top of page

Mwandishi:

Dkt. Salome A, MD

Mhariri:

Dkt. Sospeter B, MD

4 Februari 2022 19:57:35

Image-empty-state.png

Kichefuchefu na kutapika kwa mjamzito

Kichefu chefu na kutapika ni dalili zinazojitokeza sana wakati wa ujauzito, inakadiriwa kuwa asilimia 70 hadi 80 ya wajawazito hupata dalili hizi. Kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito hutokea sana katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito na dalili kupotea kuanzia wiki ya 22, hata hivyo asilimia 10 ya wanawake huwa na dalili endelevu hadi wakati wa kujifungua.


Dalili hizi zinaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na hali ya ujauzito au kuashiria maradhi/maambukizi ambayo yanaweza kutokea wakati wa ujuzito. Wajawazito wengi huwa na kichefuchefu na kutapika unakohusiana na hali ya ujauzito, ambapo inaweza kuwa kichefu chefu na kutapika kwa kawaida kunakojulikana kama homa za asubuhi, au kichefu na kutapika sana. Kichefu chefu na kutapika kusikohusiana na ujauzito husababishwa na magonjwa kama vile UTI, malaria, minyoo nk.


Hali ya kichefu chefu nakutapika humuweka mama katika hatari ya kukosa virutubisho muhimu kwa ujauzito kupitia chakula, wajawazito hasa wale wenye tatizo la kutapika sana huwa katika hatari ya kuwa na sonona, kupungukiwa damu, kuwa na uchungu kabla ya muda, kuzaa watoto wenye uzito mdogo nk.


Imezoeleka kuwa kichefuchefu na kutapika ni dalili za awali za ujauzito hivyo kumekuwa na changamoto ya kugundua maradhi/maambukizi yanayoweza kuambatana na dalili hizi kwa mjamzito na kutibiwa kwa wakati.


Visababishi vya kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito


Hakuna sababu fulani ambayo inathibitishwa kuwa chanzo cha dalili hizi, hivyo huwa na muunganiko wa sababu mbali mbali tata zinazotokana na vinasaba, mfumo wa homoni, maambukizi, saikolojia na sababu za kijamii. Visababishi vimegawanyika katika makundi makuu mawili kama ifuatavyo;


Sababu zinazohusiana na ujauzito

Wakati wa ujauzito mabadiliko mbali mbali hutokea katika mifumo ya mwili wa mwanamke kutokana na mabadiliko ya homoni na sababu nyinginezo. Ongezeko la homoni hCH (human chorionic gonadotropin), estrogen na progesterone husababisha mabadiliko katika mfumo wa umeng’enywaji wa chakula na kumuweka mwanamke katika hali ya kuwa na kichefuchefu na kuptaika, homoni nyingine zinazoleta mabadiliko haya ni thyroxin, prolactin, leptin na homoni za adrenocortical.


Dalili huanza kuonekana kati ya wiki ya 2 hadi ya 4 baada ya mimba kutungwa, na hufikia kilele kati ya wiki 9 hadi wiki 12 na kisha kuanza kuisha kuanzia wiki ya 22, na dalili zinaweza kuendelea hadi wakati wa kujifungua kwa asilimia ndogo ya wanawake.


Zifuatazo ni sababu na aina za kichefuchefu na kutapika zinazohusiana na hali ya ujauzito


Kichefuchefu na kutapika kwa kawaida (homa za asubuhi)

Hutokea katika kipindi cha kwanza cha ujauzito, mara nyingi mjamzito huwa na dalili asubuhi baada ya kuamka kisha kupotea kadri masaa yanavyosogea, japo zinaweza kutokea wakati wowote wa siku.


Kichefuchefu na kutapika sana

Hutokea katika kipindi cha kwanza cha ujauzito, dalili huwa kali na kuathiri utendaji kazi au maisha ya kila siku ya mjamzito (kusoma zaidi rejea)


Shinikizo la juu la damu linaloelekea kifafa cha mimba

Hutokea baada ya wiki ya 20, huwa na dalili za kihefuchefu na kutapika, shinikizo la damu kuwa juu, kichwa kuuma, kuvimba miguu nk


Mimba ya mapacha na ujauzito wa mola

Ujauzito wa aina hii huambatana na uzalishwaji wa homoni (human chorionic gonadotropin), estrogen na progesterone.


Sababu zisizohusiana na ujauzito

Hujimuisha maambukizi na magonjwa ambayo huweza kutokea wakati wa ujauzito na kuwa na dalili za kichefuchefu na kutapika, lakini pia huambatana na dalili na viashiria vingine. Baadhi ya magojwa haya ni;


 • Minyoo

 • Homa ya matumbo

 • Maambukizi ya h.pylori

 • Uti

 • Malaria

 • Homa ya ini

 • Kidole tumbo

 • Uvimbe kwenye ovari

 • Vidonda vya tumbo

 • Mawe kwenye mfuko wa nyongo


Madhara ya kichefu chefu na kutapika wakati wa ujauzito


Hakuna madhara yoyote kwa mjamzito mwenye kichefu chefu na kutapika kawaida, athari huwapata wale wenye dalili hizi kulikopitiliza.


