top of page

Mwandishi:

Dkt. Sima A, CO

Mhariri:

Dkt. Benjamin M, MD

Imeboreshwa;

8 Machi 2026, 08:13:08

Kipimo cha glukosi

Kipimo cha glukosi hutumika kutambua kiwango cha sukari ya glucose kwenye damu. Mgonjwa mwenye dalili ya kupoteza fahamu, kukojoa mara kwa mara, kiu ya mara kwa mara na njaa ya mara kwa mara atafanyiwa kipimo hiki kutambua kama dalili hizo zinahusiana na sukari na pia kuchunguza ufanisi wa matibabu anayopata mgonjwa wa kisukari n.k


Vipimo cha glucose vipo vya aina mbili

Kipimo cha glukosi baada ya kula: Sampuli huchukuliwa muda wowote bila kujali mtu alikula nini muda uliopita. Majibu ya kipimo hiki yanapaswa kuwa chini ya milimole 11.1 kwa kila lita moja ya damu. Endapo yatazidi zaidi kiwango hiki itasemekeana kuwa una kiwango cha sukari kilichozidi kiwango cha kawaida


Kipimo cha glukosi kwenye mfungo: Sampuli huchukuliwa asubuhi kabla ya kula chochote au angalau masaa 8 kabla ya bila kula chochote. Majibu ya kawaida yanapaswa kuwa kati ya milimole 5.6 hadi 6.9 kwa kila lita moja ya damu. Kama majibu yatakuwa zaidi ya milimole 7.0 kwa kila lita moja ya damu, utasemekana kuwa na kiwango cha sukari kilicho zaidi ya kiwango cha kawaida


Kipimo hiki ni nini?

Glukosi ni aina ya sukari yenye kazi ya kuipa nishati mwili ili uweze kufanya kazi zake hata hii ya kusoma makala hii. Unaweza kupata glukosi kutoka kwenye matokeo ya mmeng’enyo wa wanga uliokula mfano ugali, wali, na vyakula vingine. Kiwango cha glukosi kwenye damu huathiriwa na magonjwa au tabia ya ulaji wa mtu.


Umuhimu wa kipimo cha glukosi

Kipimo cha glukosi ni kipimo muhimu sana katika uchunguzi wa afya kwa sababu husaidia madaktari kufahamu hali ya kiwango cha sukari kwenye damu ya mgonjwa. Kupitia kipimo hiki, daktari anaweza kugundua mapema matatizo yanayohusiana na sukari na kuchukua hatua za matibabu kwa wakati. Umuhimu wa kipimo cha glukosi ni pamoja na yafuatayo:

Umuhimu wa Kipimo

Maelezo

Kutambua ugonjwa wa kisukari

Kipimo cha glukosi husaidia kugundua kama mtu ana kisukari (diabetes) au la kwa kupima kiwango cha sukari kwenye damu. Ugonjwa huu ukigunduliwa mapema unaweza kudhibitiwa vizuri kabla haujasababisha madhara makubwa.

Kugundua hatari ya kupata kisukari

Kipimo hiki kinaweza kuonyesha kama mtu yuko katika hatari ya kupata kisukari hata kabla ugonjwa haujaanza rasmi. Hii humsaidia mgonjwa kufanya mabadiliko ya maisha mapema.

Kufuatilia maendeleo ya matibabu

Kwa wagonjwa wa kisukari, kipimo cha glukosi husaidia kufuatilia kama dawa, lishe na mazoezi wanayofuata vinafanya kazi vizuri kudhibiti sukari kwenye damu.

Kutambua kiwango cha chini cha sukari

Kipimo hiki husaidia kugundua hali ambapo kiwango cha sukari kwenye damu kimeshuka sana, hali ambayo inaweza kusababisha kizunguzungu, jasho jingi au hata kupoteza fahamu.

Kuchunguza dalili zinazohusiana na sukari

Watu wenye dalili kama kukojoa mara kwa mara, kiu kali, njaa ya mara kwa mara, uchovu au kupoteza uzito bila sababu wanaweza kufanyiwa kipimo hiki ili kubaini kama dalili hizo zinatokana na kiwango kisicho cha kawaida cha sukari.

Kuzuia madhara ya muda mrefu ya kisukari

Kupima sukari mara kwa mara husaidia kudhibiti ugonjwa mapema na hivyo kupunguza hatari ya madhara kama magonjwa ya moyo, figo, macho na mishipa ya fahamu.

