Jibu: Hapana, hakuna ushahidi wa tafiti iliyoangalia ufanisi wa tiba hii pekeyake katika kutibu kiharusi cha hivi punde.
Uvumi:
Kuna uvumi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii unaodai kwamba ‘Kutoboa miishio ya vidole 10 vya mikono vya mtu aliyepatwa na stroke huokoa maisha yake kwa kurejesha fahamu, kuondoa stroke na kuzuia uharibifu unaoweza kusababishwa na stroke.
Uvumi umedai zaidi kwamba ‘kama mgonjwa mdomo wake umepinda, vuta masikio yake mpaka damu ivilie kisha yatoboe kwa sindano mpaka yatoe damu’. Uvumi huu unaamini kuwa ‘kufanya hivi kunazuia kupasuka kwa mishipa ya damu ya mtu aliyepigwa na stroke’. Uvumi huu umeendelea unadai kwamba ‘njia hii ina ufanisi wa asilimia 100 na inaweza kuokoa maisha ya mtu aliyepata stroke’.
Picha: Sindano nyembamba sana inayotumika kwenye tiba ya kutoboa mwili
Baada ya kupata uvumi huu timu ya ULY CLINIC iliamua kurejea kwenye tafiti zilizowahi kufanyika na kuchapishwa kwenye majarida ya afya yanayoaminika (ikiwa pamoja NCBI na Science direct) na kurejea kwenye vyanzo maalumu ili kutoa majibu kuhusu kutoboa vidole vya mikono katika tiba asili ya stroke.
Ujumbe huu umeanza kuvuma lini?
Baada ya kufanya uchunguzi wa habari hii mtandaoni inaonekana kuwa, ujumbe huu umeanza kusambaa mtandaoni tangu mwaka 2003.
Pia imeonekana kuwa tovuti ya ‘The New York Times’ imeshawahi kutolea majibu kuhusu uvumi huu kuwa ni wa kupotosha jamii, majibu yalitolewa na wataalamu wa afya katika kitengo cha kiharusi, kutoka Duke stroke centre.
Tiba ya kutoa damu kwa kutoboa vidole imekuwepo tangu lini?
Inaonekana kuwa tiba ya kutoboa vidole kwenye maeneo ya ‘The 12 jing well-point’ ina zaidi ya miaka 30 sasa. Tiba hii inatumika huko China kama tiba asili ya kutibu magonjwa mbalimbali na hufanywa na wataalamu kwa umakini mkubwa.
Stroke ni nini na hutokeaje?
Stroke hufahamika pia kama kiharusi, ni uharibifu wa tishu za ubongo kutokana na kukatwa kwa mzunguko wa damu kunakosababisha ubongo kukosa oksijeni.
Aina za kiharusi
Kuna aina mbalimbali za kiharusi, kiharusi cha ‘kupasuka kwa mshipa wa damu’ na kiharusi cha ‘kuziba kwa mishipa wa damu’. Kiharusi cha kupasuka kwa mshipa wa damu husababishwa na kuvia kwa damu ndani ya ubongo wakati kiharusi cha kuziba kwa mshipa wa damu hutokana na kukosa damu sehemu zinazopelekewa damu na mshipa ulioziba. Maranyingi mishipa inayopasuka au kuziba huwa ile iliyo midogo.
Zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaopatwa na kiharusi hupatwa na kiharusi cha kuziba kwa mshipa wa damu katika ubongo. Endapo dalili za kiharusi hiki zitapotea ndani ya masaa 24, hufahamika kama kiharusi cha mpito cha kuziba kwa mshipa wa damu’. Tafiti zinaonyesha wagonjwa waliopata kiharusi cha mpito dalili zake hupotea ndani ya dakika chache.
Kiharusi cha kuziba kwa mshipa wa damu wa ubongo kinaweza kuambatana pia na kupasuka kwa mshipa midogo ya damu kwenye ubongo kutokana na uharibifu uliofanyika kwenye tishu na mshipa wa damu ulioziba.
