top of page

Mwandishi:

Dkt. Adolf S, MD

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

7 Agosti 2021 14:03:30

Image-empty-state.png

Mtoto njiti

Mtoto njiti humaanisha mtoto aliyezaliwa hai kabla ya kukamilika kwa wiki 37 za ujauzito. Kwa kawaida viungo na mifumo mbalimbali ya mwili wa mtoto hukomaa na kufanya kazi vema katika wiki ya 37 na kuendelea, kama mtoto atazaliwa chini ya wiki ataitwa mtoto ambaye hajakomaa au mtoto njiti.

Neno ‘Mtoto njiti’ mara nyingi huchanganywa na watu wengi kuwa ni mtoto aliyezaliwa na uzito mdogo ( mtoto mwenye uzito mdogo kuliko umri wa ujauzito) kwa sababu ya watoto njiti huzaliwa pia na uzito mdogo. Hata hivyo tofauti iliyopo kati yao ni kwamba mtoto mwenye uzito mdogo kuliko umri huzaliwa kuanzia wiki ya 37 na kuendelea na uzito wake huwa haulingani na umri kwa sababu ya kudumaa akiwa tumboni wakati mtoto njiti ni mtoto aliyezaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito.


Mtoto njiti ni janga la kidunia, inakadiriwa kuwa watoto njiti milioni 15 huzaliwa kila mwaka Duniani sawa na zaidi ya mtoto mmoja kati ya watoto kumi. Ulimwenguni kote unjiti ni sababu namba moja ya vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Kutokomaa kwa viungo na mifumo ya mtoto kutokana na unjiti husababisha matatizo mengi baada ya kuzaliwa kama vile kushindwa kupumua, kushuka kwa joto la mwili, kushuka kwa sukari nk. Matatizo hayo husababisha vifo na ulemavu wa kudumu kwa wale wanaonusurika kufa.


Asilimia kubwa ya watoto njiti huzaliwa kwa sababu ya wajawazito kupata uchungu kabla ya wakati sahihi kulingana na sababu mbali mbali, na asilimia ndogo huzaliwa kwa sababu ya mama kuzalishwa kabla ya muda kutokana na sababu za kitabibu.


Watoto njiti wanaweza kuokolewa dhidi ya vifo na matatizo mbalimbali ya unjiti kwa kutoa kupata huduma nzuri wakati wa kliniki ili kuzuia sababu zinazopelekea uchungu kabla ya wakati. Pia kupata huduma za kitiba hospitali katika chumba maalumu cha kuhudumia watoto njiti na ufuatiliaji wa karibu baada ya kuzaliwa.


Lengo la makala hii ni kukuelimisha mjamzito kuhusu mtoto njiti kwa ujumla


Aina za unjiti


Kuna makundi matatu ya mtoto njiti yanayotokana na umri wa mimba kwa wiki wakati wa kuzaliwa na uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa.


Mgawanyo huo husaidia kutambua ukomavu wa mtoto na matatizo ya unjiti yanayoweza kutokea na hivyo kuyazuia itiba


Mtoto njiti kulingana na umri wa mimba


  • Unjiti Uliokithiri – mtoto njiti aliyezaliwa chini ya wiki 28

  • Unjiti wa kati – mtoto njiti aliyezaliwa kati ya wiki 32 mpaka wiki 32

  • Unjiti wa wastani – mtoto njiti aliyezaliwa kati ya wiki 32 na kabla ya wiki 37


Mtoto njiti kulingana na uzito


Uzito sio njia sahihi ya kufahamu kama mtoto ni njiti au la, njia hii hutumika kujua uzito wa mtoto njiti wakati wa kuzaliwa;


Uzito mdogo uliokithiri- chini ya gramu 1000

Uzito mdogo sana – kati ya gramu 1000 mpaka 1499

Uzito mdogo – kati ya gramu 1500 mpaka 2500



Sababu zinazo pelekea mtoto njiti


Kuzaliwa kwa mtoto njiti hutokea katika namna mbili aidha kwa mama kupata uchungu kabla ya muda sahihi au mama kuzalishwa kabla ya muda kutokana na sababu za kitabibu.


