top of page

Mwandishi:

Dkt. Salome A, MD

Mhariri:

Dkt. Benjamin, MD

18 Januari 2022 09:53:10

Image-empty-state.png

Kisukari kwa mjamzito

Kisukari ni ugonjwa sugu usiombukiza unaosababishwa na kuathirika kwa mfumo unaohusika na uchakatwaji na utumiaji ya sukari yaani glukosi katika mwili kutokana na kushindwa kuzalishwa au kufanya kazi kwa homoni ya insulin.


Kuna aina tatu za kisukari kwa mjamzito ambazo ni kisukari aina ya kwanza, kisukari aina ya pili na kisukari cha ujauzito. Katika makala hii tutaongelea kuhusu kisukari ambacho mwanamke hupata kabla ya ujauzito yaani kisukari aina ya kwanza au kisukari aina ya pili (kusoma zaidi kuhusu kisukari cha ujauzito na kisukari kwa ujumla bofya hapa.


Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye kisukari ulimwenguni wakiwamo wanawake walio katika umri wa kubeba mimba, kisukari kimekuwa miongoni mwa magonjwa ambayo hujitokeza sana wakati wa ujauzito. Pia ongezeko la wajawazito wanaopata kisukari cha mimba huwaweka wanawake wengi katika hatari ya kupata kisukari baada ya ujauzito.


Kisukari ni ugonjwa ambao una madhara mengi kwa mama na mtoto wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua, hata matibabu yake huwa na changamoto wakati wa ujauzito kwasababu ya kuzalishwa kwa homoni zinazo ongeza uhitaji wa insulin kadri mimba inavyokua nakusababisha kiwango cha sukari kuwa juu hivyo kuongeza hatari ya madhara kwa mama na mtoto.


Ili kuwa na matokeo mazuri ya ujauzito mwanamke mwenye kisukari anatakiwa kuonana na daktari na wataalaamu wengine wa afya wanaohusika katika matibabu ya kisukari kabla ya kubeba ujauzito na kipindi chote cha ujauzito.


Madhara ya kisukari kwa mjamzito


Yafuatayo ni madhara na athari mbali mbali za kisukari zinazoweza kutokea kwa mama na mtoto


Madhara ya kisukari kwa mama

Madhara ya kisukari kwa mjamzito hutokea wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua, baada ya kujifungua na wakati wa kunyonyesha kama ifuatavyo.


Wakati wa ujauzito


  • Kuharibu mimba

  • Kuwa na maji mengi ya amniotiki

  • Kuwa katika hatari ya kuwa na maambukizi

  • Kupata uchungu kabla ya wakati

  • Kupata shiniko la juu la damu la ujauzito (pre-eclampsia)

  • Kuongezeka kwa hatari ya kupata athari za kisukari kama vile kuharibika kwa figo, macho nk.


Wakati wa kujifungua


  • Kuwa na uchungu uliopitiliza

  • Kuwa na uchungu pingamizi

  • Kujifungua kwa upasuaji

  • Kuchanika kutokana na mtoto kuwa mkubwa

  • Kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua


Baada ya kujifungua


  • Kuwa katika hatari ya kupata maambukizi kama vile UTI

  • Kukosa maziwa


Madhara ya kisukari kwa mtoto

Madhara ya kisukari kwa mtoto huweza kutokea kabla hajazaliwa, baada ya kuzaliwa na hata ukubwani kama ifuatavyo.


Akiwa tumboni


Kuwa na kasoro za kimaumbile katika mfumo wa fahamu, mfumo wa moyo na mishipa ya damu, mfumo wa mifupa, mfumo wa uzazi na mkojo na kasoro nyinginezo;


  • Kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi

  • Kudumaa tumboni endapo figo za mama zimeathiriwa na kisukari

  • Kufia tumboni


Akiwa kichanga


  • Majeraha ya kuumia wakati wa kuzaliwa (birth injuries)

  • Kuzaliwa njiti

  • Matatizo ya upumuaji

  • Kushuka kwa sukari

  • Kuwa na manjano

  • Ugonjwa wa ongezeko la seli nyekundu za damu (polythycemia)