Kutoboa masikio au vidole vya aliyepigwa na kiharusi kutasababisha kupoteza kiwango kidogo cha damu ambacho hakitaathiri mfumo mzima wa mzunguko wa damu, na hata kama kiwango kikubwa kitapotea kiasi cha kuathiri mzunguko wa damu, mgonjwa hatapata nafuu badala yake ataathirika zaidi kutokana na kupungukiwa zaidi oksijeni kwenye sehemu ya ubongo iliyoathirika.
Tafiti zinazoendana na uvumi huu
Tafiti zilizopitiwa na wataalamu wa ULY CLINIC ni kama zifuatazo:
Tafiti ya 1
Tafiti ya China iliyofanywa mwaka 2005 na chuo cha tiba asili china kinachoitwa Tianjin College of Traditional Chinese Medicine iliyochunguza ‘Madhara ya kutoa damu kwa kuchoma sindano maeneo 12 ya mikono kwenye ufahamu na mapigo ya moyo ya mgonjwa aliyepoteza fahamu kutokana na degedege’ na kuja na majibu yafuatayo:
Kuchoma sindano ya kutoa damu maeneo 12 ya mkono huimarisha ufahamu na kuongeza shinikizo la damu la systolic kwa wagonjwa wenye majeraha ya wastani kwenye ubongo kutokana na kupigwa degedege. Hata hivyo, itambulike kuwa wagonjwa hawa walioonekana kupata matokeo chanya walitambulika kitaalamu, walilazwa hospitali na kupatiwa matibabu ya kitaalamu mbali na kutobolewa pia walikuwa na majeraha ya wastani kutokana na degedege.
Watafiti hawa hawajashauri wala kusema kuwa njia hii ya kutoa damu kwa kutoboa mikono itumike kama tiba ya awali nyumbani kwa wagonjwa waliopatwa na kiharusi hivi punde badala ya kutafuta msaada wa haraka kutoka kwa wataalamu wa afya.
Picha. Baadhi ya maeneo 12 ya 'The 12 Jing well-point'
Tafiti ya 2: Makala ya mapitio ya tafiti mbalimbali kuhusu ufanisi wa tiba hii
Makala hii ilipitia tafiti mbalimbali zilizofanyika kuangalia madhara ya kutoa damu kwa kutoboa kwa pini maeneo 12 yanayofahamika kama ‘The 12 jing well-point’ kwenye matibabu ya uharibifu mkali wa hivi punde kwenye mfumo wa kati wa fahamu na namna inavyofanya kazi.
Majibu ya mapitio ya tafiti
Majumuisho ya mapitio ya tafiti mbalimbali kwenye makala hiyo ilionyesha kuwa aina hii ya tiba inaweza kuimarisha fahamu kutokana na bughudha iliyotokea kwenye mfumo wa fahamu, madhaifu kwenye mishipa ya fahamu, kuvimba kwa tishu za ubongo kutokana na kiharusi, majeraha kwenye ubongo kutokana na ajali na kuathiriwa na sumu ya ukaa.
Tiba hii imeonekana kufanya kazi kwa kuongeza mzunguko wa damu na kiwango cha oksijeni kwenye tishu za ubongo pamoja na kurekebisha kiwango cha chuma.
Wachunguzi wa tafiti wameshauri majaribio ya kitaalamu yafanyike ili kuchunguza kwa undani ufanyaji kazi wa tiba hii kabla ya kutumika kwa binadamu hapo mbeleni.
Hitimisho kutoka ULY CLINIC kuhusu tiba ya kiharusi kwa kutoboa vidole
Kwa kutumia tafiti, timu ya ULY CLINIC inapenda kuhitimisha kwa kutumia tafiti na makala zilizo kwenye rejea kwamba;
Kwa kuwa tafiti nyingi zilizofanywa kuangalia ufanisi wa matibabu haya zilitumia wagonjwa waliokuwa wanapata matibabu ya kitaalamu mbali na matibabu ya kutoboa mikono maeneo ya ‘The 12 jing well-point’, ni vigumu kusema kuwa tiba aina hii pekee inaweza kuokoa maisha ya mgonjwa.
