Mwandishi:
Dkt. Lugonda M, MD
Mhariri:
Dkt. Charles W, MD
16 Novemba 2021, 18:19:04

Matunzo ya kangaruu
Matunzo ya kangaruu ni matunzo kwa watoto wachanga yanayofanyika kwa kugusanisha ngozi ya mtoto na ngozi ya kifua cha mama. Matunzo haya ni thabiti na rahisi ambayo huimarisha afya na ustawi wa mtoto mchanga.
Kina nani wanapasswa kufanyiwa matunzo haya?
Watoto wanaoapswa kufanyiwa matunzo ya kangaruu ni wale
waliozaliwa na uzito pungufu yaani wale wenye uzito chini ya gramu 2,500
watoto njiti yaani waliozaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito
Vidokezo maalumu kuhusu matunzo ya kangaruu
Hutolewa mfululizo mchana na usiku
Yanaweza kukatishwa kwa muda mfupi wakati mama anapooga au anapokuwa na shughuli zake binafsi
Mwenza au wanafamilia wanapaswa kutoa ushirikiano kutoa huduma hii
Hatua za kutoa matunzo ya kangaruu

Zifuatazo ni hatua za kutoa matunzo ya kangaruu
Kaa na uegame kidogo
Mvue mtoto nguo taratibu isipokuwa kofia, nepi na soksi
Mweke mtoto kwenye kifua chako katikati ya matiti ili ugusanae naye ngozi kwa ngozi
Geuza kichwa cha mtoto upande mmoja hakikisha mtoto anapumua vizuri na Mtoto abaki hivyo muda wote
Mfunike mtoto na nguo zako, kisha jifunike pamoja na mtoto kwa kutumia blanketi na mvalishe mtoto kofia
Hakikisha mtoto ananyonya kila wakati
Ikiwezekana hakikisha chumba unachokaa kina joto la kutosha
Mbadala wa kangaruu upo?
Mbadala wa njia ya kangaruu ni kutumia kiota chenye joto ambavyo hupatikana kwenye baadhi ya hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya.
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
21 Novemba 2021, 09:36:02
Rejea za dawa
WHO. Kangaroo mother care a practical guide. http://apps.who.int/iris/bitstream/handle/10665/42587/9241590351.pdf. Imechukuliwa 16.11.2021