Unjiti kutokana na kuzalishwa kabla ya muda kutokana na sababu za kitiba

Hii hufanyika kama kuendelea kubeba ujauzito ili ufikie muda wa kujifungua kutaleta madhara kwa mama na mtoto. Njia pekee ya kuzuia kupata madhara hayo ni kusitisha ujauzito kwa kuanzishiwa uchungu au kwa kufanyiwa upasuaji.


Hakuna umri maalum wa mimba kwa wiki ambapo maamuzi ya kusitisha ujauzito yanatakiwa kufanyika ila hutegemea sababu iliyosababisha ujauzito kuwa hatari mfano;


  • Mimba ya mapacha yenye matatizo

  • Shinikizo la damu la juu linaloelekea kifafa cha mimba ( pre eclampsia)

  • Kifafa cha mimba

  • Kutokwa damu wakati wa ujauzito baada ya wiki 28

  • Kupasuka kwa chupa ya uzazi kabla ya wiki 37


Unjiti kutokana na kuanza kwa uchungu kabla ya muda muafaka

Watoto njiti wengi ni matokeo ya mjamzito kupata uchungu kabla ya wakati sahihi. Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea mama kupata uchungu na kujifungua mtoto njiti kama ifuatavyo;


  • Mahudhurio hafifu au kutokuhudhuria kabisa kliniki

  • Historia ya kujifungua mtoto njiti

  • Historia ya kuharibika kwa mimba zilizopita

  • Ujauzito uliopatikana kwa upandikizaji kijusi

  • Mimba ya mapacha

  • Lishe duni wakati wa ujauzito

  • Upungufu wa damu

  • Umri mdogo au umri mkubwa wa mama mjamzito(Chini ya miaka 16 na zaidi ya miaka 35)

  • Maambukizo ya vimelea wa magonjwa

  • Uvutaji wa sigara

  • Matumizi ya dawa za kulevya

  • Kutojimudu kwa shingo ya kizazi


Matatizo yanayoambatana na unjiti


Hali ya kutokomaa kwa viungo na mifumo ya mwili hunasababisha matatizo mbalimbali kwa mtoto.

Ukubwa wa matatizo yanayoambatana na unjiti hutegemea umri na uzito wa mtoto wakati wa kuzaliwa, jinsi umri na uzito unavyokuwa mdogo ndivyo matatizo huwa mengi.


Wakati mwingine matatizo huisha kabisa baada ya matibabu na wakati mwingine humsababishia mtoto ulemavu wa viungo mbalimbali vya mwili.


Baadhi ya matatizo ambayo huonekana sana kwa watoto njiti huweza kuwa ya muda mfupi au muda mrefu ambayo ni;


Matatizo ya muda mfupi


  • Kushuka kwa joto la mwili

  • Kushindwa kunyonya na kumeza

  • Kushuka kwa sukari

  • Sindromu ya upumuaji wa shida

  • Vipindi vya kusimama kwa upumuaji

  • Upungufu wa damu

  • Maambukizo ya vimelea

  • Manjano

  • Kuvuja kwa damu

  • Kuoza kwa utumbo


Matatizo ya muda mrefu ya unjiti


  • Upungufu wa damu

  • Kutofunga kwa daktasi arteriosas

  • Retinopathi ya unjiti

  • Kudumaa kwa maendeleo ya kineva


Mtatizo ya muda mfupi ya unjiti


Haya ni matatizo yanayotokea mara baada ya kuzaliwa na huisha baada ya wiki kadhaa, huwa ni dharura na huchangia sana vifo vya watoto njiti endapo yasiposhughulikiwa mapema.


Kushuka kwa joto la mwili

Kushuka kwa joto la mwili hutokea endapo joto la mwili lipo chini ya nyuzi za joto za sentigredi 36.5


Husababishwa na wepesi wa ngozi ya mtoto unaotokana na kukosa mafuta chini ya ngozi ambayo hufanya kai ya kutunza joto la ndani ya mwili ili lisipotee kwenye mazingira.


