Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
18 Januari 2022, 09:33:57

Sonona kwa mjamzito
Sonona ni ugonjwa wa akili unaosababisha mtu kuwa katika hali ya majonzi na kupoteza hamu ya kufanya vitu ambavyo awali vilikuwa vinampa furaha au hamasa. Japo ni kawaida kwa binadamu kuwa na hali ya huzuni katika vipindi tofauti vya maisha hali hii huwa ya muda wa wiki 2 au zaidi inayoambatana na dalili katika mwili kama vile kukosa hamu ya kula, kupungua uzito, kukosa usingizi nk.
Sonona ni miongoni mwa magonjwa ya akili yanayotokea sana, inakadiriwa kuwa watu milioni 280 ulimwenguni wana sonona. Ugonjwa huu usipotibiwa huleta madhara kwa mgonjwa na katika jamii kama vile kupungua kwa ufanisi katika masomo, kazi, kukosa mahusiano mazuri na jamii na kujiua.
Sonona huwapata Zaidi wanawake kuliko wanaume, kwa sababu hii na Kutokana na mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito na majukumu ya uzazi, wajawazito huweza kuwa na sonona wakati wa ujauzito na/au baada ya kujifungua. Idadi ya wanawake wajawazito wenye sonona imekuwa ikiongezeka na inakadiriwa kuwa kati ya wanawake 8 waliojifungua 1 huwa na sonona.
Sonona wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua huathiri afya ya mama na mtoto kwani mama hushindwa kuwa na ukaribu na mtoto na wakati mwingine hukataa kunyonyesha na kushindwa kujihudumuia mwenyewe.
Visabishi Vya Sonona Kwa Mjamzito
Sonona husababishwa na muunganiko wa sababu mbali mbali za kijamii, kisaikolojia, na kibaiolojia. Sababu zifuatazo huchangia sana sonona wakati wa ujauzito.
Historia ya kuugua sonona
Historia ya ukatili wa kijinsia
Hali duni ya Maisha
Ujauzito ambao hakutarajiwa
Migogoro katika mahusiano ya kimapenzi
Hali ya kuwa na wasiwasi kuhusu ujauzito na malezi
Kukosa msaada kutoka kwa mwenza, familia au jamii
Majanga yanayoleta msongo kama vile kufiwa na mtu/watu wa karibu, kuachika nk
Utambuzi wa sonona kwa mjamzito
Hakuna vipimo vinavyoweza kutumika kutambua ugonjwa wa sonona, hutambuliwa kwa dalili na uchunguzi wa akili. Mgonjwa huwa na dalili zifuatazo
Wakati wa ujauzito
Kuwa katika hali ya huzuni na wasiwasi
Kukosa matumaini na kujilaumu
Hali ya kujitenga na watu
Kukosa usingizi au kulala sana
Kula sana au kukosa hamu ya kula
Kupungua uzito
Kufikiria au kujaribu kujiua
Maumivu ya mwili ambayo hayaponi kwa dawa
Baada ya kujifungua
Kulia bila sababu yoyote
Kuwa na hasira na ukali
Mawazo ya kumdhuru mtoto au kujidhuru mwenye
Kuwa na wasiwasi na kutokujiamini kuhusu malezi ya mtoto
Kukosa ukaribu na mtoto na wakati mwingine kukataa kunyonyesha
Madhara ya sonona kwa mjamzito
Yafuatayo ni madhara ya sonona kwa mjamzito wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua;
Uchungu kabla ya wakati
Kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo
Kuzaa njiti
Kukosa mapenzi na mtoto
Kumdhuru mtoto
Kujidhuru mwenyewe
Matibabu ya sonona kwa mjamzito
Matibabu ya sonona wakati wa ujauzito huwa saw ana watu wengine ambao hawapo kwenye kundi hili.Sonona hutibiwa kwa dawa na ushauri wa kisaikolojia, uchaguzi wa njia ya matibabu hutegemea ukubwa wa ugonjwa na namna unavyoaathiri Maisha yake ya kila siku.