  • Upungufu wa madini ya kalsiamu

  • Upungufu wa madini ya magniziamu


Ukubwani


  • Kuwa katika hatari ya kupata kisukari

  • Kuwa katika hatari ya kupata obeziti


Matibabu kwa mjamzito mwenye kisukari


Matibabu hutolewa kwa ushirikiano wa wataalamu mbali mbali wa afya wa ambao ni; mtaalamu wa uzazi na mgonjwa ya wanawake, mtaalamu wa magonjwa ya ndani, mtaalamu wa magonjwa ya watoto, mtaalamu wa lishe, wauguzi na madaktari.


Ili kuwa na matokeo mazuri ya ujauzito mwanamke mwenye kisukari anapaswa kuwa katika uangalizi mzuri kuhakikisha sukari yake inakuwa katika kiwango kinachotakiwa kabla ya kubeba ujauzito na baada ya kujifungua.


Matibabu kabla ya kubeba ujauzito

Kabla ya kubeba ujauzito mwanamke mwenye kisukari anatakiwa kuonana na daktari na wataalamu wengine wa afya wanaohusika na matibabu ya kisukari, hii itamsaidia kupunguza hatari ya madhara na athari mbali mbali ya kisukari katika ujauzito. Wanawake wenye kisukari wanaopata ushauri na matibabu kabla ya kubeba ujauzito huwa na matokeo mazuri kuliko wale ambao hawapati ushauri na tiba kabla ya ujauzito.


Kwa pamoja daktari na wataalamu wengine wa afya wataangalia maendeleo ya kiwango cha sukari na kama kuna athari zozote ambazo zimeshatokea kupitia vipimo na uchunguzi wa mwili na kupatiwa matibabu kulingana na athari husika. Kisha mama hupata matibabu na ushauri wa jinsi ya kufanya sukari kuwa katika kiwango kinachotakiwa kama ifuatavyo;


  • Namana ya kujipima sukari nyumbani

  • Mazoezi endapo ana uzito mkubwa uliopitiliza

  • Lishe ya kisukari

  • Kubadilishiwa dawa au kuongezewa dozi endapo itahitajika

  • kupewa virutubishi vya folate ili kupunguza hatari ya mtoto kuzaliwa na kasoro za kimaumbile hasa zile zinazotokea katika mfumo wa fahamu


Matibabu wakati wa ujauzito

Mwanamke mwenye kisukari anatakiwa kuanza kiliniki mara tu anapohisi ana ujauzito na kuhudhuria mara nyingi zaidi ya mjamzito ambaye hana tatizo lolote kama inavyopendekezwa. Wakati wa kliniki timu ya wataalamu wa afya hushirikiana kuhakikisha sukari yake inakuwa katika kiwango kinachotakiwa na huduma zifuatazo


Kufanyiwa vipimo


Vipimo mbali mbali hufanyika ili kujua maendeleo ya mama na mtoto na kubaini madhara ya kisukari kipindi cha ujauzito. Vipimo hivi ni;


  • Ultrasound ya uzazi

  • Kipimo cha mkojo

  • Kipimo cha figo

  • Fundoscopy

  • Kuangalia kiwango cha haemoglobin yenye sukari (HBA1C)

  • Kuangalia picha nzima ya damu nk.


Kufundishwa namna ya kujipima sukari akiwa nyumbani

Husaidia kuwa na kumbukumbu nzuri ya kiwango cha sukari katika kipindi chote cha ujauzito, hata hivyo si wajawazito wote wanaweza kujipima nyumbani kutokana na gharama za kipimo hivyo hutegemea kupimwa wakati wa kliniki.

