top of page

Mwandishi:

Dkt. Adolf S, MD

Mhariri:

Dkt. Sospeter M, MD

29 Septemba 2021 18:15:58

Image-empty-state.png

Leba kabla ya wakati

Kwa kawaida ujauzito wa binadamu hukomaa kati ya wiki 37 hadi 41, wiki hizi huhesabiwa kutoka tarehe ya mwisho ya kuanza hedhi kabla ya ujauzito. Leba kabla ya mimba kukomaa humaanisha kuanza uchungu na kufunguka kwa shingo ya kizazi muda wowote baada ya wiki 28 na kabla ya wiki 37. Leba kabla ya wakati hufahamika kwa jina jingine uchungu kabla ya wakati.


Kiwango cha chini cha umri wa ujauzito kinachotumika kuelezea leba kabla ya mimba kukomaa hutofautiana kati ya nchi zinazoendelea na zile ziilizoendelea. Kwa nchi zilizoendelea leba kabla ya mimba kukomaa humaanisha leba muda wowote baada ya wiki 20 wakati kwa nchi zinazoendelea huwa baada ya wiki 28.


Leba kabla ya mimba kukomaa ni sababu kuu ya kuzaliwa kwa watoto njiti na kupelekea ongezeko la vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ulimwenguni kote, si hivyo tu pia watoto njiti wanaonusurika kifo hupata matatizo kadha wa kadha kama vile ulemavu, kushindwa kujifunza, utindio wa ubongo nk. Pia kupata uchungu kabla ya wakati husababisha taharuki kwa mjamzito na jamii kwa ujumla na kuongezaka kwa gharama za matibabu ya aatoto njiti na kuathiri uchumi.


Zipo sababu mbalimbali ambazo husababisha mjamzito kupata uchungu kabla ya wakati japokuwa huwa hakuna sababu maalumu kwa idadi kubwa ya wajawazito wanaoanza leba kabla ya mimba kukomaa, hali hii hupelekea jitihada za kuzuia tatizo hili kuwa ngumu. Hata hivyo miongoni mwa sababu hizo nyingi zinaweza kuzuilika kwa kuhudhuria kliniki na kupata huduma zote kama inavyopendekezwa na shirika la afya duniani.


Lengo la Makala hii ni kutoa elimu kwa ujumla kuhusu leba kabla ya mimba kukomaa


Visababishi


Uchungu kabla ya mimba kukomaa ni matokeo ya kuchochewa kwa fiziolojia ya mchakato mzima wa leba kabla ya wakati au sababu zingine za ki patholojia zinazokinzana na kuendelea kwa ujauzito mpaka muda wa kukomaa.


Zipo sababu nyingi ambazo hupelekea kuanza kwa uchungu kabla ya mimba kukomaa zinazojulikana na zisizojulikana kama ifuatavyo;


Sababu zisizojulikana

Takribani asilimia 50 ya visa vya leba kabla ya mimba kukomaa huwa havina sababu yoyote iliyobainishwa kitaalamu na huhusishwa na kuchochewa kwa fiziolojia ya mchakato mzima wa leba kabla ya wakati.


Sababu zinazojulikana

Ni sababu ambazo huchangiwa aidha na mama, mtoto, sababu za kitabibu au matatizo ya kizazi. Zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo ambazo huonekana sana;


 • Historia ya kuharibika kwa mimba

 • Ujauzito uliopatikana kwa kupandikiza

 • Ujauzito wa mapacha

 • Mimba zinazokaribiana au zinazopishana sana (chini ya miezi 18 na Zaidi ya miezi 60)

 • Maambukizi ya vimelea wa magonjwa wanaopitia katika mfumo wa nje wa uzazi mfano magonjwa ya zinaa nk

