Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Sospeter B, MD, Dkt. Adolf S, MD
16 Februari 2026, 12:11:29

Chumvi na presha ya kupanda
Matumizi ya muda mrefu ya chakula chenye chumvi nyingi husababisha ugonjwa wa presha ya kupanda. Watu zaidi ya milioni 7 hufa kwa ugonjwa huu kila mwaka duniani, walionusurika kifo hupata kiharusi na magonjwa mbalimbali ya moyo. Usiache kutumia chumvi, tumia kwa kiwango kinachoshauriwa kiafya.
Shinikizo la juu la damu ni nini?
Shinikizo la juu la damu hufahamika kwa jina jingine la presha ya kupanda hutokea pale endapo shinikizo la sistoliki litazidi mililita za mekyuli 140 na lile la dayastoliki kuzisi mililita za mekyuli 90.
Katika Afrika inakadiliwa kuwa kati ya watu wazima 100, 31 huwa na shinikizo la juu la damu, wakati huo kuna zaidi ya watu 50 kati ya 100 wenye shinikizo la juu la damu katika mataifa ya watu wenye rangi nyeupe.
Tafiti zinaonyesha pia, asilimia 40 ya watu wenye shinikizo la juu la damu huwa hawafahamu kuwa wanapo mpaka pale wanapogundulika wanapokuwa wameenda kwa ajili ya matibabu ya magonjwa mengine au kufanya kipomo cha shinikizo la damu.
Je ni kweli presha ya kupanda husababishwa na chumvi?
NDIO!
Matumizi ya chakula chenye chumvi nyingi ni kihatarishi kikuu cha kupata shinikizo la juu la damu, hii imethibitishwa na tafiti mbalimbali pamoja na majaribio ya kisayansi yaliyofanyika kwa binadamu na wanyama.
Chumvi nyingi huambatana na kudhuru mfumo wa renin-angiotensin unaofanya kazi ya kurekebisha shinikizo la damu. Mfumo huu unapofanya kazi huamrisha shinikizo la damu lipande au kupungua kuendana na mahitaji ya mwili. Mfano unapokuwa unakimbia, mfumo huu huongeza shinikizo la damu ili kurahisisha usambazaji wa virutubisho muhimu pamoja na oksijeni kwenye chembe mbalimbali za mwili. Hata hivyo endapo umelala, umfumo huu hupunguza shinikizo la damu kwa kuwa mwili wakati huu hauhitaji mzunguko mkubwa wa damu.
Kiasi gani cha chumvi kinashauriwa kwa mgonjwa mwenye presha kwa siku?
Mbali na kushauriwa punguza uzito kwa wenye obeziti au uzito mkubwa kupita kiasi ( uwiano wa uzito kwa urefu zaidi ya kilo 25 kwa kila skwea mita), kula mlo sahihi pamoja na kufanya mazoezi, watu wenye shinikizo la juu la damu wanatakiwa kudhibiti kiwango cha chumvi wanachotumia kwa siku mpaka gramu zisizozidi 1.5 katika masaa 24
Kiasi gani cha chumvi kinashauriwa kutumia kwa siku?
Kwa siku inashauriwa kutotumia zaidi ya gramu 2 za chumvi kwa wa watu wenye rangi nyeusi, wenye umri wa kati na wazee, watu wenye shinikizo la juu la damu, kisukari au magonjwa sugu ya figo. Mbali na hili, inashauriwa kupunguza kiasi cha pombe na kuongeza utumiaji wa vyakula vyenye madini potasiamu kwa wingi.