Madhara hutokea kwa mama na mtoto kama ifuatavyo;


Madhara kwa mama

 • Kupungukiwa maji mwilini

 • Kupungukiwa sukari mwilini

 • Kutapika damu

 • Kuwa na manjano

 • Kupata vidonda vya tumbo

 • Kupungukiwa damu

 • Kupata na uchungu kabla ya muda

 • Kupata sonona

 • Figo kufeli

 • Athari mbali mbali katika mfumo wa fahamu kama vile degedege nk.


Madhara kwa mtoto

 • Kudumaa tumboni

 • Kuzaliwa na uzito mdogo

 • Kuzaliwa njiti


Matibabu kwa mjamzito mweye kichefuchefu na kutapika


Kama ilivyoainishwa hapo awali dalili hizi huweza kutokea kwasababu ya ujauzito au kwasababu ya maambukizi, lakini imezoeleka kwamba kichefu chef una kutapika ni kawaida kwa mjamzito na mara nyingi wajawazito wamekuwa wakijitibu nyumbani bila kutafuta msaada wa kitabibu.


Kwa ujumla matibabu hutegemea chanzo na ukubwa wa tatizo, mjamzito anaweza kutibiwa kma mgonjwa wan je na pengine huitajika kulazwa hospitali endapo dalili ni kali na zina athiri afya na maisha yake ya kila siku.


Matibabu kwa vyanzo visivyohusiana na ujauzito

Ili kuweza kubaini vyanzo vingine vya kichefuchefu na kutapika mjamzito mwenye dalili hizi hufanyiwa vipimo mbali mbali kulingana na dalili na viashiria. Baada ya majibu kuthibitisha maambukizi mgojwa hutibiwa kulingana na aina ya ugonjwa/maabukizi, na kama hakuna ugonjwa wowote uliothibitika mjamzito hutibiwa kama dalili zinazohusiana na ujauzito.


Matibabu ya kichefuchefu na kutapika kunakohusiana na ujauzito

Mara nyingi dalili huisha bila kutumia dawa yoyote hasa kwa wajawazito wenye kichefuchefu na kutapika kwa kawaida, na baadhi huitaji matibabu mbali mbali na wakati mwingine kulazwa hospitali (hasa wale wenye kichefuchefu na kutapika sana).


Matiababu huanza kwa kubadili mlo na ikishindikana dawa hutumika


Matibabu kwa kubadili mlo

Hii ni hatua ya kwanza ya matibabu na hufanya kazi kwa asilimia kubwa ya wajawazito. Mama hushauriwa mambo yafuatayo;


 • Kuwa na milo mingi na kula kiasi kidogo cha chakula katika kila mlo

 • Kuacha kula vyakula vyenye mafuta mengi

 • Kula chakula laini ambacho hakina viungo vingi na chenye kiwango kidogo cha nyuzi nyuzi

 • Kula protini kwa wingi na kiasi kidogo cha wanga

 • Kutumia tangawizi (husaidia pia kuzuia kuzaliana kwa bakteria H. Pylori ambaye anahusishwa na kichefuchefu na kutapika sana)


Matibabu kwa dawa

Dawa hutolewa endapo ukubwa wa dalili unaendelea licha ya kufanya mambo tajwa hapo juu na wakati mwingine huitajika kutibiwa akiwa wodini hususani kwa wajawazito wanaotapika sana.

Kwa mjamzito mwenye kichefuchefu na kutapika kwa kawaida hupewa dawa za kuzuia kutapika na dalili hupona bila kuhitaji matibabu zaidi ukilinganisha na yule anayetapika sana, kwani huitaji kuongezwa dripu ya maji yenye chumvi chumvi za madini, dawa za vitamin ink (kusoma zaidi kuhusu matibabu ya kichefuchefu na kutapika sana kwa mjamzito rejea kwenye makala hii

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

4 Februari 2022 20:08:01

Rejea za dawa

 1. Lee, noel m, and sumona saha. “nausea and vomiting of pregnancy.” Gastroenterology clinics of north America vol. 40,2 (2011): 309-34, vii. Doi:10.1016/j.gtc.2011.03.009.

 2. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/pmc3676933/ imechukuliwa 02.02.2022

 3. Emily e. Bunce, md, and robert p. Heine, md. Nausea and vomiting during early pregnancy. Gynecology and obstetrics - msd manual professional edition. Last full review/revision dec 2020.https://www.msdmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/symptoms-during-pregnancy/nausea-and-vomiting-during-early-pregnancy. Imechukuliwa 02.02.2022

 4. Dc dutta’s textbook of obstetrics. Vomiting in pregnancy. Seventh edition november 2013 (p. 154-155)

bottom of page