Imeandikwa na Daktari wa ULY CLINIC
Jumapili, 19 Aprili 2020
Korodani (testis)
Korodani ni jozi ya tezi mbili zinazo zalisha shahawa, manii na homoni ya testosterone, tezi hii huitwa tezi ya jinsia au Gonadsi.
Tezi hii hupatikana ndani ya kimfuko kinachoitwa pumbu chini ya shina la uume. Kwa wastani ukubwa korodani moja ya mtu mzima ni urefu wa sentimita 5, upana wa sentimita 2 na unene was sentimita 3. Uzito wa korodani kama hii ni Kati ya gramu 10 hadi 15.
Kila korodani imezungukwa na matabaka matatu ambayo ni tunika vaginalisi, tunika albujenia na tunika vaskulosa.
Korodani huning'inia ndani ya pumbu kana kwamba zipo nje ya mwili ili kurekebisha joto kwa uzalishaji sahihi wa mbegu za kiume.
Uzalishaji huu unahitaji joto ambalo ni pungufu kidogo ya joto la mwili kwa nyuzijoto 3. Hii ni kumaanisha kwamba korodani uzalisha shahawa kwa usahihi katika joto la wastani wa nyuzijoto 35 wakati wastani wa joto la mwili ni nyuzijoto 37.5.
Joto kali sana ama dogo sana huweza kudhuru uzalishaji wa mbegu za kiume.
Katika mazingira ya joto kali pumbu hulegea na korodani huning'inia chini zaidi ili kushusha joto la korodani. Katika mazingira ya baridi pumbu husinyaa kupandisha korodani karibu na mwili ili kuzipatia joto.
Ni hali ya kawaida korodani moja kuning'inia chini zaidi kuliko korodani nyingine kwa sababu ya utofati wa urefu wa mishipa inayoning'iniza kila korodani.
Wakati mtoto anaumbiaka tumboni, uumbaji wa korodani hutokea ndani ya fumbatio karibu na figo. Kadri mtoto anavyokua tumboni , korodani hushuka kuelekea chini ya tumbo na mwezi wa nane wa ujauzito zinakua zimeshafika kwenye pumbu.
Kazi za korodani ni zipi?
Korodani huwa na kazi kuu mbili ambazo ni;
• Kuzalisha mbegu za kiume
• Kuzalisha homoni ya kiume 'testosterone'
Baadada ya kubalehe manii moja hutengenezwa kwa wastani wa siku 65 hadi 70 na zaidi ya shahawa milioni 100 hutengenezwa kila siku tangia kubarehe hadi uzeeni. Hii nitofauti na kwa wanawake ambapo kwao kila mwezi yai moja hukomaa kuanzia anapopevuka hadi anopokoma kuana hedhi hivyo wastani wa mayai 385 hukomaa katika maisha ya mwanamke.
Utengenezaji wa shahawa hufanyika katika mirija ya seminiferasi iliyopo ndani ya korodani. Kuta za mirija hii zina seli mama ambazo hukomaa na kuwa shahawa. Kukomaa kwa seli hizi huanzia ukuta wa nje ambao umeundwa na seli changa zaidi kuelekea ukuta wa ndani ambao umeundwa na seli zilizizo komaa Zaidi. Seli zilizokomaa Zaidi hubadilika kuwa manii na kuhifadhiwa kwa miezi kadhaa katika mirija ya epedidimisi.
Wakati wa msisimko wa kujamiana misuli ya mirija ya epididimisi husukuma shahawa na kutolewa katika uume kupitia njia ya mkojo.
Kama shahawa zitabaki kwa mda mrefu zikiwa zimehifadhiwa, mwili huzifyonza kama virutubisho.
Korodani pia imeundwa na seli maalumu ziitwazo seli za setoli ambazo hutunza shahawa zinazotengenezwa kwa kuzipa oksijeni na virutuisho vingine na kulinda mbegu mpya zisishambuliwe na mfumo wa kinga wa mwili.
