top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

9 Julai 2021 21:20:31

Image-empty-state.png

Seli mundu na ujauzito

Makala hii imelenga kumwelimisha mjamzito mwenye tatizo la seli mundu. Elimu hii ni itakufanya uelewe vema afya yako na aina ya huduma na matibabu yanayopatikana kwa ajili yako kwenye ujauzito na kupata mwisho mzuri wa ujauzito.


Ugonjwa wa seli mundu ni nini?


Seli mundu ni ugonjwa wa kurithi utokanao na kuathirika kwa chembe nyekundu za damu pamoja na himoglobin zilizo ndani yake. Kama jina lilivyo, chembe nyekundu za damu kuna wakati hubadilika na kuwa umbo la mundu, umbile ambalo linafanana mwonekano wa nusu mwezi.

Madhara ya chembe nyekundu kuwa na umbile la mundu ni nini?


Mgonjwa wa seli mundu huwa na chembe nyekundu za damu zilizo dhaifu na zinazobadilika mara kwa mara umbile lake kuwa umbile la mundu. Udhaifu huu hufanya chembe hizo ziharibiwe mapema na kupelekea upungufu wa damu mwilini. Mabadiliko ya umbile pia huweza pelekea kuziba kwa mishipa midogo ya damu, endapo mishipa ya damu itaziba kwa sababu ya chembe za umbile la mundu, mgonjwa atapata maumivu makali na dalili zingine. Mfano mishipa ya mifupa ikiziba, maumivu makali ya mifupa yatatokea, endapo ni mapafu maumivu makali ya kifua yatatokea n.k.Tatizo la maumivu ya mifupa hutokea sana wakati wa ujauzito. Kuziba kwa mishipa ya damu inaweza kutokea pia kwenye mishipa ya mapafu, moyo, macho na figo hivyo kupelekea ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, matatizo ya figo, vidonda miguuni na kuharibika kwa maungio ya mwili.


Ni nini husababisha ugonjwa wa seli mundu


Ugonjwa wa seli mundu hutokana na mabadiliko yanayotokea kwenye jeni inayotengeneza protini muhimu ya kubeba oksijeni mwilini yenye jina la hemoglobin. Mabadiliko katika jeni huweza rithiwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto. Ili uonyeshe dalili ya seli mundu ni lazima uwe na jeni mbili zote ambazo ni za seli mundu.

Kubeba jeni moja hakumfanyi mbebaji aonyeshe dalili bali anaweza kumpelekea mwanae jeni au kupata ugonjwa endapo atakutana na baba aliyebeba jeni ya seli mundu pia. Mifano Endapo mama na baba kila mmoja amebeba jeni ya ugonjwa bila kuonyesha dalili zozote zile, asilimia 50 ya watoto watakaozaliwa watakuw ana seli mundu.

Endapo mama amebeba jeni tu na baba anaugonjwa wa seli mundu, asilimia 75 ya watoto watakaozaliwa watakuwa na seli mundu na wengine watabeba ugonjwa bila kuonyesha dalili. Endapo mama na wana ugonjwa wa seli mundu watoto wote wakakaozaliwa watakuwa na ugonjwa wa selim mundu pia. Endapo mama ana ugonjwa wa seli mundu na baba hana ugonjwa wala kubeba jeni za seli mundu, watoto watakaozaliwa watabeba jeni za seli mundu. Watoto hao endapo wataoa au kuolewa na wapenzi waliobeba jeni za seli mundu, wataweza kupata watoto wenye jeni au ugonjwa wa seli mundu kwa kufuata maelezo yaliyoandikwa hapa juu.


Ugonjwa wa seli mundu unaambukizwa?


Hapana. Kutokana na maelezo ya hapo juu, ugonjwa wa seli mundu huwa hauambukizwi, bali hurithiwa kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto.


Tatizo la seli munduni kubwa kiasi gani?


Ugonjwa wa seli mundu ni moja ya magonjwa ya kurithi unaotokea sana duniani haswa katika nchi za Afrika, India na maeneo ya ukanda wa bahari ya Mediterania huku Tanzania ikiwa inaongoza kuleta duniani watoto wenye seli mundu, kufikia idadi ya vichanga 11,000 kwa mwaka. Taarifa za UK zinaonyesha kuwa kati ya watu 12,000 hadi 15,000 wana ugonjwa wa seli mundu na zaidi ya watoto 300 wanazaliwa na seli mundu kila mwaka. Kwa nchi zilizoendelea, vichanga wanaozaliwa hupewa fursa ya kupima kipimo cha utambuzi wa jeni za seli mundu, kipimo kilicho msingi kwa ushauri wa namna gani mtoto atakavyoishi.