Hivyo sababu yoyote ile inayopelekea kukaa katika hali ya hewa ya baridi hupelekea joto kushuka zaidi.


Kushindwa kunyonya na kumeza

Kwasababu ya kutokomaa kwa ubongo mtoto njiti hukosa rifleksi nyingi ikiwamo ile ya kunyonya na kumeza na hivyo kumuweka katika hatari ya kupaliwa wakati wa kunyonya


Licha ya kukosa rifleksi ya kunyonya, mtoto njiti huwa na tumbo dogo pia linalopelekea kujaa haraka na kumfanya apaliwe kirahisi akinyonya sana.


Kushuka kwa sukari kwenye damu

Sukari hutunzwa kwenye ini kama glaikojen na kubadilishwa kuwa glukosi pindi inapohitajika. Kwa sababu ya kutokomaa kwa kongosho na ini la mtoto, umetaboli wa glaikojeni kuzalisha glukosi huwa haufanyiki kama kwa watoto wasio njiti na hivyo kupelekea kushuka kwa sukari kwenye damu.


Sindromu ya upumuaji wa shida

Ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa ute kwenye mapafu kutokana na kutokomaa kwa mapafu. Ute huu huwa na protini na mafuta ambao hufunika kuta za alveoli (vifuko vya hewa). Ute huu huzalishwa na mapafu wiki ya 34 kwa hiyo watoto njiti chini ya wiki hizo hupata shida ya kupumua.


Ute huu husaidia kufanya kuta za alveoli zisishikane ili kuruhusu hewa kuingia na kutoka wakati wote. Ukosefu wa ute wa mapafu hupelekea alveoli kushindwa kufunguka na kufunga ili kuruhusu mbadilishano wa hewa kutokea na kupelekea mtoto kukosa hewa ya oksijeni.


Sindromu ya upumuaji wa shida hupelekea ugonjwa sugu wa mapafu unaoitwa Displezia ya mapafu


Vipindi vya kusimama kwa upumuaji

Apnia ni hali ya shughuli za upumuaji kusimama kwa sekunde 20 au zaidi au hali ya shughuli za upumuaji kusimama kwa zaidi ya sekunde 10 kunakoambatana na kushuka kwa mapigo ya moyo (chini ya mapigo 100 kwa dakika moja) au hali ya mwili kubadilika rangi kuwa bluu wakati huo.


Hali hii hutokea kwasababu ya kutokomaa kwa sehemu ya ubongo inayoratibu shughuli za mfumo wa upumuaji.


Upungufu wa damu mara baada ya kuzaliwa

Upungufu wa damu hutokea kwa sababu mwili hukosa akiba ya kutosha ya madini ya chuma yanayotumika kuzalisha damu.


Mtoto hupata kiwango kikubwa cha madini chuma kutoka kwenye damu ya mama miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, hivyo kuzaliwa kabla ya muda hupelekea tatizo hili.


Pia upungufu wa damu wakati wa kuzaliwa huweza kuzidishwa na sababu mbalimbali kama vile, hali ya kutokwa na damu, maambukizi ya vimelea, uchukuaji wa damu kwa ajili ya vipimo nk.


Maambukizi ya vimelea wa maradhi

Mfumo wa kinga ya mwili wa mtoto njiti huwa sio imara kuweza kukabiliana na vimelea mbalimbali wanaosababisha magonjwa, hivyo wanakuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya vimelea.


Magonjwa yanayoonekana kusumbua sana ni watoto njiti ni;


  • Homa ya mapafu (nimonia)

  • Sumu ya vimelea kwenye damu (sepsis)

  • Goma ya Uti wa mgongo

  • Maambukizi ya vimelea katika mfumo wa mkojo (UTI)


Kuongezeka kwa bilirubini kwenye damu

Kuongezeka kwa bilirubin kwenye damu hupelekea mtoto kupata manjano. Hali hii husababishwa na ini kushindwa kutoa bilirubini kutokana na uchanga wake na hii hupelekea kuzidi kwa kiwango cha bilirubini katika damu na wakati mwingine huingia kwenye ubongo na kuuharibu (kenikterasi) kisha kusababisha matatizo ya kuona, kusikia nk.


