top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

Imeboreshwa:

8 Juni 2025, 14:06:53

Kwa nini hedhi yangu imekoma kwa muda mrefu? Je, natakiwa kutumia dawa gani Ili irudi?

Kwa nini hedhi yangu imekoma kwa muda mrefu? Je, natakiwa kutumia dawa gani Ili irudi?

Swali la Msomaji


"Nimepoteza hedhi kwa miaka minne sasa, je, natakiwa kutumia dawa gani ili nirudishe hedhi kama kawaida?"


Majibu ya Kitaalamu

Kutokupata hedhi kwa muda mrefu kama miaka minne ni hali inayoitwa kitiba kama amenorea. Amenorea inaweza kuwa ya Kuzaliwa nayo kama msichana hajawahi kupata hedhi hadi kufikia umri wa miaka 16 au ya kutokea baadae kama mwanamke aliyewahi kupata hedhi anaacha kupata kwa zaidi ya miezi 3–6 au zaidi.


Visababishi vya kukopsa hedhi kwa muda mrefu

Hali hii inaweza kusababishwa na sababu mbalimbali kama:


1. Matatizo ya homoni
  • Tezi tharoid (Upungufu au kuzidi kwa homoni thairoidi)

  • Kuzidi kwa homoni ya prolactin

  • Homoni za uzazi (FSH, LH, estradiol) zilizo katika viwango visivyokawaida


2. Matatizo ya ovari
  • Sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi

  • Upungufu wa hifadhi ya mayai

  • Komahedhi ya mapema


3. Matatizo ya mfuko wa uzazi

Makovu ndani ya mfuko wa uzazi (Sindromu ya Asherman), hasa baada ya kuharibu mimba au upasuaji


4. Mambo ya mtindo wa maisha

Msongo mkubwa wa mawazo

  • Mazoezi ya kupita kiasi

  • Kupungua sana kwa uzito au kunenepa kupita kiasi


5. Matumizi ya dawa au historia ya upasuaji
  • Dawa zinazobadilisha homoni kama dawa za uzazi wa mpango.

  • Historia ya upasuaji wa nyonga, ovari au mfuko wa uzazi


Je, Kuna Dawa ya Moja kwa Moja ya Kurudisha Hedhi?

Jibu fupi ni hapana.Hakuna dawa moja tu ya kichunguu ya kuanza kutumia bila kujua chanzo cha tatizo.Kuanza dawa bila uchunguzi wa kitaalamu kunaweza kuharibu afya zaidi au kupoteza muda muhimu wa kupata tiba sahihi.


Uchunguzi unaotakiwa kufanyika

Kabla ya kuanza matibabu yoyote, mwanamke mwenye tatizo hili anapaswa kufanya uchunguzi wa awali ambao unajumuisha:

  • Historia ya afya ya uzazi na ya jumla

  • Vipimo vya damu vya homoni:

    • FSH, LH, estradiol

    • Prolactin

    • TSH (thyroid)

  • Ultrasound ya nyonga kuangalia hali ya ovari na mfuko wa uzazi

  • Ikiwa kuna viashiria, vipimo zaidi vinaweza kupendekezwa


Matibabu

Matibabu Hutegemea Sababu, baada ya uchunguzi, daktari atapendekeza matibabu yanayofaa, kama vile:

  • Tiba ya homoni kama kuna upungufu au mabadiliko ya homoni

  • Tiba ya sindromu ya ovari yenye vifukomaji vingi kama hiyo ndiyo sababu

  • Tiba ya matatizo ya tezi (Thairoidi)

  • Tiba ya makovu ndani ya mfuko wa uzazi (kwa mfano kwa upasuaji mdogo wa hysteroscopy)

  • Mabadiliko ya mtindo wa maisha kama sababu ni lishe duni, mazoezi kupita kiasi, au msongo mkubwa


Wakati mwingine daktari anaweza kutumia projesteroni (mfano: medroxyprogesterone acetate kwa siku chache) ili kuona kama mzunguko wa hedhi unaweza kurudi, lakini hii inafanyika chini ya uangalizi wa daktari tu, baada ya uchunguzi kamili.


Ushauri wa kitaalamu

Ikiwa umekosa hedhi kwa zaidi ya miezi 3–6, na zaidi hasa kwa muda wa miaka 4, ni muhimu sana kuonana na daktari au mtoa huduma ya afya haraka.Hii ni hatua ya kwanza kuelekea tiba sahihi. Kuanza kutumia dawa yoyote bila uchunguzi kunaweza kuwa hatari kwa afya yako.


Jihadhari: Dawa za kienyeji au dawa za mitaani zinazodai "kurudisha hedhi" mara nyingi hazina uthibitisho wa usalama wala ufanisi na zinaweza kuharibu afya ya uzazi.


Hitimisho

Kutokupata hedhi kwa muda wa miaka 4 ni hali inayoashiria kuwa kuna sababu kubwa ya msingi inayohitaji kutambuliwa na kutibiwa. Matibabu bora zaidi hutegemea utambuzi sahihi wa chanzo cha tatizo. Unashauriwa utafute msaada wa kitaalamu mapema, hili ni tatizo linaloweza kutibika mara nyingi, lakini lisiposhughulikiwa linaweza kuwa na madhara ya muda mrefu kwa afya ya uzazi.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

8 Juni 2025, 14:06:53

Rejea za mada hii

  1. Practice Committee of the American Society for Reproductive Medicine. Current evaluation of amenorrhea. Fertil Steril. 2008;90(5 Suppl):S219–25.

  2. ACOG Practice Bulletin No. 222: Amenorrhea. Obstet Gynecol. 2020;136(4):e111–e122.

  3. World Health Organization. Selected practice recommendations for contraceptive use. 3rd ed. Geneva: WHO; 2016.

  4. Ministry of Health, Tanzania. Muongozo wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto. Dar es Salaam: MoHCDGEC; 2022.

bottom of page