Je ujauzito wangu utaathirika kama nimebea jeni za seli mundu?


Hapana, kama umebeba jeni za seli mundu, hutaonyesha dalili yoyote ya ugonjwa wa seli mundu, hivyo ujauzito wako utakuwa kawaida tu kama ujauzito wa wanawake wasio na seli mundu.


Kama nina ugonjwa wa seli mundu, ni nini nifanye kabla ya kuwa mjamzito?


Kabla ya kuwa mjamzito, ni muhimu kumtaarifu daktari wako kuwa unatarajia kupata ujauzito ili akusaidie kufahamu ni nini cha kufanya ili uwe na ujauzito wenye maudhi kidogo.


Mambo ya kufahamu kabla ya kuwa mjamzito


Ni mambo gani ya kufahamu? Kabla ya kupata ujauzito unatakiwa kufahamu kama mpenzi wako anajeni za seli mundu kwa kupima, hii itasaidia kufahamu hali yake na uwezekano wa kupata mtoto mwenye seli mundu au la. Endapo mpenzi wako ana jeni za seli mundu, uwezekano mkubwa wa kupata mtoto mwenye ugonjwa wa seli mundu, baada ya kupima shaurianeni endapo kuna faida ya kuwa na mtoto au la. Endapo mpenzi wako hana seli mundu wala hajabeba jeni, mtoto mtakayepata hatakuwa na ugonjwa wa seli mundu ila atabeba jeni za ugonjwa. Baada ya kupima mtafanya uamuzi wenyewe wa nini kitafuataVipimo vya kufanya kabla ya kuwa mjamzito

Kabla ya kupanga kupata mtoto unatakiwa kupima angalau kila mwaka;

 • Hali ya moyo (kipimo cha ECHO)

 • Shinikizo la juu la damu

 • Vipimo vya mkojo

 • Vipimo vya damu

 • Kipimo cha macho ( retina)


Kuna mabadiliko ya matibabu natakiwa fanya kabla ya kuwa na ujauzito?


Kama unatumia dawa ya hydroxyurea, unapaswa kuacha dawa hiyo na kutumia dawa za uzazi wa mpango angalau kwa muda wa miezi mitatu (3) kabla ya kupata ujauzito Dawa zingine unazotumia pia kabla ya kuwa mjamzito zinapaswa kuchunguzwa na daktari kama zina mwingiliano au madhara kwenye ujauzito unaotarajia kupata.


Je nitahitaji matibabu ya ziada kabla ya kupata ujauzito?


Ndio, kwa sababu kuwa na ugonjwa wa seli mundu huongeza hatari kubwa ya kupata maambukizi ya bakteria n.k, utashauriwa utumie dawa za antibayotiki aina ya penicillin kila siku.

Utapatiwa chanjo ya kirusi cha homa ya ini B, na nimonia kama kuna program ya kutoa dawa hiyo kabla ya kupata ujauzito Utashauriwa pia kutumia dozi kubwa ya vitamin Folic acid kila siku


Je ujauzito wangu utakuwa na madhara gani?


Wanawake wengi wenye seli mundu, huwa na ujauzito usio na maudhi makubwa kipindi kizima cha ujauzito na kujifungua. Hata hivyo, kuamka kwa vipindi vya dalili ya maumivu hutokea sana wakati wa ujauzito. Hatari za ugonjwa wa seli mundu kwenye ujauzito ni


 • Upungufu wa damu na maumivu ya mapafu

 • Kuganda kwenye miguu

 • Shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba

 • Kujifungua kabla ya wakati

 • Kujifungua mtoto njiti


Maelezo zaidi yameandikwa hapo chini


Upungufu wa damu na maumivu ya mapafu


Endapo una tapika sana wakati wa asubuhi, hali hii hupelekea kuishiwa maji mwilini na kuamka kwa dalili za mshiko wa seli mundu


Kuganda damu miguuni


Mjamzito mwenye seli mundu ana hatari zaidi ya kuganda kwa damu kuliko wakati hana ujauzito, kuganda kwa damu hupelekea kufanyika kwa mabonge ya damu yanayoweza kubomoka na kusafiri kwenye mishipa. Endapo yatakutana na mishipa midogo ya damu huiziba, hii huweza kuamsha maumivu makali ya mifupa, kiharusi na maumivu ya kifua.


Shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba


Shinikizo la damu linaloelekea kifafa cha mimba hufahamika kwa jina jingine la pre eklampsia, huweza tokea baada ya wiki 20 za ujauzito. Pre- eklampsia huambatana na shinikizo la juu la damu, na huweza kusababisha degedege kwenye ujauzito.


Kujifungua kabla ya wakati


Kuna uwezekano mkubwa wa kupata uchungu kabla ya wakati, endapo uchungu utachelewa kuja, utashauriwa uanzishwe ili ujifungue mapema na kuzuia madhara kwako na kichanga tumboni. Wanawake wengi wenye seli mundu, hujifungua mara nyingi kwa njia ya upasuaji kwani huwa salama kwao. Hata hivyo kuwa na seli mundu haina maana kuwa ndo kigezo cha kujifungua kwa upasuaji, bali mpaka kuwa na sababu.


Ni nini huamsha mshiko wa dalili za maumivu ya seli mundu?


Vipindi vya maumivu vinavyotokana na mabadiliko ya chembe nyekundu kuwa na umbo la mundu huamshwa na;


 • Hali ya hewa ya baridi

 • Kupungua kwa maji mwilini

 • Maambukizi kwenye damu

 • Kufanya kazi ya kutumia pumzi nyingi ( kazi nzito)


Ni matunzo gani unatakiwa kuzingatia wakati nina ujauzito?


Unatakiwa kuwasiliana na daktari wako kwa ushauri wa kupewa chanzo zinazotakiwa kama ya Hepatiti B n.k

Unatakiwa kuhudhuria kliniki angalau kila baada ya wiki 4 mpaka utakapofikisha wiki 24 kwa uangalizi wa karibu, kisha kila baada ya wiki 1 hadi 2 mpaka utakapojifungua. Kwenye kila mahudhurio utapimwa shinikizo la juu la damu na mkojo, pia utafanyiwa vipimo vingine ambavyo hufanyika kwa wanawase wasio na seli mundu kila wanapohudhuria kliniki ili kuhakikisha kuwa mtoto anakuwa vema tumboni. Baadhi ya wakati inaweza hitajika kuongezewa damu itahitajika.

Kwa sababu damu ina hatari ya kuganda, kama una vihatarishi vingine mfano, kuwa na uzito mkubwa kupita kiasi, utashauriwa kuchoma sindano ya dawa heparin kwenye ujauzito wako wote ili kuzuia hatari ya damu kuganda kwenye mapafu au miguuni. Dozi ya heparini kwenye ujauzito ni salama na inaweza kuendelezwa kwa muda wa wiki 6 baada ya kujifungua ili kupunguza hatari ya damu kuganda.

Kuwa na mawasiliano ya daktari au nesi wako ili endapo umepata shida uweze kupiga simu na kupatiwa huduma ya karibu. Wasiliana nao haraka unapopata dalili za maumivu au zingine za seli mundu na pia hudhuria kliniki au kwenye huduma za dharura hata kama tarehe zako hazijafika bado.

Dawa gani natakiwa kutumia wakati wa ujauzito?


Kwa baadhi ya nchi na madaktari hushauri matumizi ya dawa zilizoorodheshwa hapa chini muda wote wa ujauzito kwani hufanya ujauzito usiwe na vipindi vingi vya maudhi au amdhara ya seli mundu;


 • Dozi kubwa ya folic acid

 • Dozi ya kila siku ya penicillin

 • Dozi ndogo ya aspirini


Aspirini ina umuhimu wa kuzuia damu kuganda.


Unaweza kutumia pia dawa jamii ya parasetamo na kodeini kwa ajili ya maumivu yanapotokea.


Dawa ambazo huapswi tumia kwa maumivu wakati wa ujauzito ni zipi?


