top of page

Mwandishi:

Dkt. Sospeter M, MD

Mhariri:

Dkt. Adolf S, MD

12 Mei 2022, 11:58:50

Image-empty-state.png

Mate mengi wakati wa ujauzito

Utokaji wa mate mengi wakati wa ujauzito hufahamika kama ptayalizimu (ptyalism) au sialorea (sialorrhea). Wajawazito wenye tatizo hili hupata shida kumeza mate na huchagua kuwa na chombo cha kutemea mate au kitambaa cha kufutia mate hayo muda wote.


Baadhi ya wanawake wamekuwa wakitafuna bablishi au kumung'unya vipande vidogo vya barafu ili kudhibiti hali hii kwa muda hata hivyo uzalishaji wa mate unaweza kupungua wakati umelala


Mara nyingi tatizo hili huisha baada ya kupita kipindi cha kwanza cha ujauzito kupita yaani miezi mitatu ya mwanzo. Lakini baadhi ya wanawake wanaweza kuendelea na dalili hii mpaka wakati wa kujifungua.


Dalili zinazoambatana na utokaji mate kwenye ujauzito


Wajawazito wenye tatizo hili pia wamekuwa wakipata dalili zingine kama;

  • Hisia ya ladha mbaya kinywani

  • Kichefuchefu na kutapika kama wakimeza mate

  • Kuamka mara kwa mara baada ya kulala usiku

  • Kupaliwa mate wakati umelala


Nini kisababishi cha utokaji mate mengi wakati wa ujauzito?


Wanasayansi hawajaweza kutambua mpaka sasa ni nini kisababishi halisi cha utokaji mate mengi wakati wa ujauzito licha ya kuhusianisha tatizo hili na mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa ujauzito.


Kisayansi inafahamika kwa ujumla kwamba utoaji wa mate hudhibitiwa na mfumo wa neva. Uchochezi wa mfumo wa neva wa parasympathetic huamsha tezi za mate mdomoni na kusababisha uzalishaji mwingi wa mate. Hii ndio maana mpaka sasa baadhi maandiko ya kitiba yameshauri kutumia dawa za kutuliza mfumo wa fahamu wa kati jamii ya barbiturates na anticholinergics na baadhi ya dawa asili kama alpinia oxyphylla kudhibiti tatizo hili. Dawa hizi hazina matokeo ya kuridhisha na baadhi ya wataalamu wa afya na wanawake pia hawachagui kutumia njia hii kwa kuhofia madhara yanayoweza kutokea kwa watoto, haswa katika kipindi cha uumbaji wa viungo yaani kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.


Visababishi vingine


Mbali na kuwa hali ya kawaida, utokaji mate mengi wakati wa ujauzito unaweza kusababishwa na hali na magonjwa mengine pia kama vile

  • Mabadiliko ya homoni mwilini

  • Ugonjwa wa kutapika sana kwa wajawazito ( homa kali ya asubuhi)

  • Kiungulia

  • Matumizi ya dawa aina fulani

  • Magonjwa mengine kama UTI, magonjwa ya tumbo n.k


Ili kutofautisha visababishi mbalimbali, kama una tatizo hili, unapaswa kuwasiliana na daktari wako kwa vipimo na tiba.


Matibabu ya utokaji mate mengi wakati wa ujauzito


Hakuna matibabu yanayofahamika kufanya kazi nzuri ya kutibu tatizo hili, licha ya baadhi ya dawa zinazozuia uzalishaji wa mate kuwepo, ufanisi wake unatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine.


Wataalamu wengi wanashauri wanawake kubadili mtindo wa maisha ili kukabiliana na tatizo hili badala ya kutumia dawa kwa kuhofia madhara yake kwa mtoto tumboni.


Matumizi ya dawa za kuzuia uzalishaji wa mate


Baadhi ya dawa zinazofahamika kuzuia uzalishaji wa mate ni

  • Dawa jamii ya barbiturates kama phenobarbital, piperidolate HCL

  • Dawa jamii ya anticholinergics kama belladonna alkaloid au phosphorated carbohydrate

  • Dawa ya kushusha shinikizo la juu la damu clonidine hydrochloride

  • Dawa asili kutoka kwenye mmea alpinia oxyphylla


Matumizi ya dawa phenobarbital, piperidolate HCL, belladonna alkaloid au phosphorated carbohydrate hazina matokeo mazuri sana ya kuzuia utokaji mate mengi wakati wa ujauzito.


