top of page

Mwandishi:

Dkt. Salome A, MD

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

16 Julai 2021 16:27:53

Image-empty-state.png

Malaria kwa mjamzito

Malaria ni ugonjwa hatari wa kuambukiza unaosababishwa na kimelea anayeitwa plasmodium anayeenezwa na mbu jike aina ya anofelesi. Ugonjwa huu bado ni tatizo kubwa hasa katika nchi zilizo kwenye ukanda wa kitropiki kama vile Afrika, America na Asia. Uenezi mkubwa wa malaria unaonekana Afrika, na inakadiriwa katika mwaka 2019 kuwa asilimia 94 ya visa na vifo vilitokea kutokana malaria.


Watu gani wapo hatarini kupata malaria?


Malaria inaweza kumpata mtu yoyote, hata hivyo kuna makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ya kupata malaria ambayo ni;


 • Watoto walio katika umri chini ya miaka mitano

 • Wazee

 • Wajawazito

 • Wageni wanaotoka maeneo yasiyo na ugonjwa wa malaria

 • Watu wenye upungufu wa kinga ya mwili kwa mfano watu wenye UKIMWI.

 • Kutokana na mabadiliko ya kifiziolojia yanayotokea katika kipindi cha ujauzito, wajawazito wapo katika hatari ya kupata malaria kuliko watu wengine wasio kwenye makundi hayo.


Ukubwa wa tatizo la malaria kwenye ujauzito


Inakadiriwa kuwa kila mwaka wanawake wa ki Afrika milioni 25-30 hupata ujauzito katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya malaria, pia kila mwaka malaria husababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo kati ya 75,000-200,000 kwa sababu ya watoto kudumaa tumboni na kuzaliwa njiti. Hivyo basi kundi hili linahitaji kukingwa na kupatiwa matibabu mara tu wanapogundulika kuwa na malaria.


Aina za vimelea wa malaria


Kuna aina tano za spishi za vimele vya malaria ambao wapo katika jenasi ya plasmodium kama ifuatavyo;


 • Plasmodium falciparum

 • Plasmodium malariae

 • Plasmodium vivax

 • Plasmodium ovale

 • Plasmodium knowlesi


Sifa za vimelea mbalimbali wa malaria


Katika spishi hizi tano, kimelea aina ya Plasmodium falciparum na Plasmodium vivax ni hatari zaidi kuliko wengine. Pia Plasmodium falciparum huongoza kusababisha malaria ulimwenguni kote.

Inaadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi ya ugonjwa wa malaria husababishwa na plasmodium falciparum na isipotibiwa huleta madhara makubwa na hata kifo. Malaria inayosababishwa na falciparum malariae, plasmodium vivax na plasmodium ovale husababisha ugonjwa ambao sio shahidi sana kwa binadamu. Plasmodium knowlesi husababisha malaria kwa nyani aina ya makaku lakini pia huweza kuambukiza binadamu, yaani malaria kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.


Uenezwaji wa malaria


Njia kuu ya uenezi wa malaria ni kupitia mbu jike jamii ya anopheles, ili mtu apate malaria inabidi awe ameng’atwa na mbu ambaye amebeba vimelea wa maambukizi baada ya kufyoza damu ya mtu mwenye maambukizi. Mbu anapomng’ata mtu mwenye malaria hufyonza damu yenye vimelea wa malaria. Baada ya wiki moja mbu anapomng’ata mtu mwingine ili kupata chakula, vimelea hao huingia kwa binadamu aliyeng’atwa kupitia mate yake hivyo kusababisha malaria.