Usitumie dawa ibuprofen kabla ya wiki 12 za ujauzito na baada ya wiki 28 za ujauzito bila kushauriwa na daktari mwenye weredi na dawa hizo kwa sababu zinaweza kusababisha matatizo kwa kijusi tumboni. Kama una shinikizo la juu la damu na unatumia dawa jamii ya ACEIs au ARBs, unapaswa kuacha kutumia dawa hizo kabla ya kuwa mjamzito Dawa zingine ambazo hazipaswi kutumika kwenye ujauzito ni sawa na zile ambazo hazipaswi kutumia kwa wajawazito wengine. Soma kwenye Makala za dawa zisizopaswa kutumika wakati wa ujauzito ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC


Unaposhikwa na dalili za seli mundu ufanyaje?


Endapo umepata mshiko wa dalili za seli mundu, unapaswa kutafuta huduma za dharura mara moja.


Utakapofika hospitali, utapewa dawa za kupunguza maumivu na oksijeni ili kusaidia mwili wako upate hewa hiyo ya kutosha. Utawekewa dripu ya maji pia endapo kisababishi ni upungufu wa maji na pia dawa za antibayotiki kama kuna ishara za maambukizi. Utapatiwa dozi ya heparin na mtoto tumboni atafanyiwa uchunguzi wa hali yake ya kiafya kwa kipimo cha picha ya mionzi sautiWakati gani sahihi wa kujifungua?


Baada ya kutumiza wiki 38 unaweza kuanzishiwa uchungu


Njia gani sahihi ya kujifungua endapo nina umwa seli mundu?


Si kwamba unapokuwa na seli mundu ni lazima ujifungua kwa upasuaji, bali endapo hakuna hatari ya kujifungua kwa njia ya kawaida kwako na kwa mtoto. Mtafanya maamuzi wewe na daktari wako kuhusu njia gani sahihi ya kujifungua.Seli mundu na uchungu wa kujifungua


Kabla ya uchungu au wakati uchungu unaanza, unatakiwa kufika hospitali haraka bila kusubiria ili ufanyiwe matunzo ya karibu na kujifungua salama. Utapewa uangalizi na huduma muhimu ili kuzuia kuamka kwa dalili za seli mundu kwa;


 • Kuwekwa chumba maalumu chenye joto ili usipigwe na baridi wakati unapata uchungu

 • Kutundikiwa dripu ya maji

 • Kupewa oksijeni

 • Kuongezewa damu endapo una damu kidogo

 • Uchunguzi mapigo ya moyo ya mtoto kwa ukaribu sana


Dawa za kuzuia uchungu zitahitajika?


Utaongea na daktari wa dawa za usingizi kabla ya kupatiwa dawa yoyote ya kuzuia uchugu au dawa za ganzi kama utajifungua kwa upasuaji. Hata hivyo dawa nyingi huwa hazina matatizo isipokuwa pethidine inayoweza kuleta madhara kwenye ujauzito.


Nini cha kufanya baada ya mtoto kuzaliwa?


Baada ya kujifungua, unapaswa kuendelea kukaa kwenye eneo lenye joto, kufunikwa vema kwa nguo, kutundikiwa dripu ya maji na kutumia oksijeni kama itahitajika ili kuepusha mshiko wa dalili za mshiko wa seli mundu. Utashauriwa kufanya mazoezi kitandani kwanza kwa kuchezesha misuli ya mguu na vidole kisha mazoezi ya kutembea tembea ili kuepusha hatari ya damu kuganda baada ya kujifungua. Unaweza kutumia soksi maalumu pia zinazozuia damu kutuwama sehemu moja miguuni kwa muda mrefu

Kama unatumia heparini, utashauriwa kuendelea kutumia mpaka zitakapopita wiki 6 za ujauzito kama unavihatarishi mfano endapo umejifungua kwa upasuaji. Utashauriwa kunyonyesha mtoto kama kawaida na utafundishwa namna ya kunyoneysha pia Endapo kuna kipimo cha kupima jeni za seli mundu kwenye damu, utapatiwa ushauri kufanya kipimo hiki wiki moja baada ya mtoto kuzaliwa.


Natakiwa tumia uzazi wa mpango baada ya kujifungua?