Mtoto huwa na rangi ya njano kwenye macho, soli za miguu, viganja na kwenye ngozi, bilirubini inapoingia kwenye ubongo husababisha huonesha dalili kama vile kulegea, kuwa na kisirani, kukakamaa nk.


Madhaifu ya kuvuja kwa damu

Hii ni hali ya hatari inayowapata njiti, huweza kutokea mara baada ya kuzaliwa au baada ya siku kadhaa.


Damu hutoka katika kitovu, kinyesi, matapishi na hata sehemu ambazo amechomwa sindano wakati wa matibabu.


Pia hutokea katika ubongo (intraventicular hamorrghage), mara nyingi ndani ya siku 3 baada ya kuzaliwa na huwapata zaidi watoto njiti chini ya wiki 32.


Shida ya kutokwa na damu hutokea kwasababu ya upungufu wa vitamin K, upungufu wa chembe sahani .n.k.


Kuoza kwa utumbo mpana

Ni ugonjwa hatari unaotokea katika matumbo, bakteria huvamia kuta za matumbo na kusababisha maambukizi yanayopelekea mzio mkubwa na kuharibu kuta za matumbo. Matumbo huoza na kutoboka na pia ugonjwa huu husambaa kwenye sehemu kubwa ya utumbo, bila matibabu ya haraka huweza kuathiri utumbo wote.


Dalili na viashiria vyake huwa ni kuvimba kwa tumbo, kutapika, damu katika kinyesi na homa. Bado hakuna sababu maalumu ya ugonjwa huu kutokea kwa watoto njiti


Mtatizo ya muda mrefu ya unjiti


Haya ni matatizo yanayoanza kuonkana miezi kadhaa baada ya kuzaliwa na katika kipindi cha utoto


Matatizo ya muda mrefu ya unjiti ni;


  • Upungufu wa damu

  • Kutofunga kwa daktasi arteriosas

  • Retinopathi ya unjiti

  • Kudumaa kwa maendeleo ya kineva


Upungufu wa damu kwa njiti baada ya kuzaliwa

Upungufu wa damu unaotokea baadae, huanza kujitokeza miezi minne ya maisha ya mtoto.


Husababishwa na kiwango kidogo cha akiba ya madini chuma wakati wa kuzaliwa, na kuongeza kwa matumizi ya madini chuma kadri mtoto anavyoendelea kukua.


Retinopathi ya unjiti

Hii hutokea kwasababu ya kutokutengenezwa vizuri kwa mishipa ya damu katika eneo hili muhimu la jicho, huwapata sana watoto njiti ambao wamekuwa kwenye matibabu ya oksijeni zaidi ya asilimia 95


Kutofunga kwa daktasi arteriosas

Watoto wote huzaliwa na na tundu ambalo hufunga kabisa mtoto anapozaliwa, hii ni kinyume na kwa watoto njiti kwani tundu hili hushindwa kufunga na moyo kufeli na kushindwa kusukuma damu ipasavyo.


Kuchelewa kwa ukuaji wa kineva

Kutokomaa kwa mfumo wa fahamu pamoja na uharibifu wa ubongo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kutoka damu, manjano nk husababisha matatizo ya kudumu kama ifuatavyo;


  • Utindio wa ubongo (mental retardation)

  • Mtindio wa ubongo

  • Matatizo ya kusikia

  • Matatizo ya kuona

  • Kichwa maji( haidrosefalaz)


Utambuzi wa umri wa mtoto njiti


Kwa sababu mtoto njiti humaanisha kuzaliwa hai kabla ya wiki 37, kuna ulazima wa kutambua umri wa mtoto wakati wa kuzaliwa. Zifuatazo ni njia zinazoweza kutumika kutambua umri wa mtoto njiti kwa wiki;


Kipimo cha ultrasound

Kipimo hiki huweza kutambua ukomavu wa mtoto akiwa tumboni na hivyo kukadiria umri kwa wiki, hata hivyo majibu ya kipimo hiki baada ya miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito huwa sio sahihi katika kukadiria umri wa mtoto kwahiyo utambuzi wa umri huangaliwa kwa majibu ya ultrasound iliyopigwa miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito


Kipimo cha ultrasound hutumika endapo mama hakumbuki tarehe ya mwisho ya hedhi au mzunguko wa siku zake hauko vizuri.


