top of page

Mwandishi:

Dkt. Sospeter M, MD

Mhariri:

Dkt. Lugonda B, MD

2 Julai 2025, 18:34:05

Dawa Flibanserin

Dawa Flibanserin

Flibanserin ni dawa ya kuongeza hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake walioko katika umri wa kuzaa (bado hawajafikia kukoma hedhi). Dawa hii si ya kuongeza uwezo wa mwili kufanya tendo la ndoa moja kwa moja kama ilivyo kwa baadhi ya dawa kwa wanaume, bali hufanya kazi kwa kubadilisha vichocheo vya ubongo vinavyohusika na hisia na hamu ya tendo la ndoa.


Uzito na Fomu ya Flibanserin

Flibanserin hupatikana katika mfumo wa tembe zenye uzito wa miligramu 100, na humezwa kwa mdomo.

Dozi inayopendekezwa ni tembe moja (100 mg) kila usiku kabla ya kulala, kwa mfululizo kwa wiki kadhaa.


Dawa kundi moja na Flibanserin

Flibanserin ipo kwenye kundi la dawa zijulikanazo kama serotonin receptor modulators, ambazo hubadilisha uwiano wa vichocheo vya neva vinavyohusika na mhemuko na hamu ya tendo la ndoa. Kwa sasa, haina dawa nyingi kundi moja zinazotumika kwa wanawake, lakini kiutendaji, inahusiana na dawa zinazobadilisha viwango vya dopamine, norepinephrine, na serotonin.


Flibanserin hufanya nini?

Dawa hii hutibu tatizo linaloitwa Kukosa hamu ya tendo la ndao kwa wanawake — ambayo ni kupungua kwa hamu ya tendo la ndoa kwa muda mrefu, bila sababu nyingine za kiafya, kisaikolojia, au mahusiano.


Namna flibanserin inavyofanya kazi

Flibanserin hufanya kazi kwa kubadilisha uwiano wa vichocheo vya neva kwenye ubongo:

  • Huongeza dopamine na norepinephrine — ambavyo huongeza hamu ya tendo la ndoa.

  • Hupunguza serotonin — ambayo huzuia hisia za kingono.

Kwa kuboresha usawaziko huu wa kemikali, Flibanserin husaidia kurejesha hamu ya tendo la ndoa.


Watu wasiopaswa kutumia Flibanserin

Dawa hii haipaswi kutumiwa na:

  • Wagonjwa wenye mzio wa flibanserin

  • Wagonjwa wenye magonjwa ya ini

  • Wanaotumia pombe, kwa kuwa mchanganyiko huu unaweza kusababisha kushuka kwa shinikizo la damu  na kupoteza fahamu

  • Wanaotumia dawa zinazozuia kimeng’enya cha CYP3A4, kama erythromycin au ketoconazole


Utoaji taka za dawa mwilini

Flibanserin hutengenezwa kwenye ini na kutolewa nje ya mwili kupitia kinyesi na mkojo, baada ya kuvunjwavunjwa na ini kwa msaada wa kimeng'enya cha CYP3A4.


Matumizi ya Flibanserin kwa mama mjamzito

Hakuna taarifa kamili kuhusu usalama wa Flibanserin kwa mama mjamzito. Tafiti zimeonyesha hatari kwa wanyama, lakini bado haijathibitishwa kwa binadamu. Inashauriwa kutotumika wakati wa ujauzito isipokuwa kwa ushauri wa daktari.


Matumizi ya Flibanserin kwa mama anayenyonyesha

Kiasi kidogo cha dawa huingia kwenye maziwa ya mama, lakini bado haijulikani kama kina athari kwa mtoto. Hivyo, matumizi yake yanahitaji tahadhari kubwa na ushauri wa daktari.


Dawa zenye mwingiliano mkali na Flibanserin

Dawa hizi haziwezi kutumika pamoja na Flibanserin:

  • Ketoconazole

  • Itraconazole

  • Erythromycin

  • Clarithromycin

  • Ritonavir

  • Nefazodone

  • Pombe— imekatazwa kabisa


Dawa zenye mwingiliano wa wastani na Flibanserin

  • Dawa za usingizi

  • Dawa za msongo wa mawazo

  • Dawa za presha au moyo (kama propranolol)

  • Dawa za kifafa

Mgonjwa anapaswa kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa mtaalamu wa afya.


Maudhi madogo ya Flibanserin

Maudhi ya kawaida ni:

  • Kizunguzungu

  • Kichefuchefu

  • Kichwa kuuma

  • Uchovu

  • Kukosa usingizi


Maudhi makubwa ya nadra

  • Kushuka kwa presha ya damu

  • Kupoteza fahamu

  • Tatizo la ini

  • Mshtuko wa mzio (anafailaxksia)


Je endapo utasahau dozi ya Flibanserin ufanyaje?

Usipochukua dozi ya flibanserin wakati wa kulala, usitumie dozi hiyo asubuhi. Subiri hadi wakati wa dozi inayofuata (usiku ujao). Kamwe usitumie dozi mbili kwa mara moja.


Uhifadhi wa Flibanserin

  • Hifadhi dawa katika joto la kawaida

  • Iweke mbali na mwanga wa jua, joto kali, na unyevu mwingi

  • Iweke mbali na watoto


Upatikanaji Afrika/Tanzania:

  • Flibanserin haipatikani kirahisi Africa ikiwa pamoja na nchini Tanzania.

  • Si dawa maarufu kwenye maduka ya dawa ya kawaida.

  • Katika mazingira ya Afrika, tiba ya kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake mara nyingi hutegemea:

    • Ushauri wa kisaikolojia au ndoa

    • Mitishamba (kama mondia whitei, moringa, nk.)

    • Marekebisho ya mtindo wa maisha (lishe, usingizi, mazoezi)


Mbadala wa asili kwa Flibanserin:

  • Mondia whitei (Mkongoraa) – huaminika kuongeza hamu ya tendo la ndoa

  • Mlonge (Moringa oleifera) – huboresha afya ya homoni

  • Tangawizi (Ginger) – huongeza mzunguko wa damu na kuchochea hisia


Baadhi ya wataalamu wa tiba asili pia wana dawa ambazo hufanya kazi kama dawa hii ya Flibenserin na zinaweza kutumika kwa wanawake wenye uhitaji.

ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

2 Julai 2025, 18:34:05

Rejea za mada hii:-

1. Clayton AH, et al. Efficacy and safety of flibanserin in women with HSDD. J Sex Med. 2015.

2. U.S. FDA Prescribing Information – Flibanserin (Addyi). https://www.accessdata.fda.gov

3. ScienceDirect – Flibanserin Pharmacology. https://www.sciencedirect.com/topics/neuroscience/flibanserin
bottom of page