Mwandishi:
Dkt. Salome A, MD
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Jumapili, 22 Septemba 2024
Madhara ya kutoa mimba
Utoaji mimba katika makala hii inamaanisha mimba iliyotoka kwa kupanga, inaweza kuwa kwa njia ya dawa au upasuaji kupitia mlango wa uzazi.
Kiujumla, utoaji mimba wa kupanga unaonekana kutosababisha sana na madhara kwenye mimba zinazofuata. Hata hivyo tafiti zinaonyesha kuwa kuna mahusiano kati ya kutoa mimba na kupata mtoto njiti au kujifungua kabla ya umri ujauzito kutimia kwa mimba itakayofuata baada ya kutoa mimba.
Kihatarishi cha kupata madhara hutegemea njia ya utoaji mimba iliyotumika, kati ya dawa au njia ya upasuaji. NJia hizi hutumika kulingana na umri wa mimba na aina ya mgonjwa.
Njia ya dawa
Njia hii hutumika kutoa mimba kwa ujauzito wenye umri mdogo kabisa(ndani ya miezi mitatu ya kwanza). Njia hii inaonekana kutoongeza hatari ya kupata madhara kwenye ujauzito unaofuata.
Dawa zinazoweza kutumika ni pamoja na;
Methotrexate
Hutumika kwa kusimamisha uumbaji wa kijusi na hivyo mtoto kutoendelea kutofanyika tumboni. Dawa hii hutumika kwenye mimba yenye umri chini ya wiki 7
Misoprostol na mifepristone
Dawa hizi hutumika kwa ujauzito ulio chiniya wiki 11, hata hivyo si kila daktari anauwezo wa kukuandikia dawa hii. Utapata dawa hii kwa kuandikiwa cheti na daktari wako.
Dawa za kienyeji
Baadhi ya watu hutumia dawa za kienyeji au mitishamba, dawa hizi huwa hazina kipimo maalumu hivyo ULY CLINIC haishauri mtu kutumia njia hii kwa sababu wagonjwa wengi wanaotumia dawa hii, huja hospitali wakiwa wameishiwa damu kwa sababu ya kutokwa na damu nyingi. Hata hivyo zipo aina nyingi za dawa za kienyeji zinazoweza kutumika kutoa mimba, usitumie dawa hizi isipokuwa umeshauriwa na daktari wako.
Njia ya upasuaji
Njia hii hutumika kutoa mimba zilizo na umri mkubwa zaidi(miezi mitatu ya pili na kuendelea). Upasuaji mdogo hufanyika kutoa mimba kupitia tundu la uzazi. Daktari atatumia kifaa maalumu kukipitisha ukeni ili kumtoa mtoto pamoja na pampu maalumu ya kuvuta damu na tishu za mtoto kutoka kwenye kizazi. Aina hii ya utoaji mimba kwa mara chache sana inaweza kusababisha makovu ndani ya kizazi na kuleta sindromu ya asharman. Sindromu ya asharman huweza kumfanya mwanamke akashindwa kupata mimba hapo mbeleni.
Wanawake wanaotumia njia hii mara kwa mara hupata hatari zaidi ya kuchanika kizazi na kupasuka kwa shingo ya uzazi.
Njia ya upasuaji huweza kuwa za aina tofauti ikitegemea umri wa mimba;
Mimba iliyofikisha umri wa wiki 16
Ujauzito huu unaweza kutolewa kirahisi kwa kuvuta na kifaa kinachoitwa vacuum aspirator.
Ujauzito wenye umri zaidi ya wiki 14
Njia ya kutanua na kukwangua uzazi hutumika. Njia hii hutumia vifaa vyenye kipenyo tofauti ili kutanua tundu la shingo ya uzazi hivyo kuruhusu kijiko maalumu kupita na kuingia kwenye mfuko wa uzazi ili kukwangua na kuondoa kondo la nyuma pamoja na kichanga. Kwa wanawake waliotokwa mimba bila kupanga(miscariage), njia hii pia hutumika kusafisha kizazi kwa kutoa kondo la nyuma linalobaki kwenye kizazi.
Ujauzito wenye umri zaidi ya wiki 24
Ujauzito huu huweza kutolewa kwa njia iliyosemwa hapo juu lakini kabla ya hapo dawa hutumia kwa ajli ya kuanzisha uchungu na baada ya kujifungua dakatari atatumia njia ya hapo juu kusafisha kizazi na kuondoa kondo la nyuma.
