Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD
Jumatatu, 8 Novemba 2021
Msongo wa kujeruhiwa
PSD- Ni ugonjwa wa akili unaoamshwa na tukio la kuogopesha, kutisha au la hatari. Tukio hili linawezekana limekupata wewe au umeshuhudia likimpata mtu mwingine. Matukio mengi katika maisha yanaweza kusababisha majeraha ya akili na hivyokuleta ugonjwa wa akili.
Watu wengi baada ya kukutana na tukio la kuumiza(kutisha), hupitia kipidi kigumu kwa muda, hata hivyo binadamu wengi huweza kukabiliana na kusahau kuhusu matukio hayo. Endapo dalili zitadumu kwa miezi kadhaa au mwaka na kukfanya ushindwe kutimiza majukumu yako ya kila siku, unaweza kuwa na tatizo la PSD. Utahitaji matibabu makini ili kupunguza dalili na kuimarisha maisha ubora wa maisha yako.
Ni nini husababisha PSD?
Unaweza kupata tatizo la PSD endapo umeshuhudia, patwa au jifunza kuhusu mambo yanayodhuru au kuondoa uhai wa mtu, ajali mbaya au kufanyiwa ukatili wa kimapenzi. Hata hivyo madaktari hawana uhakika kwanini watu wanapata tatizo la PSD. Kama yalivyo magonjwa mengi ya akili, PSD huweza kusababishwa na;
Kipindi cha msongo wa mawazo- ikiwa pamoja na kiwango cha majeraha au mambo mazito umekutana nayo kwenye maisha
Historia ya magonjwa ya akili kwenye familia kama msongo wa mawazo na sononeko kuu
Kurithi utu wa huruka ya kukasilika haraka
Namna mwili wako unavyokabiliana na hali mbalimbali katika maisha
Majeraha gani yanaweza kusababisha tatizo hili?
Kuna aina tofauti za majeraha yanayoweza kupelekea kukumbwa na tatizo hili la PSD, baadhi yake yanayosababisha sana ni;
Kushuhudia mlipuko wa bomu lililoua watu
Ukatili dhidi yako ukiwa mtoto (mlengwa anaweza kuwa si wewe)
Kukatiliwa kimapenzi
Kutekwa/kujeruhiwa mwili
Kutishiwa kuuawa kwa silaha
Ajali(kupata ajali au kushuhudia ajali mbaya)
Kusikia/Kuambiwa unaumwa(au mtu wa karibu yako) ugonjwa unaoogopesha
Kufiwa na mtoto au ndugu wa karibu sana uliyekuwa unamtunza
Kushuhudia ajali za moto, majanga asilia (tetemeko, kimbunga), kukabwa, ajali ya gari n.k
Dalili
Dalili za PDS huweza kuanza ndani ya mwezi mmoja toka tukio la kuogopesha limetoke, hata hivyo baadhi ya dalili zinaweza zisitokee mpaka mwaka(miaka) kadhaa kupita. Dalili hizo husababisha mgonjwa kushindwa kuwa na ushirikiano mzuri kwenye jamii yake, kuacha kufanya kazi za kila siku au kuvunjika kwa mahusiano. Dalili hizo zipo kwenye makundi yaliyoorodheshwa chini;
Kumbukumbu za kujirudia
Hizi zinahusisha;
Kumbukumbu zisizotakiwa za kujirudia kuhusu jeraha lililokupata
Kuona jambo lililokupa jeraha kama vile ndo linatokea tena
Ndoto za kuogopesha au kutisha kuhusu jambo lililokujeruhi
Kusumbuliwa sana na hisia za hali au kimwili dhidi ya kitu kinachokukumbusha kuhusu jambo lililokujeruhi
Kujizuia
Dalili zinaweza kuwa;
Kujizuia kuongelea kuhusu jeraha lililokuumiza
Kujizuia kwenda maeneo au kukutana na watu wanaokukumbusha mambo au tukio lililokuletea jeraha
Mawazo na hali hasi
Dalili huwa pamoja na;
Kuwa na hisia hasi dhidi yako na watu wengine au dunia
Kukata tamaa kuhusu maisha yako ya baadae
Kupata shida ya kumbukumbu, ikiwa pamoja na kushindwa kukumbuka sehemu muhimu ya tukio lililokuumiza
Kupata shida kuwa na mahusiano ya karibu na watu
Kuhisi umetengwa na marafiki au familia
Kutopenda kufanya shughuli ambazo zilikuwa zinakufurahisha ukizifanya
Kushindwa kuwa na hisia chanya
Kupata ganzi ya hisia
Mabadiliko kwenye mwili na mwitikio wa hali
Dalili zinaweza kuwa;
Kuogopeshwa au kushitushwa na kitu au jambo dogo tu
Kuchukua tahadhari mara nyingi kabla ya hatari
Kuona umefika ukingoni wa mambo
Tabia za kujidhuru, kama vile kunywa pombe sana au kuendesha gari kwa kasi n.k
Kukosa usingizi (kushindwa kulala vema)
Kutokuwa makini kwenye jambo moja tu
Kuwa mkali, mwenye hasira au mkorofi
Kujihukumu sana au kujionea aibu
Dalili kwa watoto ni zipi?