Mjamzito anatakiwa kupima kiwango cha sukari kabla ya mlo wa asubuhi na baada ya mlo wa usiku, lengo ni kuhakikisha sukari inakuwa kati ya 3.5–5.5mmol/l kabla ya mlo wa asubuhi na 5–7.5mmol/l baada ya mlo wa usiku


Kuelekezwa matumizi ya dawa za kisukari

Dawa inayotakiwa kutumika wakati wa ujauzito ni insulin tu, kwani dawa za vidonge zinauwezo wa kusafiri kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kumsababishia madhara kama vile kushuka kwa sukari na kasoro za kimaumbile. Hata hivyo si dawa zote za vidonge zina madhara kwa mtoto, tafiti zinaonesha kuwa dawa ya Metformin na glyburide (glibenclamide) ni salama kwa mjamzito na mama anayenyonyesha.


Inashauriwa kuwa mwanamke mwenye kisukari anapogundulika kuwa ni mjamzito aanzishiwe insulin kama alikuwa anatumia dawa za vidonge, lakini kutokana na gharama na njia ya utolewaji wa insulin kwa sindano na athari nyingine za insulin wajawazito wengi hushindwa kuzingatia dozi.


Hivyo inashauriwa kuanza na dawa za vidonge kwa wale ambao wanashindwa kuzingatia dozi au kukataa insulin au wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu, na watalazimika kutumia insulin endapo kiwango cha sukari kinachotakiwa hakitaweza kufikiwa kwa dawa za vidonge baada ya dozi ya juu kabisa kufikiwa.


Kupanga muda wa kujifungua

Maamuzi ya muda sahihi wa kujifungua hutegmea na hali ya mama na mtoto, kama kiwango cha sukari kimedhibitiwa na hakuna madhara yoyote kwa mama na mtoto ujauzito huachwa hadi tarehe za makadirio na kusubiri uchungu wa kawaida.


Endapo kuna viashiria vya madhara na kiwango cha sukari hakijaweza kudhibitiwa mjamzito hutakiwa kujifungua kabla ya tarehe za makisio na kuazishiwa uchungu, mara nyingi huwa kati ya wiki ya 37 hadi wiki ya 39.


Lishe ya kisukari

Kama wagonjwa wengine wa kisukari, majamzito mwenye kisukari anatakiwa kula mlo kamili kutoka katika makundi yote ya vyakula ambao ni maalumu kwa kisukari.


Mazoezi ya mwili

Mazoezi ya viungo husaidia kupunguza hatari ya kuongezeka uzito kuliko pitiliza hivyo husaidia katika kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Mama huelekezwa mazoezi yanayofaa kwa mjamzito na kiwango kinachotakiwa.


Matibabu wakati wa kujifungua


Njia ya kujifungua inayopendekezwa ni ya kawaida, njia ya upasuaji hufanyika kama kuna dalili na viashiria vya mtoto kuwa na uzito mkubwa uliopitiliza au sababu nyingine za kikunga na kitabibu.


Wakati wa leba/ kujifungua kwa upasuaji mambo yafuatayo hufanyika


  • Kupima kiwango cha sukari kila baada ya masaa mawili

  • Kuendelea na insulin inayowekwa kwenye dripu katika dozi ya chini kulingana na kiwango cha sukari

  • Kama mjamzito amezuiliwa kula kwasababu za kitabibu huongezwa maji ya glukosi katika hatua ya kwanza ya leba.

  • Mara baada ya kujifungua mtoto huweka katika uangalizi maalumu, hupimwa sukari kila baada ya masaa manne kabla ya kunyonyeshwa hadi itakapo onekana kiwango chake cha sukari kipo sawa kwa vipimo mfulilizo walau vinne.


Matibabu baada ya kujifungua


Baada ya kujifungua matumizi ya homoni ya insulin katika mwili hupungua hivyo mama aliyekuwa akitumia dawa ya insulin hurejea kwenye dawa za vidonge ambazo ni salama kwa mtoto wakati wa kunyonyesha


Katika wiki 6 za mwanzo mama anatakiwa kuendelea kupima kiwango cha sukari kabla ya kifungua kinywa na wakati wa kulala na kuendelea na matibabu mengine ya kisukari (lishe, mazoezi nk)


Pia anataikwa kupata ushauri kuhusu uzazi wa mpango kwani ni hatari kwa mwanamke mwenye kisukari kubeba mimba zinazokaribiana.

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

4 Februari 2022 20:03:00

Rejea za dawa

bottom of page