top of page

Mwandishi:

Dkt. Mangwella S, MD

Mhariri:

Dkt Peter A, MD

19 Desemba 2021 11:13:35

Image-empty-state.png

Uchungu

Uchungu hutokana na kujongea kwa misuli ya kizazi, tendo linalopelekea kusukumwa kwa mtoto nje ya tumbo la uzazi na mwishowe mjamzito kujifungua. Kuta za mimba, kitovu na kondo la nyuma hutolewa katika mfuko wa tumbo. Mabadiliko haya ni ya kifiziologia na yanahusisha homoni mbalimbali mwilini na mfumo wa fahamu

Hatua za uzazi ama kujifungua

Uzazi umegawanyika katika sehemu kuu tatu endelevu kulingana na mgawanyo uliofanywa na wataalamu wa uzazi.

Hatua ya kwanza ya Uzazi

Huanza kwa kubana na kuachia kwa mfuko wa uzazi, mama hupata maumivu ya tumbo kutokana na mfuko wa tumbo kubana na kuachia. Kipimo cha kipenyo cha shingo ya kizazi cha kutumia vidole kinaweza onyesha mlango wa kizazi umetanuka kufikia sentimeta 10. Hatua hii imegawanyika katika sehemu ndogo mbili, hatua ya ukimya na hatua ya utendaji.


Hatua ya ukimya


Hatua ya ukinywa au iliyojificha huwa na sifa ya kusababisha


 • Maumivu kiasi ya kubana na kuachia

 • Maumivu yasio na mtiririko sahihi

 • Shingo ya kizazi kupungua urefu na huwa laini


Kubana na kuachia kwa tumbo huendelea kuongezeka kwa kila baada ya muda fulani na kuwa makali zaidi na safari hii inaweza kusababisha maumivu makali zaidi.


Hatua ya utendaji


Mama anapoingia katika hatua ya utendaji shingo ama mlango wa uzazi huwa tayari umehafikia sentimeta 3 hadi 4 na hatua hii huwa na uongezekaj wa kutanuka kwa mlango wa uzazi kwa kasi zaidi, mtoto pia huanza kushuka kutoka katika mfuko wa uzazi

Hatua ya pili ya uzazi

Huanza na kutanuka kamili kwa mlango wa kizazi(kipenyo cha shingo ya kiazazi hufika sentimita 10) na humalizika kwa kuzaliwa kwa mtoto.


Kuchelewa kwa hatua ya pili ya uzazi


Kwa mama ambaye hajawahi kujifungua, hatua hii itasemekana imechelewa au kuchukua muda mrefu endapo itazidi masaa 3 bila mama kujifungua kama amepata dawa za nusu kaputi, ama ikichukua zaidi ya masaa mawili (2) kama hajapata dawa yoyote ya kaputi


Kwa wanawake ambao wameshawahi kujifungua zaidi ya mara moja, hatua hii ya uzazi huchukua masaa mawili tu 2. Hivyo uzazi husemekan umechelewa kama hatua hii ikichukua zaidi ya masaa 2 kama amepata dawa za nusu kaputi ama saa moja (1) kama hajapata dawa za nusu kauti

Hatua ya tatu ya uzazi

Hatua ya tatu ya uzazi hutokea baada ya mtoto kuzaliwa, hatua hii huwa maalumu kwa ajili ya kondo la nyuma kutoka katika uzazi ( kujifungua kondo la uzazi), na baadhi ya kuta za mtoto zilizobaki ndani baada ya mtoto kutoka.

 • Kutoka kwa kondo la nyuma huchukua dakika 10 ama chini ya mda huo, lakini hatua ya tatu hukaa kwa muda wa dakika 30.

 • Uzazi wa kondo la nyuma hutokea wenyewe bila kusaidiwa na mtaalamu wa afya au mkunga

 • Hatua hii endapo itachukua zaidi ya dakika 30 pasipo kutoka kwa kondo la nyuma basi .husemekana imechelewa ama kuchukua mda mrefu na msaada wa haraka unahitajika ili mama asipoteze damu nyingi kutokana na kubaki kwa kondo la nyuma ndani ya mfuko wa uzazi.