Kwa vile katika umri huu kichanga huwa amefanyika na anaweza ishi, sheria nyingi za nchi mbalimbali haziruhusu kutoa mimba kwenye umri huu.
Sheria za Tanzania haziruhusu kutoa mimba katika umri wowote ule, hata hivyo kuna baadhi ya matatizo ambayo kitiba yanaweza kuruhusu utoaji mimba ili kumwokoa mama.
Kama umetoa mimba na unahisi una hatari ya kutoka kwa mimba yako inayofuata, ongea na daktari wako kwa ushauri zaidi kulingana na hali yako. Daktari atakushauri zaidi namna ya kufanya ili kuepuka madhara na kupata ujauzito weneye matokeo mazuri.
Baadhi ya madhara ya utoaji mimba ni pamoja na;
Kutokwa na damu
Haya ni madhara ya njia yoyote ile ya utoaji mimba, mwanamke anaweza kupoteza damu zaidi na kupata tatizo la upungufu wa damu. Upungufu wa damu unaweza kutokea endapo mwanamke ametokwa na damu nyingi zaidi ya siku tatu kwa wanaotokwa damu kidogo, lakini zaidi ya masaa 24 kwa anayetokwa na damu nyingi.
Dalili zingine za upungufu wa damu huweza kutokea. Bonyeza hapa kuzisoma.
Endapo unatokwa na damu mwendelezo ufanye nini?
Wasiliana na daktari wako haraka ili kufanya mpango wa kupimwa kiwango cha damu na kuongezewa damu. Mbali na hivyo, daktari atatafuta ni nini kinasababisha damu isikatike, utafanyiwa uchunguzi na kusafishwa kizazi pia ili kuondoa kondo la nyuma(endapo sababu ndo hiyo) linalobaki kwenye kizazi na kusababisha damu iendelee kutoka.
Mimba kubaki kwenye kizazi
Baadhi ya mimba zinazotolewa, tishu za kondo la nyuma na sehemu ya mwili wa kichanga unaweza kubaki tumboni, hii inaweza kupelekea damu kuendelea kutoka na hivyo kuleta upungufu wa damu. Endapo umetumia dawa au umetumia njia ya upasuaji na damu nyekundu au mabonge yanaendelea kutoka kidogodogo baada ya siku 3 mwone daktari wako haraka. Na endapo damu inatoka nyingi zaidi ya masaa 48, onana na daktari wako pia ili akuchunguze kama kuna tishu za mtoto zimebaki kwenye kizazi na kukusafisha.
Maambukizi kwenye uzazi na uke
Kwa sababu njia za kutoa mimba hufungua shingo ya kizazi na kuiacha wazi kwa masaa kadhaa, maambukizi yanaweza kupita kutoka ukeni na kuingia kwenye kizazi. Maambukizi haya yanaweza kuambatana na maumivu makali ya tumbo la chini, kutokwa na damu au majimaji yanayonuka ukeni, homa, na dalili zingine. Onana na daktari endapo umeona dalili hizi au zingine ambazo hazieleweki.
Kutobolewa kwa kizazi na ogani zingine ndani ya nyonga
Kwa bahati mbaya na mara chache, daktari anweza kutoboa kizazi endapo hana uzoefu na zoezi hili la kutoa mimba, endapo uzazi utatobolewa mama anaweza kupata dalili za maumivu makali ya tumbo la chini na baadae huweza sambaa tumbo lote, homa, kuzimia au kupoteza maisha n.k
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi
Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.
Imeboreshwa,
22 Septemba 2024 08:36:43
Rejea za mada hii:
1. Steinauer J, et al. Overview of pregnancy termination. https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 04.07.2020
2. Cedars MI. Intrauterine adhesions. https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 04.07.2020
3. Harwood B, et al. First trimester medication abortion (termination of pregnancy). https://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 04.07.2020
4. Frequently asked questions. Special procedures FAQ043. Induced abortion. American College of Obstetricians and Gynecologists. http://www.acog.org/Patients/FAQs/Induced-Abortion. Imechukuliwa 04.07.2020
5. Induced abortion in the United States [Fact sheet]). guttmacher.org/fact-sheet/induced-abortion-united-states. Imechukuliwa 04.07.2020
6. Infertility FAQs.cdc.gov/reproductivehealth/infertility/index.htm. Imechukuliwa 04.07.2020
7. Jatlaoui TC, et al. (2018). Abortion surveillance — United States 2020.cdc.gov/mmwr/volumes/67/ss/ss6713a1.htm. Imechukuliwa 04.07.2020