Pia husaidia kujua umri wa mtoto na kufanya maamuzi hasa yale yanayohusisha kuzalishwa kabla ya wakati kwasababu za kitabibu


Umri wa mimba kwa wiki

Umri wa mimba hupimwa kwa wiki kutoka tarehe ya mwisho ya kuanza hedhi mpaka tarehe ya makadirio ya kujifungua, ambapo huwa ni wiki 40.


Endapo mama hakumbuki tarehe yake ya mwisho ya hedhi umri wa mimba hupatikana kwa kupima kimo cha mimba kwa sentimita na kulinganisha na majibu ya kipimo cha ultrasound


Umri wa mimba kwa wiki haumaanishi umri halisi wa mtoto tumboni bali ni namna ambayo imepitishwa na wataalamu wa mambo ya uzazi ulimwenguni ili kuweza kujua hatua za ukuaji wa mtoto tumboni.


Mtoto anayezaliwa chini ya wiki 37 kutoka tarehe ya mwisho ya kuanza hedhi mpaka tarehe ya makadirio ya kujifungua huwa ni njiti.


Uchunguzi wa mwili wa mtoto

Uchunguzi huu hufanyika kwa kufanya tathmini ya ukomavu wa mtoto kwa kuhesabu alama za ballard . Alama za ballard huangalia muonekano wa mwili pamoja na ukomavu wa misuli na mfumo wa fahamu na hufanyika mara baada ya kuzaliwa hadi siku 4 baada ya kuzaliwa.


Kwa kuangalia vitu tajwa hapo juu umri wa mtoto kwa wiki hupatikana.


Dalili na viashiria vya unjiti


Licha ya kutumia umri wa mimba kutambua kama mtoto ni njiti au la, viashiria vifuatavyo vinathibitisha unjiti

  • Uzito mdogo chini ya gramu 2500

  • Ngozi nyembamba inayong’aa, yenye rangi ya pinki na mishipa ya damu huonekana kwa urahisi

  • Kuwa na nywele nyingi mwilini (lanugo)

  • Kuwa na mafuta kidogo mwilini

  • Kupumua kwa shida na kuwa na vipindi vya kutokupumua kabisa

  • Kutepweta kwa misuli ya mtoto au ulegevu

  • Mtoto huwa amenyoosha miguu na mikono badala ya kukunja

  • Masikio kuwa laini yanayokunjika kwa urahisi

  • Kwa mtoto wa kiume ngozi ya korodani huwa haina mikunjo, na

  • Kukosa korodani

  • Kwa mtoto wa kike mashavu makubwa ya uke huwa hayajafunika mashavu madogo ya uke na kuwa na kinembe kikubwa


Matibabu ya mtoto njiti


Watoto njiti wote ni lazima wawe katika matibabu kwasababu ya matatizo mbalimbali kama ilivyo ainishwa hapo awali. Lengo la matibabu haya ni kutokomeza vifo vya watoto njiti vinavyotokea ndani ya siku kadhaa baada ya kuzaliwa.


Matibabu hufanyika hospitali katika chumba maalumu chenye vifaa maalumu, na baadhi yao huudumiwa katika chumba cha watoto wachanga walio mahututi, hivyo basi mtoto njiti aliyezaliwa nyumbani au katika zahanati ni lazima apelekwe hospitali haraka kwa huduma zaidi.