 • UTI hasa inayojirudia

 • Kutokwa damu wakati wa ujauzito baada ya wiki 28

 • Magonjwa sugu kama shinikizo la damu na kisukari

 • Magonjwa ya shinikizo la damu yanayosababishwa na ujauzito

 • Kuwa na msongo wakati wa ujauzito

 • Uvutaji wa sigara

 • Obeziti

 • Upungufu wa damu

 • Lishe duni na hali duni ya maisha

 • Shingo ya kizazi kulegea (cervical insufficiency) na shingo ya kizazi kuwa fupi

 • Kasoro za kimaumbile za mtoto au mji wa uzazi

 • Kupasuka kwa chupa kabla ya wiki 37

 • Maji mengi ya amniotic (polyhydramnios)

 • Matibabu yanayohusisha kukata nyama katika shingo ya kizazi

 • Kuanzishiwa uchungu kabla ya muda kutokana na sababu mbalimbali za kitabibu


Dalili na viashiria


Huwa sawa na zile zinazotokea mimba inapokuwa imekomaa kama ifuatavyo;


 • Kuhisi mgandamizo kwenye nyonga

 • Kutokwa na ute ute uliochanganyikana na damu ukeni

 • Maumivu ya tumbo la chini na kiuno yanayoongezeka kadri muda unavyokwenda

 • Kupasuka kwa chupa

 • Mlango wa kizazi kufunguka


Matibabu


Lengo la matibabu ni kubaini chanzo pale inapowezekana na kujaribu kuzuia uchungu kwa muda flani ili kupata nafasi ya maandalizi mema ya huduma kwa mtoto atakayezaliwa njiti.


Vipimo


Utambuzi wa leba kabla ya mimba kukomaa huusisha umri wa mimba, dalili na viashiria vya leba, vipimo husaidia kubaini baadhi ya visababishi ambavyo hupelekea tatizo hili lakini pia kuwa kama sehemu ya matibabu.


Kipimo cha ultrasound

Hutumika kutambua umri wa ujauzito kwa wiki pale ambapo mama hakumbuki tarehe yake ya mwisho ya kupata hedhi na kujua hali ya mtoto kwa ujumla. Pia huweza kutumika kujua urefu wa shingo ya kizazi


Kipimo cha picha nzima ya damu

Hutumika kutambua wingi wa damu na kusaidia kupanga matibabu kulingana na makundi ya upungufu wa damu


Kipimo cha mkojo

Hutumika kutambua magonjwa ya mfumo wa mkojo (UTI)


Kipimo cha kuotesha vimelea kutoka katika ute unaotoka ukeni (HVS)

Hutumika kutambua uwepo wa vimelea wanaosababisha magonjwa katika mfumo wa uzazi kupitia ukeni hasa magonjwa ya zinaa


Kipimo cha Fetal fibronectin

Husaidia kubashiri hatari ya kujifungua ndani ya siku 7 kwa mjamzito mwenye dalili za uchungu kabla ya mimba kukomaa au yule mwenye visababishi vinavyo ongeza hatari ya kupata uchungu kabla ya wakati.

Fetal fibronectin ni protrotin inayotolewa na seli za mtoto, kwa kawaida huonekana katika ute ute wa mlango wa shingo ya kizazi wiki za mwanzoni na kuanzia wiki ya 36 ambapo mimba huanza kukomaa.

Protini hii huwa kama gundi inayoshikilia mimba katika mji wake na haitakiwi kuthibitika katika ute ute unaotoka ukeni kati ya wiki 22 hadi 35 kwani uwepo wake huashiria hakuna uimara wa mimba katika mji wake hivyo mtoto anaweza kutoka muda wowote.


Kipimo cha kuchunguza wingi wa damu

Husaidia kutambua kama mama anaupungufu wa damu unaoambatana na uchugnu kabla ya wakati na madhara kwa mtoto.