Dawa zingine za kuzuia utokaji mate


Scopolamine imekuwa ikitumika kudhibiti kutoka mate kwa wagonjwa wenye tatizo la kutokwa udenda, ufanisi na madhara yake wakati wa ujauzito hata hivyo hayafahamiki.


Sindano ya Botulinum toxin pia imekuwa ikitumika kudhibiti kutokwa mate kwa wagonjwa wenye matatizo haswa katika mfumo wa fahamu, hata hivyo matumizi ya dawa hii bado hayajafanyiwa tafiti za kutosha kuweza kuangalia usalama wake kwa kichanga tumboni na hivyo haitumiki wakati wa ujauzito.


Kubadili mtindo wa maisha


Ili kukabiliana na tatizo la utokaji mate mengi wakati wa ujauzito, matumizi ya njia zifuatazo yameonekana kudhibiti tatizo hili kwa muda.


1. Kula mlo kidogo mara kwa mara

Badala ya kula mara tatu kwa siku, inashauriwa kula mara 6 hadi 8 kwa siku kiwango kile kile cha chakula unachokula kwa siku.


2. Kusukutua au kusafisha kinywa mara kwa mara

Kupiga meno mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye minti au kusukutua kwa maji yenye minti mara kwa mara. Hii husaidia kuondoa uchafu na mabaki ya chakula kwenye kinywa yanayoweza kusababisha utokaji wa mate mengi na pia huleta ladha nzuri kinywani.


3. Kutafuta au kumung'unya kitu

Kutafuna bablishi isiyo na sukari wakati mwingi au kumung'unya pipi ngumu au tetele ya tunda kama ukwaju au ubuyu. Njia hii hufanya umeze mate kirahisi pasipo kuhisi kuwa unameza mate na pia huzuia kupata kichefuchefu na ladha mbaya ya mate.


4. Kunywa maji

Imeonekana kuwa, upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha utokaji wa mate mengi wakati wa ujauzito na pia kupelekea mate kuwa mazito kiasi cha kushindwa kuyameza na kuleta hali ya kuhisi kichefuchefu. Ili kuzuia kutapia kutokana na kunywa maji mengi, inashauriwa kunywa maji kidogo ( kijiko kimoja cha chai) mara kwa mara kwa siku ili kuzuia upungufu wa maji mwilini. Kunywa maji kidogo kidogo na mara kwa mara hulainisha mate na hivyo kukufanya uyameze kirahisi kama watu wengine.


5. Kunyonya barafu

Baadhi ya wanawake wameripoti kupungua kwa hali hii endapo wametumia barafu au maji ya baridi. Maji ya baridi na barafu husababisha hali ya ganzi kinywani na hivyo kupelekea kupungua kwa uzalishaji wa mate. Pia kunywa maji ya baridi na kumung'unya barafu pia hupelekea kulainisha mate na hivyo kuyameza kirahisi.


6. Tiba ya kusisimua mishipa ya fahamu ya uti wa mgongo

Tiba hii imeonekana kufanya kazi kwa baadhi ya wanawake. Mtaalamu wa afya anayefahamu kuhusu mishipa ya fahamu ya uti wa mgogo, hukanda uti wa mgongo kwa kutumia nguvu kiasi ili kuisisimua mishipa ya fahamu. Tiba hii hufahamika kwa lugha ya kiingereza kama tiba ya chiropractic.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

12 Mei 2022, 11:58:54

Rejea za dawa

  1. Suzuki S, Igarashi M, Yamashita E, Satomi M. Ptyalism gravidarum. N Am J Med Sci. 2009;1(6):303-304.

  2. Freeman JJ, Altieri RH, Baptiste HJ, Kao T, Crittenden S, Fogarty K, Moultrie M, Coney E, Kangis K. Evaluation and management of sialorrhea of pregnancy with concominant hyperemesis. J Natl Med Assoc. 1994;86:704–708.[PMC free article] [PubMed] [Google Scholar]

  3. NCT. Excessive saliva in pregnancy. https://www.nct.org.uk/pregnancy/worries-and-discomforts/common-discomforts/excessive-saliva-pregnancy. Imechukuliwa 12/5/2022

  4. Dental choice. Excessive Saliva During Pregnancy? Here’s What You Need to Know. https://www.dentalchoice.ca/excessive-saliva-during-pregnancy-heres-what-you-need-to-know/. Imechukuliwa 12/5/2022

  5. VictoriaDe Braga, et al. Successful treatment of ptyalism gravidarum with clonidine hydrochloride: A case report. https://doi.org/10.1016/j.crwh.2022.e00409. Imechukuliwa 12/5/2022

bottom of page