Kufuatilia afya ya wanawake wajawazito

Wanawake wajawazito wanaweza kufanyiwa kipimo cha glukosi ili kugundua kisukari cha ujauzito ambacho kinaweza kuathiri afya ya mama na mtoto.


Kwa ujumla, kipimo cha glukosi ni muhimu sana katika kulinda afya ya mtu na kugundua mapema matatizo ya sukari kwenye damu, hivyo inashauriwa watu kufanya kipimo hiki mara kwa mara hasa wale walio katika hatari ya kupata kisukari.


Mgonjwa gani anapaswa kufanya kipimo hiki?

Malengo ya kufanya kipimo cha glukosi ni;

  • Kipimo huagizwa kama daktari anataka kufahamu kiwango cha glukosi au mgonjwa yeye mwenyewe kutaka kufahamu kiwango chake cha sukari glukosi kwenye damu

  • Kutambua maradhi ndani ya mwili kama kisukari n.k

  • Kutambua sababu ya mgonjwa kupoteza fahamu, kuishiwa nguvu, kukojoa sana, kiu sana na njaa iliyopitiliza inatokana na nini

  • Kupima madhara ya matibabu kwa mgonjwa aliyekuwa na upungufu wa sukari mwilini. Daktari ataagiza kipimo hiki kufahamu kama kiwango cha sukari yako kimerejea kawaida, kimepanda na kama kimeshuka.


Aina ya sampuli inayotakiwa

Sampuli inayochukuliwa ni sampuli ya damu kutoka kwenye kidole au mishipa mkubwa wa damu. Sampuli kutoka mshipa mkubwa wa damu inaweza kuhifadhiwa kwenye tube ya vakyumu kwa ajili ya kufanyiwa kipimo baadae.


Namna ya kukusanya sampuli

Sampuli ya damu huchukuliwa kwa kuchoma sindano ndogo kwenye kwenye kidole haswa cha pete au kidole cha tatu. Damu hiyo huwekwa kwenye ulimi wa kipimo uliochomekwa kwenye kifaa cha glucometer. Majibu ya kipimo hiki husomeka hapo hapo.


Sampuli inayokusanywa kutoka kwenye mshipa mkubwa wa damu ili kuhifadhiwa kwa kufanya kipimo baadaye huhifadhiwa kwenye chupa yenye citrate au chupa ya glucomedics ambayo ina NaF/KOx, citrate, na EDTA zinazofanya kazi kuzuia uvunjwaji wa sukari wakati damu imehifadhiwa. Kiasi cha damu kinachoweza kukusanywa kwa ajili ya kipimo hiki ni kati ya mililita 3 hadi 5


Kwa wanawake

Kwa wanawake. Hakuna utofauti wa kuchukua sampuli kati ya mwanamke na mwanamme. Sampuli inayochukuliwa ni ya aina moja.


Kwa wanaume

Kwa wanaume . Hakuna utofauti wa kuchukua sampuli kati ya mwanamme na mwanamke. Sampuli inayochukuliwa ni ya aina moja.


Ukusanyaji wa sampuli kwa njia zingine

Sampuli zingine zinazoweza kutumika kupima kiwango cha sukari ni;

  • Damu ya kitovu cha mtoto

  • Maji ya uti wa mgongo

  • Mkojo


Utunzaji wa sampuli

Sampuli kutoka kwenye kidole haihitaji kutunzwa, bali hutumika hapo hapo. Sampuli inayokusanywa kutoka kwenye mshipa mkubwa wa damu ili kuhifadhiwa kwa kufanya kipimo baadaye huhifadhiwa kwenye chupa yenye citrate au chupa ya glucomedics ambayo ina NaF/KOx, citrate, na EDTA zinazofanya kazi kuzuia uvunjwaji wa sukari wakati damu imehifadhiwa.


Muda wa sampuli kuwa hai

Sampuli inayohifadhiwa kwenye tyubu maalumu yenye citrate tu au yenye NaF/KOx, citrate na EDTA zinazofanya kazi kuzuia utengenezaji wa sukari wakati damu imehifadhiwa hutakiwa tumika ndani ya masaa 4 ili kuzuia kupungua kwa kiwango cha sukari kutokana na kuvunjwa na vimeng'enya.


Muda wa kupata majibu ya kipimo chako

Majibu yanaweza kupatikana ndani ya dakika 5 hadi masaa 24 toka umechukuliwa sampuli, hii pia hutegemea aina ya maabara na wingi wa sampuli zinazopimwa.


