top of page

Imeandikwa na ULY CLINIC

 

Kujifungua kwa upasuaji

 

Kujifungua kwa upasuaji katika makala hii imetumika kumaanisha neno tiba caesarian delivery, ambacho ni kitendo cha kuchana kuta za tumbo na uzazi ili kutoa mtoto aliye kwenye mji wa mimba.  Kitendo hiki hufahamika kitiba kwa jina la caesarian section.

Kuna sababu mbalimbali zinaweza kuchangia mwanamke kujifungua kwa upasuaji, hata hivyo kujifungua kwa njia hii huweza kupangwa kabla ya uchungu kutokea au wakati wa uchungu endapo kuna ishara zimetokea zinazokufanya ushindwe kujifungua kwa njia ya kawaida.

 

Endapo wewe ni mjamzito unapaswa kufahamu njia za kujifungua ili uweze kufanya maamuzi sahihi wa njia gani sahihi na kwa nini njia hiyo itumike wakati wa kujifungua.

 

Sababu zinazofanya mtu ajifungue kwa upasuaji;

 

Zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kupelekea mwanamke akajifungua kwa njia ya upasuaji ambazo ni;

 

Kutoendelea vema kwa uchungu

 

Kutoendelea au kusimama kwa uchungu ni moja ya sababu kubwa inayopelekea wamama wengi wajifungue kwa upasuaji. Uchungu ukisimama au kutoendelea kama inavyotakiwa hupelekea shingo ya kizazi kutofunguka na hivyo mtoto kutoweza kutoka. Daktari au nesi kwa kawaida huangalia hali ya shingo ya kizazi kila baada ya masaa manne au pungufu yake ikitegemea mwitikio wake dhidi ya uchungu kwa kuingiza vidole viwili kupitia uke. Kwa kufanya hivi huweza kutambua hali yake ikoje na imetanuka kwa sentimita ngapi. Njia hii ni njia mojawapo ya kuangalia maendeleo ya uchungu.

 

Mtoto kuchoka

 

Kitiba hufahamika kwa jina la fetal distress, hali hii hugunduliwa endapo mapigo ya moyo ya mtoto yameshuka au yamepanda juu ya kiwango cha kawaida ambacho hupimwa kwa kifaa maalumu kinachowekwa kwenye tumbo. Kiwango cha kawaida cha mapigo ya moyo wa mtoto huwa kati ya midundo 110 hadi 160 kwa dakika (110-160b/min).

Mtoto kulala vibaya kndani ya kizazi

 

Kwa kawaida mtoto anatakiwa kutanguliza kichwa kabla ya mwezi wa mwisho wa kujifungua. Endapo mtoto ametanguliza matako au mabega au amelala mshazari badala ya kutanguliza kichwa, daktari atakuambia mtoto amelala vibaya hivyo utajifungua kwa upasuaji. Kuna baadhi ya milalo ya mtoto inaweza kufanyiwa kazi ili kufanya mtoto alale kwa kutanguliza kichwa, hata hivyo endapo juhudi zitaferi utatakiw akujifungua kwa upasuaji.

 

Kuwa na mimba ya mapacha au zaidi

 

Kuwa na mimba ya mapacha si kigezo pekee cha kujifungua kwa njia ya upasuaji hata hivyo sababu zinazoweza kukufanya ujifungue kwa upasuaji unapokuwa na mimba ya mapacha huwa pamoja na; mtoto wa kwanza kutanguliza makalio au kulala vibaya na kuwa na mimba ya watoto zaidi ya wawili.

 

Kondo la nyuma kujishikiza karibu na kizazi

 

Kitiba huitwa placenta previa, hii hutokea pale endapo kondo la nyuma limejishikiza karibu na shingo ya kizazi, hutajifungua kwa njia hii kwa sababu mtoto atashindwa kupita vema au atakandamiza kondo hilo. Kondo la nyuma huwa na kazi ya kuingiza virutubisho kwa mtoto, kumpa hewa safi ya oksijen na kuondoa hewa chafu ya carbon dioxyside. Endapo kondo hilo limetangulia au limejishikiza kwenye shingo ya kizazi ni rahisi kunyofoka au kukandamizea wakati wa mtoto anapita na kupelekea mtoto kukosa hewa na kufa.