Vyakula vyenye chumvi kwa wingi
Chumvi inayozungumziwa kusababisha shinikizo la juu la damu ni ile aina ya sodiam ambayo hupatikana kwenye vyakula mbalimbali pia hutumiwa kama kiungo cha chakula majumbani. Chumvi aina ya sodiamu hutumika kuhifadhi chakula kisiharibike na hivyo huweza kupatikana kwenye vyakula vingi vya kusindikwa vinavyouzwa madukani. Mfano wa vyakula ambavyo vinahifadhiwa kwa chumvi ni;
Mfano wa vyakula vyenye chumvi nyingi;
Nyama choma iliyotiwa chumvi
Soseji
Samaki waliochomwa na kutiwa chumvi
Nyama iliyohifadhiwa kwa kutiwa chumvi
Vyakula vya kwenye kopo
Karanga zenye chumvi
Maharagwe ya kopo yaliyotiwa chumvi
Tabia ambazo zinafanya ule chumvi nyingi ni;
Kuongezea chumvi kwenye chakula unachokula mezani
Kula mayai kwa kuchovya kwenye chumvi
Kula matunda kwa kupaka chumvi
Kula mahindi ya kuchoma au chemshwa yaliyopakwa chumvi
Kula bisibisi na vyakula vinavyofanana na hivyo kutoka supermarket
Kula chakula katika migahawa au hoteli zisizozingatia kiasi cha chumvi ya kiafya
Vyakula vyenye madini potasiamu kwa wingi
Vyakula vyenye madini potasiamu kwa wingi hufanya kazi kinyume na vile vyenye madini ya sodiamu kwa wingi. Matumizi ya mara kwa mara ya vyakula vyenye potasiamu kwa watu wenye shinikizo la juu la damu na wasio na shinikizo husaidia kushusha shinikizo la damu.
Vyakula vyenye madini potasiamu kwa wingi ni pamoja na;
Ndizi
Machungwa
Zabibu
Matunda ya kukaushswa kama tende, zabibu
Spinachi
Viazi vitamu
Viazi mviringo
Brokoli
Uyoga
Tango
Mbaazi
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Kwa nini baadhi ya watu hupata presha kirahisi zaidi kuliko wengine?
Kiwango cha mtu kuathiriwa na chumvi hutofautiana kutokana na vinasaba, uzito kupita kiasi, umri mkubwa, matumizi ya pombe, msongo wa mawazo, na shughuli ndogo za mwili. Baadhi ya watu wana mfumo wa mwili unaoitwa mwili wa mwitikio mkali kwenye chumvi, ambao huchochea kupanda kwa shinikizo la damu kwa haraka wanapotumia chumvi nyingi.
2. Je, mtu asiye na dalili anaweza kuwa na shinikizo la juu la damu?
Ndiyo. Shinikizo la juu mara nyingi huitwa “muuaji wa kimya kimya”, kwa sababu watu wengi hawana dalili kwa miaka mingi. Zaidi ya asilimia 40 ya wagonjwa hawajui kama wanashinikizo la juu la damu mpaka wanapogundulika hospitalini kwa bahati tu. Ndiyo maana kipimo cha mara kwa mara ni muhimu.
3. Je, kupunguza chumvi peke yake kunaweza kushusha presha?
Kwa watu wengi, kupunguza chumvi huleta matokeo makubwa. Tafiti zinaonyesha kuwa kupunguza ulaji wa chumvi mpaka gramu1.5–2 kwa siku kunaweza kushusha shinikizo la damu kwa kiasi kikubwa, hasa kwa watu wazee, wenye kisukari na wenye uzito mkubwa.
4. Je, chumvi yenye iodini ni hatari kama chumvi nyingine?
Kikemikali, chumvi yenye iodini bado ina sodium, hivyo ikiwa inatumiwa kupita kiasi inaweza kuongeza presha ya damu. Tofauti kuu ni kwamba inaongezewa iodini inayolinda dhidi ya ugonjwa wa goita, lakini haina madhara tofauti kuhusu shinikizo la damu.
5. Je, kuondoa chumvi kabisa ni salama?
Hapana. Mwili unahitaji kiasi kidogo cha chumvi kufanya kazi muhimu kama mzunguko wa damu, kazi za mishipa ya fahamu na usawa wa maji. Lengo si kuacha kabisa, bali kutumia kiasi kinachoshauriwa ( gramu 1.5 hadi 2 kwa siku) kulingana na hali ya afya.