Matibabu ya haraka yanahusisha kuchomwa sindano ya dawa inayoitwa oxytocin ama dawa zingine za aina ya prostaglandin au ergot alkaloid, kufunga-kubana kondo la nyuma na kukata na kuvuta kwa njia ya kubana mkono moja kwenye tumbo katika kibofu na mwingine ukiwa unavuta kitovu

Historia ya mama anayejifungua

Uchunguzi wa awali unatakiwa kuulizia taarifa za mahudhurio ya kliniki, ikiwa pamoja na kuhakiki tarehe ya matarajio iliyoandikwa. Historia inayolenga nia inatakiwa ihusishe mambo yafuatayo

 • Wingi na muda ambapo maumivu ya tumbo au kubana na kuachia kwa tumbo kulipoanza

 • Hali ya chupa ya uzazi, kama imeshapasuka na kama imeshapasuka, rangi ya maji ikoje yaani ni meupe au meusi- ikimaanisha maji yanakinyesi cha mtoto

 • Kuuliza kama Mtoto anacheza tumboni

 • Kutokwa na damu au kutotoka kwa damu ukeni

Jambo la msingi kukumbuka ni kwamba, wamama wakati mwingine wanapata maumivu ya tumbo ya kubana na kuachia yasiyo ya uchungu wa kweli n amepewa jina kama Braxton-hicks contraction. Kubana na kuachia kwa tumbo huwa na sifa zifuatazo

 • Hutokea si zaidi ya mara moja au mbili kwa lisaa, na mara nyingi huwa marachache kwa siku

 • Huwa yasiyofuata utaratibu na hayaongezeki namba wala makali mda unapoendelea

 • Huisha kwa kutembea ama kubadili kufanya kazi nyingine

Sifa za uchungu wa kujifungua

 • Yanaweza kuanza kwa kutokuwa mengi katika kila dakika 10 hadi 15, lakini mara nyingi huongezeka kwa jinsi mda unavyosonga na hubadili mda na sasa kutokea kila baada ya dakika 2 hadi 3 kwa kila uchungu

 • Uchungu hukaa kwa muda mrefu na huwa makali zaidi ya yale ya Braxton hicks contraction

 • Maumivu haya husababisha kutanuka kwa malango wa kizazi

Vipimo wezeshe


Mtaalamu wa afya anatakiwa kufanya uchunguzi wa vipimo vingine kuangalia


 • Vipimo vya ishara muhimu

 • Kitangulizi cha mtoto

 • Kuangalia uhai wa mtoto

 • Wingi, muda na ukubwa wa kubana na kuachia kwa tumbo ama uchungu

 • Kufanya kipimo cha kuchunguza tumbo yaani leopold maneuvers

 • Uchunguzi wa maeneo ya via vya uzazi kwa kutumia mikono iliyovalisha glavu safi

Mambo utakayofanyiwa wakati wa uchungu

Hatua ya kwanza

Mara utakapoandikiwa kulala wodini kwa sababu ya uchungu, utashauriwa mlalo ambao unajisikia vizuri na ikiwezekana

 • Kutembea tembea

 • Kulalia mgongo

 • Kukaa

 • Kulalia ubavu wa kushoto

Wakati huu mtaalamu wa afya atakuwa anafanya vipimo vya kuangalia kipenyo cha mlango wa uzazi kila baada ya masaa manne na kupima kwa mapigo na mwendo kasi wa moyo wa mtoto kila baada ya dakika 15.

Hatua ya pili ya uzazi

Kama njia ya uzazi imeshatanuka na kufkia mwisho yaani sentimeta 10, mapigo ya moyo ya mtoto yatapimwa kila baada ya dakika 5 na kila baada ya kubana na kusinyaa kwa tumbo. Kuzidi ama kuchelewa kwa kipindi cha pili cha uzazi kama chenyewe hakitoi ruhusa ya kujifungua kwa upasuaji kama kuna hatua za uchungu zimeendelea sana. Mambo utakayofanyiwa katika kipindi hiki ni;

 • Kusubiliwa na kuchunguza hali yako na mtoto

 • Kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto tumboni

Wakati wa kujifungua kwa mtoto

Mama anaweza kulala milalo tofauti wakati wa kujifungua kama vile

 • Kulala chali

 • Kulala ubavu

 • Kukaa kiasi ama kuchuchumaa kiasi ukiwa ameshika mikono na miguu chini.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

24 Desemba 2021 05:54:29

Rejea za dawa

 1. Julia Hutchison, et al. Stages of Labor. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK544290/. Imechukuliwa 19.12.2021.

 2. Prabhcharan Gill, et al. Abnormal Labor. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK459260/.Imechukuliwa 19.12.2021.

 3. Steer, P, and C Flint. “ABC of labour care: physiology and management of normal labour.” BMJ (Clinical research ed.) vol. 318,7186 (1999): 793-6. doi:10.1136/bmj.318.7186.793

 4. Labor, et al. “The Pain of Labour.” Reviews in pain vol. 2,2 (2008): 15-9. doi:10.1177/204946370800200205.

bottom of page