 

Kunyofoka kwa kondo la nyuma

 

Endapo kondo la nyuma limenyofoka lote au sehemu kidogo tu kutoka kwenye ukuta wa kizazi, daktari ataamua ufanyiwe upasuaji haraka ili kuokoa maisha ya mtoto. Sababu ya upasuaji ni ile ile kwamba mtoto huwa anakosa virutubisho na hewa safi ya oksijeni ambayo inamsaidia kuishi. Kuchelewa kufanya upasuaji kutasababisha mtoto kuzaliwa amechoka au kufia tumboni.

 

Kutangulia kwa kitovu cha mtoto

Endapo kitovu cha mtoto kimetangulia mbele ya uke kabla ya mtoto hii itakuwa ni sababu ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua. Hii ni kwa sababu ya hofu ya mtoto kukandamiza kondo hilo wakati anapita kwenye tundu la uzazi, sababu hii inaweza kupelekea kifo cha mtoto.

 

Kuwa na nyonga ndogo

 

Endapo nyonga yako ni ndogo au imekakamaa ikimaanisha haiwezi kufunguka ili kuruhusu mtoto kupita kirahisi, daktari ataamua kukufanyia upasuaji wa kumwondoa mtoto. Hali hii ya kuwa na nyonga ndogo hutambulika kabla ya uchungu kuanza wakati unaenda kuhudhuria kliniki. Hata hivyo endapo umefika wakati wa uchungu, daktari au nesi atakupima kuangalia uwezo wa nyonga yako.

 

Kizuizi kwenye njia ya uzazi

 

Endapo kuna kizuizi katika kizazi kinachosababisha mtoto asipite kirahisi, kwa mfano kuwa na fibroid kubwa, au mtoto kuwa na kichwa kikubwa mfano mtoto mwenye kichwa maji, daktari atakushauri ujifungue kwa upasuaji ili kukuokoa wewe na mtoto.

 

Kuwa na historia ya upasuaji kwenye ujauzito uliopita

 

Unaweza kufanyiwa upasuaji kwa ujauzito wa sasa endapo ujauzito uliopita ulifanyiwa upasuaji endapo sababu iliyosababisha kufanyiwa upasuaji imejirudia au kuwepo kwa sababu zingine ambazo zinaongeza hatari yaw ewe kujifungua kwa upasuaji. Mama aliyejifungua kwa upasuaji ujauzito mmoja uliopita anaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida endapo Hakuna sababu kama ile ya awali,kovu lake limepona vema na sababu zingine endapo zipo vizuri ambazo zimeelezewa kwenye Makala nyingine ndani ya tovuti hii.

 

Mtoto wa kipekee

 

Endapo ujauzito huu ni wa kipekee, ikinamaanisha mtoto uliyenaye ndo mtoto wa kwanza na umekuwa ukimtafuta baada ya muda mrefu sana hii inaweza kuwa sababu ya wewe kufanyiwa upasuaji ili kuhakikisha kwamba mama na mtoto hawapati madhara wakati wa kujifungua. Hii hufanyika kwa wanawake wenye mimba ya kwanza kwenye umri mkubwa sana mfano wenye umri Zaidi ya miaka 35, wanawake waliokuwa na matatizo ya mimba kutoka au kuharibika wakati wa kujifungua. Hata hivyo njia hii haishauriwi endapo una mpango wa kuwa na watoto wengi zaidi

Ombi la mama

 

Mama mjamzito anaweza kuomba afanyiwe upasuaji endapo anahitaji kutokana na sababu binafsi. Daktari anaweza kuamua kumsikiliza mgonjwa na kumshauri njia salama kulingana na ombi la mama. Hata hivyo njia hii haishauriwi endapo una mpango wa kuwa na watoto wengi zaidi

 

Hatari ya kufanyiwa upasuaji ni nini?

