top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

26 Aprili 2025, 19:39:32

Kutokwa usaa kwenye uume: Sababu za kujirudia na jinsi ya kukabiliana nazo

Kutokwa na usaa kwenye uume visababishi vya kujirudia ni nini na jinsi ya kukabiliana navyo?

Swali la msingi


Mwezi wa 11 mwaka jana nilipata tatizo la kutokwa na Usaa kwenye uume. Nilienda hospital nikapimwa wakasema ni maambukizi ya kawaida. Nikapewa Dawa ya maji na vidonge nilitumia na nikapona kabisa. But hili tatizo limejirudia tena leo hii tarehe 26 April. Mimi nina mke na mara ya mwisho tulikutana kimwili kama siku 5 hivi zimepita. Naomba ushauri wenu dawa gani nitumie na kipi naweza kufanya ili isirudie tena.


Majibu

Asante sana kwa kuelezea kwa uwazi hali yako. Pole sana kwa maumivu na usumbufu unaoupitia.

Kwa maelezo yako kutokwa na usaha kwenye uume mara mbili (Novemba mwaka jana na sasa tena Aprili) inaonyesha kuna maambukizi ya njia ya mkojo au uume  ambayo yanaweza kusababishwa na vimelea kama:


  • Bakteria wa kawaida (kama E. coli),

  • Maambukizi ya ngono (kama Gonorrhea au klamidia).


Hata kama mara ya kwanza waliita "maambukizi ya kawaida", kurudia kwa tatizo kunaweza kuashiria:

  • Maambukizi hayakuisha kabisa mara ya kwanza, au

  • Kuna maambukizi mapya, au

  • Unaweza kuwa na maambukizi ya ngono yasiyotibika kwa dawa ulizotumia mwanzo.


Ushauri wangu wa haraka

  1. Usianze kutumia dawa bila kupima tena au ushauri wa daktari. 

    • Kusanya mkojo wa mwanzo wa asubuhi kwa ajili ya kupima vimelea vya ngono (Gonorrhea, klamidia),

    • Kupima mkojo wa kawaida

    • Ikiwezekana pia kuchukua usaha kutoka kwenye uume kwa kipimo cha "Kuotesha vimelea".

  2. Usitibie tu peke yako bila mke wako kupima:Kama una maambukizi ya ngono, hata ukitibiwa wewe peke yako bila mkeo kutibiwa, utarudishiwa tena maambukizi.

  3. Dawa zinazotumika kwa maambukizi kama haya zinategemea na vimelea vinavyosababisha tatizo hili. Unaweza pewa mchanganyiko wa dawa kama itashauriwa na daktari kulingana na majibu ya vipimo.


Mambo ya kuzingatia ili isirudie tena

  • Kamilisha dozi ya dawa yote kwa uaminifu.

  • Pima na mke wako pia (hata kama hana dalili).

  • Epuka tendo la ndoa hadi utakapomaliza matibabu na dalili zimetoweka.

  • Hakikisha unafuata usafi wa sehemu za siri vizuri.


Kwa kifupi

  • Nenda hospitali upimwe tena kabla ya kutumia dawa yoyote.

  • Pimeni wote wawili (wewe na mkeo).

  • Tumia dawa baada ya majibu sahihi kutoka kwa daktari, na mtumie wote wawili(au yeyote unayeshiriki naye ngono) hata kama hana dalili.


Ufanye nini ukiwa nyumbani?

Ushauri wa nini cha kufanya nyumbani kwa mtu anayetokwa na usaa kwenye uume;


1. Safisha sehemu za siri kwa uangalifu:

  • Tumia maji safi na sabuni isiyo na kemikali kali.

  • Safisha kwa upole mara mbili kwa siku ili kuondoa usaha na kuzuia kuenea kwa maambukizi.

2. Epuka kujichua au kushika uume bila sababu:

  • Kugusa mara kwa mara kunaweza kusambaza maambukizi zaidi au kuingiza vijidudu vingine.

3. Epuka kufanya ngono hadi utakapopona

  • Ngono inaweza kuongeza maambukizi au kuambukiza mwenza. Tumia kondomu kama utashindwa.

4. Vaa nguo za ndani safi na za pamba:

  • Pamba huruhusu hewa kupita na husaidia sehemu za siri kukauka vizuri, kupunguza unyevunyevu unaoweza kustawisha bakteria.

5. Kunywa maji mengi:

  • Husaidia kusafisha mfumo wa mkojo na kupunguza maumivu wakati wa kukojoa.

6. Tumia dawa za kupunguza maumivu ikiwa kuna maumivu makali:

  • Mfano: Paracetamol 500mg–1000mg kila masaa 6 inapohitajika.

7. Usitumie dawa za antibayotiki bila ushauri wa daktari:

  • Matibabu sahihi yanategemea chanzo cha maambukizi (k.m. Kisonono, Klamidia, Trikomonasi nk.).

  • Dawa zisizo sahihi zinaweza kuzidisha tatizo na kuongeza usugu wa vimelea.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

26 Aprili 2025, 19:50:17

Rejea za mada hii

  1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

  2. Barbee LA. Sexually Transmitted Urethritis: Epidemiology, Diagnosis, and Management. Infect Dis Clin North Am. 2013 Dec;27(4):755–64.

  3. Horner PJ. The natural history of untreated chlamydia infection. Curr Opin Infect Dis. 2006 Feb;19(1):49–54.

  4. Centers for Disease Control and Prevention. Gonorrhea - CDC Fact Sheet (Detailed). CDC; 2022. Available from: https://www.cdc.gov/std/gonorrhea/stdfact-gonorrhea-detailed.htm

  5. Martin DH. The microbiology of urethral infections in men. Clin Infect Dis. 2008 Jun 1;46(Suppl 2):S23–6.

bottom of page