Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
6 Novemba 2025, 13:24:02

Ugonjwa wa PID
PID (Pelvic Inflammatory Disease) ni ugonjwa unaotokea sana kwa wanawake waliowahi kuathiriwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Asilimia kubwa husababishwa na vimelea vya gonorrhea na chlamydia (wanaosababisha kisonono na pangusa). Ugonjwa huu huweza kubabisha tatizo la kutopata mimba, kati ya wanawake 8 walio ugonjwa huu mwanamke 1 huweza kupata ugumba.
Mara baada ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa na kutotibiwa , vimelea hawa hupanda katika mfulko wa kizazi na hatimaye kufikia katika mirija ya uzazi, wanapokuwa katika mfumo wa kizazi kinga ya mwili huamka kupambana nao. kemikali mbalimbali hutolewa kutokana na mpambano huo na ikiwa ugonjwa umekaa kwa mda mrefu basi kemikali hizi zinazotolewa huharibu kuta za mfuko wa kizazi na kusababisha michomo na mishikamao ya ukuta wa uzazi, mirija ya mayai na viungo vingine vilivyo kwenye uzazi na hivo inasababisha kuwa vigumu kwa mimba kutungwa au kukua katika kuta hizo
Jinsi maambukizi ya PID hupatikana
PID mara nyingi ni matokeo ya kutotibiwa magonjwa ya zinaa kama gonorrhea na chlamydia. Vimelea hivi huingia kupitia njia ya uke na kusafiri hadi kwenye viungo vya uzazi vya ndani.
Sababu zinazoongeza hatari ya PID
Kuambukizwa na kutotibiwa magonjwa ya zinaa.
Kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja.
Kuwa na mpenzi ambaye ana wapenzi wengi.
Historia ya PID hapo awali.
Kujisafisha uke kwa kutumia maji au vidole au sabuni na kemikali kali.
Kutumia njia za uzazi wa mpango zinazowekwa ndani ya kizazi (kama IUD) bila usafi sahihi au uchunguzi kabla ya kuweka.
Dalili za PID
Baadhi ya wanawake hawapati dalili mwanzoni, jambo linalosababisha ugonjwa kuendelea bila kutambuliwa. Hata hivyo, dalili kuu zinazoweza kujitokeza ni:
Maumivu ya tumbo chini ya kitovu.
Homa au kutetemeka mwili (hasa kwa maambukizi mapya).
Uchafu usio wa kawaida kutoka ukeni wenye harufu mbaya.
Maumivu au kutokwa damu wakati wa tendo la ndoa.
Maumivu au hisia za kuungua wakati wa kukojoa.
Kutokwa damu katikati ya mzunguko wa hedhi.
Uchunguzi wa PID
Daktari atafanya tathmini ya historia ya afya, uchunguzi wa mwili, na vipimo mbalimbali kama:
Uchunguzi wa uke na shingo ya kizazi.
Vipimo vya maabara (kuangalia maambukizi ya gonorrhea, chlamydia, au vimelea vingine).
Ultrasound kuangalia uvimbe au usaha kwenye mirija ya uzazi.
Laparoscopi katika kesi sugu au zisizoeleweka.
Matibabu ya PID
PID hutibiwa kwa mchanganyiko wa dawa za antibayotiki, ambazo hutolewa kwa mdomo au kwa sindano kulingana na ukali wa ugonjwa.
Kanuni muhimu za matibabu
Anza matibabu mara moja baada ya utambuzi.
Maliza dozi yote ya dawa, hata kama dalili zimepungua.
Tibu pia mpenzi wako ili kuzuia maambukizi kurudi tena.
Epuka tendo la ndoa hadi daktari athibitishe kuwa maambukizi yameisha.
Kumbuka:Madhara kama makovu na kuziba kwa mirija ya uzazi hayawezi kurekebishwa, hivyo matibabu ya mapema ni muhimu ili kuzuia ugumba.