Njia za uenezaji wa malaria


Kwa sababu vimelea wa malaria huishi katika chembe nyekundu za damu, vimelea hao huweza kuenezwa pia kwa njia zifuatazo;


 • Kuongezwa damu ya mtu mwenye malaria

 • Kuwekewa kiungo cha mtu mwenye malaria

 • Kuchangia na mgonjwa vitu vyenye ncha kali

 • Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito


Sababu za mama mjamzito kuwa katika hatari ya kupata malaria


Wajawazito hasa katika ujauzito wa kwanza wapo katika hatari ya kupata malaria kuliko wanawake wasio wajawazito. Wakati wa ujauzito kinga dhidi ya malaria hupungua, hata hivyo chanzo au sababu za kushuka kwa kinga hiyo haijulikani.Kushuka kwa kinga ya mwili huonekana sana katika ujauzito wa kwanza na wa pili. Katika utafiti uliofanyika Gambia mwaka 2000 ilionekana kuwa wajawazito huwavutia mbu wanaoneza malaria hivyo kupelekea kupata malaria kuliko watu wengine, sababu zikiwa ni kuongezeka kwa joto la mwili na kutoa harufu inayowavutia sana mbu. Mjamzito katika umri mdogo yupo katika hatari ya kupata malaria zaidi ya mjamzito mwenye umri mkubwa katika baadhi ya maeneo ya Afrika.


Madhara ya malaria kwa mjamzito, mtoto aliye tumboni na mtoto aliyezaliwa


Kutokana na kushuka kwa kinga mwili wakati wa ujauzito, mwili hushindwa kuzuia kuzaliana kwa vimelea. Vimelea hujificha katika kondo la nyuma na kuzaliana kwa wingi kisha kusababisha malaria kali pamoja na athari zake zilizoorodheshwa hapo chini.


Madhara ya malaria kwa mjamzito


 • Malaria ya kupanda kichwani

 • Kujaa maji kifuani

 • Upungufu wa damu

 • Kupata uchungu kabla ya siku za makadirio ya kujifungua


Madhara ya malaria kwa mtoto aliyetumboni


 • Kudumaa

 • Kufia tumboni

 • Mimba kutoka


Madhara ya malaria kwa mtoto aliyezaliwa


 • Kuzaliwa na uzito mdogo

 • Mtoto njiti

 • Kuzaliwa na malaria

 • Upungufu wa damu

Ishara na dalili za malaria kwa mjamzito


Dalili na ishara za malaria kwa mjamzito hazitofautiani na watu wengine, wajawazito walio katika maeneo yenye uenezi mkubwa huwa na dalili chache ambazo huweza kuchanganywa na dalili za magonjwa mengine.Pia wajawazito walio katika maaeneo haya vimelea hujificha kwenye kondo la nyuma na kupelekea utambuzi kuwa mgumu. Wajawazito walio katika maeneo yenye kiwango kidogo cha uenezi huonesha dalili za malaria kali kwasababu miili yao hukosa kinga ya malaria, vimelea wachache hutosha kuleta malaria kali. Dalili na ishara za malaria zimegawanyika katika makundi mawili kulingana na ukubwa au ukali wake kama ambazo ni;


 • Ishara na dalili za malaria isiyo kali

 • Ishara na dalili za malaria kali


Ishara na dalili za malaria isiyo kali


 • Homa

 • Kutapika

 • Kuharisha

 • Maumivu ya kichwa

 • Maumivu ya mwili

 • Kukosa hamu ya kula

 • Maumivu ya maungio

 • Kuvimba kwa bandama

 • Kupauka kwa viganja vya Mikono au macho( ishara ya upungufu wa damu)


Ishara na dalili za malaria kali


 • Kulegea kwa mwili kiasi cha kushindwa kukaa au kutembea bila msaada

 • Kuzimia au Kupoteza fahamu au kupata koma

 • Kuchanganyikiwa

 • Kutapika kila kitu baada ya kula au kunywa

 • Degedege

 • Kushindwa kupumua

 • Manjano

 • Kutokwa na damu (DIC)

 • Shoki

 • Kushuka kwa sukari mwilini

 • Kufeli kwa figo

 • Kupauka sana kunakoashiria upungufu wa damu


Dalili na ishara za malaria kali kwa mjamzito


 • Homa kali

 • Kushuka kwa sukari kwenye damu

 • Upungufu wa damu

 • Malaria ya kichwani

 • Mapafu kujaa maji

 • Kiwango kikubwa cha vimelea kinachoonekana katika kipimo cha hadubini


Vipimo vya malaria


Vimelea wa malaria huweza kuonekana kwenye damu ya mtu kwa kutumia vipimo vya;


 • Malaria Rapid Diagnostic Tests (mRDTs)