Kwa sababu kuna hatari kubwa ya kupata ujauzito mwingine, unashauriwa kutumia za uzazi wa mpango, njia ya kizuizi huwa nzuri kwa sababu haitumii homoni. Hata hivyo njia za uzazi wa mpango zinazoweza kutumika ni


 • Matumizi ya dawa za progesterone tu

 • Sindano ya depo provera

 • Njiti

 • Au lupu

 • Vizuizi


Dalili za kukufanya umpigie daktari wako simu haraka


Ni vema siku zote, unapokuwa mjamzito uwe na mipango ya namna gani unaweza kufika hospitali haraka kwa ajili ya matibabu ya dharura wakati wowote pasipo kuchelewa. Hii itasaidia kunusuru afya yako na mwanao tumboni. Wasiliana na daktari au mtoa huduma wako kwa ushauri na matibabu ya haraka endapo;


 • Una homa inayozidi nyuzi joto 38 za sentigredi

 • Unapumua kwa shida

 • Maumivu ya kifua

 • Maumivu ya tumbo

 • Kuvimba kwa tumbo

 • Maumivu makali ya kichwa

 • Kupooza ghafla upande mmoja wa mwili

 • Kupotea kwa hisia sehemu yoyote ya mwili

 • Degedege

 • Dalili zingine za hatari kipindi cha ujauzito


Wapi unaweza kupata taarifa zaidi kuhusu seli mundu na ujauzito?


Pata taarifa zaidi kuhusu sel mundu kwenye makala ya seli mundu ndani ya tovuti hii ya ULY CLINIC au kupitia rejea chini ya makala hii


Majina mengine ya ujauzito na seli mundu


Mimba ya mgonjwa mwenye seli mundu

Mimba ya mgonjwa wa sickle cell

Hatima ya ujauzito wa mgonjwa mwenye seli mundu


Unaweza kuwa msaada mkubwa kwa wengine


Kopi linki hii inayofuata kisha washirikishe wengine kwenye mitandao ya kijamii kuhusu 'seli mundu wakati wa ujauzito'. Kufanya hivyo, utasaidia maelfu ya wajawazito wengi.

https://www.ulyclinic.com/elimu-kwa-mjamzito-magonjwa/seli-mundu-na-ujauzito Kuwashirikisha wengine kuhusu app ya 'ULY CLINIC' kopi kisha watumie linki hii inayofuata; https://play.google.com/store/apps/details?id=com.ulyclinic.ulyclinic&hl=en&gl=US Toa maoni yako nini unatala lufahamu kupitia linki ya 'mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeboreshwa,

30 Oktoba 2021 14:54:49

Rejea za dawa

 1. NHS Sickle Cell and Thalassaemia Screening Programme: https://www.gov.uk/topic/population-screening-programmes/sickle-cell-thalassaemia. imechukuliwa 09.07.2021

 2. NHS – Sickle cell anaemia: www.nhs.uk/conditions/Sickle-cell-anaemia. Imechukuliwa 09.07.2021 3. Sickle Cell Society: www.sicklecellsociety.org. Imechukuliwa 09.07.2021

 3. Furahini Tluway, et al. Sickle cell disease in Africa: an overview of the integrated approach to health, research, education and advocacy in Tanzania, 2004–2016. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC5558871/#. Imechukuliwa 09.07.2021

 4. NHS Sickle Cell and Thalassaemia Screening Programme at: https://www.gov.uk/topic/population-screening-programmes/sickle-cell-thalassaemia. imechukuliwa 09.07.2021

 5. Aken’ova YA, etal. Septicaemia in sickle cell anaemia patients: the Ibadan experience. The Central African Journal of Medicine. 1998;44:102–104.

 6. Appiah B, et al. Science reporting in Accra, Ghana: sources, barriers and motivational factors. Public Understanding of Science. 2015;24:23–37.

 7. Balasegaram M, et al. Neglected diseases in the news: a content analysis of recent international media coverage focussing on leishmaniasis and trypanosomiasis. PLoS Neglected Tropical Diseases. 2008;2:e234. 36.

 8. Booth C, et al. Infection in sickle cell disease: a review. International Journal of Infectious Diseases: IJID: Official Publication of the International Society for Infectious Diseases. 2001;14:e2–e12.

 9. Charache S, et al. Hydroxyurea: effects on haemoglobin F production in patients with sickle cell anaemia. Blood. 1992;79:2555–2565.

 10. Management of SCD in pregnancy. https://www.guidelinecentral.com/summaries/management-of-sickle-cell-disease-in-pregnancy/#section-420. Imechukuliwa 29/09/2021

 11. CDC. Sickle Cell Disease Emergency Guide. https://www.cdc.gov/ncbddd/sicklecell/healthyliving-emer-guide.html. Imechukuliwa 10.07.2021

bottom of page