Kipimo cha kuchunguza maambukizi

Husaidia kufahamu visababishi mbalimbali kutokana na vimelea mfano, kisonono,


Kuzuia uchungu


Lengo ni kujaribu kuongeza muda wa mtoto kukomaa (rejea mtoto njiti) au kupata muda wa kumpa mama dawa za kukomaza mapafu ya mtoto endapo uchungu umeanza kabla ya wiki 34.


Mara nyingi haishauriwi kuzuia uchungu kwa mjamzito aliyeanza leba kabla ya wakati katika baadhi ya visababishi kwani kufanya hivyo huweza kuleta mdhara makubwa kwa mtoto na mama.


Uchungu utazuiliwa endapo;


 • Hali ya mama na mtoto ni nzuri

 • Njia haijafunguka zidi ya sentimeta 4 na

 • Chupa haijapasuka.


Zifuatazo ni njia ambazo hutumiwa ili kuzuia uchungu kwa muda flani.


Kupata muda mwingi wa kupumzika

Hii ni njia ya kwanza ambayo imekuwa ikitumiwa sana ili kuzuia uchungu, mjamzito huwekwa katika mapumziko ya muda mrefu ambapo hatakiwi kufanya kazi na kushiriki tendo la ndoa, na hutakiwa kutumiwa muda mwingi kulala . Mapumziko haya huweza kufanyika hospitali au nyumbani.


Hata hivyo tafiti nyingi zinaonesha kuwa hakuna ushahidi wowote wa ufanisi wa njia hii katika kuzuia uchungu kabla ya mimba kukomaa na kubaini kuwa kufanya hivyo kuna madhara kama vile kuongezeka uzito uliopitiliza ambao ni hatari kwa mama na mtoto.


Dawa za kuzuia uchungu

Ni dawa zinazozuia kutanuka na kusinyaa kwa misuli ya mji wa uzazi hivyo kuzuia fiziolojia nzima ya leba, licha ya kuzuia uchungu dawa hizi husaidia kupunguza vifo na matatizo mbali mbali yanayoambatana na unjiti kama vile utindio wa ubongo nk.


Dawa hizi zina uwezo wa kuzuia leba kwa muda mfupi kuanzia masaa 48 mpaka siku 7, na hutolewa kwa mjamzito mwenye dalili na viashiria vya leba ambaye njia haijafunguka zidi ya sentimeta 4. Kipindi ambacho uchungu umezuiliwa hutumiwa kwa matibabu mengine ambayo yata msaidia mtoto

Dawa za kuzuia uchungu zipo katika makundi tofauti tofauti kama ifuatavyo;


 • Dawa kundi la beta adregenic antagonist kama salbutamol, terbutaline n.k

 • Dawa kundi la calcium channel blocker mfano nifedipine

 • Dawa kundi la Oxytocin antagonist kama atosiban

 • Dawa kundi la prostaglandin inhibitors kama indomethacin

 • Magnesium sulfate


Miongoni mwa dawa hizi magnesium sulfate, nifedipine na indomethacin hutumika zaidi na zina madhara machache kwa mama na mtoto ukilinganisha na makundi mengine tajwa hapo juu.


Magnesium sulphate hutolewa kwa ujauzito chini ya wiki 32 kuzuia uchungu lakini pia hukinga mfumo wa fahamu wa mtoto dhidi ya uharibifu unaoweza kusababisha kuvuja damu katika ubongo, matatizo ya kujifunza, utindio wa ubongo nk


Dawa katika kundi la beta adregenic antagonist hazitumiki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwani tafiti zinaonesha kuwa zinasababisha madhara kwa mama na mtoto kama vile mapafu kujaa maji, magonjwa ya mapigo ya moyo nk.


Dawa za kuzuia maambukizi ya bakteria

Dawa za kuua bacteria hutolewa endapo tu mama ana dalili na viashiria vya maambukizi ya vimelea au kuthibitika kwa maambukizi kupitia vipimo, au chupa kupasuka kabla ya uchungu kuanza.


