top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Alhamisi, 9 Septemba 2021

Majibu 7 ya kipimo cha HIV 1/2 SD bioline 3.0

Majibu 7 ya kipimo cha HIV 1/2 SD bioline 3.0

Kipimo cha SD bioline huweza kutoa aina 7 za majibu yanayopaswa kutafsiriwa kwa usahihi. Kufahamu aina hizo kabla ya kufanya kipimo huepusha gharama na athari zinazoweza kutokea kwa mpimaji na anayejipima mwenyewe.


Kwanini ufahamu aina 7 za majibu kabla ya kufanya kipimo cha HIV 1/2 SD Bioline 3.0?


Watu wengi wamezoea kusoma majibu ya kawaida ya kipimo cha HIV 1/2 SD bioline 3.0, majibu tofauti yanapotokea, utafsiri wa watu wengi hubadilika na hivyo kutoa majibu yasiyo sahihi ambayo huweza pelekea gharama zisizotarajiwa na kuathiri maisha ya anayepimwa kwa kuanza dawa pasipo kuwa na uhaja wa kuanza dawa au kwa kujifahamu kuwa hana maambukizi wakati anavyo. Uelewa wa aina tofauti za majibu ni muhimu sana kwa sababu hiyo.


Katika makala hii, majibu ya kipimo yanatakiwa kufanyika ndani ya muda wa dakika 10 hadi 20. Baada ya muda huu, majibu si ya kutegemewa.


Aina 7 za majibu ya kipimo cha HIV ½ SD bioline


Majibu ya HIV SD bioline 3.0 kinachotumika kupima uwepo wa maambukizi ya VVU1 na VVU2 (HIV1 na HIV2) kwenye damu ni;


  1. Majibu chanya ya HIV1/2- huonekana kama mstari umejichora kwenye alama namba 1, 2 na C (angalia picha namba A)

  2. Majibu chanya ya HIV1- huonekana kama mstari umejichora kwenye alama namba 1 na C (angalia picha namba B, F na G)

  3. Majibu chanya ya HIV2- huonekana kama mstari umejichora kwenye alama namba 2 na C (angalia picha namba C)

  4. Majibu hasi ya HIV2- huonekana kama mstari umejichora kwenye alama namba C tu (angalia picha namba D)

  5. Majibu batili ya HIV- huonekana kama mstari umejichora kwenye alama namba 1 au 2 tu bila kuonekana kwa mstari mwingine kwenye alama C (angalia picha namba E)

  6. Majibu ya kueleweka huonekana pale endapo mistari iliyojichora inaonekana vema kama kwenye picha A, B,C, D na E

  7. Majibu yanayohitaji umakini kusomwa ni yale yanayokuhitaji umakini wako katika kutofautisha ukali wa rangi, Mfano majibu kwenye picha F ni ‘majibu chanya ya HIV1’ au uwezo wa kuona mstari uliofifia katika kipimo kama kwenye picha namba G yanayomaanisha ‘majibu chanya ya HIV 1’


Nani anaweza kufanya kipimo hiki cha HIV SD bioline


Kwa Tanzania kipimo cha HIV1/2 SD bioline hufanywa na mtaalamu wa afya aliyefundishwa mbinu mbalimbali za kutoa ushauri na elimu inayohusu VVU, hatima na matibabu. Elimu hii ni muhimu kwa mpimwaji kuipata kabla ya kupima ili kabla au baada ya kupima aweze kuchukua hatua sahihi. Hata hivyo mtu yeyote anaweza kufundishwa namna ya kupima na kutafsiri majibu ya kipimo hiki, kitakachokosekana na namna ya kukabiliana mteja mwenye majibu chanya au hasi.


Majibu hasi isiyo kweli


Upimaji mbaya wa majibu, haswa kwa mistari ambayo haionekani vema huchangia kutoa majibu hasi isiyo kweli. Jambo hili linaweza kufanywa na mtu au mtaalamu wa afya asiye na uzoefu wa kusoma majibu au kutokuwa na elimu ya ziada kuhusu majibu mbalimbali ya kipimo cha HIV SD bioline 3.0


Majibu chanya isiyo kweli


Majibu chanya isiyo kweli hutokea kama kipimo kimeonyesha kuwa mpimwaji ana maambukizi ya VVU wakati kiuhalisia hana majibu hayo( baada ya kuthibitisha kwa vipimo vingine). Majibu haya huweza kusababishwa na msomaji kama hajatafsriri/ kusoma majibu kama inavyotakiwa. Kwa kufahamu namna sahihi ya kusoma majibu kutaepusha majibu chanya isiyo kweli na madhara yake yanayoweza kujitokeza.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

6 Oktoba 2021 16:17:09

Rejea za mada hii:

Chiu, et al. Photographed Rapid HIV Test Results Pilot Novel Quality Assessment and Training Schemes. PloS one. 6. e18294. 10.1371/journal.pone.0018294. Imechukuliwa 09.09.2021

Chappel RJ, et al. Immunoassays for the diagnosis of HIV: meeting future needs by enhancing the quality of testing. Future Microbiol 4: 963–982.

bottom of page