 

Kama ilivyo sawa na upasuaji wa aina nyingine, mama anayefanyiwa upasuaji kwa ajili ya kujifungua huwa kwenye hatari ya matatizo yafuatayo;

 

Kujeruhiwa wakati wa upasuaji

 

Ingawa ni kwa nadra sana nja ni kwa bahati mbaya, mama anaweza kujeruhiwa katika sehemu yoyote ya tumbo, mirija ya mikojo. Mtoto pia anaweza kujeruhiwa, kuna baadhi ya watoto huweza kukatwa ngozi sehemu yoyote ya mwili lakini ni kwa nadra sana nah ii hutegemea uzoefu pia wa daktari.

 

Mtoto kupata matatizo ya upumuaji

 

Watoto wanaozaliwa kwa njia hii hupata kipindi cha mpito cha kupumua haraka haraka kinachodumu kwa siku chache baada ya kujifungua.

 

Hatari zingine ni pamoja na;

 • Mama kupata maambukizi kwenye kuta za kizazi

 • Kutokwa na damu nyingi baada ya upasuaji

 • Kuganda kwa damu ndani ya mishipa ya damu haswa kwenye mishipa ya miguu na viungio ndani ya nyonga. Endapo damu iliyoganda itanyofoka na ksuafiri kwenda kwenye mapafu mgonjwa atapata tatizo la pulmonary embolism.

 • Maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji, hutokea endapo kidonda hakitunzwi vema na kutiwa maji

 • Kupata hatari ya kujifungua kwa upasuaji ujauzito zinazofuata

 • Kutokwa na damu nyingi

 

Hatari za muda mrefu ni

 

Kupata Kovu baya kwenye eneo la mshono

 

Kupata kovu kwenye mwili ambalo litaharibu mwonekano wako- hii hutokea endapo kwenye eneo la mshono wa kidonda pia hutegemea mbinu aliyotumia daktari kushona kidonda chako. Baadhi ya watu wenye tabia ya kuwa na keloid huweza kupata kelod kwenye maeneo haya ya tumbo.

 

Kuchanika kizazi kwenye ujauzito unaofuata

 

Maandalizi ya kufanya kabla ya kujifungua

Endapo utafanyiwa upasuaji, utakuwa umeandaliwa tayari kwa kuzungumza na mtu wa usingizi kisha kusaini conset form ambayo unaweza kuisaini wewe kama unajitambua au ndugu yako wa karibu endapo hujitambui.

Utafanyiwa pia vipimo vya damu ili kuangaliwa wingi wa damu pamoja na kundi la damu yako ili endapo kutatokea shinda baada ya upasuaji uongezewe damu kiurahisi na hata hivyo kuweza kumsaidia daktari wako kupima kipimo cha kuchunguza wingi wa damu siku kadhaa baada ya kujifungua. Endapo hospitali ina upungufu wa damu unaweza kuombwa kuleta ndugu wa kuchangia damu

 

Baada ya upasuaji utatakiwa kupata muda wa kupumzika nyumbani kwa wiki kadhaa ili kupona. Hakikisha unafanya maandalizi mapema kupata mtu wa kuweza kukutunza wiki kabla ya kufanyiwa upasuaji.

 

Kabla ya kufanyiwa upasuaji nini hufanyika?

 

Kabla ya kufanyiwa upasuaji utafanyiwa mambo yafuatayo

 • Utawekewa catheter kwenye mshipa wa damu ili kuongezewa maji kabla au wakati upasuaji uanendelea

 • Utawekewa mpita wa mkojo ili kukusanya mkojo katika kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini

 • Utachomwa sindano ya kaputi kisha kulazwa kwenye kitanda cha upasuaji. Wakati mwingine inaweza ikahitajika kuchomwa sindano ya kaputi ambapo utakuwa hutambui nini kinachoendelea mpaka utakapoamka

 • Utasafishwa tumbo lako katika eneo ambalo litafanyiwa upasuaji kisha

 • Utavalishwa nguo maalumu kwenye eneo ambalo litafanyiwa upasuaji

 • Utafanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto na baada ya mtoto kutoka utapewa mtoto umuone jinsia yake na sura kisha kwenda kusafishwa na nesi wakati daktari akiendelea kufunga sehemu aliyochana kutoa mtoto

 

Baada ya upasuaji kufanyika

 

Baada ya kufanyiwa upasuaji, utakaa kidogo kwa siku chache (kati ya siku 2 hadi 3) kulingana na utakavyoshauriwa na daktari wako. Utashauriwa pia baada ya madhara ya dawa za usingizi kuisha kuanza kufanya mazoezi, kunywa maji ya kutosha pamoja na kula vyakula laini ili kuzuia kupata haja ngumu na kuganda kwa damu mwilini.