 • Hadubini


Kipimo cha haraka cha malaria


Malaria Rapid Diagnostic Tests (mRDTs) Kipimo cha haraka cha malaria hufahamika pia kama Malaria Rapid Diagnostic Tests (mRDTs) ni kipimo cha haraka kinachotoa majibu ndani ya muda mfupi na hivyo kuharakisha utambuzi na matibabu ya malaria, hatahivyo kipimo hiki hakiwezi kupima idadi ya vimelea wa malaria isipokuwa kinapima au kugundua uwepo wa vimelea. Kuna aina mbili za vipimo cha haraka cha malaria (mRDTs) ambazo ni;


 • Convetional Malaria Rapid Diagnostic Tests

 • High specific Malaria Rapid Diagnostic Tests


Convetional Malaria Rapid Diagnostic Tests


Kipimo hiki hutoa majibu ndani ya dakika 15 hadi 30 na hutumia tone la damu tu kutoka kwenye kidole. Kipimo hiki rahisi kutumia na hakiitaji utaalamu mkubwa. Convetional Malaria Rapid Diagnostic Tests ziko za aina mbili ambazo ni specific antigen mRDT na pan specific antigen mRDT. Tofauti iliyopo katika vipimo hivi ni kwamba specific antigen mRDT inauwezo wa kutambua aina moja tu ya vimelea wa malaria, wakati pan specific antigen mRDT unauwezo wa kutambua spishi zote za vimelea wa malaria


High specific Malaria Rapid Diagnostic Tests


Kipimo hiki kinauwezo mkubwa wa kupima vimelea wa spishi ya plasmodium falciparum, hata hivyo uwezo wake ni shahidi sana pale ambapo maambukizi ni makubwa na hivyo hasara yake ni kwamba hakiwezi kugundua vimelea katika maeneo yenye maambukizi kidogo. Matumizi ya kipimo hiki bado yapo kwenye uchunguzi.


Kupima malaria kwa hadubini


Hiki ni kipimo kikuu kinachopendekezwa kupima vimelea wa malaria, kinauwezo wa kujua idadi na aina ya vimelea wa malaria. Ufanisi wa majibu ya kipimo hiki hutegemea ujuzi na uzoefu wa mpimaji, hivyo ili kupata majibu sahihi ni lazima kutumia mpimaji mzoefu. Hii ndio sababu kwanini kipimo cha mRDTs kinatumika zaidi katika utambuzi wa malaria.


Matibabu ya malaria kwa mjamzito


Matibabu ya malaria kwa mjamzito hutolewa kulingana na ukali wa ugonjwa pamoja na hali zinazoambatana na ugonjwa, ambayo yanahusisha matibabu ya malaria kali au isiyo kali.

Matibabu ya malaria isiyo kali


Dawa ambayo imethibitishwa kuwa salama ni Artemether Lumefantrine (ALU), inaweza kutumiwa katika kipindi chochote cha ujauzito bila kuleta madhara yoyote kama ilivyokuwa ikidhaniwa. Kila mjamzito aliyegundulika kuwa na malaria anapaswa kuanzishiwa vidonge vya ALU kwa muda wa siku tatu, matibabu mengine hutegemea hali ya mgonjwa kwamfano paracetamol endapo anahoma nk.


Matibabu ya malaria kali kwa mjamzito


Malaria kali ni dharura hivyo mgonjwa hutakiwa kupata mtibabu mapema katika kituo cha huduma ya afya au hospitali, ili asipate athari zitokanazo na malaria na kuzuia vifo vya wajawazito. Dawa inayotumika kutibu malaria kali kwa wajawazito ni Artesunate, dawa hii hutolewa kwa njia ya sindano na hutumika katika kipindi chochote cha ujauzito . Mgonjwa hupewa dozi tatu za artesunate ndani ya masaa 24au zaidi na kisha kuendelea na vidonge vya artemether lumefantrine masaa 8 baada ya sindano ya mwisho kwa muda wa siku tatu. Matibabu mengine hutegemea hali ya mgojwa na athari za malaria alizonazo kwa mfano homa, degedege, upungufu wa damu nk.


