top of page

Imeandikwa na daktari wa ULY CLINIC

Maziwa ya mama

Maziwa ya mama yameonekana kuwa chanzo kizuri cha lishe kwa mtoto, wanasayansi wamekuwa wakiendelea kujifunza kuhusu mchanganyiko huo wa maziwa ya mama ili kuweza kutengeneza maziwa yanayofanana na mchanganyiko huo.

Kemikali za nukliotaidi zilizo kwenye  maziwa ya mama na baadhi ya maziwa ya fomula, zimeonekana kufanya  kazi kubwa katika kuimarisha mfumo wa kinga za mwili uitwao hyumoro baada ya kupewa chanjo. Mama mwenye maambukizi ya VVU hashauriwi kumnonyesha mtoto

 

Kunyonyesha inasemekana kuwa ni njia moja kubwa kumlisha mtoto aliyetimiza umri, hii ndio sababu wazalishaji wa maziwa wanaendelea kujifunza kutengeneza maziwa yanayotaka kufanana mchanganyiko wa maziwa ya mama.

Tazama katika jedwali chini ya makala hii kuangalia vilivyomo kati ya maziwa ya mama na maziwa ya fomula.

Maziwa ya mama huwa na umuhimu katika ukuaji wa ubongo wa mtoto na kukomaza mfumo wa tumbo ili mtoto asipate magonjwa ya kuharisha, hii ni kutokana na mchanganyiko wake wa viini ambavyo havipo kwenye maziwa ya fomula.

Namna ya kuhifadhi maziwa ya mama

 

Endapo unanyonyesha na unataka kwenda kazini lakini pia unahitaji mwanao anyone maziwa yako, unaweza kuhifadhi maziwa yako na akapewa baadae mwanao wakati wewe haupo. Fuata ushauri ulioandikwa hapa chini mara utakapofikiria kukamua na kuhifadhi maziwa yako

 

Maziwa ya mama yaliyokamuliwa yanatakiwa kuhifadhiwa kwenye chombo gani?

Kabla ya kukamua maziwa, hakikisha umenawa mikono kwa maji safi na sabuni, kausha mikono yako kwa kitambaa safi kisha anza kukamua ziwa moja baada ya jingine. Unaweza kutumia mashine ya kukamulia maziwa inayopatikana madukani, lakini endapo huna tumia mikono yako safi.

 

Wakati unakamua, hakikisha unakamulia maziwa katika kikombe kisafi chenye mfuniko, kinaweza kuwa cha plastiki (isiwe plastiki ya chupa za maji ya kunywa au soda au plastiki iliyotengenezwa kwa kemikali ya bisphenol A (BPA)) au cha glasi na iwe na kiwe na uwezo wa kufunikwa. Unaweza kutumia mifuko maalumu ya plastiki iliyotengenezwa huhusani kwa ajili ya kuhifadhia maziwa.

 

Unatakiwa uyahifadhi wapi baada ya kukamua?

 

Mara unapomaliza kukamua maziwa yako, hakikisha unabandika lebo kwenye chupa ya maziwa yenye  tarehe na muda ulipokamua maziwa hayo, hii itakusaidia kutumia maziwa yaliyokamuliwa zamani kwanza na kuacha mapya ili yasiharibike. Endapo mtoto anatunzwa hospitali ambayo watoto wanalishwa na nesi, hakikisha unaandika jina la mwanao kwenye chupa. Hifadhi maziwa yaliyokamuliwa kwenye fridge au mtungi wa maji baridi ambapo yatapata ubaridi. Unaweza kutumia pia boksi maalumu zenye barafu kuhifadhia maziwa hayo kwa muda.

Hakikisha unajaza maziwa kwa kiwango ambacho mtoto atakunywa na kukimaliza, usizidishe ili kuepuka kubakisha maziwa. Jaza kwa mfano chupa yenye mililita 60 hadi 120, au chupa yenye mililita 30 hadi 60 kwa ajili ya hali za dharura mfano mtoto atakaposhindwa kumaliza maziwa hayo. Usijaze maziwa mpaka kwenye mdomo wa kikombe unapotaka kuhifadhi kwa sababu maziwa ya mama huwa na tabia ya kutanuka yakipata ubaridi.