Vipimo kwa mtoto njiti


Mtoto hupata matibabu na huchukuliwa vipimo mbalimbali kulingana na tatizo alilonalo kama ifuatavyo


Vipimo vifuatavyo hufanyika;


  • Kipimo cha damu (FBP)

  • Kipimo cha group la damu

  • Kipimo cha kiwango cha sukari kwenye damu

  • Kipimo cha chumvi za madini kwenye damu

  • Kipimo uchunguzi maji ya uti wa mgongo

  • Kipimo cha X-ray

  • Kipimo cha ultrasound


Maelezo zaidi kuhusu matibabu ya mtoto njiti


Matibabu ya maambukizi ya vimelea wa magonjwa

Watoto njiti chini ya wiki 34 na uzito chini ya gramu 2000, na wale walio katika hatari ya maambukizi wanatakiwa kupewa antibayotiki kama kinga


Dawa zinazotumika ni ampicillin na gentamycin, ambazo hutolewa kwa njia ya sindano za mishipa.


Matibabu ya kushuka kwa joto la mwili

Njia za kuzuia kushuka au kupotea kwa joto la mwili ni pamoja na zifuatazo;


Wakati wa kuzaliwa


  • Kumzalisha mama katika chumba chenye hali ya joto

  • Kumfuta mtoto majimaji mara baada ya kuzaliwa

  • Kumuweka mtoto kifuani mwa mama

  • Kuanza kunyonyesha kama mtoto anaweza kunyonya


Baada ya kuzaliwa


  • Kumuweka katika chumba maalumu cha watoto njiti chenye joto na vifaa vya kutoa joto mpaka atakapopata nafuu

  • Kumpa huduma ya kangaroo, mtoto anapokuwa na hali nzuri huduma hii huanza kwa kumbeba kwa kugusanisha ngozi kwa ngozi. Kumpa joto mtoto kwa njia hii kunasaidia sana mtoto kuwa katika hali nzuri na kuonezeka uzito kuliko kumuweka katika mashine ya joto

  • Kutokumuogesha kwa muda flani


Matibabu ya kushuka kwa sukari

Mtoto huweza kuonesha dalili na viashiria vya sukari kushuka na wakati mwingine asioneshe dalili na viashiria vya kushuka kwa sukari.


Kwa mtoto mwenye dalili na viashiria vya kushuka kwa sukari hupimwa kiwango chake cha sukari katika damu na hupewa maji maalumu ya sukari kulingana na kiwango change cha sukari katika damu.


Kwa mtoto asiye na dalili na viashiria vya kushuka kwa sukari mama hushauriwa kumpa maziwa mara kwa mara kwa kuzingatia umri na uzito wake.



Matibabu ya sindromu ya upumuaji wa shida (RDS)

Mtoto husaidiwa kupumua kwa kumuweka kwenye mashine ya oksijeni. Lengo ni kuhakikisha kiwango cha oksijeni kinakuwa kati ya asilimia 88-95. Mtoto mwenye RDS huwekewa tyubu maalumu ya kupitisha hewa ya okjiseni kupitia koo la hewa (continuous positive airway pressure CPAP). Pia hupewa surfactant kupitia tube hii endapo inapatikana.


Matibabu ya kushindwa kunyonya na kumeza

Mtoto huwekewa mpira maalumu wa kulishia na mama hukamua maziwa na kumlisha kupitia mpira huo.

Mama huelekezwa kiwango cha maziwa na muda wa kumlisha mtoto kulingana na umri na uzito.


Matibabu ya kutokwa na damu

Mtoto huchomwa sindano ya Vitamin k baada ya kuzaliwa kama watoto wengine. Kwa mtoto ambaye ameanza kuonesha dalili na viashiria vya kutokwa na damu huchomwa sindano vitamin k kwa muda wa masaa 72, hii ni tofauti na ile ya kuzaliwa. Hakuna matibabu maalumu ya kutoka damu katika chemba za ubongo, mtoto huwa katika uangalizi tuu ili kuzuia shida kuwa kubwa.


Matibabu ya upungufu wa damu

Matibabu hutegemea kiwango cha damu kwa mujibu wa kipimo cha haemoglobin, dalili na viashiria vya upungufu wa damu pamoja na umri wa mtoto

Kulingana na mchanganuo huo mtoto huongezwa damu au kupewa dawa za kuongeza damu.


