top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Jumamosi, 31 Julai 2021

Matiti makubwa kwa kichanga

Matiti makubwa kwa kichanga

Asilimia 70 ya watoto wanaozaliwa na matiti makubwa husabaishwa na kiwango kikubwa cha homon estrogen kutoka kwa mama wakati wa ujauzito. Chunga kile unachokula au kunywa kwa kuwa baadhi ya vyakula huchangia ongezeko la estrogen.


Kwanini kichanga anazaliwa na matiti makubwa?


Kichanga kuzaliwa na matiti makubwa au kukua mara baada ya kuzaliwa husababishwa na madhara ya homoni estrogen kutoka kwa mama kwa asilimia 70 ya watoto walio tumboni.


Estrogen hufanya kazi ya kukuza matiti ya mama mjamzito ili yajiandae na uzalishaji wa maziwa kabla ya kujifungua.


Kiasi cha homoni estrogen huingia kwa mtoto kupitia kitovu hivyo kupelekea kuchochewa kwa ukuaji wa matiti yake kabla au wakati mfupi baada ya kuzaliwa na mara nyingi matiti hufikia sentimita 1 hadi 2 au zaidi.


Visababishi vingine vya kukua kwa matiti havifahamiki lakini baadhi ya vihatarishi ni matumizi ya baadhi ya dawa kama dawa za ARV, dawa za uzazi wa mpango, matumizi ya pombe, msongo wa mawazo wakati wa ujauzito na ulaji mbovu wa mama. Vihatarishi vingi vilivyotajwa hapa husababisha ongezeko la homoni estrogen inayomfikia mtoto akiwa amezaliwa au akiwa tumboni.


Sifa za chuchu iliyokuwa kutokana na homoni nyingi za estrogen;

  • Huwa gumu na linalouma likibinywa au kushikwa

  • Huwa kubwa kuanzia sentimita 1, 2 au zaidi

  • Huweza kutoa maziwa

  • Maziwa haya ya mtoto hufanana na maziwa ya mama kwa kuwa huwa na antibodi za IgA, IgG, laktoferrin, lizozaimu na laktoalbumin


Madhaya matiti kwa kichanga


Kutokana na kutokuwa na mirija ya kutosha, maziwa yanaweza kukusanyika na kutengeneza kifuko cha maziwa na kuonekana kwa nje kama uvimbe.


Madhara mengine ni kufanyika kwa usaha na maambukizi ya titi


Magonjwa mengine yanayoweza kusababisha kuota kwa matiti ya kwa kichanga


Mbali na ukuaji wa kawaida wa kifiziolojia kutokana na homoni nyingi ya estrogen, matiti ya kichanga kuonekana makubwa kutokana na;


  • Kufanyika kwa vifuko maziwa kwenye titi

  • Ukuaji wa kasi wa mtoto

  • Usaha kwenye titi

  • Uvimbe wa michomo kinga kwenye matiti

  • Maambukizi kwenye matiti


Maambukizi ya titi hutokea sana kwa viachanga wenye jinsia ya kike waliotimiza siku zao wiki la tatu hadi nne la ujauzito lakini mara nyingi huhusisha titi moja la upande wowote ule. Kisababishi kikuu kilifahamika kuwa maambukizi ya bakteria jamii ya Staphylococcus kwa asilimia 60. Madhara yake maranyingi hupelekea kufanyika kwa usaha ndani ya titi unaohitaji kutolewa kwa kuvutwa na sindano au kufanyiwa upasuaji pamoja na kupewa dawa kwa njia ya mishipa


Ushauri kwa mama na mlezi mwenye mtoto aliye na matiti makubwa


Kukua kwa matiti ya kichanga kutokana na kuwa na homoni estrogen kwa wingi hakupaswi kukupa hofu, unatakiwa kuwa mvumilivu mpaka pale matiti au titi la mtoto litakaposinyaa pia kwa kusikiliza ushauri wa mtaalamu wa afya kwa matibabu atayokupatia.


Watoto wenye matiti makubwa kutokana na homoni huwa hawapewi matibabu au dawa yoyote kwani hali hii huisha yenyewe wiki chache baada ya kuzaliwa.


Wakati gani titi la kichanga husinyaa?


Mara nyingi matiti ya kichanga husinyaa wiki moja au mbili baada ya kuzaliwa kutokana na kupungua kiwango cha homon estrogeni, baadhi ya watoto huchukua takribani miezi sita kabla ya kupotea. Wakati kiwango cha estrogeni kinapungua kwenye damu ya mama na mtoto, kiwango cha homoni prolactin kwa mtoto huongezeka na hivyo kupelekea matiti kuzalisha maziwa baada ya kuzaliwa.


Dalili ya uzalishaji wa maziwa inaweza kupotea wiki moja hadi mbili baada ya kuzaliwa. Mambo usiyotakiwa kufanya ni kukamua maziwa ya mtoto, hii ni hatari kwa husababisha ongezeko la muda wa maziwa kuzalishwa na kuongeza hatari ya kupata maambukizi kwenye titi.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma vidokezo hivi

Wasiliana na daktari wa ULY CLINIC kwa elimu na ushauri zaidi kupitia namba za simu au kubonyeza 'Pata Tiba' Chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

7 Februari 2022 17:43:41

Rejea za mada hii:

1. Amer A, et al. Neonatal breast enlargement. N Engl J Med. 2009; 360: 1445

2. Brett A, et al. Neonatal mastitis: 12 years of experience [Article in Portuguese]. Acta Med Port. 2012; 25: 207-12.

3. Devidayal. A male infant with gynecomastia-galactorrhea. J Pediatr. 2005; 147: 712

4. Forbes TR. Witch's milk and witch's marks. Yale J Biol Med. 1950; 22: 219 - 225

5. Jayasinghe Y, et al. Establishment of normative data for the amount of breast tissue present in healthy children up to two years of age. J Pediatr Adolesc Gynecol. 2010; 23: 305-11

6. Madlon-Kay DJ. Witch’s milk: Galactorrhea in the newborn. Am J Dis Child. 1986; 140: 252-3

7. McKiernan JF, et al. Prolactin, maternal oestrogens, and breast development in the newborn. Arch Dis Child. 1981; 56: 770-4

8. Rudoy RC, et al. Breast abscess during the neonatal period. A review. Am J Dis Child. 1975; 129: 1031 - 1034

9. Ruwaili NA, et al. Neonatal mastitis - controversies in management. J Clin Neonatol. 2012; 1: 207-10

10. Stricker T, et al. Mastitis in early infancy. Acta Paediatr. 2005; 94: 166-9

11. V Raveenthiran. Neonatal Mastauxe (Breast Enlargement of the Newborn). https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC4422278/. Imechukuliwa 29.07.2021

12. Yap PL, Mirtle CL, Harvie A, McClelland DB. Milk protein concentrations in neonatal milk (witch's milk). Clin Exp Immunol. 1980; 39: 695-7

bottom of page