Njia za kujikinga na malaria kwa mjamzito


Kuna njia mbalimbali zinaweza kutumika kuzuia vifo na madhara yatokanavyo na malaria kwa wajawazito ambazo ni;


Matumizi ya chandarua cha kudumu chenye dawa

Kutumia dawa kinga ya malaria wakati wa ujauzito


Matumizi ya chandarua cha kudumu chenye dawa


Wajawazito wote wanatakiwa kupewa vyandarua vilivyowekewa dawa ili kuwakinga na mbu waenezao malaria. Matumizi ya chandarua chenye dawa yanaonekana kupunguza uenezwaji wa malaria, kupunguza makali ya ugonjwa pamoja na madhara yake. Dawa zinazotumika kutibu chandarua ni salama kwa mama na mtoto aliye tumboni, zinauwezo wa kumkinga mama dhidi ya mbu pia kuua wadudu wengine. Endapo watu wengi katika jamii wakitumia vyandarua hivi idadi ya mbu hupungua na kwasababu hawapati chakula muda wao wa kuishi huwa mfupi na hivyo kasi ya uambukizwaji kupungua . Chandarua cha kudumu chenye dawa kinauwezo wa kutopoteza kiwango cha dawa kwa muda usiopungua miaka 3 licha ya kufua mara kwa mara.


Kutumia dawa kinga ya malaria wakati wa ujauzito


Matumizi ya dawa kinga ya malaria wakati wa ujauzito hujulikana pia kama intermittent preventive treatment (IPT) huhushisha hupewa dozi kamili ya malaria katika vipindi tofauti vya ujauzito hata kama mjamzito hana dalili au viashiria vya malaria. Lengo la IPT ni kumkinga mama na mtoto dhidi ya madhara yatokanayo na malaria pamoja na kupata malaria kali. IPT haizuii mjamzito kupata malaria, mjamzito anaweza kuumwa malaria hata baada ya kupata IPT. Shirika la afya duniani (WHO) lilipendekeza kutoa IPT katika maeneo yenye kiwango cha kati na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria, kwahiyo maeneo yasiyo na malaria au yenye kiwango kidogo sana cha uenezi wajawazito wanaweza kukingwa dhidi ya malaria kwa njia nyingine kama vile kutumia vyandarua vya kudumu vyenye dawa. IPT itatolewa tu kama mjamzito alisafiri kutoka kwenye eneo lisilo na malaria kwenda kwenye eneo lenye kiwango cha kati na kiwango kikubwa cha uenezi wa malaria. Endapo kusafiri katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha uenezi wa malaria ni kwa lazima sana basi mjamzito anapaswa kupewa kinga ya malaria kwa kunywa dawa ya mefloquine katika kipindi chochote cha ujauzito.


Dawa gani hutumika kukinga malari kwenye ujauzito?


Katika maeneo ambayo yana kiwango cha kati na kiwango kikubwa cha uenezi wa malaria dawa inayotumika katika IPT ni sulfadoxine-pyrimethamine (SP) pia huitwa fansidar ambayo imethibitishwa kuwa ni salama kwa mjamzito. Tafiti zilizofanyika zinaonesha matokeo mazuri kwa wajawazito waliotumia dawa SP na inaweza tumika kwa dozi 3 mpaka 5 bila kuleta madhara yoyote. Dawa nyingine zinazoweza kutumiwa kama kinga ya malaria ni doxycycline na proguanil/atovaque, lakini dawa hizi huleta madhara katika kipindi cha ujauzito na kunyonyesha kwahiyo hazitumiki.


Wakati gani kinga ya malaria hutolewa kwa wajawazito?


Wajawazito wanapoanza kliniki wanatakiwa kupewa dozi ya kwanza ya SP kuanzia wiki ya 16 na kurudiwa kila baada ya wiki nne mpaka muda wa kujifungua. IPT kwa kutumia dawa ya SP hutolewa na mtoa huduma katika kliniki na mjamzito hunywa dawa kwa uangalizi wake kila anapohudhuria kliniki kama ilivyopangwa.


