Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Helen L, M.D
Alhamisi, 21 Januari 2021
Usipende kutumia nishati kutoka kwenye vinywaji
Vinywaji vyenye sukari huwa na nishati nyingi zaidi ya ile inayohitajika na mwili wako. Nishati ya ziada huchangia kupata uzito mkubwa kupita kiasi. Tumia vyakula vigumu kudhibiti uzito na kujikinga na magonjwa mengi.
Kwanini usitumie vinywaji vyenye sukari?
Vinywaji vingi vyenye sukari huwa na nishati nyingi zaidi ya ile inayohitajika na mwili wako. Licha ya kuwa na sukari nyingi, mwili wa binadamu huwa hautosheki kirahisi na sukari kutoka kwenye vinywaji kama ilivyo kutoka kwenye vyakula vigumu. Mtu anayetumia vinywaji hivyo, huhitaji kutumia mara kwa mara, au kila baada ya muda mfupi kupita bila njaa kukata
Kwa kawaida mwili unahitaji nishati kidogo ili uweze kufanya kazi mbalimbali ikiwa pamoja na kutembea, kulima, kuendesha gari, kufikiria, kuandika n.k. Nishati ya awali ambayo inatumika sana mwilini hutengenezwa kutoka kwenye sukari yenye jina la glucose. Vinywaji vingi vya kusindikwa kama soda, vinywaji vya kutia nguvu(energy drink) n.k vimewekewa sukari kwa wingi ambayo huzidi kiwango ambacho kinahitajika kwa siku na pia huddanganya ubongo na kufanya upende kuvitumia mara nyingi. Unashauriwa endapo hutegemei kufanya kazi nzito, usitumie vinywaji vya kusindikwa venyesukari.
Kwa nini utumie sukari itokanayo na vyakula badala ya vinywaji?
Sababu ni pamoja na;
Chakula kinapokuwa kinatafunwa toka mdomoni na kugusa mfumo wa chakula, hugusa chembe maalumu zinazotuma taarifa kwenye ubongo wako ili utoe vimeng'enya mbalimbali kumeng'enya chakula hicho. Baada ya kiasi kadhaa cha chakula kupita katika mfumo wa chakula na kuingia tumboni, chembe hizo hutuma taarifa zingine ili zikufanye ujihisi umeshiba, hii ni tofauti na wakati unakunywa vinywaji, taarifa za kushiba huchelewa kwenda kwenye ubongo na pia hushindwa ruhusu mwili wako kutoa vimeng'enya na homoni ambazo zinakufanya ujihisi umeshiba. Matokeo yake ni kwamba utakunywa vinywaji vingi, utahisi umeshiba, lakini baada ya muda mfupi utapatwa na njaa tena mpaka ule kitu kigumu.
Chakula kigumu na chenye nyuzinyuzi, huwa na kiasi kidogo cha sukari, mwili pia hufyonza kiasi kidogo pia cha sukari kutoka kwenye chakula hicho na hivyo kusababisha kupata kiasi kinachotakiwa na mwili.
Vyakula vigumu ni vipi
Vyakula vigumu ni kama vile;
Vyakula asilia mfano matunda mbalimbali
Mazao ya nafaka na unga wa nafaka zisizokobolewa
Madhara yanayotokana na kutumia nishati nyingi kutoka kwenye vinywaji ni nini:
Madhara makubwa unayoweza kuyapata ni ongezeko la uzito lisilo la kawaida linalopelekea kupata hatari ya magonjwa mbalimbali kama vile; kisukari aina ya pili, mshituko wa moyo, kiharusi n.k
Taarifa zingine za afya unaweza pata wapi?
Endelea kusoma kuhusu makala zingine za kiafya katika linki ambazo zipo ndani ya tovuti hii.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
19 Julai 2023 20:41:55
Rejea za mada hii:
1.D P DiMeglio 1, etal. Liquid versus solid carbohydrate: effects on food intake and body weight. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/10878689/. Imechukuliwa 20.01.2021
2.An Pan 1 etal. Effects of carbohydrates on satiety: differences between liquid and solid food. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/21519237/. Imechukuliwa 20.01.2021
3.Jason MR Gill Naveed Sattar. Fruit juice: just another sugary drink? https://www.thelancet.com/journals/landia/article/PIIS2213-8587(14)70013-0/fulltext. Imechukuliwa 20.01.2021
4.Lenny R. Vartanian etal. Effects of Soft Drink Consumption on Nutrition and Health: A Systematic Review and Meta-Analysis. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC1829363/. Imechukuliwa 20.01.2021
5.D S Ludwig etal. Relation between consumption of sugar-sweetened drinks and childhood obesity: a prospective, observational analysis. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/11229668/. Imechukuliwa 20.01.2021
6.Sanjay Basu etal. The Relationship of Sugar to Population-Level Diabetes Prevalence: An Econometric Analysis of Repeated Cross-Sectional Data. https://journals.plos.org/plosone/article?id=10.1371/journal.pone.0057873. Imechukuliwa 20.01.2021