Lengo la dawa hizi ni kuzuia kupata leba kabla ya mimba kukomaa kunakosababishwa na maambukizi ya bakteria na kumkinga mtoto dhidi ya maambukizi hayo akiwa tumboni na baada ya kuzaliwa.


Mojawapo kati ya dawa hizi hutumika kwa njia ya mishipa;


 • Ampicillin

 • Ceftriaxone

 • Clindamycin

 • Vancomycin


Dexamethasone

Hutolewa kwa majamzito ambaye ana dalili na viashiria vya uchungu na yupo katika hatua za mwanzo za leba (latent phase) mwenye ujauzito chini ya wiki 34. Inasaidia kukomaza mapafu ya mtoto na kuzuia shida ya kupumua (RDS) baada ya kuzaliwa. Kabla ya kutoa Dexamethasone mjamzito hupewa dawa za kuzuia uchungu kwa masaa 48 ili kupata muda wa dawa kufanya kazi.Kuzuia leba kabla ya mimba kukomaa


Kutokana na matibabu ya kuzuia leba kabla ya wakati sahihi kutozaa matunda njia pekee inayoweza kupunguza tatizo hili ni kuzuia, hata hivyo kuna changamoto mbalimbali zinazopelekea jitihada za kuzuia kutokufanikiwa kwa asilimia 100.Zifuatazo ni njia ambazo zinaweza kusaidia kupunguza tatizo hili


Kuhudhuria kliniki


Sababu nyingi zinazojulikana huweza kubainika na kushughulikiwa wakati wa kiliniki kwa kufanya vipimo, kupata matibabu na elimu ya afya kwa ujumla.


Baadhi ya huduma zinazoweza kusaidia ni kama vile;


 • Kupima na kutibu magonjwa ya mfumo wa mkojo na magonjwa ya zinaa

 • Kupima na kutibu upungufu wa damu

 • Utoaji wa dawa za madini chuma na folate

 • Kubaini wajawazito walio katika hatari kubwa ya kupata uchungu kabla ya mimba kukomaa na kuwafuatilia kwa karibu

 • Utoaji wa elimu ya afya kuhusu lishe, matumizi ya dawa nk


Upasuaji wa kukaza shingo ya kizazi


Ni upasuaji mdogo wa kukaza shingo ya kizazi ili isifunguke kabla ya wakati sahihi, upasuaji huu hufanyika kwa mjamzito mwenye historia ya kuanza leba katika kipindi cha pili cha ujauzito na yule mwenye shingo fupi ya kizazi ambaye hana shida zifuatazo;


 • Njia iliyofunguka Zaidi ya sentimeta 4

 • Kutokwa na damu ukeni

 • Kupasuka kwa chupa kabla ya uchungu

 • Maambukizi (chorioamnionitis)


Hufanyika kati ya wiki ya 16 hadi wiki ya 18 na wakati mwingine kati ya wiki 24 hadi wiki 28 kama dharura. Shingo ya kizazi hukazwa kwa kutumia nyuzi maalumu na nyuzi huondolewa kati ya wiki 36 hadi 37 au huondolewa muda wowote endapo kuna dalili na viashiria vya kuanza leba ili kuzuia kuchanika kwa shingo ya kizazi.


Pesari ya shingo ya kizazi

Ni kifaa kilichotengenezwa kwa silikoni ambacho huweka katika mlango wa kizazi ili kuzuia kufunguka kwa kupunguza uzito wa mji wa uzazi na mtoto katika eneo la ndani la shingo ya kizazi.

Kifaa hiki hutumika kwa mama mwenye ujauzito wa mtoto mmoja mwenye shingo fupi ya kizazi. Vigezo, muda wa kuweka na kutoa pesari hufanana na upasuaji wa kukaza shingo ya kizazi.


Homon progesterone

Progesterone ni homoni ambayo huzuia misuli ya mji wa uzazi kusinyaa na kutanuka mpaka pale mimba inapokomaa. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa dawa zenye homoni hii (17α-hydroxyprogesterone caproate) husaidia kuzuia kupata uchungu kabla ya wakati sahihi.