Madhara ya PID ikiwa haitatibiwa
Kuziba kwa mirija ya uzazi kutokana na makovu.
Mimba kutunga nje ya kizazi.
Ugumba.
Maumivu sugu ya tumbo chini ya kitovu.
Mtungo wa usaha usaha kwenye ovari na mirija ya uzazi hivyo kusababisha uvumbe.
Jinsi ya kupunguza hatari ya kupata PID
Fanya ngono salama kwa kutumia kondomu kila mara.
Epuka ngono zembe au kuwa na wapenzi wengi.
Fanya vipimo vya magonjwa ya zinaa mara kwa mara, hasa ikiwa una mpenzi mpya.
Epuka kujisafisha ndani ya uke kwa maji, vidole, kemikali au sabuni kali.
Tibu mara moja magonjwa ya zinaa unapogundulika.
Hakikisha uchunguzi unafanywa kabla ya kutumia njia ya uzazi wa mpango ya IUD.
Wakati wa kumwona daktari
Muone daktari haraka kama una dalili zifuatazo:
Maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu.
Homa kali au kutetemeka.
Kutokwa na damu isiyo ya kawaida.
Maumivu makali wakati wa tendo la ndoa.
Harufu mbaya kwenye uchafu wa uke.
Hitimisho
PID ni ugonjwa hatari unaoweza kuharibu mfumo wa uzazi wa mwanamke endapo hautatibiwa kwa wakati. Kwa kuwa chanzo kikubwa ni magonjwa ya zinaa, kinga bora ni kuepuka ngono zisizo salama, kupima mara kwa mara, na kutibu maambukizi mapema.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Je, PID inaweza kutokea bila kuwa na magonjwa ya zinaa?
Ndiyo. Ingawa sababu kuu ni magonjwa ya zinaa, maambukizi yanaweza pia kutokea baada ya kujifungua, kutoa mimba, au kufanyiwa upasuaji wa kizazi.
2. Je, PID inaweza kupona kabisa?
Ndiyo, ikiwa itagunduliwa mapema na kutibiwa ipasavyo. Lakini madhara yaliyotokea kama makovu hayawezi kuondolewa.
3. Je, mwanamke mwenye PID anaweza kupata ujauzito tena?
Ndiyo, lakini uwezekano hupungua ikiwa mirija ya uzazi imeziba. Tiba ya mapema huongeza nafasi ya kupata ujauzito.
4. Je, mwanaume anaweza kuambukizwa PID?
Hapana, lakini wanaume wanaweza kuwa wabebaji wa vimelea vinavyosababisha PID kwa wanawake (mfano, chlamydia na gonorrhea).
5. Je, PID inaweza kurudi tena baada ya matibabu?
Ndiyo, ikiwa mpenzi hakutibiwa au kama maambukizi mapya ya zinaa yatatokea.
6. Je, ni salama kushiriki tendo la ndoa wakati wa matibabu?
Hapana. Inashauriwa kusubiri hadi daktari athibitishe kuwa maambukizi yamekwisha kabisa.
7. Je, PID husababisha hedhi isiyo ya kawaida?
Ndiyo, baadhi ya wanawake hupata mzunguko usio wa kawaida kutokana na mabadiliko ya homoni na uchomezi wa viungo vya uzazi.
8. Je, PID inaweza kutibiwa kwa dawa za mitishamba?
Hapana. Hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha tiba ya mitishamba kwa PID. Tiba pekee ni kupitia dawa za hospitali.
9. Je, kuna chanjo ya kuzuia PID?
Hakuna chanjo maalum ya PID, lakini chanjo dhidi ya HPV na hepatitis B husaidia kupunguza hatari za baadhi ya maambukizi yanayohusiana na afya ya uzazi.
10. Je, PID inaweza kuzuia kwa kutumia kondomu pekee?
Kondomu hupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa, lakini si asilimia 100. Kuepuka wapenzi wengi na kupima afya ya ngono mara kwa mara kunasaidia zaidi.