Watoto si rahisi kutambua dalili zao haswa walio chini ya miaka sita, pamoja na dalili za hapo juu watoto Zaidi ya miaka sita wanawez akuwa na dalili za;
Kujikojolea kitandani licha ya kujua kutumia choo
Kusahau namna ya kuongealicha ya kujua kuongea
Kuogopa sana mchezo wa kuogopesha wakati wa kucheza
Kumg’ang’ania mzazi kwa nguvu au mtu mwingine mkubwa bila sababu
Ukubwa wa tatizo
Dalili za PSD zinaweza kutofautiana ukubwa jinsi muda unavyowenda. Dalili mara nyingi huwa kali pale unapopata jambo la kukuvuruga akili au unapokutana na vitu vinavyokukumbusha majeraha. Mfano unaweza kusikia kwenye habari kuhusu mtu amebakwa na ghafla ukamezwa na hilo tukio au kusikia mtu aliyekufa kwa ugonjwa Fulani kisha ukamezwa na hilo tukio.
Utambuzi
Namna tatizo linavyotambuliwa
Ili uweze kusemekana kuwa unatatizo la PSD unatakiw akuwa na angalau na dalili idadi kadhaa katika makundi hayo juu;
Angalau dalili moja ya kumbukumbu za kujirudia kwa tukio
Angalau dalili moja ya Kujizuia
Angalau dalili mbili za mabadiliko kwenye mwili na mwitikio wa hali
Angalau dalili mbili za mawazo na hali hasi
Wakati gani wa kumwona daktari wako;
Kama una mawazo yanayokusimbua au hisia kuhusu majeraha uliyopata akilini Zaidi ya mwezi mmoja, au kuwa na dalili kali zinazokufanya ushindwe kuishi maisha yako ya zamani, ongea na daktari wako au daktari wa akili kuhusu afya yako ili uanze matibabu mapema kabla ugonjwa huo haujawa mkali Zaidi.
Endapo una mawazo ya kujiua, pata msaada haraka kwa kufanya yafuatayo;
Nenda kwa rafiki yako wa karibu au mpendwa kisha mwelezee shida yako akusikilize na kukushauri, epuka kukaa mwenyewe
Onana na kiongozi wa maombi au kiroho au mtu wa Imani yako akupe msaada wa kiroho
Panga kuonana na daktari wako
Vihatarishi
Kudumu kwa jeraha kwa muda mrefu
Kuwa na historia ya jeraha jingine mwanzoni mwa maisha yako kama vile kufanyiwa ukatili wakati wa utoto
Kuwa na kazi ambayo inakuweka hatarini kupata jeraha kama vile kufanya kazi jeshini, hospitali-maiti na zimamoto
Kuwa na magonjwa mengine ya kiakili kama vile hofu ilopitiliza(ang’zayati) na sononeko kuu
Kutumia madawa ya kulevya na unywaji wa pombe wa kupindukia n.k
Kutokuwa na msaada kutoka kwa rafiki au familia yako
Kuwa na ndugu wa damu moja mwenye tatizo la akili ikiwa pamoja na ang’zayati au huzuniko
Madhara
Tatizo hili linaweza kuleta madhara kama vile;
Kupoteza kazi
Kuvunjika kwa mahusiano
kushindwa kufurahia maisha yako ya kila siku
kupata magonjwa ya akili kama ang’zayati na sononeko
Kutumia dawa za kulevya na pombe
Maadhaifu ya kula
Mawazo au matendo ya kujidhuru au kujiua
Kinga
Mara baada ya kupata jeraha katika maisha, watu wengi hupata tatizo la PSD mwanzoni pale ambapo wanashindwa kuacha kujizuia mawazo ya kufikiria kuhusu majeraha hayo.
Hofu, kushuku,hasira, sononeko na kujilaumu ni sehemu ya mwitikio wa mwili dhidi ya tukio Fulani lililotokea na hii ni kawaida, hata hivyo endapo vinadumu Zaidi ya mwezi mmoja ni ishara kuwa unahitaji msaada kutoka kwa daktari au daktari wa magonjwa ya akili ili kujizuia kupata tatizo la PSD.