Dawa ya 17α-hydroxyprogesterone caproate hutolewa kati ya wiki ya 20 mpaka 36 kwa njia ya sindano ya msuli au kupachika ukeni katika shingo ya kizazi kwa wajawazito ambao wapo katika hatari ya kupata uchungu kabla ya mimba kukomaa


Si wajawazito wote wenye hatari ya kupata uchungu kabla ya muda wanaweza kunufaika na dawa hii kutokana na kukosa ufanisi katika sababu zingine zinazoweza kupelekea tatizo hili. Tafiti zinaonesha kuwa 17α-hydroxyprogesterone caproate inaufanisi mkubwa wa kuzuia uchungu kabla ya mimba kukomaa kwa mama mwenye ujauzito wa mtoto mmoja mwenye historia ya kupata uchungu kabla ya wakati hapo awali na kwa asilimia ndogo kwa mjamzito mwenye shingo fupi ya kizazi.


Pamoja na ufanisi wake progesterone inuwezo wa kuzuia takribani theluthi ya visa vya kupata leba kabla ya mimba kukokaa kunakojirudia katika ujauzito mwingine.


ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

29 Septemba 2021 19:15:27

Rejea za dawa

 1. Bernadether T. et al. Factors associated with risk of preterm delivery in Tanzania: A case-control study at Muhimbili National Hospital. 05 December 2020 https://doi.org/10.1002/ijgo.13520

 2. Louis J. Muglia, M.D., et al. The Enigma of Spontaneous Preterm Birth. February 11, 2010.N Engl J Med 2010; 362:529-535 DOI: 10.1056/NEJMra0904308

 3. Julie S. Moldenhauer , MD. Preterm Labor. https://www.msdmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/abnormalities-and-complications-of-labor-and-delivery/preterm-labor

 4. Claire Foster 1, et al. Fetal fibronectin as a biomarker of preterm labor: a review of the literature and advances in its clinical use. :6 May 2014https://doi.org/10.2217/bmm.14.28.Judith A Maloni.Lack of evidence for prescription of antepartum bed rest

 5. Michael G Ross, MD, MPH. What are the most common tocolytic agents used to treat preterm labor?. medscape .May 04, 2021 https://www.medscape.com/answers/260998-168209/what-are-the-most-common-tocolytic-agents-used-to-treat-preterm-labor. Imechukuliwa 29/09/2021

 6. Muhimbili National Hospital (MNH). TREATMENT GUIDELINES, Obstetrics and Gynaecology disorders. Department of Obstetrics and Gynaecology August 2019 ( p.25-26)

 7. Prevention of preterm delivery: current challenges and future prospects

 8. Maud D van Zijl,1 Bouchra Koullali,1 Ben WJ Mol,2 Eva Pajkrt,1 and Martijn A Oudijk1 2016 Oct 31. doi: 10.2147/IJWH.S89317.

 9. Progesterone Supplementation and the Prevention of Preterm Birth

 10. Errol R Norwitz, MD, PhD, Louis E. Phaneuf Professor of Obstetrics & Gynecology, Chairman1 and Aaron B Caughey, MD, MPP, MPH, PhD, Professor and Chairman2Rev Obstet Gynecol. 2011 Summer; 4(2): 60–72.

 11. Allahyar Jazayeri, MD, PhD, FACOG, DACOG. Cervical Cerclage. https://emedicine.medscape.com/article/1848163-overview. Imechukuliwa 29/09/2021

 12. Use of Cervical Pessary in the Management of Cervical Insufficiency

 13. Julia Timofeev. Clin Obstet Gynecol. 2016 Jun;59(2):311-9. doi: 10.1097/GRF.0000000000000196. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26992180/. Imechukuliwa 29/09/2021

bottom of page