Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dr.Sospeter Mangwella, MD
ULY CLINIC
15 Juni 2025, 08:14:56
Uchafu ukeni baada ya kujifungua
Baada ya kujifungua, ni kawaida kwa mwanamke kutokwa na uchafu ukeni unaojulikana kama lochia. Uchafu huu ni mchanganyiko wa damu, ute wa kizazi, seli zilizokufa, na mabaki ya kondo la nyuma. Lochia ni sehemu ya mchakato wa kurudi kwa mji wa mimba katika hali ya kawaida na huendelea kwa muda wa siku kadhaa hadi wiki.
Muda wa uchafu kutoka ukeni
Kwa kawaida, lochia huisha ndani ya wastani wa siku 14, lakini kwa baadhi ya wanawake, inaweza kuendelea hadi siku 21 au zaidi bila kuwa tatizo. Mabadiliko ya rangi na kiasi cha uchafu huu huashiria hatua tofauti za kupona kwa mfuko wa mimba.
Ratiba ya mabadiliko ya rangi ya uchafu
Mabadiliko ya rangi ya lochia hufuata mpangilio maalum:

Lochia rubra (rangi nyekundu): Hii ni hatua ya awali ya uchafu na hudumu kati ya siku 1 hadi 4 baada ya kujifungua. Damu huwa nyekundu ang'avu.
Lochia serosa (rangi ya kahawia hadi ya waridi): Hii hutokea kati ya siku ya 5 hadi 9. Rangi huwa ya kahawia au waridi nyepesi na kiasi cha damu hupungua.
Lochia alba (rangi ya njano hadi ute wa kawaida): Hatua ya mwisho huanza kuanzia siku ya 10 hadi 15. Rangi ya uchafu huwa njano au nyeupe na inaonekana kama ute wa kawaida wa ukeni.
Wakati gani unapaswa kuwa na wasiwasi?
Licha ya lochia kuwa hali ya kawaida, kuna baadhi ya dalili zinazoweza kuashiria tatizo. Mwanamke anapaswa kuwasiliana na mtoa huduma ya afya endapo atakutana na mojawapo ya dalili zifuatazo:
Kupata homa au kuhisi baridi kali
Uchafu kuwa na harufu mbaya kama ya kuoza
Rangi ya uchafu kubakia kuwa nyekundu baada ya wiki moja
Kutokwa na mabonge ya damu kwa zaidi ya siku 3 za mwanzo
Maumivu makali ya tumbo la chini
Kizunguzungu au kusikia kuchoka kupita kiasi
Mapigo ya moyo kwenda kasi bila sababu ya wazi
Kutokwa na uchafu mwingi unaozidi au usiopungua kwa kadri siku zinavyoenda
Kuhisi kama kuna kitu kinashuka au kutoka ukeni
Uchafu kuendelea hadi zaidi ya siku 42 (wiki sita)
Hitimisho
Kutokwa na uchafu baada ya kujifungua ni sehemu ya kawaida ya mchakato wa kurejea katika hali ya kawaida ya mwili wa mwanamke. Hata hivyo, ni muhimu kufuatilia rangi, kiasi, harufu, na dalili nyingine zozote zisizo za kawaida ili kuhakikisha hakuna maambukizi au matatizo mengine yanayoendelea.
Rejea za mada:
Science Direct. Lochia. Available from: https://www.sciencedirect.com/topics/medicine-and-dentistry/lochia. Accessed 18 Nov 2024.
NHS. Your body after the birth. Available from: https://www.nhs.uk/pregnancy/labour-and-birth/after-the-birth/your-body/. Accessed 18 Nov 2024.
What to Expect. Postpartum Bleeding (Lochia): What's Normal and What's Not? Available from: https://www.whattoexpect.com/pregnancy/symptoms-and-solutions/postpartum-bleeding.aspx. Accessed 18 Nov 2024.
Romano M, et al. Postpartum period: three distinct but continuous phases. J Prenat Med. 2010;4(2):22–5.
Sherman D, et al. Characteristics of normal lochia. Am J Perinatol. 1999;16(8):399–402.
Oppenheimer LW, et al. The duration of lochia. Br J Obstet Gynaecol. 1986;93(7):754–7.
Chi C, et al. Puerperal loss (lochia) in women with or without inherited bleeding disorders. Am J Obstet Gynecol. 2010;203(1):56.e1–5.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