Kazi ya homoni testosterone
Testosteroni ni homoni ya kiume inayotengenzwa kwenye korodani na seli maalamu ziitwazo seli za leidigi. Testosteroni ina kazi zifuatazo:-
• Kumfanya mwanaume awe na tabia za kiume na hisia za tendo la kujamiana.
• Kuleta mabadiliko ya kiume pindi mvulana anapo balehe mfano kuota ndevu,sauti nzito, uume kukua, kutanuka kifua.
• Kusababisha uumbaji sahihi wa viungo vya uzazi wa mwanaume mtoto akiwa tumboni kabla ya kuzaliwa.
• Kuwezesha utengenezaji wa mbegu za kiume.
• Kuwezesha ukuajia wa misuli mikubwa na mifupa ya mwanaume.
Soma Zaidi kuhusu homoni ya testosterone kwa wanaume na wanawake kwenye sehemu nyingine ya tovuti hii
Dosari na magonjwa ya korodani
Busha (haidrosili)- Ni mkusanyiko wa kimiminika kinachofana na maji katikati ya tabaka la tunika vajinalisi. Pumbu huonekana kubwa na kuvimba lakini Korodani huwa haijadhurika. Hali hii hutibika kwa upasuaji.
Kutoshuka kwa korodani kwenye pumbu (Kriptochidizimu)- Ni dosari ya kuzaliwa nayo, hutokana na korodani kukwama njiani katika safari ya kushuka kutoka tumboni kuelekea kwenye pumbu wakati mtoto akiwa tumboni mwa mama. Hii hugundulika mtoto akiwa mdogo katika mwaka wa kwanza kwani korodani moja tu hupatikana kwa kupapasa pumbu.
Tatizo hili huongeza kwa kiasi kikubwa cha hatari ya saratani ya korodani na ugumba kwa mtoto. Tatizo hili hutibika kwa upasuaji kabla mtoto haja balehe.
Maambukizi ya korodani (Ochaitizi)- Hufuata baada ya maambukizi ya bakteria kwenye njia ya mkojo kama vile ugonjwa wa zinaa wa kisonono. Maambukizi huambatana na maumivu makali, uvimbe na pumbu kua nyekundu. Ugonjwa huu hutibika kwa dawa za antibakteria.
Maambukizi ya mirija ya epididimisi(epididimaitizi)- Ni maambukizi ya bakteria katika mirija ya kuhifadhia shahawa iliyopo juu ya korodani . Maambukizi huambatana na maumivu makali ya korodani upande mmoja au pande zote. Ugonjwa huu hutibika kwa dawa za antibayotiki
Kutanuka kwa mirija ya damu ya vena za korodani- Mara nyingi huusisha korodani ya upande wa kushoto. Maumivu huwa makali na huzidi wakati wa kusimama. Nafuu hupatikana kwa kujaribu kuinua korodani kwa msaada wa kifaa maalumu. Matibabu yanaweza yakahusisha au yasihusishe upasuaji.
Kujisokota kwa mishipa ya korodani(Testikula Tosheni)- Ni tatizo la kawaida kwa vijana wanao balehe. Mara nyingi hutokea nyakati za asubuhi. Maumivu huwa makali na korodani kuwa ngumu. Huweza kutibika bila upasuaji. Ni muhimu kutibu haraka kabla ya masaa sita kwani seli za korodani huweza kufa kwa kukosa damu.
Uvimbe wa korodani- Huweza kuwa uvimbe wa kawaida au saratani.
Majeraha ya korodani-Hutokana na ajali mbalimbali. Huweza kusababisha ugumba.
Kuzaliwa bila korodani
Kuzaliwa bila korodani ni udhaifu wa kiuumbaji wa viungo vya mwili, tatizo hili endapo limehusisha korodani zote mbili, hupelekea kupata utasa.
Soma makala hii zaidi kwenye makala ya 'kuzaliwa bila korodani'
Wasiliana na daktari wako endapo umeona kuwa una dalili yoyote ile katika maelezo haya kwa ushauri na tiba
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa ushauri na tiba zaidi kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii au kubonyeza hapa.
Imeboreshwa,
13 Julai 2021 18:57:42
Rejea za mada hii;