Usomaji wa majbu

Kipimo cha glukosi kwenye damu hutumika kupima kiwango cha sukari kilichopo kwenye damu. Kipimo hiki ni muhimu katika utambuzi wa ugonjwa wa kisukari aina ya II, kufuatilia wagonjwa wa kisukari na kutambua hali ya sukari kuwa juu au chini ya kiwango cha kawaida.


Vipimo vya glukosi vinaweza kufanyika kwa njia mbalimbali kama:

  • Kipimo cha glukosi kwenye mfungo

  • Kipimo cha glukosi baada ya kula

  • Kipimo cha glukosi wakati wowote


Matokeo ya vipimo hivi husaidia daktari kutathmini kama kiwango cha sukari kiko kawaida, juu au chini ya kiwango kinachotakiwa.



1. Kipimo cha Glukosi baada ya kula

Kipimo hiki hufanyika takribani saa 2 baada ya kula chakula. Husaidia kuona jinsi mwili unavyoweza kudhibiti kiwango cha sukari baada ya kupata chakula.


Jedwali: Tafsiri ya Majibu ya Glukosi Baada ya Kula

Kiwango cha Sukari

Tafsiri ya Matokeo

Chini ya 11.1 mmol/L (chini ya 200 mg/dL)

Kiwango cha kawaida

11.1 mmol/L au zaidi (≥200 mg/dL)

Kinaweza kuashiria kisukari

Ikiwa kiwango cha sukari kinaendelea kuwa juu katika vipimo vinavyorudiwa, daktari anaweza kufanya vipimo vingine kuthibitisha kisukari.


2. Kipimo cha Glukosi kwenye Mfungo

Kipimo hiki hufanyika baada ya kutokula kwa angalau saa 8 hadi 12. Hii ni mojawapo ya vipimo muhimu zaidi katika utambuzi wa kisukari.


Jedwali: Tafsiri ya Majibu ya Glukosi kwenye Mfungo

Kiwango cha Sukari

Tafsiri

Chini ya 5.6 mmol/L (chini ya 100 mg/dL)

Kiwango cha kawaida

5.6 – 6.9 mmol/L (100 – 125 mg/dL)

Hatari ya kisukari (Prediabetes)

≥ 7.0 mmol/L (≥126 mg/dL)

Kisukari kinaweza kuwepo

Kwa kawaida kipimo hurudiwa mara nyingine ili kuthibitisha matokeo kabla ya kufanya utambuzi rasmi wa kisukari.


Majibu Chanya

Majibu chanya ni pale kiwango cha sukari kinapokuwa nje ya kiwango cha kawaida, yaani:

  • sukari kuwa juu sana (haipaglaisemia)

  • au sukari kuwa chini sana (haipoglaisemia)

Hali hizi zinaweza kuashiria magonjwa au matatizo mbalimbali ya kiafya.


1. Sukari kuwa juu ya kiwango (Haipaglaisemia)

Sukari kuwa juu ya kiwango inaweza kuashiria kisukari au matatizo ya udhibiti wa sukari mwilini.


Viwango vinavyoweza kuashiria kisukari

Kipimo

Kiwango

Sukari kwenye mfungo

≥126 mg/dL (≥7.0 mmol/L)

Sukari baada ya kula

≥200 mg/dL (≥11.1 mmol/L)

2. Sukari kuwa chini ya Kiwango (Haipoglaisemia)

Kiwango cha sukari kinachochukuliwa kuwa chini ni:

Kipimo

Kiwango

Sukari chini ya kawaida

<3.0 mmol/L (chini ya takribani 54 mg/dL)


Majibu Hasi

Majibu hasi ni pale kiwango cha sukari kwenye damu kiko ndani ya kiwango cha kawaida.


Jedwali: Viwango vya kawaida vya Sukari

Aina ya Kipimo

Kiwango cha kawaida

Sukari kwenye mfungo

70–100 mg/dL (chini ya 5.5 mmol/L)

Sukari baada ya kula

≤200 mg/dL (≤11.1 mmol/L)


Viwango vya kawaida vya sukari kwa wazee

Kadiri umri unavyoongezeka, viwango vya sukari vinaweza kuwa na tofauti kidogo.