Tafiti zaidi zinahitajika kudhihirisha kwamba tiba aina hii inaweza kufanya kazi kwa kujitengemea. Na kama tiba itaruhusiwa kutumika basi inapaswa kufanywa na mtaalamu wa afya aliyesajiliwa na mabalaza ya wataalamu husika kutoa aina hii ya tiba.
Inashauriwa siku zote kutafuta msaada wa haraka kutoka kwa wataalamu wa afya ili kuokoa maisha ya mgonjwa wa kiharusi na madhara yanayoweza kujitokeza, mgonjwa anapaswa kutibiwa kama mgonjwa wa dharura.
Jinsi utakavyomuwahisha aliyepigwa na kiharusi hospitali na kupata tiba, utapunguza uwezekano wa kiharusi kuathiri sehemu kubwa ya ubongo.
Pia madaktari wabobezi kwenye mfumo wa fahamu wanashauri mgonjwa aliyepigwa kiharusi kuwahishwa hospitali kwani kila dakika inathamani katika matibabu yake.
Wapi utapata maelezo zaidi?
Unaweza pata maelezo zaidi kwa kuwasiliana na daktari wako.
Unaweza kusoma kwa undani makala zinazohusu aina za kiharusi, dalili, matibabu na namna ya kutoa huduma ya kwanza baada ya kuwasiliana na namba ya msaada wa dharura (112), kwa kubofya linki zinazofuata:
Rejea za mada hii
Yi G, Xiuyun W, Tangping X, Zhihua D, Yunchen L. Effect of blood-letting puncture at twelve well-points of hand on consciousness and heart rate in patients with apoplexy. J Tradit Chin Med. 2005 Jun;25(2):85-9. PMID: 16136931.
Zhu QM, Yu NN, Liu BH, Guo Y, Chen ZL, Tang HL, Li SS, Xu ZF. [Research advances in the clinical effect of bloodletting puncture at well-points in treatment of acute central nervous injury]. Zhen Ci Yan Jiu. 2019 Nov 25;44(11):854-7. Chinese. doi: 10.13702/j.1000-0607.180167. PMID: 31777238.
Li GD, Han YS. [Research advances in neurovascular unit mechanism in acupuncture treatment of ischemic stroke]. Zhen Ci Yan Jiu. 2019 Dec 25;44(12):863-6. Chinese. doi: 10.13702/j.1000-0607.190275. PMID: 31867903.
Zhu W, Ye Y, Liu Y, Wang XR, Shi GX, Zhang S, Liu CZ. Mechanisms of Acupuncture Therapy for Cerebral Ischemia: an Evidence-Based Review of Clinical and Animal Studies on Cerebral Ischemia. J Neuroimmune Pharmacol. 2017 Dec;12(4):575-592. doi: 10.1007/s11481-017-9747-4. Epub 2017 May 19. PMID: 28527041.
American Stroke Association. Warning signs.http://www.strokeassociation.o ccessed Aug. 25, 2017rg/STROKEORG/WarningSigns/Stroke-Warning-Signs-and-Symptoms_UCM_308528_SubHomePage.jsp. Imechukuliwa 29.05.2022.
National Stroke Association. Understand stroke. http://www.stroke.org/understand-stroke?gclid=CjwKEAjwlf_MBRDU7f7nlqqcz0ESJAA_Bo_Am2GBIUK3wUEnJ9umkpLiH_Z2EhZFXTe7rLjZx5640xoCcWDw_wcB. Imechukuliwa 29.05.2022.
American College of Emergency Physician. Emergency care for you: Stroke. http://www.emergencycareforyou.org/Emergency-101/Emergencies-A-Z/Stroke/. Imechukuliwa 29.05.2022.
コメント