6. Je, mazoezi yanaweza kupunguza madhara ya kula chumvi nyingi?
Mazoezi husaidia kupunguza presha kwa kuboresha mzunguko wa damu, kupunguza uzito na kuongeza uwezo wa moyo. Hata hivyo, hayafuti madhara ya kutumia chumvi kupita kiasi. Mazoezi na kupunguza chumvi vinapaswa kufanyika pamoja.
7. Kwa nini watu wa Afrika au wenye ngozi nyeusi wanashauriwa kula chumvi kidogo zaidi?
Utafiti unaonyesha kuwa watu wa asili ya Kiafrika huwa na mwitikio mkali zaidi kwenye sodium, hivyo presha yao ya damu hupanda haraka wanapotumia chumvi. Hii ndiyo sababu wanashauriwa kutotumia zaidi ya gramu 2 kwa siku ili kupunguza hatari ya kiharusi na magonjwa ya moyo.
8. Je, dawa za presha zinaweza kufanya mtu ale chumvi bila madhara?
Hapana. Dawa za presha hazifuti athari za chumvi nyingi. Kuendelea kula chumvi kupita kiasi huku ukitumia dawa kunaweza kufanya dawa zisifanye kazi vizuri, na kuongeza hatari ya kiharusi, ugonjwa wa figo na moyo.
9. Ni dalili gani za kula chumvi nyingi?
Ingawa wengi hawapati dalili dhahiri, baadhi huweza kupata:
Kuongezeka kwa kiu
Miguu au uso kuvimba
Maumivu ya kichwa
Mapigo ya moyo kwenda kasi
Shinikizo la damu kupanda ghafla
Dalili hizi hupungua unapopunguza ulaji wa chumvi kwa muda mfupi.
10. Ni mara ngapi mtu anapaswa kupima shinikizo la damu?
Kwa mtu mzima asiye na historia ya presha, inapendekezwa kupima angalau mara moja kila miezi 3–6. Watu wenye uzito mkubwa, kisukari, historia ya familia au wanaotumia chumvi nyingi wanapaswa kupima kila mwezi. Wenye presha tayari wanapaswa kupima kila wiki au mara kadhaa kwa mwezi kama daktari anavyoshauri.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeandikwa:
15 Agosti 2021, 13:11:47
Rejea za mada hii:
1. High-Salt Diet and Hypertension: Focus on the Renin-Angiotensin System. I. Drenjančević-Perić, et al. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC3214830/. Imechukuliwa 15.08.2021
2. William Kofi Bosu, et al. Hypertension in older adults in Africa: A systematic review and meta-analysis. https://journals.plos.org/plosone/article?id=10.1371/journal.pone.0214934. Imechukuliwa 15.08.2021
3. Adeloye D, et al. Estimating the prevalence and awareness rates of hypertension in Africa: a systematic analysis. PLoS One. 2014;9(8):e104300. pmid:25090232
4. Ataklte F, et al.. Burden of undiagnosed hypertension in Sub-Saharan Africa: A systematic review and meta-analysis. Hypertension. 2015;65(2):291–8. pmid:25385758
5. Sarki AM, et al. Prevalence of Hypertension in Low-and Middle-Income Countries: A Systematic Review and Meta-Analysis. Medicine. 2015;94(50):e1959. pmid:26683910
6. Addo J, et al. The changing patterns of hypertension in Ghana: a study of four rural communities in the Ga district. Ethn Dis. 2006;16:894–99. pmid:17061743
7. Awuah RB, et al. Prevalence, awareness, treatment and control of hypertension in urban poor communities in Accra, Ghana. J Hypertens. 2014;32(6):1203–10. pmid:24721931
8. Samson Okello, et al. Hypertension prevalence, awareness, treatment, and control and predicted 10-year CVD risk: a cross-sectional study of seven communities in East and West Africa (SevenCEWA). https://bmcpublichealth.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12889-020-09829-5. Imechukuliwa 15.08.2021
9. Patient education. Guidelines for a Low Sodiumhttps://www.ucsfhealth.org/education/guidelines-for-a-low-sodium-diet. Imechukuliwa 15.08.2021
10. Potassium rich foods. https://www.webmd.com/diet/foods-rich-in-potassium. Imechukuliwa 15.08.2021