Utafundishwa pia namna ya kunyonyesha mtoto mara moja baada ya kurejea kwenye hali yako nzuri baada ya upasuaji.

 

Unapokuwa nyumbani nini cha kufanya?

 

Mara baada ya kufanyiwa upasuaji, utakuwa ukipata maumivu sehemu ya mshono lakini usiwe na hofu unatakiw akufanya mambo yafuatayo

 • Pumzika na weka vitu ambavyo utakuwa unavihitaji karibu nawe ili usipate kazi ya kuvifikia kwa shida. Usinyanyue vitu vizito kutoka kwenye pozi la kuchuchumaa.

 • Tumia dawa za maumivu kama ulivyopewa na daktari wako ili kupunguza maumivu, unaweza kujikanda pia kwa chupa ya maji moto.

 • Usifanye ngono kipindi hiki wakati unasubiria kupona angalau kwa wiki sita toka umefanyiwa upasuaji

 • Usiendweshe gari kwa kipindi hiki chote mpaka upone

 • Usifanye mazoezi mazito pia kwa kipindi cha wiki sita au mpaka utakaposhauriwa na daktari wako ili kuepuka mshono kufumuka

 

Jambo jingine muhimu ni nini?

 

Endapo utaona dalili zifuatazo hakikisha unawasiliana na daktari wako kwa sababu huwa ni dalili za hatari na zinahitaji maamuzi ya dharura;

 • Kubadilika rangi kwa kidonda, kuvimba na kutoa usaha au majimaji yasiyo ya kawaida

 • Kupatwa na homa

 • Kutokwa na damu nyingi ukeni

 • Kuongezeka kwa maumivu ya msono

 • Kutokuwa na furaha, msongo wa mawazo na hisia mbaya dhidi ya mwanao, kutaka kumdhuru mwanao.

 

Endelea kusoma maka hii kupata mabadiliko yanayofanyika kila mara.

Imeboreshwa, 11.01.2020

ULY CLINIC inakukumbusha siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri zaidi na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba kupitia namba za simu au kwa kubonyeza pata tiba chini ya tovuti hii

Rejea za mada hii,

 

 1. Ashley Shepherd etal. The frequency and reasons for vaginal examinations in labour. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/22397830/. Imechukuliwa 10.01.2021

 2. Improving Vaginal Examinations Performed by Midwives. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3749030/. Imechukuliwa 10.01.2021

 3. Frederick C. Freed, M.D. etal. Clinical signs of fetal distress during labor.https://www.ajog.org/article/S0002-9378(15)31746-4/abstract. Imechukuliwa 10.01.2021

 4. Berghella V. Cesarean delivery: Preoperative planning and patient preparation. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 10.01.2021

 5. Nixon N, et al. Anesthesia for cesarean delivery. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 10.01.2021

 6. Berghella V. Cesarean delivery: Surgical technique. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 10.01.2021

 7. Berghella V. Cesarean delivery: Postoperative issues. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 10.01.2021

 8. Labor, delivery, and postpartum care FAQ091. FAQ Postpartum depression. American College of Obstetricians and Gynecologists. https://www.acog.org/Patients/FAQs/Postpartum-Depression. Imechukuliwa 10.01.2021

 9. Labor, delivery, and postpartum care FAQ006. FAQ. Cesarean birth (C-section). The American College of Obstetricians and Gynecologists. https://www.acog.org/Patients/FAQs/Cesarean-Birth-C-Section. Imechukuliwa 10.01.2021

 10. Gabbe SG, et al., eds. Cesarean delivery. In: Obstetrics: Normal and Problem Pregnancies. 7th ed. Philadelphia, Pa.: Elsevier; 2017. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 10.01.2021

 11. Berens P: Physiology, complications, and maternal care. Overview of the postpartum period. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 10.01.2021

kujifungua kwa upasuaji
bottom of page