top of page

Mwanshishi:

Dkt. Sospeter M, MD

Mhariri:

Dkt. Lugonda B, MD

4 Novemba 2021 16:02:46

Vasograin

Vasograin ni dawa yenye mchanganyiko wa ergotamine tartrate, caffeine, paracetamol na prochlorperazine maleate inayotumika kuzuia na kutibu maumivu ya kichwa ya kipanda uso. Dawa hii hutolewa kwa kuandikiwa cheti na daktari.


Fomu na uzito wa dawa


Vasograin hupatikana kwenye fomu ya kidonge chenye uzito wa unaotegemea uzito wa dawa zilizotengeneza kidonge hiki ambazo ni;


  • Ergotamine tartrate 1 mg

  • caffeine 100 mg

  • Paracetamol 250 mg na

  • Prochlorperazine maleate 2.5 mg


Vasograin inafanyaje kazi?


Vasograin hufanya kazi kwa kuzuia uzalishaji wa kemikali zinazoamsha maumivu, pia huzuia ubongo kupata taarifa zinazoamsha kichefuchefu na kutapika kinachoambatana na maumivu ya kipanda uso.


Vasograin inatibu nini?


Vasograin hutumika mara nyingi katika matibabu ya maumivu ya kichwa ya kipanda uso.

Vasograin pia hutibu maumivu ya kichwa yanayotokana na mishipa ya damu.


Mambo ya kufahamu kuhusu vasograin


Ergotamine ni dawa inayofanya kazi ya kupunguza kipenyo cha mishipa ya damu. Huweza kudhuru pia mishipa ya damu ya pembeni na kupunguza kiasi cha damu kinachoingia kwenye moyo. Hivyo kama ikitumia kuzidi kiasi cha siku huweza pelekea hali na magonjwa yanayotishia uhai wa mtu kama vile gangrene na thrombosis


Prochlorperazine ni dawa ya antisaitokiti inayotumika kuzuia kutapika. Ikitumika kwa muda mrefu inaweza kupelekea kukakamaa kwa misuli, kutikisika bila sababu na kushindwa kufanya kazi yake vema.


Caffeine hufanya kazi ya kupunguza maumivu kwa kudhibiti adenosine mwilini, hivyo huamsha mfumo wa kati wa fahamu na misuli ili kuimairisha umetaboli.


Paracetamol ni dawa ya kutuliza maumivu.


Vasograin ni moja ya dawa inayotumiwa sana, na kutokana uwanda wa madhara yake, inashauriwa kuwa makini au kutumia dawa zenye usalama zaidi. Tafiti nyingi hazishauri kutumia vasograin katika matibabu ya kipanda uso kutokana na madhara yake.


Maudhi ya vasograin


Maudhi madogo ya kutumia vasograin ni;


  • Kusinzia

  • Kushuka kwa shinikizo la damu kwa haraka unapokuwa unasimama

  • Kuwa katika hali ya kulewa

  • Kutuwama kwa mkojo ndani ya kibofu

  • Kukauka midomo

  • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo

  • Haja ya shida

  • Maumivu ya misuli


Kama ukipata dalili endelevu zilizotajwa hapo juu, wasiliana na daktari wako mara moja.


Matumizi kwa mama mjamzito na anayenyonyesha


Vasograin si salama kwa mama mjamzito ana anayenyonyesha hivyo haipaswi kutumika kipindi hiki.


Unaweza tumia vasograin na pombe?


Hapana, vasograin haipaswi kutumika pamoja na pombe kutokana na kuwa na mwingiliano usio usalama.


Vidokezo muhimu kuhusu vasograin


Vasograin;


  • Hutumika kuzuia na kutibu kipanda uso

  • Isitumike kwa maumivu makali ya kichwa

  • Inatakiwa kutumika wakati wa usiku ukiwa unataka kulala

  • Inaweza kusababisha usinzie, epuka kutumia wakati unaendesha chombo cha usafiri

  • Usitumie vasograin na daw zingine zenye paracetamol

  • Usiache kutumia dawa hii ghafla kuepuka kupata maumivu makali sana ya kichwa.

ONYO: Usitumie dawa yoyote bila ushauri wa daktari. Dawa zinaweza kuleta madhara mwilini na pia matumizi ya baadhi ya dawa pasipo ushauri na vipimo husababisha  vimelea kuwa sugu dhidi ya dawa hiyo.
ULY clinic inakushauri kuwasiliana na daktari wako unapotaka kuchukua maamuzi yoyote yanayohusu afya yako.
Wasiliana na daktari/Mfamasia wa ULY clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kupiga simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

4 Novemba 2021 16:02:46

Rejea za mada hii:-

1. Mathew NT, et al. Transformed or evolutive migraine. Headache 1987 Feb;27(2):102-106.

2. Mahajan A, et al. Prolonged Abuse of Vasograin Tablets. Ind J Priv Psychiatry 2018;12(1):27-28.

3. Verma A. Transformed migraine: a study of 420 consecutive patients from central India. Ann Neurosci 2007 Apr;14(2): 37-40.

4. Diener HC, et al. Medication-overuse headache: a worldwide problem. Lancet Neurol 2004 Aug;3(8):475-483.

5. Kristoffersen ES, et al. Medication-overuse headache: a review. J Pain Res 2014 Jun;7:367-378.
bottom of page