Jedwali: Sukari ya kawaida kwa umri

Umri

Kiwango cha kawaida

Miaka 60–90

82–115 mg/dL (4.6–6.4 mmol/L)

Zaidi ya miaka 90

75–121 mg/dL (4.2–6.7 mmol/L)


Bei ya Kipimo cha Glukosi

Bei ya kipimo cha glukosi inaweza kutofautiana kulingana na hospitali, maabara, aina ya kipimo kinachofanywa na eneo la kituo cha afya. Kwa kawaida kipimo hiki si ghali sana na hupatikana katika hospitali nyingi, vituo vya afya na maabara binafsi.

Kwa wastani katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, bei ya kipimo cha glukosi huwa kama ifuatavyo:

Aina ya Kipimo cha glukosi

Bei ya makadirio

Kipimo cha sukari kwenye mfungo

TSh 5,000 – 15,000

Kipimo cha sukari baada ya kula

TSh 5,000 – 15,000

Kipimo cha sukari wakati wowote

TSh 5,000 – 10,000

Kipimo cha HbA1c (wastani wa sukari miezi 2–3)

TSh 25,000 – 60,000


Mambo yanayoathiri bei ya kipimo

Bei ya kipimo cha glukosi inaweza kubadilika kulingana na mambo yafuatayo:

  • Aina ya maabara au hospitali (serikali au binafsi)

  • Teknolojia au mashine zinazotumika kupima

  • Eneo la hospitali au mji

  • Aina ya kipimo kinachofanywa

Kwa mfano, hospitali za serikali mara nyingi huwa na gharama nafuu zaidi kuliko maabara binafsi.


Ushauri wa msingi kwa mgonjwa

Unahitaji fanya maandalizi yeyote kabla ya kipimo?


Hapana huhitaji fanya maandalizi yoyote kabla ya kupima ,unatakiwa kula na kunywa kama kawaida isipokuwa endapo utafanyiwa vipimo vingine au umeambiwa usile chochote haswa kwa kipimo cha glukosi kwenye mfungo


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake kuhusu kipimo cha glukosi

1. Kipimo cha sukari kwenye damu ni nini?

Kipimo cha sukari kwenye damu ni uchunguzi wa kitabibu unaofanywa kupima kiwango cha glukosi (sukari) kilichopo kwenye damu. Sukari ni chanzo muhimu cha nishati kwa mwili, lakini ikiwa ipo nyingi au kidogo kupita kiasi inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama kisukari  au upungufu wa sukari kwenye damu.


Vipimo hivi husaidia madaktari kutambua mapema matatizo ya sukari, kufuatilia wagonjwa wenye kisukari, na kuhakikisha kiwango cha sukari kinadhibitiwa vizuri.

2. Kwa nini kipimo cha sukari kwenye damu hufanyika?

Kipimo cha sukari hufanyika kwa sababu kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na:

  • Kutambua kama mtu ana kisukari

  • Kugundua hatari ya kupata kisukari

  • Kufuatilia wagonjwa wenye kisukari

  • Kutambua kiwango cha chini cha sukari kwenye damu

  • Kupima mwitikio wa mwili kwa matibabu ya kisukari


Madaktari pia hupendekeza kipimo hiki kwa watu wenye dalili kama kiu kali, kukojoa mara kwa mara, uchovu, au kupungua uzito bila sababu.

3. Ni aina gani za vipimo vya sukari kwenye damu?

Kuna aina kadhaa za vipimo vya sukari vinavyotumika hospitalini au maabara:

1. Kipimo cha sukari kwenye mfungo-Hufanywa baada ya mtu kutokula kwa saa 8–12.

2. Kipimo cha sukari baada ya kula- Hufanywa saa 2 baada ya kula chakula.

3. Kipimo cha HbA1c-Hupima wastani wa kiwango cha sukari kwenye damu katika kipindi cha miezi 2–3.

4. Kipimo cha sukari wakati wowote- Hufanywa wakati wowote bila kujali mtu amekula au hajala.

4. Kiwango cha kawaida cha sukari kwenye damu ni kipi?

Viwango vya kawaida vya sukari hutegemea aina ya kipimo kilichofanywa.

Kwa ujumla:

  • Sukari kwenye mfungo: 70 – 100 mg/dL (chini ya 5.6 mmol/L)

  • Baada ya kula: chini ya 200 mg/dL (chini ya 11.1 mmol/L)

Kiwango kikizidi mipaka hii kinaweza kuashiria hatua za awali za kisukari au kisukari.

