top of page
Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:

Dkt. Glory, MD

ULY CLINIC

14 Julai 2025, 06:25:19

Damu au kinyama mimba ya mwezi mmoja ikiharibika (1).jpg

Kutokwa damu baada ya mimba kuharibika: Sababu, tahadhari na hatua za kuchukua

Swali la msingi


Habari daktari, nina tatizo la kutokwa sana na damu inakata inaacha badae inakata inaanza tena. Nilipoteza ujauzito mwezi 1 uliopita ambao ulikuwa na miezi 2 na week 2 . Nifanye nini?


Majibu

ree

Pole sana kwa changamoto hiyo uliyoipitia. Tatizo la kutokwa na damu mara kwa mara baada ya kupoteza ujauzito au mimba kuharibika inaweza kuwa dalili ya matatizo ya kiafya yanayohitaji uchunguzi wa haraka na matibabu sahihi. Hapa chini nimeeleza baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha hali hiyo na nini unapaswa kufanya.


Visabaishi

Zifuatavyo ni baadhi ya visababishi vya kutokwa na damu kila mara baada ya kupoteza jauuzito;


Sehemu ya kondo la nyuma kubaki ndani ya mfuko wa uzazi

Mabaki haya huweza kusababisha damu kutoka kidogo kidogo au kuanza na kuacha kwa wiki kadhaa.


Maambukizi kwenye kizazi

Hutokea iwapo kuna bakteria waliingia baada ya kupoteza mimba, dalili huwa pamoja na kutokwa na damu yenye harufu mbaya, homa, maumivu ya tumbo chini, uchovu n.k.


Mvurugiko wa homoni

Baada ya mimba kuharibika, homoni za uzazi kama projesteroie na estrojen hubadilika. Ikiwa hazijatulia, damu huweza kutoka na kuleta mzunguko wa hedhi usiotabirika.


Mzunguko wa hedhi baada ya kuharibika mimba

Baadhi ya wanawake hupata mzunguko wa hedhi mpya wiki 4–6 baada ya kupoteza ujauzito, na inaweza kuonekana kama damu inayorudia kutoka mara kwa mara.


Matatizo ya kutokwa damu

Matatizo ya kutoka damu kutokana na madhaifu ya ugandaji wa damu pia yanaweza kuchangia kutokwa damu endelevu baada ya mimba kuharibika.


Majeraha kwenye njia ya uzazi na uke

Majeraha kwenye uke na njia ya uzazi ni miongoni mwa sababu muhimu zinazoweza kusababisha kutokwa na damu baada ya mimba kutoka. Mara nyingi majeraha haya hutokea endapo mimba imetoka kwa njia isiyo salama au bila msaada wa kitaalamu. Sababu kuu ni pamoja na matumizi ya dawa au mitishamba kwa njia ya kuingizwa ukeni, matumizi ya vyuma au vifaa visivyo salama ambavyo huweza kujeruhi kuta za uke, mlango wa kizazi au mfuko wa uzazi. Pia, utoaji wa mimba bila ujuzi wa kitaalamu unaweza kusababisha kukwaruza au hata kutoboa kizazi. Utoaji wa mimba kwa kutumia nguvu, kama vile kushiriki kazi nzito au kupata ajali wakati wa ujauzito, huweza pia kuchangia majeraha haya.


Aidha, kusafishwa kwa kizazi bila uangalifu wa kutosha kunaweza kujeruhi shingo ya kizazi au kizazi chenyewe, na hivyo kusababisha kutokwa na damu ya muda mrefu au inayorudia mara kwa mara. Majeraha haya yanapopuuzwa, yanaweza kuambatana na maambukizi, maumivu makali, na matatizo ya muda mrefu kama vile utasa.


Ni nini unachopaswa kufanya?

1. Muone daktari au nenda kituo cha afya haraka

Wahudumu wa afya watafanya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na:

  • Kipimo cha picha ya kizazi kwa kutumia picha ya mionzi sauti (Ultrasound) kuangalia kama kuna mabaki.

  • Vipimo vya damu (hemoglobin, homoni, au kuangalia maambukizi).