Matibabu kwa ushauri wa kisaikolojia
Hutolewa kwa mgonjwa ambaye ana dalili za awali za sonona ambazo haziathiri utendaji wake wa Maisha ya kila siku. Mgonjwa hupewa elimu kuhusu tatizo lake na jinsi ya kukabiliana nalo kwa namna mbali mbali ikiwamo;
Tiba ya ufahamu wa tabia
Tiba ya msaada wa kisaikolojia
Matibabu ungainshi (wapenzi wawili)
Kuboresha lishe kwa kuacha vyakula vyene caffeine, nicotine, na kuacha pombe
Namna ya kuboresha usingizi
Njia za kupunguza msongo
Matibabu kwa dawa
Hufanyika kwa wale wenye dalili za ugonjwa zinazoathiri Maisha ya kila siku (moderate and severe depression). Dawa katika kundi liitwalo Selective Serotonin Reuptake Inhibtors (SSRIs) hutumika kutibu sonona kwa mjamzito, mfano wa dawa katika kundi hili ni Amitryptilyne.
Dawa hizi zinahusishwa na matokeo mabaya ya ujauzito kama vile kujifungua kabla ya wakati, mtoto kuzaliwa amechoka na kuzaliwa na uzito mdogo. Tafiti zinaonesha kuwa watoto ambao mama zao wanatumia dawa kutibu sonona wiki za mwisho za ujauzito huwa na matatizo ya kupumua na hupata degegede.
Licha ya madhara haya inashauriwa mgonjwa kutumia dawa katika kipindi chote cha ujauzito na baada ya kujifungua ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa, na Watoto kuwa katika uangalizi.ili kutibu madhara yatokanayo na dawa.
Jinsi ya kuzuia sonona kwa mjamzito
Mambo yafuatayo yanaweza kusaidia kupunguza tatizo la sonona kwa mjamzito;
Kupata ushirikano mzuri na jamii inayomzunguka
Kuwa na mahusiano mazuri na mwenza wake
Kujihusisha na vitu mbali mbali vinavyoleta furaha
Kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuzuia mimba zisizotarajiwa
ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
18 Januari 2022, 09:33:57
Rejea za dawa
WHO.Depression. 13 September 21 www.who/news-room/fact-sheets/detail/depression .Imechukuliwa 13.01.2022
CDC Reproductive Health. Depression During and After Pregnancy. https://www.cdc.gov/reproductivehealth/features/maternal-depression/index.html. Imechukuliwa 13.01.2022
Christie A. Lancaster, MD, MS, Katherine J. Gold, MD, MSW, MS, [...], and Matthew M. Davis, MD, MAPP. Risk factors for depressive symptoms during pregnancy: a systematic review.Am J Obstet Gynecol. 2010 Jan; 202(1): 5–https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2919747/#__ffn_sectitle Imechukuliwa 13.01.2022
Nilam shakeel et al. A prospective cohort study of depression in pregnancy, prevalence and risk factors in multi-ethinic population January 2015. https://bmcpregnancychildbirth.bimedcentral.com/articles/10.1186/s12884-014-0420-0. Imechukuliwa 13.01.2022
Julie S. Moldenhauer, MD, Children’s Hospital of Philadelphia. Postpartum Depression. May 2020. https://www.msdmanuals.com/professional/gynecology-and-obstetrics/postpartum-care-and-associated-disorders/postpartum-depression / Imechukuliwa 13.01.2022
Jennifer L. Melville, MD, MPH et al. Depressive Disorders During Pregnancy. Obstet Gynecol. 2010 Nov; 116(5): 1064–1070. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3068619/#_ffn_sectitle. imechukuliwa 13 /01/2022
Christina L. Wichman, DO and Theodore A. Stern, MD.Diagnosing and Treating Depression During Pregnancy.2015 April. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4560196/#__ffn_sectitle Imechukuliwa 13.01.2022