali la msingi
Mimi mke wangu amepitiliza muda wa kujifungua, hii imekaaje? na nini cha kufanya sasa?
Majibu
Kupitiliza muda wa kujifungua ni jambo linalowatokea baadhi ya wanawake wajawazito na linaweza kuleta wasiwasi kwa familia. Kwa kawaida, ujauzito huchukua wiki 40 kuanzia siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho, na huweza kuhitimishwa kati ya wiki ya 37 hadi 42. Ujauzito unapozidi wiki 42 bila mama kujifungua, hali hii huitwa ujauzito uliopitiliza muda au kupitiliza muda wa kujifungua.
Sababu za kupitiliza muda wa kujifungua
Kupitiliza tarehe ya kujifungua kunaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:
Kukosea katika kuhesabu tarehe sahihi ya kujifungua
Hasa kama mama ana mzunguko wa hedhi usio wa kawaida au hajakumbuka tarehe ya mwisho ya hedhi.
Kukosa ultrasound ya mapema (chini ya wiki 14) huongeza uwezekano wa makosa ya tarehe.
Historia ya kupitiliza kwenye mimba za nyuma
Ikiwa mama aliwahi kuchelewa kujifungua hapo awali, kuna uwezekano mkubwa hali hiyo kujirudia.
Ujauzito wa mara ya kwanza
Wajawazito wa mara ya kwanza huwa na nafasi kubwa ya kupitiliza muda.
Urithi wa familia (genetics)
Ikiwa mama au wanawake wa familia yake walikuwa wakichelewa kujifungua, inaweza kuwa ni kurithi tabia hiyo.
Mtoto wa kiume
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa watoto wa kiume huwa na uwezekano mkubwa wa kuzaliwa baada ya tarehe ya makadirio.
Unene wa kupindukia (BMI kubwa)
Uzito mkubwa kwa mama unahusishwa na ucheleweshaji wa uchungu kuanza.
Matatizo ya homoni aukondo la nyuma
Mfano: upungufu wa prostaglandins zinazochochea uchungu, au placenta kuchelewa kuzeeka.
Hatari zinazoweza kutokea kwa kupitiliza muda
Ujauzito wa zaidi ya wiki 42 unaweza kuambatana na matatizo yafuatayo:
Kupungua kwa maji ya uzazi (Maji ya chupa ya uzazi) – Hali hii huathiri ustawi wa mtoto tumboni.
Kondo la nyuma kuchakaa – Hupunguza uwezo wa kutoa virutubisho na oksijeni kwa mtoto.
Mtoto kuwa mkubwa sana (macrosomia) – Inaweza kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwa hatari au mgumu.
Matatizo ya kupumua kwa mtoto baada ya kuzaliwa.
Kuwa na haja ya kufanyiwa upasuaji (C-section).
Hatari ya kifo cha mtoto tumboni au muda mfupi baada ya kuzaliwa (kwa nadra lakini huwezekana).
Nini cha kufanya iwapo muda umepitiliza?
Ikiwa ujauzito umefika au kuzidi wiki 41, ni muhimu kuchukua hatua zifuatazo:
Kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa hali ya mtoto na mama:
Kupima kiwango cha maji ya uzazi na kukadiria afya ya mtoto.
Kupima mapigo ya moyo ya mtoto.
Kuanzisha uchungu kwa njia ya kitaalamu:
Kama hakuna dalili za uchungu na hali ya mtoto ni ya kawaida, daktari anaweza kuanzisha uchungu kwa kutumia dawa (kama oxytocin au prostaglandins), au kuchochea kwa njia nyingine kama kuchokonoa mlango wa kizazi.
Upasuaji wa kujifungua
Kama kuna viashiria vya hatari kwa mtoto au mama, daktari anaweza kupendekeza upasuaji.
Hitimisho
Kupitiliza muda wa kujifungua si jambo la ajabu, lakini linahitaji ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa wataalamu wa afya. Ikiwa mjamzito amefikisha au kuzidi wiki 41 bila uchungu kuanza, ni muhimu kupata uchunguzi wa kitaalamu haraka. Kufanya hivyo kunaweza kusaidia kuepuka hatari kwa mama na mtoto, na kuhakikisha usalama wa uzazi.
Ujumbe kwa wajawazito
"Usisubiri hadi uchungu uanze peke yake ukiwa tayari umefika wiki 41 au zaidi – muone mtaalamu wa afya mapema kwa uchunguzi na ushauri sahihi."
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
18 Mei 2025, 09:40:14
Rejea za mada hii
Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Dashe JS, Hoffman BL, Casey BM, et al. Williams Obstetrics. 25th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2018. p. 863–871.
American College of Obstetricians and Gynecologists. ACOG Practice Bulletin No. 146: Management of Late-Term and Postterm Pregnancies. Obstet Gynecol. 2014;124(2 Pt 1):390–6.
Mandruzzato G, Alfirevic Z, Chervenak F, Gruenebaum A, Heimstad R, Heimstad M, et al. Management of post-term pregnancy. J Perinat Med. 2010;38(2):111–20.
World Health Organization. WHO recommendations on induction of labour. Geneva: World Health Organization; 2011.
Caughey AB, Sundaram V, Kaimal AJ, Gienger A, Cheng YW, McDonald KM, et al. Maternal and neonatal outcomes of elective induction of labor. Evid Rep Technol Assess (Full Rep). 2009;(176):1–257.
Divon MY, Ferber A. Postterm pregnancy: How to manage, when to induce. Contemporary OB/GYN. 2003;48(12):34–49.