  • Uchunguzi wa uchafu au damu kutoka ukeni.

  • Vipimo vya kuangalia ugandaji wa damu kama PT, APTT

  • Antijeni za VWF

  • Kuhesabu kwa chembe sahani za damu


2. Epuka kutumia dawa za kuzuia damu bila ushauri

Dawa kama tranexamic acid au dawa za mitishamba bila uchunguzi zinaweza kuficha tatizo na kuchelewesha tiba sahihi.


3. Epuka kuingiza kitu chochote ukeni hadi utakapopona

Ikiwa kuna maambukizi au jeraha bado halijapona, inaweza kuzidisha hali.


Matibabu

Matibabu ya hospitali

Matibabu yanaweza Kujumuisha:

  • Dawa za kusafisha kizazi au kukaza mfuko wa uzazi.

  • Kusafishwa kwa njia ya upasuaji mdogo ikiwa mabaki yapo.

  • Dawa za kutibu maambukizi kama antibiotiki.

  • Matibabu ya upungufu wa damu kwa lishe na vidonge vya madini chuma.


Matibabu lishe

Lishe inayopendekezwa kwako ili kuzuia upungufu wa damu na kurejesha afya ni;

  • Chakula chenye madini ya chuma (maini, mchicha, dengu).

  • Matunda yenye vitamini C kusaidia kufyonzwa kwa chuma (machungwa, nanasi).

  • Maji ya kutosha.

  • Epuka kahawa nyingi na chai mara baada ya kula vyenye chuma.


Wakati gani wa kumwona daktari haraka?

Ikiwa damu inatoka kwa wingi sana, umechoka sana, unapata homa au tumbo linauma sana nenda hospitali haraka. Usisubiri hali iwe mbaya, hata kama ni miezi 1 tangu mimba ipotee.


Rejea za mada hii;

  1. American College of Obstetricians and Gynecologists. Early Pregnancy Loss: ACOG Practice Bulletin, Number 200. Obstet Gynecol. 2018;132(5):e197–e207.

  2. World Health Organization. Clinical practice handbook for safe abortion. Geneva: WHO; 2014.

  3. Neilson JP, Gyte GM, Hickey M, Vazquez JC, Dou L. Medical treatments for incomplete miscarriage (less than 24 weeks). Cochrane Database Syst Rev. 2013;(3):CD007223.

  4. Schreiber CA, Creinin MD. Medical management of early pregnancy failure: misoprostol versus surgical evacuation. Am J Obstet Gynecol. 2005;192(5):1731–6.

  5. Sheldon WR, Durocher J, Winikoff B, Blum J, Trussell J. Infection after medical abortion: a review of the literature and comparison of rates. Contraception. 2014;89(4):300–6.

  6. Hoveyda F, MacKenzie IZ. Secondary infertility following miscarriage: a retrospective cohort study. J Obstet Gynaecol. 2010;30(2):134–6.

  7. Moulder JK. Recurrent Pregnancy Loss: Evaluation and Management. Am Fam Physician. 2021;103(5):297–304.

  8. Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. The Management of Early Pregnancy Loss. Green-top Guideline No. 25. London: RCOG; 2006.

  9. World Health Organization. Clinical practice handbook for safe abortion. Geneva: WHO; 2014. p. 25-32.

  10. Haddad LB, Nour NM. Unsafe abortion: unnecessary maternal mortality. Rev Obstet Gynecol. 2009;2(2):122–6.

  11. Grimes DA, Benson J, Singh S, Romero M, Ganatra B, Okonofua FE, Shah IH. Unsafe abortion: the preventable pandemic. Lancet. 2006 Nov 25;368(9550):1908–19.

  12. Paul M, Lichtenberg ES, Borgatta L, Grimes DA, Stubblefield PG, Creinin MD. Management of unintended and abnormal pregnancy: comprehensive abortion care. 2nd ed. Chichester: Wiley-Blackwell; 2009. Chapter 12.

  13. Guttmacher Institute. Abortion Worldwide: Uneven Progress and Unequal Access. New York: Guttmacher Institute; 2017.Start with online tutorials and practice by building simple projects to gradually improve your skills.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

bottom of page