Ni kwa muda gani maziwa yaliyokamuliwa yanatakiwa kukaa bila kutumika?

 

Jibu la swali hili linategemea mazingira ya maziwa hayo;

  • Maziwa yaliyohifadhiwa kwenye joto la mazingira- yanaweza kudumu kwa masaa sita tu kabla ya kutumia, endapo chumba kina joto sana hakikisha unahifadhi maziwa hayo kwenye ubaridi mfano mtungi wa maji baridi au jokofu

  • Kwenye boksi lenye barafu-yanaweza kudumu kwa siku moja/masaa 24

  • Jokofu- sehemu yenye ubaridi kiasi, maziwa yanaweza kuishi mpaka siku tano. Unashauriwa hata hivyo kuyatumia ndani ya siku tatu

  • Jokofu- kwenye sehemu inayotengeneza barafu, maziwa yanaweza kuishi mpaka miezi 12. Unashauriwa hata hivyo kuyatumia ndani ya miezi sita.

Kumbuka maziwa yanapokaa muda mrefu yanapoteza vitamin C, hata hivyo maziwa ya mama hubadilika kulingana na mahitaji ya mtoto, mfano maziwa ya mama wakati mtoto anamwezi mmoja hayafanani na akiwa na miezi 6, hivyo si vema kukamua na kuyaacha maziwa kwa muda mrefu kabla ya kuyatumia.

 

Unayeyusha vipi maziwa yaliyohifadhiwa kwenye jokofu?

Anza kwa kuyeyusha maziwa yaliyokaa muda mrefu kwanza, hakikisha unatoa maziwa kutoka kwenye shemu ya barafu na kuyaweka kwenye sehemu ya jokofu isiyo na barafu usiku kabla ya kuyatumia. Tumia maji tiririka yenye uvuguvugu kumwagia chupa ya maji, au tumbukiza chupa ya maziwa iliyofunikwa katika maji ya uvuguvugu ili yapashike. Usipashe kwa kutumia moto wa moja kwa moja kwa sababu utaharibu kinga za mwili (antibody) zilizo kwenye maziwa hayo.

 

Ladha ya maziwa na rangi zinaweza kuwa tofauti na rangi ya mwanzoni, hata hivyo ni salama kuyatumia endapo umeyahifadhi vema

Baadhi ya tafiti zinasema maziwa ya mama ambayo yameyeyusha, endapo yakibaki ni vema ukayatuma, inamaanisha kuwa usihifadhi tena mara baada kuyatoa kwenye friji.

ULY CLINIC inakukumbusha siku zote utafute ushauri kutoka kwa daktari wako kabla ya kuchukua hatua zozote zile za kiafya 

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri zaidi na tiba kupitia namba za simu au kwa kubonyeza pata tiba chini ya tovuti hii

Imeboreshw amara ya mwisho 16.08.2020

Rejea za mada hii,

  1. Your guide to breastfeeding. Office on Women's Health. Office on Women's Health. https://www.womenshealth.gov/patient-materials/resource/guides. Imechukuliwa 16.08.2020

  2. Pumping and storing breastmilk. Office on Women's Health. https://www.womenshealth.gov/breastfeeding/pumping-and-storing-breastmilk. Imechukuliwa 16.08.2020

  3. Gleason CA, et al., eds. Breastfeeding. In: Avery's Diseases of the Newborn. 10th ed. Elsevier; 2018. https://www.clinicalkey.com. Imechukuliwa 16.08.2020

  4. Eglash A, et al. ABM clinical protocol #8: Human milk storage information for home use for full-term infants, revised 2017. Breastfeeding Medicine. 2017; doi:10.1089/bfm.2017.29047.aje.

  5. Steel C. Best practices for handling and administration of expressed human milk and donor human milk for hospitalized preterm infants. Frontiers in Nutrition. 2018; doi:10.3389/fnut.2018.00076.

bottom of page