Matibabu ya retinopathi ya unjiti

Mtoto mwenye shida ya kuona hufanyiwa upasuaji ili kurekebisha retina


Matibabu ya kuoza utumbo

  • Hii ni dharura ya kiupasuaji, mtoto anapokuwa na dalili na viashiria vya ugonjwa huu yafuatayo hufanyika

  • Mtoto kutonyonyweshwa kwa muda na badala yake kuwekea dripu za maji

  • Kuwekewa mpira wakulishia ili kupunguza gesi tumboni

  • Kupewa dawa aina ya ceftriaxone na metronidazole ili kuua vimelea wa magonjwa

  • Kwa mtoto mwenye dalili na viashiria vya kutoka damu katika matumbo hupewa dawa ya ranitidine na vitamin k

  • Kufanyiwa upasuaji ili kuondoa sehemu ya utumbo iliyoharibika



Matibabu ya kutofunga kwa daktasi arteriosas

Mtoto ambaye tundu katika moyo limeshindwa kufunga na kupelekea moyo kufeli hupewa matibabu yafuatayo;


  • Matibabu ya Oxygen

  • Dawa za kuzuia moyo kuendelea kufeli (frusemide and spironolactone)

  • Tundu dogo huweza kuziba kwa kumpa mtoto paracetamol and ibuprofen

  • Upasuaji kwa tundu kubwa ambalo limeshindwa kuziba kwa dawa


Ufuatiliaji wa maendeleo ya mtoto baada ya kuruhusiwa hospitali


Mtoto njiti huruhusiwa endapo anaweza kunyonya vizuri na hakuna matatizo yoyote yanayohitaji uangalizi wa karibu.Hakuna muda maalumu wa kuruhusiwa kutoka hospitali kwani ukubwa wa matatizo na muda wa matibabu hutofautiana kati ya mtoto na mtoto, kulingna na umri na uzito.Kabla ya kuruhusiwa mama hupewa elimu kuhusu dalili za hatari kwa mtoto, unyonyeshaji na huduma ya kangaroo.


Mtoto hupangiwa muda wa kurudi kliniki ya watoto kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ukuaji wake kulingana na uzito wake.Kwa mtoto mwenye uzito chini ya gramu 2500 huudhuria kliniki mara moja kwa wiki mpaka atakapofiksha uzito wa gramu 2500 Kwa mtoto mwenye uzito zaidi ya gramu 2500 huudhuria kliniki mara moja kwa mwezi


Pia mtoto hupangiwa vipindi vya kufatilia ukuaji wake hadi anapotimiza miezi 12 ya umri wake kwa kufuata umri wake kwa wiki


Mahudhurio ya kwanza baada ya kuruhusiwa

Mtoto anaporudi kliniki kwa mara ya kwanza yafuatayo hufanyika;


  • Hupewa virutubisho vya vitamini D

  • Virutubisho vya kalisiumu na fosiforasi kwa mtoto anayenyonya maziwa ya mama tuu kwa muda wa mwezi mmoja.

  • Virutubisho vya madini chuma kwa mtoto anayenyonya maziwa ya mama tuu, kwa muda wa miezi sita

  • Kupima wingi wa damu

  • Kupima uzito

  • Kuangalia ukuaji kwa kutumia uzito na urefu

  • Kuangalia ulaji

  • Kuangalia dalili na viashiria vya maambukizi ya vimelea

  • Kutoa chanjo kama ilivyopangwa


Mahudhurio yanayofuata

  • Kuendelea kumuhimiza mama juu ya huduma ya kangaroo mpaka pale mtoto atakapofiksha umri kamili ambao alipaswa kuzaliwa yaani umri wake kwa wiki 40, kwamfano mtoto aliyezaliwa na wiki 32 baada ya wiki 8 atakuwa na wiki 40.

