top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Helen L, M.D

Alhamisi, 4 Februari 2021

Maji na mafuta ni miongoni mwa tiba ya kupasuka midomo

Maji na mafuta ni miongoni mwa tiba ya kupasuka midomo

Kupasuka midomo ni tatizo linalowapata watu wengi kwa nyakati mbalimbali ndani ya mwaka. Visababishi vinaweza kuwa hali ya hewa ya baridi au yenye ukavu, kuungua na mwanga wa jua, kupulizwa na upepo mkali, kulamba midomo na kupumua kupitia mdomo. Kunywa maji ya kutosha, paka mafuta au 'lip balm' na kujifunika midomo huwa ni tiba pia kinga.


Dalili


Watu wengi hupata tatizo la kukauka kwa midomo mara kwa mara, kukauka kwa midomo huonekana na dalili zifuatazo;


  • Kutokwa na damu

  • Vidonda

  • Kupata magamba meusi

  • Homa ya baridi

  • Kukauka kwa midomo

  • Kubadilika rangi ya midomo au kuvimba


Visababishi vikuu


Visababishi vikuu vya kupasuka midomo ni vitu vya kawaida kama vile;


  • Hali ya hewa ya baridi

  • Hali ya hewa yenye ukavu

  • Kuchomwa na mwanga wa jua

  • Joto kali ndani ya nyumba

  • Kupulizwa na upepo mkali

  • Kupungukiwa maji mwilini

  • Homa baridi

  • Kulama midomo

  • Matumizi ya baadhi ya vipodozi na lip balm


Visababishi vya nadra


Kwa nadra sana kupasuka midomo huweza kusababishwa na;


  • Kutoa pumzi kupitia mdomo

  • Mzio(aleji) kwenye baadhi ya mazao unayotumia kama 'rangi ya midomo' na 'lip balm'

  • Maambukizi ya kirusi cha herpes simplex

  • Utapiamlo

  • Kuishiwa maji mwilini

  • Upungufu wa baadhi ya vitamin


Matibabu ya nyumbani


Endapo umepata tatizo la kupasuka midomo, huna haja ya kuhofu kwa sababu tatizo hili mara nyingi husababishwa na sababu za kawaida. Fanya mambo yafutayo ili kujitibu nyumbani.


  • Paka midomo yako mafuta ya mgando yaliyotengenezwa kwa kutumia 'Petroleum' yasiyo na manukato au tumia lip balm maalumu zenye niacin au 'zinc oxide' au 'white petrolatum', au 'essential fatty acids' za kulainisha midomo. Tembea na mafuta au lip balm ili kutumia kila mara midomo yako inapoonyesha ishara ya kukauka

  • Kunywa maji ya kutosha kama inavyoshauriwa kiafya, unaweza kutembea na chupa ya maji na kunywa unapohisi kiu au midomo kukauka

  • Acha mazoea ya kulamba midomo yako, majimaji ya mate yanapokauka husababisha midomo kukauka

  • Jifunike kwa kitambaa au leso maeneo ya midomo endapo unasafiri kwenye upepo au jua kali


Mambo ya kufanya endapo tatizo halijaisha


Matibabu ya nyumbani yanaweza kuchukua kuanzia siku tatu hadi mwezi kuondoa tatizo kabisa. Kama umetumia njia za matibabu ya nyumbani kwa kipindi hicho, bila kupata matokeo chanya, au kuonekana kwa dalili mbaya za maambukizi, wasiliana na daktari wako mara moja kwa ushauri zaidi, uchunguzi na tiba.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

19 Julai 2023 20:41:55

Rejea za mada hii:

1.American Academy of Dermatology. Dry skin relief. https://www.aad.org/public/skin-hair-nails/skin-care/dry-skin-relief. Imechukuliwa 03.02.2021

2.American Academy of Dermatology. Dry skin: Tips for managing. https://www.aad.org/public/diseases/dry-sweaty-skin/dry-skin. Imechukuliwa 03.02.2021

3. Beenish S. Bhutta, et al. Cheilitis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK470592/. Imechukuliwa 03.02.2021

4. Liborija Lugović-Mihić, et al. DIFFERENTIAL DIAGNOSIS OF CHEILITIS – HOW TO CLASSIFY CHEILITIS. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC6531998/. Imechukuliwa 03.02.2021

5. Nathan S. Trookman, MD, et al. Clinical Assessment of a Combination Lip Treatment to Restore Moisturization and Fullness. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2923945/. Imechukuliwa 03.02.2021

bottom of page