Mambo ya kuzingatia wakati wa utoaji wa IPT kwa kutumia SP


SP haitakiwi kutolewa kwa mjamzito mwenye maambukizi ya UKIMWI anayetumia dawa ya cotrimoxazole (septrin) kama kinga


Endapo mama atapimwa na kugundulika kuwa ana malaria wakati wa kliniki atatakiwa kutibiwa kwanza kabla ya kupewa SP


Endapo mama atapata malaria baada ya kuanza kutumia SP itabidi aanzishiwe matibabu kulingana na ukali wa malaria


Endapo mama ameumwa na malaria na kutibiwa ataendelea na IPT baada ya mwezi mmoja kutoka tarehe inayofuata ya kliniki, na ataendelea na dozi zingine kwa mahudhurio yatakayofuata kama inavyopendekezwa


Endapo mama ana historia ya kupata mzio anapotumia dawa jamii ya sulphonamides hatakiwi kupewa IPT kwa kutumia SP.Hakuna dawa inayoweza kutumika kama mbadala hivyo bado tafiti zinaendelea kuchunguza dawa salama ya kutumia katika IPT kwa wajawazito wanaopata mzio.


Mama anaweza kunywa SP akiwa amekula au akiwa hajala na hakuna madhara yoyote


Mjamzito anaweza kunywa SP na kuendelea na dawa za kuongeza damu zenye mchanganyiko wa ferrous sulphate yenye 200 mg na folic acid yenye 0.25 mg


Matumizi ya miligramu 5 au zaidi ya folic acid Folic acid hupunguza nguvu ya dawa SP. Endapo ni wakati wa kumeza SP, acha kutumia folic acid kwa muda wa wiki mbili toka umetumia SP kisha utaendelea na dozi yako kama ulivyopangiwa na daktari.


Muhimu


Wasaidie wajawazito wengine kusoma makala hii ya malaria ili wafahamu na kuchukua hatua za kujikinga na madhara kwenye ujauzito kwa kuwatumia linki ya makala hii.

Wapi utapata taarifa zaidi?


Unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu malaria kutoka kwenye linki zifuatazo au linki zilizo; 1. Homa ya mbu. https://www.ulyclinic.com/homa-ya-mbu-maana 2. Dalili za malaria. https://www.ulyclinic.com/homa-ya-mbu-dalili

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

24 Desemba 2021 05:09:25

Rejea za dawa

 1. Walker PGT, ter Kuile FO, Garske T, Menendez C, Ghani AC. Estimated risk of placental infection and low birthweight attributable to Plasmodium falciparum malaria in Africa in 2010: a modelling study. Lancet Glob Health. 2014

 2. CDC-Malaria-About malaria https://www.cdc.gov/malaria/about/faqs.html. Imechukuliwa 29/09/2021

 3. WHO Malaria fact sheet April 2021 https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/malaria 4. Michal Fried and Patrick E. Duffy. Malaria during pregnancy https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5453384/. Imechukuliwa 29/09/2021

 4. Lora Sabin, Evan M.S Hecht and Davidson H. Hamer.Prevention and treatment of malaria in pregnancy: what do pregnant women and health care workers in East India know and do about it? https://malariajournal.biomedcentral.com/articles/10.1186/s12936-018-2339-9. Imechukuliwa 29/09/2021

 5. CDC-Malaria-Malaria Worldwide. https://www.cdc.gov/malaria/malaria_worldwide/reduction/itn.html. Imechukuliwa 29/09/2021

 6. Guyatt HL, et al. Impact of malaria during pregnancy on low birth weight in sub-Saharan Africa. Clin Microbial Rev. 2004 8. Steketee RW, et al. The burden of malaria in pregnancy in malaria-endemic areas. Am J Trop Med Hyg.2001

 7. Lindsay S, et al. Effect of pregnancy on exposure to malaria mosquitoes. Lancet.2000

 8. Walker-Abbey A et al. Malaria in a pregnant Cameroonian women: the effect of age and gravidity on submicroscopic and mixed-species infections and multiple parasite genotypes.Am J Trop Med Hyg. 2005

 9. Tanzania MoHCDEC. National guidelines for malaria diagnosis, treatment and preventive therapies. NMCP December, 2020.

bottom of page