  • Kuendelea kupima uzito

  • kuangalia ulaji wa mtoto

  • kutoa chanjo kama ilivyopangwa


Kinga ya mtoto njiti na matatizo yatokanayo


Baadhi ya sababu za mtoto njiti huweza kuzuilika na zingine hazizuiliki na jitihada hufanyika kuzuia matatizo yanayopelekea vifo vya watoto njiti ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa

Zifuatazo ni njia ambazo zinaweza kusaidia kupunguza tatizo la kuzaliwa kwa watoto njiti na matatizo yake


Kuhudhuria kliniki

Sababu nyingi zinazosababisha mama kupata leba huweza kugundulika mapema na kutibiwa wakati wa kliniki.


Wakati wa kliniki mama hupimwa na kupewa matibabu ya magonjwa kama vile upungufu wad amu, UTI, malaria nk.


Pia hupewa elimu kuhusu dalili na viashiria vya uchungu kabla ya muda, kwahiyo mahudhurio mazuri ya kliniki yanasaidia kupunguza sana kuzaliwa kwa watoto njiti


Kupata lishe bora

Mlo kamili wenye virutubisho hufanya ujauzito kuwa wenye afya na kuzuia matatizo ya upungufu wa damu



Kutumia dawa kuzuia uchungu

Dawa hizi zinaweza kuzuia uchungu kwa muda wa masaa 48, muda huu ni muhimu kwa kufanya jitihada nyingine kama kumpa mama dawa za kukomaza mapafu ya mtoto, kupanga njia sahihi ya kujifungua na kuandaa mazingira ya kumuhudumia mtoto


Baadhi ya dawa zinazotumika ni salbutamol, nifedipine, indomethacin nk


Dawa ya kukomaza mapafu

Hutolewa kwa wajawazito wote walio katika hatari ya kupata uchungu kabla ya muda au wale wanaotakiwa kujifungua kabla ya muda kutokana na sababu za kitabu.


Dawa inayotumika ni Dexamethasone, hutolewa kwa wajawazito wenye mimba ya umri chini ya wiki 34, husaidia kupunguza hatari ya kushindwa kupumua pamoja na kutokwa damu katika ubongo


Dawa ya Magnesium sulphate

Hutolewa kwa wajawazito wote walio katika hatari ya kupata uchungu kabla ya muda au wale wanaotakiwa kujifungua kabla ya muda kutokana na sababu za kitabu. Inasaidia kupunguza matatizo ya kuharibiwa kwa neva za fahamu (neurological damage) hivyo kuzuia matatizo ya muda muda mrefu ya kiukuaji. Pia inauwezo wa kuzuia uchungu kwa muda.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

29 Septemba 2021 18:48:51

Rejea za dawa

  1. Tanzania MoHCDEC.National guideline for Neonatal care and establishment of Neonatal Care Unit. Fith edition august 2019

  2. Bernadether T Rugumisa et al. Factors associated with risk of preterm delivery in Tanzania: A case-control study at Muhimbili National Hospital. Int J Gynaecol Obstet. 2021 Aug https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/33277704/. Imechukuliwa 01.08.2021

  3. University of Pittsburgh, School of Medicine. Premature Infants. https://www.msdmanuals.com/professional/pediatrics/perinatal-problems/premature-infants. Imechukuliwa 01.08.2021

  4. University of Pittsburgh, School of Medicine. Gestational Age. https://www.msdmanuals.com/professional/pediatrics/perinatal-problems/gestational-age. Imechukuliwa 01.08.2021

  5. Mortality and Acute Complications in Preterm Infants.https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK11385/. Imechukuliwa 01.08.2021

  6. R A Kambarami et al. Kangaroo care versus incubator care in the management of well preterm infants--a pilot study . Ann Trop Paediatr. 1998 Jun. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/9924567/. Imechukuliwa 01.08.2021

  7. WHO. Preterm birth. https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/preterm-birth. Imechukuliwa 01.08.2021

  8. CDC. Preterm birth|maternal and infant birth| reproductive health. https://www.cdc.gov/reproductivehealth/maternalinfanthealth/pretermbirth.htm. Imechukuliwa 01.08.2021

  9. PREMATURITY – Mediscape https://emedicine.medscape.com/article/975909-workup#c5. Imechukuliwa 01.08.2021

bottom of page