5. Dalili gani zinaweza kuashiria kuwa na sukari nyingi kwenye damu?

Mtu mwenye sukari nyingi kwenye damu anaweza kupata dalili zifuatazo:

  • Kiu kupita kiasi

  • Kukojoa mara kwa mara

  • Uchovu mkubwa

  • Kupungua uzito bila sababu

  • Maono kuwa hafifu

  • Vidonda kupona polepole

Dalili hizi zikionekana ni muhimu kufanya kipimo cha sukari mapema.

6. Ni dalili gani za sukari kuwa chini sana kwenye damu?

Sukari ikiwa chini sana (haipoglaisemia) inaweza kusababisha dalili kama:

  • Kutetemeka

  • Jasho jingi

  • Kizunguzungu

  • Njaa kali

  • Kuchanganyikiwa

  • Mapigo ya moyo kwenda haraka

Ikiwa hali hii ni kali inaweza kusababisha kupoteza fahamu, hivyo matibabu ya haraka yanahitajika.

7. Ni nani anapaswa kufanya kipimo cha sukari mara kwa mara?

Makundi yafuatayo yanashauriwa kufanya kipimo cha sukari mara kwa mara:

  • Watu wenye uzito mkubwa

  • Wenye historia ya kisukari katika familia

  • Watu wenye shinikizo la damu

  • Wanawake waliowahi kupata kisukari wakati wa ujauzito

  • Watu wenye umri zaidi ya miaka 45

Uchunguzi wa mara kwa mara husaidia kugundua ugonjwa mapema.

8. Je, ninahitaji kufunga kabla ya kipimo cha sukari?

Inategemea aina ya kipimo.

  • Kipimo cha sukari wakati wa mfungo : lazima ufungue kwa saa 8–12 bila kula

  • Kipimo cha sukari wakati wowote : huhitaji kufunga

  • Kipimo cha sukari baada ya kula: hufanywa saa 2 baada ya kula

Ni muhimu kufuata maelekezo ya daktari au maabara kabla ya kufanya kipimo.

9. Nifanye nini kama matokeo ya kipimo cha sukari yako ni ya juu?

Ikiwa matokeo yanaonyesha kiwango cha sukari kiko juu ya kawaida, daktari anaweza:

  • Kupendekeza vipimo zaidi kuthibitisha kisukari

  • Kushauri mabadiliko ya lishe

  • Kupendekeza mazoezi ya mwili

  • Kutoa dawa za kudhibiti sukari

Kudhibiti mapema husaidia kuzuia madhara makubwa kama magonjwa ya moyo, figo, macho na mishipa ya fahamu.

10. Ninawezaje kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu?

Kudhibiti sukari kunahitaji mabadiliko ya maisha kama:

  • Kula chakula chenye afya na nyuzinyuzi nyingi

  • Kupunguza sukari na vyakula vya wanga mwingi

  • Kufanya mazoezi mara kwa mara

  • Kupunguza uzito uliopitiliza

  • Kufuatilia kiwango cha sukari mara kwa mara

Kwa wagonjwa wa kisukari, kufuata ushauri wa daktari na kutumia dawa kama ulivyoelekezwa ni muhimu sana.


ULY clinic inakushauri siku zote ufanye mawasiliano na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyte ile ya kiafya.

ULY clinic inakushauri siku zote ufanye mawasiliano na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyte ile ya kiafya.

Imeandikwa,

3 Septemba 2021, 11:51:10

Rejea za mada hii

  1. 1. Mayoclinic. Diabetes.https://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/diabetes/diagnosis-treatment/drc-20371451. Imechukuliwa 19/08/2021

  2. CDC. Blood Glucose. https://www.cdc.gov/diabetes/basics/getting-tested.html. Imechukuliwa 19/9/2021

  3. NCBI. Blood Glucose. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK555976/. Imechukuliwa 19/08/2021

  4. PubMed. What is normal blood glucose?. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/26369574/. Imechukuliwa 19/08/2021

  5. Diabetes. Blood Glucose. https://www.diabetes.co.uk/diabetes_care/blood-sugar-level-ranges.html. Imechukuliwa 19/08/2021

  6. Goce Dimeski, et al. What is the most suitable blood collection tube for glucose estimation?. https://pubmed.ncbi.nlm.nih.gov/25002707/. Imechukuliwa 02.09.2021

  7. Blood Sugar Converter. https://www.diabetes.co.uk/blood-sugar-converter.html. Imechukuliwa 02.09.2021

bottom of page