Wakati huu inamaanisha pia, kuwatafuta marafiki wa karibu ambao wanaweza kukusikiliza na kukupa tumaini, kumwona daktari au kurejea kwenye Imani yako na kufanya maombi.
Matibabu
Matibabu makuu kwa wagonjwa wenye madhaifu ya PSD ni dawa na tiba saikolojia(tiba maongezi). Kila mtu yupo tofauti na mwingine, na tatizo la PSD linadhuru watu kwa namna tofauti, hivyo matibabu yatakayofanya kazi kwa mtu A hayatakuwa sawa na mtu B. Baadhi ya wagonjwa wa PSD wanahitaji kujaribu matibabu aina tofauti kabla ya kutambua ni yapi haswa yanawasaidia. Hata hivyo ni vema kupata matibabu kwa daktari mzoefu aliyezoea kukutana na wagonjwa aina hii.
Kama mtu mwenye PSD yupo na kwenye majeraha yanaoendelea kama vile mahusiano mabaya n.k matatizo yake yote yanatakiwa kutatuliwa. Matatizo mengine yanayoendelea ikiwa pamoja na udhaifu wa kupaniki, sononeko kuu, matumizi ya dawa za kulevya au hisia za kujiua zinatakiwa kufanyiwa kazi pia.
Dawa
Dawa zinayotumika na zimefanyiwa tafiti kukabiliana na tatizo hili ni dawa zilizo kwenye kundi la antidepressant, dawa hizi husaidia kudhibiti ishara na dalili za huzuni, woga, hasira na ganzi ya hisia. Dawa aina nyingine zinaweza kukusaidia kudhibiti dalili za kushindwa kupata usingizi na ndoto za kutisha
Daktari atashirikiana nawe kwa pamoja kutafuta dawa nzuri au machanganyiko wa dawa inayofanya kazi vema na kwenye dozi sahihi.
Tiba saikolojia
Wakati mwigine huitwa tiba maongezi, inahusisha kuongea na daktari wa magonjwa ya akili. Inaweza kufanyika kwenye kundi au kati yako wewe na daktari tu. Tiba maongezi ya PSD mara nyingi huchukua wiki 6 hadi 12 kukamilia au inaweza kudumu Zaidi ya muda huo wakati mwingine. Tafiti zinaonyesha kuwa mgonjwa akipata msaada kutoka kwa familia na marafiki huchangia sana kupona haraka.
Aina nyingi za tiba saikolojia zinaweza kumsaidia mgonjwa, nyingi hulenga dalili za PSD, zingine zinalenga jamii, na matatizo ya kazini. Daktari anaweza kuchanganya aina tofauti kulingana na mahitaji ya mtu.
Matibabu yanayofaa hukazia kuhusu vitu muhimu kama, elimu kuhusu dalili, kufundishwa ujuzi wa namna ya kutambua viamsha dalili na namna ya kudhibiti dalili. Aina nyingine ya tiba inayosaidia inahusisha;
Kujiingiza kwenye tukio
Hii husaidia mtu kukabiliana na mashaka yake. Tiba hii hufanyika kwa kumpeleka mgonjwa kwenye tukio kidogodogo mpaka azoee lakini kwa tahadhari. Inaweza kufanyika kwa kutumia picha, kuandika, au kutembelea maeneo ambapo tukio lilitokea. Daktari atatumia nyenzo hizo ili kukusaidia ukabiliane na kuzoea hali hiyo.
Kupitia tukio upya
Hii huwasaidia watu walione jeraha kwa jicho la karibu na kuliumba upya lilete mantiki akilini na kuonekana tofauti na jinsi mgonjwa anavyolifikiria. Hii humfanya mgonjwa aondokane na mawazo hasi na kumfanya aone si kosa lake. Mgonjwa na daktari mtatazama upya tukio kiuhalisia.
Tiba ya maongezi
Namna gani tiba maongezi inasaidia watu kuondokana na tatizo la PSD?
Tiba maongezi inawasaidia watu kufahamu njia muhimu za kukabiliana na matukio ya kuogopesha yanayoamsha PSD. Ikitegemea madhumuni ya tiba, aina tofauti zinaweza;
Kukufundusha kuhusu tukio na madhara yake
Kukufunza kukabiliana na hasira
Kukupa dondoo za kupata usingizi vema, kula vema na kufanya mazoezi
Kukusaidia kutambua na kukabiliana na hisia za kujilaumu, aibu na zingine kuhusu tukio
Kukufanya ubadilike namna gani watu wanaitikia kwenye tatizo la PSD, mfano kukusaidia uweze kukabiliana na vitu vinavyokukumbusha kuhusu jeraha